MLIMA KILIMANJARO WAPOTEZA ASILIMIA 30 YA THELUJI YAKE



Mlima Kilimanjaro umepoteza takribani asilimia 30 ya theluji kuanzia mwaka 1912 mpaka sasa, Bunge limeelezwa. 
Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Ummy Mwalimu, alisema  kuyeyuka kwa theluji katika kilele cha mlima huo kumechangiwa na mabadiliko ya tabia nchi. 
Mwalimu alifafanua kwa kuzingatia utafiti ulifanywa na Taasisi ijulikanayo kama Intergovernmental Panel on Climate Change (IPCC).
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Ole, Rajabu Mbarouk Mohamed (CUF) aliyetaka kujua juhudi zilizofanywa na serikali kulinda mlima na wananchi wa vijiji vya karibu. 
Pia alitaka kujua ni kiasi gani cha theluji kilichopungua kutokana na athari ya mabadiliko ya tabia nchi.
Mwalimu alitaja baadhi ya juhudi za serikali na jumuia za kimataifa kuwa ni pamoja na kukabiliana na uharibifu unaochangiwa na mabadiliko ya tabia nchi kwa asilimia 5.3 kulingana na Mkataba wa Itifaki ya Kyoto na wa Umoja wa Mataifa (UNFCCC).
Alisema Mkoa wa Kilimanjaro unatekeleza progamu ya maendeleo endelevu ya matumizi ya ardhi katika kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi, mpango ambao pia unatekelezwa katika nchi za Afrika. 
Alisema mpango huo wa miaka minne (2011-2015) umefadhiriwa na Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa gharama ya Dola za Marekani milioni tatu (TSh bilioni 4.95)
“Tunatambua madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi kwa Mlima Kilimnajaro. Serikali kwa kushirikiana na jumuia za kimataifa tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali kuulinda,” alisisitiza Mwalimu.
Aidha, Mwalimu alisema serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) wametekeleza kazi ya upandaji miti na kudhibiti uchomaji moto misitu.
Akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, (Chadema) aliyetaka kauli ya serikali kuhusu kukatazwa wazee kuvuna miti yao waliyopanda miaka 20, Mwalimu alikiri kuwapo kwa zuia hilo na kuwa taka wazee hao kuvuna kwa kibali maalumu.

No comments: