Moja
ya kampuni nne zilizofikia makubaliano na Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa
Uwekezaji nchini (EPZA) kutoa huduma mbalimbali kwa kampuni kubwa zinazofanya
utafiti wa mafuta na gesi mkoani Mtwara, imetoa malipo ya awali kwa ajili ya
kufanikisha nia hiyo.
Kampuni
hiyo, Altus Oilfield Services FPZ ya Singapore imetoa hundi ya dola za
Kimarekani 526, 280 sawa na Sh milioni 800 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa
miundombinu ya eneo hilo.
Mkurugenzi
Mkuu wa EPZA, Dk Adelhelm Meru aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar
es Salaam wakati wa kupokea hundi hiyo kuwa fedha hizo zitatumika kuanza
kujenga miundombinu ya msingi kama barabara, umeme, maji na njia ya maji taka
katika eneo la kampuni hiyo.
“Uwekezaji katika eneo hilo utasaidia kukuza
ajira na uchumi wa nchi kuimarika zaidi,” alisema. EPZA inaendeleza hekta 10 za
eneo huru la Bandari ya Mtwara.
Mwakilishi
wa Kampuni ya MAC Group Limited aliyekabidhi hundi hiyo, Nagarayan
Sankaranarayanan alisema kampuni yake imejiandaa kuanza kufanya kazi ya kutoa
huduma kwa kampuni za utafutaji gesi na mafuta.
Eneo
hilo ni kati ya hekta 110 za eneo hilo huru la bandari ambalo limetengwa na
serikali kwa ajili ya uwekezaji mbalimbali.
Hekta
hizo 10 zitaendelezwa kwa kuwekewa miundombinu inayotakiwa na kisha kugawiwa
kwa kampuni za kimataifa zinazofanya kazi za kutoa huduma mbalimbali kwa
kampuni zinazofanya utafiti wa mafuta na gesi katika Mkoa wa Mtwara.
Imeelezwa
kituo hicho cha huduma kwa kampuni zinazofanya utafiti, kitakapokamilika
kitakuwa cha kipekee si kwa Tanzania pekee, bali katika ukanda mzima wa
Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Kampuni
nyingine zilizoingia Mkataba na EPZA mwezi uliopita kuwekeza katika eneo
hilo, ni Slumberger Seaco Inc ya Marekani, Tans Ocean Industries and
Services LTD ya Dubai na Lenna ya Iran.
Kazi
ya kupata wawekezaji katika eneo hilo, ilianza mwaka 2010 baada ya kampuni za
utafutaji gesi na mafuta kuomba kuwepo kwa kampuni za watoa huduma.
Miongoni
mwa vitu vitakavyokuwepo katika eneo hilo, ni karakana kubwa kwa ajili ya
kufanyia ukarabati na matengenezo ya vifaa vya mafuta na gesi.
Karakana
hizo zitajengwa kisasa na zitakuwa na uwezo pia wa kuhudumia nchi jirani kama
vile Kenya, Msumbiji, na Afrika Kusini.
No comments:
Post a Comment