MADANGURO NA 'GESTI' VYAATHIRI WATOTO



Ukatili, udhalilishaji na ukiukaji wa haki za mtoto, ikiwemo tabia ya wazazi au walezi kuwatuma watoto  vileo na kwenda nao kumbi za starehe vinadaiwa kukithiri hali ambayo serikali imeshauriwa kuchukua hatua kuvidhibiti. 
Wakati wanasheria kupitia Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wamepaza sauti kukemea vitendo hivyo, kwa upande wao watoto kutoka maeneo tofauti nchini, wametaka haki zao ziheshimiwe ikiwa ni pamoja na kuhakikisha  serikali inadhibiti nyumba za wageni na madanguro karibu na shule zao. 
Hayo yamesemwa jana katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika jana katika maeneo mbalimbali nchini. 
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa LHRC, Harold Sungusia, alisema matukio ya ukiukwaji wa haki za watoto yanaongezeka. 
Alizungumzia pia matumizi mabaya ya picha za watoto katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari hususani walioathirika na  vitendo vya ukatili.
Alisema vitendo vyote vinavyonyima watoto haki vinakwenda kinyume na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.
“Kumekuwepo na tabia ya wazazi ama walezi kuwatuma watoto wao vileo kama pombe na sigara na hata wengine kudiriki kwenda  na watoto wao katika kumbi za starehe mpaka majira ya usiku sana… hivyo vyote ni vitendo ambavyo vinakwenda kinyume na haki ya mtoto,” alisema Sungusia.
Alisema  wazazi hawajasimamia vyema wajibu wao  kuhakikisha watoto wao wanakua katika malezi yenye maadili salama  kwa kuwathamini na kuwalinda katika matukio mbalimbali ambayo yanaweza kuwanyima haki stahiki.
Alisema katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, wazazi  na walezi waitumie kwa kutokuruhusu kuwepo kwa picha mbaya za watoto walioathirika na vitendo vya ukatili,  katika mitandao ya kijamii. Alisema picha hizo huwaumiza watoto. 
Kuhusu watoto kufanyishwa kazi za ndani, alisema yamekuwepo matukio mengi ya watoto kupelekwa maeneo ya mijini kwa ajili ya kufanya kazi za ndani na kusababisha kuishi katika mazingira magumu.
“Watoto kama hao wanapopelekwa mijini hujikuta wakiishi katika mazingira magumu sana na kuanza kufanyiwa ukatili wa kimwili, kiakili na hata kingono,” alisema Sungusia.
Pia matukio ya watoto kubakwa na kulawitiwa  ni vitendo vya ukatili ambavyo kituo hicho cha wanasheria, kimesema vinaendelea kufanywa na wazazi, walezi na jamaa wa karibu.
Sungusia alisema ukatili huo unaendelea licha ya kuwepo sheria ya kumlinda mtoto. Alisema kutokana na kukithiri kwa matukio yasiyojali haki ya mtoto, ni wakati wa jamii kuthamini na kuheshimu nafasi ya watoto. 
Katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mkoani Dar es Salam, wanafunzi wameomba Serikali  kudhibiti nyumba za wageni na madanguro yaliyojengwa karibu na shule zao.
Katika risala yao, walisema moja ya changamoto kubwa wanazokutana nazo, uwepo wa nyumba hizo hufanya  wanafunzi wengi kuacha maadili yao na kufuata vitendo ambavyo havina maadili.
Maadhimisho hayo huadhimishwa kila Juni 16, kila mwaka  na nchi  za Afrika  51 kutokana na vifo vya watoto vilivyotokea Soweto Afrika Kusini mwaka 1976 na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kupata elimu iliyobora na isiyo na vikwazo ni haki ya kila mtoto.”
 Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi aliyekuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo,  alisema serikali imejipanga vyema  kukomesha vitendo vya ukatili kwa watoto. Alisema pia inajipanga kudhibiti ujenzi holela wa nyumba za muziki karibu na shule.
Katika hatua nyingine, Halmashauri ya Wilaya ya Hai,  mkoani Kilimanjaro ikishirikiana na viongozi wa serikali, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Shirika la Save the Children, imezindua kituo cha huduma jumuishi, kitakachosaidia wanawake na watoto  walioathiriwa na ukatili. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,  Charles Pallangyo, alisema kituo kitatoa msaada wa kisaikolojia, ulinzi, usalama na msaada wa kisheria. 
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Unicef Tanzania, Dk  Jama Gulaid, alisema anaamini wadau wakishirikiana na serikali, watapata suluhu katika kumaliza ukatili dhidi ya watoto. 
Kwa mujibu wa Utafiti juu ya Ukatili Dhidi ya Watoto, uliozinduliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto mwaka 2011, wastani wa msichana  kati ya watatu na mvulana kati ya wavulana saba, wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono. 
Utafiti unaonesha, zaidi ya asilimia 70 ya wasichana na wavulana wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili kabla hawajafikia umri wa miaka 18. Hata hivyo, waathirika wengi hawajamwambia mtu yeyote ukatili waliofanyiwa na ni kesi chache zimefikishwa polisi. 

No comments: