SHERIA YA KUSIMAMIA TAASISI NDOGO ZA HUDUMA ZA FEDHA YAANDALIWA


Muswada wa Sheria ya Kusimamia Taasisi ndogo za Huduma za Fedha, zikiwemo Vicoba, unaandaliwa na serikali. 
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alipojibu swali la mbunge wa Nkenge, Asumpta Mshama (CCM). 
Mwigulu alisema kumekuwa na ongezeko la asasi ndogo za kifedha za kundi la sekta ya fedha isiyo rasmi, ambazo zinatoa huduma za kifedha mijini na vijijini na ambazo hazijasajiliwa wala hazisimamiwi na mamlaka yoyote. 
Alisema serikali ilimwajiri Mshauri Elekezi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi (ESRF) mwaka jana kufanya utafiti wa mapitio ya Sera ya Taifa ya Taasisi ndogo za Huduma za Fedha ya mwaka 2000 ili hatimaye kuwa na sera, ambayo inazingatia mabadiliko yaliyopo katika sekta hiyo muhimu. 
Nchemba alisema ripoti ya awali kuhusu utafiti wa mapitio ya Sera ya Taifa ya Sekta ya Huduma ndogo za Fedha imekamilika na imebainisha maeneo muhimu ya kuyafanyia kazi, kama vile mafanikio, wigo, upungufu na changamoto. 
“Baada ya zoezi la mapitio ya Sera ya Taifa ya Huduma ndogo za Fedha kukamilika, Serikali itaandaa Muswada wa Sheria ya Kusimamia Taasisi Ndogo za Huduma za Fedha zikiwemo VICOBA,”  alisema. 
Katika swali lake, Mshama alihoji, “Je, serikali haioni ni wakati muafaka wa kuwezesha Vicoba kama inavyofanya  kwa Saccps kwa Saccos?”

No comments: