MAADHIMISHO SIKU YA KUCHANGIA DAMU KUFANYIKA KIGOMA


Maadhimisho ya siku ya wachangia damu duniani inatarajiwa kufanyika kitaifa mkoani  Kigoma huku Mwenyekiti wa Taasisi  ya Wanawake na Mandeleo (Wama) Mama Salma Kikwete akitarajiwa kuwa mgeni rasmi. 
Hayo yalisemwa jana na na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Suleiman Rashid wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. 
Alisema maadhimisho hayo yatafanyika Juni 14 mwaka huu mjini Kigoma na kaulimbiu ni ‘damu salama uhai wa mama’ ikilenga kutambua wajibu wa kila mwananchi katika kusaidia kuokoa maisha ya kina mama kwa kuchangia damu. 
Pia alisema madhumuni ya kampeni ya mwaka huu ni kuhamasisha sekta ya afya na wadau wengine hususani nchi zenye vifo vingi vya kina mama kuchukua hatua ya kuhakikisha upatikanaji wa damu na mazao yake. 
Wakati huo huo alisisitiza, “Hakuna damu inayouzwa katika hospitali yoyote na atakaebainika kuuza hatua kali zitachukuliwa dhidi yake,” aliongeza. 
Aidha kutokana na mahitaji kuwa makubwa kuliko upatikanaji baadhi ya ndugu hulazimika kuchangia pale inapokosekana. 
Inakadiriwa mahitaji ya damu kwa mwaka ni wastani wa chupa 400,000 mpaka 450,000. Kwa sasa uwezo wa mpango unakusanya kati ya chupa 150,000 hadi 180,000 kwa mwaka.

No comments: