NBAA, BOT WATAKIWA KUFANYA KAZI PAMOJA KUSAIDIA UMMA


Waziri wa Viwanda na Biashara, Abdallah Kigoda ametaka Benki Kuu Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Bodi ya Uhasibu Tanzania (NBAA), kuhakikisha wanaboresha utoaji huduma za kifedha, ili kupanua wigo wa watumie huduma hizo. 
Alitoa mwito huo jana mjini hapa wakati akifungua semina iliyoandaliwa na BoT na  NBAA na kushirikisha na wahasibu kutoka taasisi za kifedha nchini, kujadili masuala mbalimbali ya kifedha, ikiwemo ya kuweka utaratibu mpya wa utoaji huduma za kifedha unaofanana na kimataifa. 
Alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha huduma hizo, kwani sekta hiyo ina mambo mengi na yanayobadilika kila mara. 
“Lakini kubwa ninaloomba katika masuala yote mtakayojadili hili la kupeleka huduma za kifedha zilizo rasmi  kwa watanzania wengi ni la msingi na la kulifanyia kazi,” alisema. 
Aidha aliwapongeza kwa kuamua kukutana kila mwaka mara moja kuimarisha kazi zao ambazo kimsingi hubadilika kila wakati na itasaidia kuimarisha ujuzi wa wafanyakazi wa sekta hiyo. 
“Lakini pia hili suala la kuweka utaratibu mpya wa utoaji huduma za kifedha unaofanana na viwango vya kimataifa au duniani kote ni mzuri sana na utawezesha kuongeza uwazi maeneo ya kazi,” alisema. 
Mkurugenzi wa Bodi ya NBAA, Pius Maneno alisema semina hiyo ina washiriki  zaidi ya 300. 
Watazungumzia viwango vya kiuhasibu, masoko mapya ya mitaji na taasisi za fedha, lakini zaidi watajikita kuangalia jinsi ya kuboresha na kuendesha taasisi za kifedha ili kutoa taarifa zilizo sahihi kwa wadau wao. 
“Hili litatusaidia sana katika utoaji taarifa zetu za kifedha kwa wadau  na tutaboresha sana utendaji kazi wetu,” alisisitiza.

No comments: