Waziri
Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali kwa sasa imeanza kusambaza kompyuta katika
vyuo vikuu nchini kwa lengo la kuboresha elimu kwa wanafunzi.
Pia,
amesema baadaye Serikali itaanza kusambaza kompyuta ndogo zinazobeba vitabu
kidijitali, maarufu kama tabuleti (tablets) kwa wanafunzi.
Alisema
hayo bungeni jana wakati wa kipindi cha
maswali ya papo kwa hapo. Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Maryam Msabaha (Chadema).
“Nchi
zilizoendelea zimewekeza sana katika elimu, lakini sisi Tanzania kwa nini hatuwekezi katika elimu ?”
Alihoji.
“Sisi
hapa mtoto akienda shule asubuhi anabeba fagio, lakini kwa wenzetu anabeba
kompyuta. Hata kwa majirani zetu Kenya, mtoto anabeba lap top asubuhi.”
Msabaha
aliongeza “Je huoni kwamba wakati umefika sasa kwa wanafunzi wetu wa darasa la
Kwanza hadi la Saba wawe na lap top?”
Akijibu
swali hilo, Pinda alisema Serikali imejitahidi kuboresha Sekta ya Elimu nchini,
kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo na vyuo vikuu.
Waziri
Mkuu alisema inachofanya Serikali kwa sasa ni kutatua matatizo hayo ya msingi
katika Sekta ya Elimu hatua kwa hatua.
Kuhusu
suala la kusambaza kompyuta shuleni na vyuoni, Waziri Mkuu alisema kwa sasa
lengo la Serikali ni kusambaza kompyuta katika vyuo vikuu na baada ya hapo
ndipo zitafuata shule za sekondari na msingi.
Waziri
Mkuu alisema Serikali ingependa wanafunzi wawe na tabuleti na lap top, lakini
uwezo wa Serikali ni mdogo na ndiyo maana wameamua kuanza na wanafunzi wa vyuo
vikuu.
Waziri
Mkuu aliulizwa swali lingine na Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia (Chadema),
ambaye alitaka kujua ni lini atawarejesha madarakani madiwani watatu wa Jimbo
la Ilemela Mkoa wa Mwanza, waliofukuzwa na Meya wa Manispaa hiyo.
“Meya wa Ilemela alifukuza madiwani watatu wa
Chadema, kwa madai hawakushiriki vikao vitatu vya Baraza la Madiwani.
Nilikuletea vielelezo na wewe ulifanya uamuzi wa kuwarejesha, lakini nasikia
ulipata pingamizi kutoka Mkoa wa Mwanza. Sasa ni mwaka mmoja na miezi sita
tangu wamefukuzwa. Je, ni lini utawarejesha?” Alihoji Kiwia.
Waziri
Mkuu alisema hakuna kitu chochote cha makusudi kinachochelewesha kutoa uamuzi
wa mwisho wa suala hilo. Alisema ni kweli alishafanya uamuzi wa kuwarejesha,
lakini alipata pingamizi (counter request) kwamba maelezo aliyopewa hayakuwa
sahihi.
Alisema
baada ya hapo, alirejesha tena suala hilo kwa wataalamu na mamlaka zingine ili
wamshauri tena na kwamba ni juzi tu amepata mapendekezo ya wataalamu hao na
mamlaka hizo.
Pinda
alimtaka Mbunge huyo kuwa na subira, kwani uamuzi atautoa hivi karibuni.
“Tarehe siwezi kusema ni lini. Lakini suala hili nitalipa umuhimu mkubwa.
Nitafanya uamuzi hivi karibuni na nitarejesha uamuzi huo mkoani Mwanza,”
alisisitiza. Waziri Mkuu ndiye mwenye dhamana na Serikali za Mitaa.
No comments:
Post a Comment