DK BILAL AHIMIZA UMUHIMU WA UTUNZAJI MAZINGIRA



Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, umetolewa mwito wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira  kufanyika kila siku badala ya kusubiri Siku maalumu ya Maadhimisho ya Mazingira Duniani.
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal alitoa ushauri huo  wakati akifunga maadhimisho ya kilele cha Siku ya Mazingira yaliyofanyika kitaifa mkoani Mwanza kwenye viwanja vya Furahisha.
Alisema ili kupunguza na kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotishia jitihada za kujiletea maendeleo ni muhimu kuchukua hatua za kuhakikisha  mazingira yanatunzwa na kuhifadhiwa vizuri.
“Tupande miti na kutunza misitu yetu ili itusaidie kunyonya hewa ukaa zinazosababisha mabadiliko ya tabianchi na katika nchi zilizoendelea tutashinikiza zichukue  hatua mahususi za kupunguza uzalishaji wa gesijoto,” alisema Dk Bilal.
Alisema pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, mazingira ni sehemu ya maisha ya binadamu lakini wameendelea kushuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kilimo, mifugo, viwandani, matukio ya moto na uchomaji wa misitu na mrundikano wa taka katika maeneo ya miji na makazi.
Alisema Tanzania imeshuhudia athari za madadiliko ya tabianchi katika sekta zote za kiuchumi zikiwemo za kilimo, nishati, maji, miundombinu, mifugo, afya na maliasili.
Kwa upande wa kilimo, Makamu wa Rais alisema imeathiriwa kutokana na ukosefu wa mvua za uhakika na ukame wa mara kwa mara unaosababisha uzalishaji hafifu wa mazao ya kilimo hivyo kuchochea tatizo la njaa nchini nakulazimisha serikali kuwapa chakula wananchi.
Akizungumzia athari kwenye miundombinu alisema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi ya mafuriko ambapo kwa mwaka huu yamegharimu maisha ya Watanzania na kuharibu miundombinu.
Alisema katika Jiji la Dar es Salaam zaidi ya Sh bilioni 20 zinahitajika kwa ajili ya kurejesha miundombinu ya barabara na kwamba mafuriko yaliyotokea Morogoro yameleta hasara kubwa kwa taifa.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,  Dk Seif Rashid alisema njia rahisi ya kupambana na ugonjwa wa homa ya dengue ni usafi wa mazingira. Alisema wananchi wanatakiwa kushiriki kikamilifu katika kuweka mazingira safi kwenye maeneo yanayowazunguka.
Alisema tangu ugonjwa huo ulipuke kumekuwa na wagonjwa 1,119 na vifo vya watu wanne.
Katika kilele cha maadhimisho hayo ya Siku ya Mazingira, zawadi na tuzo mbalimbali zilitolewa kwa taasisi na watu binafsi walioshiriki kwenye utunzaji wa mazingira.

No comments: