OFISA MASOKO KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA KUIBA MILIONI 69.8/-



Ofisa Masoko wa Kampuni ya NN General Supplies Simon Lyatuu (47) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka ya wizi wa Sh milioni 69.8.
Lyatuu alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali Celina Kapange mbele ya Hakimu Mkazi Gabriel Mirumbe.
Wakili Kapange alidai kuwa kati ya Januari mosi, 2012 na Aprili 30, mwaka jana katika kampuni hiyo iliyopo mtaa wa Gerezani barabara ya Kilwa, Lyatuu aliiba Sh milioni 69,885, 525 mali ya mwajiri wake.
Mshitakiwa alikana mashitaka na upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Mirumbe alisema mshitakiwa atapata dhamana endapo atakuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya Sh milioni 20 na mmoja awasilishe hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Mshitakiwa alirudishwa rumande kwa kuwa hakukidhi masharti ya dhamana ambapo upande wa Jamhuri ulikwenda kuhakiki hati ya nyumba iliyowasilishwa na wadhamini wa mshitakiwa. Kesi itatajwa tena Juni 18, mwaka huu.

No comments: