MBUNGE WA UKEREWE AACHIWA HURU TUHUMA ZA UCHOCHEZI


Mbunge wa Ukerewe, mkoani Mwanza,  Salvatory  Machemli  ameachiwa huru na Mahakama baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka ya uchochezi yaliyokuwa yakimkabili.
Hukumu  hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe, Faustine Kishenyi. 
Hakimu Kishenyi alisema mahakama imeridhika mshitakiwa hana hatia    baada ya  upande wa mashitaka  kushindwa  kuthibitisha  kosa  lake. 
Alisema mbali ya Polisi kushindwa kuwasilisha vielelezo mahakamani kama ilivyo katika hati ya mashitaka,  pia  ushahidi uliotolewa na  upande wa mashitaka unaonekana  kuzingatia  zaidi maslahi yake;  hivyo haujitoshelezi kumtia mshitakiwa hatiani. 
Kwa mujibu wa hakimu, upande wa  mashitaka umeshindwa kuwasilisha  CD  iliyochukuliwa wakati  mshitakiwa akitenda kosa  huku polisi watatu wakiwa ndio pekee wametoa ushahidi dhidi ya mshitakiwa. 
Amesema  ushahidi  uliothibitishwa na  shahidi  kutoka nje ya  jeshi hilo ambalo ndio linadai kulengwa,  unaonekana  kuwa  na maslahi ya upande mmoja  hivyo  hauwezi kutumika  kumtia hatiani mshitakiwa. 
Awali ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka wa  Polisi,  Samwel  Onyango kuwa  Machemli  (39) alitenda kosa la uchochezi  Oktoba 23 mwaka 2011 wakati anahutubia mkutano wa  hadhara katika Kijiji cha Nyamanga kisiwani Ukara. 

Ilidaiwa Machemli kwa makusudi alichochea  wananchi  wazuie  shughuli za polisi na hata   kuwashambulia wakienda  katika  maeneo yao  kutafuta  wahalifu.

No comments: