HALMASHAURI DAR ZAASWA KUTUNZA MAZINGIRA



Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam zimeaswa  kushirikiana na Serikali za Mitaa kusimamia sheria ya utunzaji wa mazingia ili kufikia malengo ya kuimarisha usafi.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sophia Mjema aliyasema hayo jana jijini  wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira ambayo kitaifa yamefanyika jijini Mwanza.
Maadhimisho hayo huadhimishwa  Juni 5,  kila mwaka, yameanza rasmi Juni Mosi mwaka huu yenye  kaulimbiu ‘’Utunzaji wa mazingira kukabili mabadiliko ya tabia ya nchi.’’
Alisema sheria hizo zinapaswa zisimamiwe ili kuzuia wanaojenga nyumba kwenye kingo za mito ambazo zinasababisha maji kushindwa kupita katika njia zake na kusababisha mafuriko.
Aidha,  aliwataka kuzuia utiririshaji wa majitaka kwenye mitaro ya barabara na makazi ya watu wakati wa mvua, kwani wanahatarisha maisha na  badala yake kutafuta magari ya majitaka kuondoa uchafu huo.
‘’ Tunaendelea kusisitiza kwamba Jiji la Dar es Salaam hakuna machimbo ya mchanga wala vifusi hivyo viongozi wa Serikali za Mitaa wasimamie kwani chanzo cha kubomoka kwa madaraja yanaleta maafa kutokana na uchimbaji,’ ’alisema Mjema.
Aliongeza kuwa watendaji wazuie wafanyabiashara walio katika hifadhi za barabara kwa kuwa maeneo hayo si salama na kwamba waende maeneo waliyoandaliwa na Serikali.
Alisema  lazima kutambua mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yameongezeka kutokana na shughuli za binadamu  hivyo kutafuta njia ya kutatua matatizo yatokanayo na mabadiliko hayo.
Naye, Mwenyekiti wa Taasisi isiyo ya kiserikali inayoshughulikia masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa (Forum cc), Euster Kibona alitoa mwito kwa viongozi wa Mkoa kutoa kipaumbele kwa taasisi hizo kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Alisema wanajamii wanahitaji kutoa ushirikiano katika kukabiliana na tatizo hilo kwa kudhibiti uzalishaji mkubwa wa taka na matumizi ya kuni kwa vijijini.
‘’Elimu ya ziada inatolewa kuhusu matumizi ya kuni licha ya  matumizi ya gesi kuwa juu hivyo tunaiomba Serikali iangalie jinsi ya kudhibiti gharama za gesi kuwasaidia wengine kuepuka ukataji wa miti,’’ alisema Kinabo.

No comments: