RUKWA WALENGA KUSHUSHA MAAMBUKIZI YA VVU HADI ASILIMIA 2



Shirika lisilo la kiserikali Resource Oriented Development Initiative (RODI) limedhamiri kusaidia kupunguza kiwango cha maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) mkoani Rukwa kutoka asilimia 6.2 ya sasa hadi kufikia asilimia 2.0 ifikapo 2015.
Mkurugenzi wa RODI mkoani Rukwa, Gideon Mpina alibainisha hayo hivi karibuni alipokuwa anazungumzia mikakati ya shirika lake katika mapambano dhidi ya Ukimwi.
RODI inatekeleza  miradi ya  mapambano  dhidi  ya maambukizi  ya VVU  na kutoa  Elimu  ya Afya ya Uzazi  na Ujinsia (TMEP) kwa ufadhili  wa Taasisi  ya Kimataifa  ya Elimu  ya Afya na Uzazi  kutoka  nchini Sweden (RFSU) ambapo  kiwango  cha maambukizi  ya VVU  kimeripotiwa  kuongezeka kutoka  asilimia  4.9  mwaka 2010  hadi  kufikia  asilimia 6.2  mwaka  huu.
Alizitaja mbinu  zitakazotumiwa na RODI  kupunguza  maambukizi  hayo  ya VVU  kwa  kipindi  cha mwaka mmoja  kuanzia sasa  zikiwemo  kusambaza  kondomu  na  kutoa  elimu  sahihi  ya matumizi  yake  pia  kuwaelimisha  wakazi  wa mkoani  humo  umuhimu  wa tohara  kwa  wanaume.
Alibainisha  kuwa  kiwango  cha maambukizi  wilayani Sumbawanga  kinatisha  ambapo  kiwango  cha maambukizi  katika    Mji Mdogo wa Laela na Mji wa Mpui  wilayani  humo  ni  asilimia  10  kila  mmoja.
Kwa mujibu  wa takwimu  za  Afya mkoani Rukwa, kiwango  cha maambukizi  ya VVU Manispaa ya Sumbawanga  kimefikia  asilimia 5.2.

No comments: