WAKULIMA WA UFUTA NACHINGWEA WALIPWA NOTI BANDIA



Wafanyabiashara wilayani Nachingwea mkoani Lindi  wanadaiwa kutumia fedha bandia kununulia zao la ufuta.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Regina Chonjo wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi.
Alisema wachuuzi hao wanaenda kwa wakulima kununua ufuta vijijini, kuwalaghai  na kuwapa fedha za bandia bila wao wenyewe kufahamu na hatimaye kuzipokea.
Chonjo alisema ni vyema wakulima wakafanya mauzo ya fedha taslimu kupitia benki za NMB au CRDB kwani wao wana mashine maalumu ambazo itawezekana kubaini uhalali wa noti hizo.
Alisema ulipwaji wa fedha hizo za bandia kufanyika huku pia wakulima wakiwa wamelaghaiwa kwa bei ndogo ya zao kutoka Sh 2,500 kwa kilo moja hadi kufikia Sh 1,200 katika msimu wa mwaka huu.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa uongozi wa Wilaya utafuatilia kwa makini matendo ya wanunuzi hao ya kuwalaghai wakulima kwa kuwapa bei ya chini chini ya utaratibu uliokubaliwa, huku wakiwalipa fedha feki.

No comments: