Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na
Ushirika, Godfrey Zambi amemtaka mmiliki wa kiwanda cha mvinyo cha CETAWICO
kilichopo Dodoma kuhakikisha analipa deni lote la wakulima wa zabibu lipatalo
Sh milioni 700 kabla ya mwisho wa mwezi huu.
Wakulima hao kutoka Kijiji cha Hombolo
waliitaka Serikali kuwasimamia ili waweze kulipwa madai yao ya zaidi ya Sh
milioni 700 wanazomdai mwekezaji wa kiwanda cha Cetawico.
Madai hayo yalithibitishwa na Mhasibu
wa kiwanda cha Cetawico Jacson Temu ambaye alimwambia Naibu huyo kwamba kiwanda
hicho kinadaiwa kiasi cha Sh milioni 703.
Naibu Waziri Zambi amesema kwamba kama
muda huo utapita na mwekezaji huyo hajawalipa wakulima, Serikali itamchukulia
hatua kali.
Katibu wa Ushirika wa Wakulima wa
Zabibu na Masoko Hombolo Ramadan Mkombozi alisema wakulima wanamdai mwekezaji
wa kiwanda hicho cha Cetawico Dk Florenzo Chesini, raia wa Italia fedha hizo
kwa zaidi ya miezi 9.
Alisema pamoja na jitihada mbalimbali
walizofanya zikiwemo kushirikisha Serikali ya Wilaya na Mkoa ili madeni yao
yalipwe hawajafanikiwa kutokana na kutopewa ushirikiano na badala yake kuishia
kupewa majibu yasiyoridhisha.
‘’Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuwa
umekuja tunaweza kupata madai yetu lakini huyu mwekezaji hii siyo mara yake ya
kwanza kutotulipa hata mwaka jana msimu wa mwezi wa pili ilibidi Waziri Chiza
aingilie kati ndiyo tukalipwa, japo si malipo yote,“ alisema na kuongeza kwamba
pamoja na kukosa ushirikiano pia bei yenyewe si nzuri na hupanga bei yeye.
Alisema akipelekewa zabibu huwa
zinapimwa zinaachwa kiwandani na kisha anajipangia bei. Alisema wakati wa
kiangazi analipa kilo moja Sh 800 au 1000
na wakati wa masika 500 au 400 bila kujali gharama za uendeshaji hali
inayowapa hasara kubwa wakulima.
No comments:
Post a Comment