KIKWETE AHIMIZA WANAWAKE KUJITOKEZA KUPIMA SARATANI



Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha inapunguza vifo vinavyotokana na saratani ya mlango wa kizazi na matiti nchini. 
Hayo yameelezwa na Rais Jakaya Kikwete wakati akizindua kampeni ya uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi na ile ya matiti  uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Chipukizi mjini hapa.
Alisema Serikali itahakikisha vifo vinavyotokana na saratani ya mlango wa kizazi vinapungua kwa kiasi kikubwa kwani tayari wizara inajipanga kufanya hivyo.
Alisisitiza kuwa, saratani inatibika na kupona kabisa ila kikubwa ni kuhakikisha wanawake wanajitokeza kufanyiwa uchunguzi wa afya zao mara kwa mara, angalau mara moja kila baada ya miaka mitatu huku wale wenye matatizo ya Ukimwi wakishauriwa kuchunguzwa mara moja kwa mwaka.
Rais Kikwete alisema mpango uliopo ni kuhakikisha huduma za uchunguzi zinafanyika kila hospitali hapa nchini.
Alisema licha ya taarifa iliyotewa na Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) inaonesha kuwa ni miaka tisa tu iliyofikiwa kwa ajili ya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti.
Alisema kwamba kwa sasa MEWATA kupitia Wizara ya Afya na Ustawi ya Jamii inapaswa kuwezeshwa kufikia wanawake wengi nchi kote ili kuwapunguzia umbali wa safari.
Aidha Rais Kikwete aliwataka wanawake kujitokeza kwa wingi katika kampeni hiyo ili wafanyiwe uchunguzi wa mlango wa kizazi na matiti ili waweze kupata tiba haraka.
Alisema iwapo mgonjwa atafikishwa hospitali na kufanyiwa uchunguzi wa awali anaweza kupona, lakini wanaokwenda baada ya ugonjwa kufikia hatua za mwisho hupata shida kupona. Aliyataja makundi ya wanawake yanayoathirika zaidi ni wenye umri wa kati ya miaka 30 na 60.
Akizungumzia ujenzi wa vituo vya afya, alisema tayari vimejengwa vituo 97 kwa ajili kutoa huduma za aina hiyo  kwa lengo la kusaidia MEWATA ambao wameonesha nia njema kwa jamii.
Awali, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kebwe Stephen Kebwe alisema wizara yake inapambana kuhakikisha ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti kwa wanawake unatoweka nchini.
Akitoa taarifa ya MEWATA, Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Dk Sarafina Mkuwa alisema katika wilaya za Urambo, Nzega na Tabora Mjini wanatarajia kuhudumia wanawake 5,000, lengo likiwa kuhakikisha mama anakuwa na afya njema kwa ajili ya kukuza uchumi na maendeleo ya Taifa.

No comments: