Wiki mbili baada ya kuitwaa rasmi
Ikulu ya Malawi, Rais mpya wa nchi hiyo, Profesa Peter Mutharika anatarajiwa
kufunga ndoa na Gertrude Maseko Jumamosi ijayo, baada ya kuishi maisha ya
ukapera kwa zaidi ya miaka 30.
Mutharika, mdogo wa Rais wa Pili wa
Malawi, Bingu wa Mutharika ambaye kwa sasa ni marehemu, alikuwa mume wa
Christophine G. Mutharika, raia wa Visiwa vya Carribean na kubahatika kuzaa
naye watoto watatu, Monique, Moyenda na Mahopela ambao wote ni wanasheria
mahiri kwa sasa nchini Marekani.
Hata hivyo, Mutharika alimpoteza
mkewe huyo kwa ugonjwa wa kansa mwaka 1990, hivyo kumfanya asioe kwa muda
mrefu, huku akijikita zaidi katika kazi zake za uwakili kwa zaidi ya miaka 40
nchini Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya
Malawi iliyosainiwa na Mwandishi wa Habari wa Rais, Chikondi Juma imeeleza kuwa
ndoa ya Rais Mutharika na Maseko itafungwa Jumamosi ya Juni 21 mwaka huu katika
Kanisa la Mtakatifu Michael na Malaika Wote, jijini Blantyre.
Harusi hiyo inafanyika huku Wamalawi
wakifanya chereko za kuwasili kwa mara ya kwanza nchini Malawi kwa mabinti wa
rais huyo, Monique na Moyenda, siku chache baada ya uchaguzi uliomwingiza Ikulu
baba yao akiwa Rais wa Tano wa nchi hiyo.
Taarifa hiyo ya Ikulu imeongeza
kuwa, Maseko ambaye alikuwa mbunge wa jimbo la Balaka Kaskazini kwa tiketi ya
chama cha Democratic Progress (DPP) cha Mutharika, ni mwandani wa muda mrefu wa
Rais mpya na kwamba alikuwa sambamba naye katika kampeni za uchaguzi mkuu
uliofanyika Mei 20, mwaka huu na kuhitimisha utawala wa miaka miwili na ushee
wa Rais Joyce Banda.
“Baada ya shughuli za kanisani,
chereko zitahamia katika familia ya Mutharika iliyopo Ndata katika Wilaya ya
Thyolo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Tukio la kuoa na kuwasili kwa watoto
wake, kumeelezwa kumaliza uvumi uliokuwa umeenezwa na wapinzani wake kisiasa
kuwa, Mutharika hakuwa mwanamume aliyekamilika.
Uvumi huo ulijibiwa na Katibu Mkuu
wa DPP, Chimwemwe Chipungu mara baada ya kuwapokea mabinti hao kwenye Uwanja wa
Ndege wa Lilongwe wakitokea Marekani, akisema: “Watu walikuwa na hofu kama Rais
Mutharika ana watoto. Ni uvumi wa kijinga. Waliokuwa wakieneza uvumi huo sasa
watapata aibu. Rais wetu ana watoto na ni baba wa familia.”
Na Rais Mutharika mwenyewe, wakati
wa kampeni aliyasigina maneno ya wapinzani wake kwa kusema ana watoto wenye
afya njema, akili timamu na wanasheria maarufu Marekani, mmoja akiwa Profesa
katika moja ya vyuo vikuu vya huko.
“Ukiachana na watoto, pia nina
wajukuu kadhaa,” alisema Mutharika mwenye umri wa miaka 74 sasa ambaye akiwa
mwanazuoni katika masuala ya sheria, aliwahi kufundisha katika vyuo kadhaa,
kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika miaka ya 1970.
Kabla ya kuutwaa urais wa Malawi,
Profesa Mutharika aliyebobea katika masuala ya sheria ambaye pia ni mwanasiasa
mzoefu na mashuhuri, ameshika nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali
zikiwamo Wizara ya Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia, nafasi aliyoishika hadi anaingia katika uchaguzi mkuu hivi
karibuni.
No comments:
Post a Comment