Ahadi za wadau wa uhifadhi na vita dhidi ya ujangili nchini
wameanza kutimiza ahadi zao baada ya jana kukabidhi helikopta ya kisasa
itakayotumika katika kazi hiyo maalumu kwa ajili ya Pori la Akiba la Selous.
Helikopta hiyo aina ya Robertson R44
yenye thamani ya dola za Kimarekani 500,000 (sh milioni 800), ni moja ya ahadi
za Howard Buffett, mtoto wa bilionea wa Marekani anayeshika nafasi ya tatu kwa
utajiri duniani, Warren Buffet mwenye utajiri wa dola za Kimarekani bilioni
64.8 (sh trilioni 105).
Howard, akiwa nchini miezi ya hivi
karibuni alikutana na Rais Jakaya Kikwete Ikulu, Dar es Salaam na kuahidi
kuchangia helikopta katika kukabilia na ujangili hususan wa tembo kwa kile
alichosema ameguswa na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Tanzania katika
kukabili ujangili.
Mbali ya helikopta hiyo, Buffet pia
anakusudia kusaidia vifaa vyenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 5 (sh
bilioni 8) katika kuimarisha ulinzi dhidi ya wanyamapori na uhifadhi kwa
ujumla.
Na jana, Balozi wa Marekani Mark
Childress alikabidhi helikopta hiyo yenye uwezo wa kubeba watu wanne kwa Waziri
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli na Waziri Kivuli wa
Wizara ya Maliasili, Mchungajui Peter Msigwa pia walihudhuria hafla ya
makabidhiano hayo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam.
Balozi Childress alisema vita dhidi
ya ujangili inahitaji vifaa na teknolojia ya kisasa, akisema helikopta ni
sehemu ya kampeni katika mapambano hayo. Ujangili dhidi ya tembo umesababisha
vifo 20,000 katika muongo mmoja, asilimia 80 kati yavifo hivyo vikitokea katika
nchi za Afrika Mashariki.
Akipokea helikopta hiyo, Nyalandu
aliishukuru Serikali ya Marekani na juhudi za wahisani, kwa kuunga
mkono juhudi za serikali ya Tanzania katika vita dhidi ya ujangili, huku
akisema serikali itaongeza helikopta nyingine mbili kwa ajili ya kupambana na
majangili.
Alisema moja itakuwa aina ya Bell
206 na nyingine Robertson 44 zitanunuliwa ili kuimarisha ulinzi dhidi ya
majangili katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro na nyingine zenye matukio
yanayohusiana na ujangili.
Naye Lembeli alielezea kufurahishwa
kwake na juhudi za serikali za kuonesha kwa vitendo mikakati ya kukomesha
ujangili nchini, huku akitaka wanaobeza kazi nzuri ya serikali wapuuzwe.
“Jamani, kazi nzuri inafanywa na
Nyalandu na wizara yake na serikali kwa ujumla, badala ya kuwakatisha tamaa na
kuingiza siasa, tuwaunguze mkono ili kulinda rasilimali hizi za taifa kama
lilivyokuwa lengo la mwasisi wa taifa hili, Hayati baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere…,” alisema.
Kwa upande wa Mchungaji Msigwa,
alisema anashukuru kuona kelele nyingine wanazopiga kwa lengo la kuisukuma
serikali kufanya kazi zinafanyiwa kazi, na sehemu ya matunda hayo ya kupatikana
kwa helikopta ya kusaidia vita dhidi ya ujangili.
Alisema kwa kazi nzuri inayofanywa
na serikali, atashangaa kusikia watu wakibeza hatua zinachukuliwa kukabili
ujangili, huku akisisitiza kuwa, watakuwa sawa na wendawazimu kwani dhamira ya
Watanzania wengi ni kuona inapatikana tiba ya kudumu dhidi ya mauaji ya wanyama
kama tembo.
Rubani wa helikopta hiyo, Peter
Achammer alisema chombo chake ni imara na kinaweza kuwa hewani kwa saa tatu na
kusafiri kwa kasi ya kilomita 240 kwa saa.
Ofisa wanyamapori kutoka kikosi cha
ujangili Kanda ya Mashariki na Pwani inayohusisha mikoa ya Dar es Salaam,
Tanga, Lindi, Mtwara and Morogoro, Dickson Machumu alisema helikopta hiyo
itaongeza ufanisi katika majukumu, huku ofisa mwingine katika kikosi hicho,
Mariam Haji akisema itasaidia katika mambo mengi, ikiwa pamoja na kuwawahisha
hospitali wapiganaji inapotokea wamejeruhiwa katika mapambano na majangili.
No comments:
Post a Comment