Siku moja baada ya mlipuko wa kitu
kinachosadikiwa kuwa ni bomu na kusababisha kifo na kujeruhi watu saba eneo la
Darajani mjini Unguja, mmoja wa majeruhi ameelezea jinsi mwenzao alivyouawa
wakati wakisubiri daladala baada ya kutoka kuswali msikitini.
Shuhuda huyo, Khalid Ahmed amesema
mwenzao alipigwa kwa kitu kinachosadikiwa ni bomu kilichorushwa na kutua
mwilini na kufa papo hapo huku wengine wakijeruhiwa.
Tukio hilo limethibitishwa na Naibu
Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Kamishna Yussuf Ilembo na kumtaja
marehemu kuwa ni Muhammad Khatib Mkombalaguha (26), Msambaa na mkazi wa Tanga
ambaye alikufa papo hapo.
Aidha, kutokana na tukio hilo, Jeshi
la Polisi limewatangazia hali ya hatari wahusika, huku uchunguzi ukianzia
kwenye mabaki ya vitu vilivyokutwa katika eneo la tukio.
Akielezea tukio hilo, Ilembo alisema
mtu aliyekufa na wengine waliojeruhiwa, walikuwa wametoka Msikiti wa
Darajani baada ya Ibada ya Swala ya Isha inayoswaliwa kuanzia saa 1:45 usiku na
kuendelea, lakini huishia kabla ya swala ya alfajiri. Mbali ya Ibada, pia
walitoa mawaidha msikitini.
Alisema mara baada ya kumaliza ibada
hiyo walitoka msikitini na kufika eneo la Darajani wakisubiri gari na ndipo
mlipuko mkubwa uliposikika ambao unasadikiwa kuwa ni bomu na kuwajeruhi saba na
wanane kufa papo hapo.
“Jeshi la Polisi linaendelea na
uchunguzi zaidi wa tukio hilo ambalo limezusha
taharuki kubwa kwa wananchi wa
Zanzibar katika kipindi hiki kumekuwepo na ugeni wa watu mbalimbali,” alisema.
Katika hatua za kwanza za upelelezi,
Ilembo alisema wamekusanya baadhi ya vielelezo ikiwemo vipande vya mabaki ya
gundi ya karatasi (solar tape) na vitu vingine ambavyo vinasadikiwa vimetumika
kwa ajili ya kutengeneza bomu hilo.
Pia katika mlipuko huo, magari
mawili, moja aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili Z 675 na
jingine aina ya Toyota IST lenye namba za usajili Z 268 yaliharibiwa kwa
kuvunjwa vioo na matairi yake kupasuka.
Katika ajali hiyo waliojeruhiwa na
kulazwa katika hospitali ni Hamad Nassor Kassim (46), ambaye ameumia kichwa,
Khalid Ahmed Haidar (16), Ahmed Haidar Jabir Alfarsy (47) ambao wamelazwa
katika Hospitali ya Al-Rahma. Wengine ni Suleiman Ali Juma (21) amelazwa katika
Hospitali ya Al-Rahma huku Kassim Issa Muhammad akiruhusiwa baada ya kupata
matibabu.
Naye Ahmed ambaye ni mmoja ya
mashuhuda wa ajali hiyo, alisema kitu hicho kinachosadikiwa kuwa ni bomu
kilirushwa kwa mkono na kumpata moja kwa moja Mkombalaguha na baadaye
kuwajeruhi watu wengine.
“Bomu lile linaonekana moja kwa moja
kuwa ni la kurushwa kwa mkono kwa sababu lilimfikia mwilini marehemu na baadaye
kutuathiri wengine,” alisema.
Mji wa Zanzibar wiki hii umekuwa na
ugeni mkubwa kutoka nchi mbali mbali za Afrika ya Mashariki wakihudhuria ibada
ya Kiislamu ya Ijitimai inayofanyika huko Fuoni.
Aidha, wageni mbalimbali
wanahudhuria Tamasha la Filamu la Kimataifa la Zanzibar (ZIFF) ambalo
huwakutanisha wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi
zaidi katika eneo la Darajani lenye mkusanyiko
mkubwa wa watu pamoja na kuweka
vizuizi katika baadhi ya barabara zinazotoka vijijini kuingia mjini.
No comments:
Post a Comment