PINDA KUSHIRIKI MKUTANO WA MASHAURIANO DART


Mkutano wa mashauriano ya uwekezaji wa awamu ya kwanza ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart) unafanyika leo huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. 
Katika mkutano huo wa siku mbili , unakutanisha wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje kwenye kituo cha mikutano Mlimani City, jijini Dar es Salaam. 
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART), Asteria Mlambo, aliwaambia waandishi wa habari jana jijini kuwa mkutano huo wa mashauriano utatoa nafasi kwa wawekezaji kujua fursa mbalimbali za uwekezaji zitakazopatikana kwenye mradi huo unaojengwa kwa mabilioni ya pesa. 
“Washiriki wote kwenye mkutano wa majadiliano watapata fursa ya kutembelea eneo la mradi na watapata nafasi ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wake kuhusu mradi,” alisema Mlambo. 
Akifafanua zaidi, Mtendaji huyo Mkuu alisema   benki  na taasisi mbalimbali za kifedha, kampuni za kutengeneza mabasi, kampuni za mawasiliano, mifuko ya kijamii na mengineyo mengi yamealikwa kwenye mkutano huo. 
“Mada mbalimbali kuhusu mradi zitatolewa ambapo Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini atawasilisha mada kuhusu mradi wa DART,” alisisitiza. 
Hivi karibuni, Wakala huo uliandaa mkutano ambao ulikutanisha wamiliki wote wa daladala jijini Dar es Salaam pamoja na Kampuni ya Usafirishaji Dar es Salaam (UDA) na wadau wengine  kuwafahamisha na kushauriana ni jinsi gani wataweza kunufaika na mfumo mpya wa usafiri jijini Dar es Salaam. 
Aprili mwaka huu, wakala wa DART ulikamilisha kusajili mabasi ya daladala yanayopita katika barabara ya Morogoro au kukatiza katika njia hiyo. 
Hatua hiyo ya kuandikisha mabasi hayo ilikuwa moja ya matayarisho ya kupisha mradi huo wa mabasi yaendayo haraka. 
Kwa sasa wakala yuko kwenye mchakato wa kuwezesha upatikanaji wa watoa huduma kwenye mfumo mpya wa mabasi yaendayo haraka awamu ya kwanza ambayo inajumuisha barabara ya Morogoro, Kawawa na mtaa wa Msimbazi kwa njia kuu na nyingine za kiungo. 
Kulingana na mpango wa uendeshaji wa mfumo wa DART, barabara zinazohusika zitapaswa kutumiwa na mabasi ya mfumo huo pekee.  Jumla ya njia 64 jijini Dar es Salaam zitakoma kutumika kutokana na kuanza kwa mradi huo.

No comments: