TAZARA YATAKIWA KULIPA FIDIA KWA KUSTAAFISHA KABLA YA UMRI


Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeiamuru Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) iwalipe fidia wafanyakazi 270 kwa kuwastaafisha kwa lazima kabla ya umri halali wa kustaafu. 
Wafanyakazi hao walikuwa wanadai uamuzi wa Tazara kuwalazimisha kustaafu kwa umri wa miaka 55 badala ya miaka 60 ulio lazima kisheria ni kinyume cha sheria. 
Katika uamuzi wa rufaa hiyo uliotolewa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Agustine Mwarija, wameamuru Tazara iwalipe wafanyakazi hao mishahara ya miaka miwili kila mmoja kama fidia ya kuwakosesha kipato kwa kuwastaafisha kabla ya wakati. 
Pia, iwalipe fidia kwa kutokuwasilisha michango yao waliyokuwa wakikatwa kila mwezi katika mifuko ya hifadhi za jamii iliyokuwa ikiwahudumia. 
Katika uamuzi wao jopo la majaji hao likinukuu Waraka wa Hazina namba moja wa mwaka 2000, umri wa kustaafu kwa lazima kwa watumishi wote wa umma ikiwemo wafanyakazi wa Tazara ni miaka 60. 
Jopo lilidai kuwa marekebisho ya Sheria ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ya mwaka 2000, umri wa kustaafu kwa lazima uliongezeka kutoka miaka 55 hadi 60 na kwamba mabadiliko hayo hayo yanaigusa Tazara pia. 
Kati ya mwaka 2000 na 2005 Tazara iliwastaafisha kwa lazima wafanyakazi hao 270 baada ya kutimiza miaka 55 ikidai ni umri wa kustaafu kwa lazima kwa mujibu wa kanuni zake za mwaka 1968 zilizoboreshwa mwaka 1999. 
Hata hivyo wafanyakazi hao walipinga wakidai kuwa kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria ya NSSF na Waraka wa Hazina, walitakiwa kustaafu kwa lazima walipofikisha miaka 60. 
Walifungua kesi katika Mahakama ya Kazi wakipinga uamuzi huo, wakitaka warejeshwe kazini. Pia wakilalamikia kitendo cha Tazara kutowasilisha michango yao katika mifuko ya hifadhi za jamii tangu mwaka 1994 hadi walipostaafishwa. Mahakama hiyo ilitoa ushindi kwa Tazara kuwa walistaafishwa kihalali. 
Wastaafu hao hawakuridhika na uamuzi huo, na kukata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupinga uamuzi huo ndipo jopo hilo lilikubali hoja zao na kuamuru Tazara iwalipe fidia.

No comments: