NBAA WAZINDUA MITAALA MIPYA YA MASOMO


Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu za Serikali (NBAA) imezindua mitaala  mipya ya masomo na imetakiwa kutoa elimu inayokidhi viwango na kumuwezesha mhitimu kufanya kazi mahali popote duniani. 
Akizindua mitaala hiyo jijini Dar es Salaam, jana, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi, Geogre Yembesi aliitaka bodi hiyo kuhakikisha inafanya kazi ya ziada kuiuza taaluma ya uhasibu ya Tanzania (CPA) nje ya mipaka ya nchi kutangaza elimu hiyo inayotolewa nchini. 
“Tuhakikishe kwamba “CPA” ya Tanzania inatambulika kwa mataifa mengine hasa yale yaliyoko kwenye Shirikisho la Wahasibu Duniani (IFAC) ikizingatiwa kuwa hivi sasa dunia imekuwa kama kijiji,” alisema Yembesi. 
Aidha alisema NBAA pia inatakiwa ianze kutahini kwa mitihani ya nje ya nchi kama zinavyofanya taasisi nyingine za kihasibu duniani. Alisema matumaini ni kuwa bodi hiyo itaendelea kuandaa mazingira kwa lengo la kuhakikisha kuwa mitaala hiyo mipya inaanza na kutekelezwa katika viwango vinavyotakiwa. 
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA aliyemaliza muda wake Profesa Mussa Assad alisema kutokana na sheria ndogo za mitihani na mafunzo, mitaala ya NBAA inapaswa kupitiwa na kurekebishwa kila baada ya miaka mitano.

No comments: