DPP AIOMBA MAHAKAMA KUU ITUPE OMBI LA SHEHE PONDA


Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ameiomba Mahakama Kuu  Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali ombi la Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Shekhe  Issa Ponda kusimamisha kesi ya uchochezi inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro. 
Katika pingamizi la DPP alilowasilisha kupitia kwa Mawakili Waandamizi  wa Serikali,  Bernad Kongora na Peter Njike. DPP ameiomba mahakama hiyo kutupilia mbali ombi hilo kwa kuwa linapoteza muda wa Mahakama.
Ponda  kupitia Wakili wake Juma Nassoro aliwasilisha ombi lililopangwa kusikilizwa na Jaji Lawrance Kaduri akiomba  Mahakama hiyo itoe amri ya kuzuia kesi ya uchochezi inayomkabili  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
Aliomba kesi hiyo isimame hadi rufaa  aliyoikata mahakamani hapo kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyotolewa Mei 9 mwaka jana ambayo ilimtia hatiani kwa kosa Moja la kuingia kwa jinai  katika kiwanja cha Chang'ombe Makrasi na kuhukumiwa kifungo cha  mwaka mmoja nje. 
Hata hivyo DPP aliomba Mahakama hiyo itupilie mbali ombi hilo kwa kuwa linapoteza muda wa Mahakama pia  Ponda alishawahi kuwasilisha ombi la aina hiyo na Mahakama hiyo ilitupilia mbali. 
Jaji Kaduri aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 16 mwaka huu, kwa ajili ya kuanza kusikiliza pingamizi hilo lililowasilishwa na DPP.

No comments: