ALOE VERA NI SALAMA KWA UTENGENEZAJI VIPODOZI


Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamiii imesema matumizi  ya mmea wa Aloe Vera ni salama katika utengenezaji wa vipodozi. 
Kutokana na hali hiyo, ndio maana Mamlaka ya Chakula, Dawa  na Vipodozi (TFDA) hadi sasa imeshasajili na kuruhusu kuwepo sokoni bidhaa za vipodozi vyenye viambato vya mmea wa Aloe Vera. 
Vipodozi hivyo vilivyosajiliwa na TFDA ni 70, zikiwemo sabuni, dawa za meno, mafuta ya kujipaka, mafuta ya kuoshea nywele na vipodozi vya kupaka usoni. 
Naibu Waziri wa Afya, Dk Kebwe Stephen Kebwe alisema  hayo wakati akijibu swali la Waride Bakari Jabu wa Kiembe Samaki (CCM). 
Alisema hakuna  tafiti zilizofanyika duniani kuhusu matumizi ya mmea wa Aloe Vera, ila ulikuwa ukitumika kwa matumizi mbalimbali na Wamisri wa Kale miaka 2000 iliyopita na kuonesha manufaa makubwa katika matumizi hayo. 
Akifafanua, alisema Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia TFDA, imefanya tathmini mbalimbali kuhusu matumizi ya mmea huo, kutumika kama mojawapo ya kiambato salama katika bidhaa za vipodozi. 
“Hii hufanyika katika kipindi cha usajili ambapo viambato vyote vilivyoorodheshwa katika kila kipodozi hufanyiwa tathmini ya kina kuona kama matumizi yaliyotajwa na mtengezaji ni sahihi, kwa aina ya kipodozi anachotarajia kukiweka sokoni, ikiwemo viambato vyake” alisema. 
Naibu Waziri alisema mmea wa Aloe Vera una viambato takribani 126 na viambato hivyo vina manufaa mengi katika mwili wa binadamu, ambapo vikitumika katika vipodozi, husaidia kulainisha, kung’arisha ngozi na kuondoa mpauko wa ngozi na pia kuikinga na mionzi ya jua. Hutumika pia kurutubisha nywele na kuzifanya ziwe imara na kulinda kinywa na meno inapotumika kwenye dawa za meno. 
Katika swali lake, Jabu alisema “Katika miaka ya karibuni bidhaa zinatozokana na mmea wa Aloe Vera zimezagaa katika maeneo mengi hapa nchini na hutumika kutengenezea sabuni, mafuta ya kujipaka n.k. Je Serikali imeshafanya utafiti kuhusu matumizi ya mmea huo?”

No comments: