HATARI! MACHINJIO 20 TU YALIYOSAJILIWA KATI YA 900


Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imesema kati ya machinjio zaidi ya 900 yaliopo nchini, ni 20 pekee yamesajiliwa jambo linalochangia huduma mbovu isiyozingatia viwango vinavyotakiwa. 
Imesema ilitoa agizo la maboresho zaidi ya miaka mitatu iliyopita na sasa inaandaa mikakati kuleta mapinduzi katika sekta ya nyama hasa machinjio ili kuboresha huduma, afya ya jamii na kuhakikisha sheria na miongozo inazingatiwa. 
Hayo yalisemwa jana, jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa TFDA, Raymond Wigenge alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua semina ya siku mbili kwa wajasiriamali wadogo wa vyakula kutoka mikoa mbalimbali nchini. 
Wigenge aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu katika ufunguzi wa semina hiyo, alisema TFDA inatambua changamoto zinazoikabili sekta ya nyama, ikiwemo uchafu na miundombinu duni katika machinjio na imejiandaa kuweka mikakati mipya kupambana na hali hiyo. 
“Serikali haijakaa kimya, sasa tunaandaa mikakati mipya kuangalia kwa undani sekta ya nyama hasa machinjio, miaka mitatu iliyopita tuliagiza pia mabucha yote wawe na misumeno ya umeme, lakini kuna sehemu nyingine hakuna umeme wanapaswa kutafuta ya plastiki, mambo haya ni changamoto bado,” alisema Wigenge. 
Alisema nchini kuna zaidi ya machinjio 900 lakini ni takribani 20 pekee yamesajiliwa. Pia alisema wanashirikiana na halmashauri kuboresha usafi katika masoko na alisisitiza kuwa bidhaa zozote za chakula hazipaswi kuwekwa chini wakati zikiuzwa ni hatari kwa afya. 
Kuhusu mafunzo hayo, alisema TFDA kwa kushirikiana na taasisi ya sekta binafsi ya TPSF imeandaa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo 80 kutoka mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kujifunza kanuni, sheria na miongozo ya uandaaji na usindikaji wa vyakula kuboresha kipato na afya za walaji. 
Naye  Mkurugenzi wa Bodi ya TPSF akiwakilisha wanawake, Anna Matinde alisema fursa hiyo imetokana na utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete kwamba wajasiriamali wadogo wapatiwe vyeti vya usindikaji vya TFDA na Shirika la Viwango (TBS) hivyo kabla ya kupewa vyeti lazima wafahamu na kufuata sheria.

No comments: