Tukio
la mtoto Nasra Mvungi kuteswa kwa kufungiwa katika boksi ndani ya nyumba kwa
zaidi ya miaka mitatu na kufariki dunia baada ya kuokolewa na wasamaria,
limefanikisha kupatikana kwa mtoto mwingine mwenye matatizo ya kiafya ambaye
licha ya kuzaliwa miaka 18 iliyopita, inaelezwa hajawahi kulia, kuongea, kukaa
wala kutembea.
Mtoto
huyo mwenye mwonekano kama wa mtoto mwenye umri wa miaka mitano, amepatikana
baada ya wasamaria kutoa taarifa Dawati
la Jinsia katika Jeshi la Polisi wilayani hapa, wakiarifu kuwapo kwa mtoto
mlemavu anayenyanyaswa kama ilivyokuwa kwa mtoto Nasra `Mtoto wa Boksi’.
Katibu
wa Dawati la Jinsia, Koplo Janeth Maeda amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo,
akisema walipokea taarifa za kuwapo kwa mtoto anayenyanyaswa, hivyo kukimbilia
eneo la tukio ili kumwokoa mtoto aliyedaiwa kuwapo katika mateso ikiwa pamoja
na kunyimwa huduma muhimu.
Hata
hivyo, anasema walichokishuhudia si mateso, bali ni hali duni ya kimaisha ya
wazazi wake, hivyo kulilazimu Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ustawi wa
Jamii kumwokoa kwa kumkimbiza hospitali kwa uchunguzi zaidi wa afya yake.
Anasema:
“Kwa kweli tulipopata taarifa hizo tulishtuka sana tukaamua kuwasha gari na
kuelekea eneo la Lukobe ambako ndiko tuliambiwa kuwa kuna mtoto huyo na kumkuta
mtoto huyo, lakini tofauti na tulivyoambiwa, tulimkuta akiwa katika mazingira
mazuri.
"Labda
kilichoonekana kwa wengine kama ni mateso ni kwa sababu wazazi wake kutokuwa na
uwezo wa kumudu matibabu tumeamua kusaidiana na ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa
kumsaidia mtoto huyo kwa kuhakikisha anapatiwa huduma ya matibabu
anayostahili.”
Kwa mujibu wa wazazi wa mtoto huyo wa
kike aitwaye Farida, baba Abdallah Kipingu na mkewe, Mwajuma Abdallah, wakazi
wa Lukobe katika Manispaa ya Morogoro, binti yao huyo alizaliwa mwaka 1996 na
kwamba tangu azaliwe hajawahi kulia.
Mama wa mtoto, Mwajuma akiwa sambamba
na mumewe alisema walimzaa Farida huko Muheza mkoani Tanga na kwamba walimzalia
nyumbani, lakini kutokana na kushindwa kulia, wiki moja baadaye walikwenda
Hospitali ya Wilaya ya Muheza ili kujua kilichomsibu mtoto wao.
“Hatukupata msaada, tukaendelea kumlea
alipofikisha miezi minne ambao mara nyingi ni muda wa kukaa, tulijaribisha
kumkalisha, lakini hakukaa hivyo kwa mara nyingine tukaenda hospitali, safari
hii ya Mkoa wa Morogoro ambako tumekuwa tunaishi, tukaambiwa mtoto ahudhurie
mazoezi ya viungo.
“Tulihudhuria mazoezi kwa muda mrefu
hatukuona mabadiliko baadaye tukaamua kuhamia kwenye kituo cha kulea watoto
walemavu cha Amani Center, tukaambiwa tuendelee ingawa hakukuwa na mabadiliko,
tulipohamia Lukobe mwaka jana hatukuweza tena kumpeleka kwenye mazoezi kutokana
na kukosa uwezo wa kifedha za kufanya mizunguko,” anasema.
Anasema wamekuwa wakiendesha maisha kwa
kutegemea biashara ya bidhaa ndogondogo katika genge lao, msimamizi mkuu akiwa
mumewe na kwamba yeye huhangaika zaidi na mtoto.
“Hayo ndiyo yamekuwa maisha yetu hadi
kufikia wakati huu tulipopata msaada wa Polisi na Ustawi wa Jamii,” anasema
mama huyo aliyeiomba jamii kuwaombea na kuwapa msaada wa hali na mali katika
kufanikisha matibabu na malezi ya binti yao ambaye kwa sasa amefikishwa katika
Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa uchunguzi zaidi.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa
Morogoro, Oswin Ngungamtitu aliwashukuru wananchi kwa kuitikia mwito wa kutoa
taarifa za matukio kama ya mtoto Nasra, kwani imewafanya wafumbue macho na
kutoa taarifa mbalimbali.
Alisema taarifa zao zinaweza kuwa
faraja kwa watoto na wazazi wengi wasiojua cha kufanya baada ya kuelemewa na
majukumu ya kutunza watoto wenye uhitaji maalumu.
Hata
hivyo, aliitaka jamii kuwapeleka watoto wenye ulemavu na wenye matatizo katika
sehemu zinazohusika ili watoto hao waweze kupatiwa msaada na hatimaye kuweza
kuimarisha afya zao.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi, Mganga Mkuu Mfawidhi, Dk Rita Lyamuya alisema
baada ya kupata taarifa hizo taratibu za kumfanyia uchunguzi zinaendelea ikiwa
ni pamoja na kumpatia virutubisho.
No comments:
Post a Comment