KIKONGWE WA MIAKA 97 ASAKA MTOTO WA NDOA

Babu aliyefunga ndoa mwaka 2011 akiwa na umri wa miaka 94, Mathias Kisokota mkazi wa Kitongoji  cha Isunta, Namanyere  wilayani Nkasi  ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 97, amehamia na mkewe katika Mji wa Mpulungu  mwambao wa Ziwa Tanganyika  nchi jirani  ya Zambia  miezi  sita iliyopita kwa lengo la kufanya tambiko la kumwezesha mkewe mwenye umri wa miaka 83 kupata mtoto wa uzeeni.
Mke  wa  mzee huyo, Uria Mwamanzi ni  mwenyeji  wa nchi jirani  ya Zambia alizaliwa na  kukulia  katika  Mji  wa Mpulungu  mwambao  mwa Ziwa Tanganyika  ambapo  kwa mujibu  wa  wajukuu zao  ndiko  babu yao  alipokutana  naye  na kuwa  na  mahusiano  hadi  walipofunga  ndoa  miaka mitatu  iliyopita.
Wanandoa hao ambao waliacha gumzo kubwa baada ya kufunga pingu za maisha katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Anthony, alasiri ya Juni 18, 2011 mjini Namanyere Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi.
Akizungumza na  mwandishi  wa  habari  kwa njia ya simu  kutoka  katika Mji  wa Namanyere  jana, Salvatory Adolf (19), mjukuu  wa wazee hao kutoka kwa mtoto wao kitindamimba mwenye umri wa miaka 40 sasa, alisema babu yake  amemsindikiza mkewe  huyo  ili kwenda kutambikia  mizimu  ya kwao.
“Bibi  hakuwa  na  raha  mara kwa mara alikuwa  akitamani  kurudi  nchini  kwao  Zambia  kuwasalimia nduguze  pia akiwa  huku alikuwa  akiugua  mara kwa  mara  hivyo  babu aliona  bora  amsindikize  bibi  akatambike  kwa mizimu  ya babu  zake  nchini  humo,” alisema.
Hata hivyo, hakutaka kueleza kwa undani juu ya kiu ya babu yake ya kutaka kupata mtoto, habari ambazo zinazungumzwa na watu wa karibu waliopo ndani ya  familia ya wanandoa  hao.
Miongoni mwao, Agnes ambaye ni mtoto wa mwisho wa Mzee Kisokota akizungumza na mwandishi  wa habari  hizi  kwa njia ya simu  kutoka  mjini Namanyere, Nkasi alisema baba  yake  amekuwa  na hamu  hadi  sasa  ya  kupata mtoto katika ndoa yake changa.“Anasali  sana  akiomba  kila  siku apate mtoto katika ndoa yake. Bado  ana matumaini makubwa ….. nikianza kukusimulia  tutakesha, tena  anasema  siku akijaliwa  mtoto  katika  ndoa yake  hiyo  atajawa  na  furaha   kubwa na kufanya sherehe ya aina yake… amemsindikiza  bibi (mkewe) Zambia  kusalimia  ndugu zake  pia kutambika  kwa  kuwa  baba  ana hamu  ya mtoto  atatumia  fursa hii  nae kutambikia  kwa  wakwe  zake  ili  mkewe  huyo  ashike  mimba,“ alieleza Agnes.
Hali hiyo inakuja licha ya ukweli kwamba, umri wa mke wa Mzee Kisokoto kuzaa umeshapitiliza, lakini kwa pamoja wamedaiwa kuamini kwa Mungu hakuna kisichowezekana hivyo anaweza kutenda miujiza kwa kuwapa baraka ya mtoto wa ndoa yao ya uzeeni.
Mjukuu  huyo alipoulizwa juu ya ziara hiyo kuhusisha pia kusaka mtoto kutoka kwa `mizimu’ ya ukoo  wa mke wa babu yake, hakuwa na majibu ya moja  kwa moja.
“Bibi  alipoondoka  alikuwa  akisumbuliwa  na  maumivu ya mwili  lakini  tangu  atambike  nchini Zambia  inadaiwa amepona kabisa  na  sasa  wanaishi  raha mustarehe  na  babu… ila  watarudi  huku  kwetu baadae mwaka  huu …”,  alisema.
Katika safari ya wazee hao, Adolf anasema bibi na babu yake walisindikizwa na Claudio Mathias (21), kaka wa mjukuu huyo na kwamba kaka huyo amesharejea nchini.
Wanandoa  hao  kwa mujibu  wa  wajukuu  zao  kabla ya kufunga  ndoa katika Kanisa Katoliki  Jimbo  la Sumbawanga  mjini Namanyere  miaka  mitatu iliyopita  walikuwa  wakiishi  ‘kinyumba’  kila mmoja wao  akibahatika  kuwa  na  watoto katika mahusiano yake ya awali.
Kwa pamoja  wana wajukuu zaidi  ya  30 na  vitukuu zaidi ya 40 wengi wao  wakiishi  nchi jirani ya Zambia.  Mzee Kisokoto alifiwa na mke wa kwanza zaidi ya miaka 39 iliyopita.

No comments: