BREAKING NEWS!! GWIJI WA VICHEKESHO MZEE SMALL AFARIKI DUNIA

Habari zilizotufikia muda mfupi uliopita zinasema kwamba, msanii mkongwe wa vichekesho nchini Said Ngamba, maarufu kama Mzee Small amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, Mzee Small alikuwa amelazwa hospitalini hapo kwa wiki kadhaa akipatiwa matibabu kufuatia kuzorota kwa afya yake katika siku za hivi karibuni.
Kabla ya kulazwa hospitalini, miezi kadhaa iliyopita Mzee Small alipatwa na maradhi ya kupooza (Stroke) hali iliyosababisha kusitisha shughuli zake zote za sanaa ya uigizaji pamoja na matangazo ya biashara kadhaa aliyokuwa ameingia na makampuni mbalimbali.
Mzee Small atakumbukwa mno kwa mchango wake mkubwa katika sanaa za maonesho kutokana na umahiri wake mkubwa wa kumiliki jukwaa ambapo aliwika sana wakati akiigiza na wasanii kama Chausiku Salum 'Bi Chau', Branco wa Chitosa na wengineo.
Mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwa marehemu Tabata Mawenzi, jijini Dar es Salaam. Taarifa zaidi zitawajia hapahapa baadaye.
Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi, Amina.

No comments: