DAR WAELEZEA KILIO CHA ENEO LA KUFANYIA BIASHARA



Baadhi ya wafanyabiashara ndogo wa Dar es Salaam ambao wamegoma kuondoka katika maeneo yasiyoruhusiwa, wamesema suluhisho pekee ni wao kutafutiwa maeneo mazuri ya kufanyia shughuli zao.
Wafanyabiashara hao ambao awali waliondolewa kufanya biashara zao katika maeneo yasiyoruhusiwa na askari waliokuwa wakisafisha jiji, wameonekana kurudi katika maeneo hayo na kuendelea na shughuli zao.
Wakizungumza na mwandishi, baadhi yao wamedai kuwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafanyabiashara ni machache hivyo yanachukua wafanyabiashara wachache, jambo linalowafanya wao waendelee kutafuta riziki katika maeneo hayo.
Mfanyabiashara Said Kudra anayefanya shughuli zake katika eneo la Ilala alisema, kitendo cha wao kuondolewa katika maeneo ya shughuli zao bila kuoneshwa maeneo yanayoruhusiwa si sahihi.
 "Unajua ndugu mwandishi nikuhakikishie tu, kwamba hakuna mtu anayependa usumbufu wa aina hii wa kufukuzwa na kurudi, lakini hii inatokea kwa sababu tunafukuzwa lakini hakuna maeneo tunayoelekezwa twende," alisema Kudra.
Alisema hata inapotokea wanaelekezwa maeneo ya kwenda, tayari maeneo hayo yanakuwa yameshajaa na hayana nafasi jambo linalowalazimu wao kurudi walipoondolewa.
Naye Ester Julius wa Buguruni alisema kwa kiasi kikubwa baadhi yao wamekuwa wakitegemea maeneo hayo kupata riziki, hivyo serikali ione umuhimu wa kuongeza maeneo zaidi ambayo wanaweza kufanya biashara zao.
Aidha, mfanyabiashara mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mama Dora wa Kinondoni Mkwajuni alisema, kikubwa ni serikali iweze kuangalia namna ya kuwasaidia badala ya kuwatimua maeneo hayo na kusababisha mitaji yao kupotea.
Alisema baadhi yao wako tayari kuondoka katika maeneo hayo endapo wataelekezwa maeneo sahihi ya kufanyia biashara zao.
Ofisa habari wa Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba alisema manispaa hiyo inatarajia kujenga soko jipya la kisasa na lenye hadhi ya wilaya  ambalo litatumiwa na wafanyabiashara ndogo.
"Hii iko kwenye mpango wa DMDP (Dar es Salaam Metropolitan Development Project) na tayari utafiti wa awali umeshafanyika na kuangalia linaweza kuchukua watu wa ngapi na ubora wake kwa ujumla," alisema Joyce.
Aidha kwa Manispaa ya Kinondoni, wafanyabiashara hao walishatangaziwa masoko wanayotakiwa kwenda kufanya biashara zao. Aidha Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala tabu Shaibu, mapema mwaka huu alisema manispaa hiyo imebaini kuwa wafanyabiashara 21,500 hawana maeneo ya kufanyia biashara jambo linalosababisha wavamie hifadhi za barabara.
Alisema manispaa hiyo imerenga Sh milioni 240 kwa ajili ya ujenzi wa mabanda ya masoko ili wafanyabiashara hao waweze kupata sehemu za kufanyia shughuli zao.

No comments: