KALAMBO YATUMIA SHILINGI MILIONI 8.5 KUKABILI UKIMWI


Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kalambo Mkoa wa Rukwa kupitia kitengo cha Ukimwi, imetumia Sh milioni 8.5 kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo. 
Fedha hizo zimetumika kununulia wanafunzi yatima wanaoishi katika mazingira magumu sare za shule, viatu pamoja vifaa vya kujifunzia ikiwemo madaftari na kalamu.  Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Godfrey Sichona alikabidhi vifaa hivyo kwa walengwa kwa niaba ya Halmashauri. 
Halmashauri hiyo pia imenunua vifaa vya muziki kwa ajili ya vikundi viwili vya Sayuni kilichopo kata ya Legezamwendo na Sayuni cha Kata ya Mambwenkoswe vihamasishe wananchi kujikinga na ugonjwa huo. 
Baadhi ya vifaa vya muziki vilivyotolewa na Halmashauri hiyo ya Kalambo ni gitaa tatu kwa  kila kikundi, spika, maikrofoni, jenereta pamoja na vifaa vingine vya umeme. 
Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo, mwenyekiti huyo alikumbusha wakazi wa Wilaya ya Kalambo na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla kuwa, mapambano dhidi ya Ukimwi siyo ya serikali pekee bali ni jukumu la kila mwanajamii zikiwezo taasisi za dini. Katika hatua nyingine, Mkuu  Mkoa wa Ruvuma,  Said Thabit Mwambungu ametaka watalamu wa afya kushirikiana na wakunga wa jadi katika kuzuia maambukizi ya VVU na Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.  
Mwambungu alisema hayo mjini Songea kwenye uzinduzi wa kampeni ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

No comments: