ATAKA WANAVYUO KUIAMINI CCM


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewahakikishia wanavyuo kwamba changamoto zote wanazokabiliana nazo ikiwamo suala la mikopo pamoja na mazingira yasiyo rafiki kwao, vitaendelea kufanyiwa ufumbuzi na serikali. 
Katibu wa CCM Wilaya ya Dodoma Kanuti Ndaghine, alisema hayo jana kwenye hafla ya kukabidhi kadi za chama kwa wanafunzi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini ( IRDP). 
“Nawahakikishieni matatizo yote haya yatakwisha kuweni wavumilivu kwa kukiamini na kukipa nguvu chama chenu cha Mapinduzi,” alisema Ndaghine. 
Aidha aliwaambia wanachama hao wapya kwamba CCM imeanza kujipanga kwa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu na uchaguzi mkuu 2015. 
Alisema kujipanga huko ni pamoja na kuanza kutangaza sera, mafanikio na changamoto zilizopo katika kuhudumia umma na jinsi changamoto hizo zinavyoshughulikiwa na serikali ya chama hicho. 
Alitaka vijana hao kuhakikisha wanasaidia chama hicho kiendelee kutawala kwa kushinda chaguzi hizo. 
Alisema chama kina imani kubwa na vijana wa chuoni  na kwamba ni matumaini yake vijana hao wapya watatumia uelewa wao kuhakikisha CCM inashinda katika chaguzi zijazo. 
Aidha alishukuru vijana hao kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo wa kuingiza wanachama wapya na kusema hiyo ni dalili njema. 
Katibu huyo ambaye alifanya kazi hiyo kwa niaba ya Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete aliyealikwa kwa ajili ya kuzindua tawi na kugawa kadi, alisema CCM ni jamii isiyobaguana na imejijenga katika kusaidiana bila ubaguzi kwa ajili ya kujenga taifa imara lenye mshikamano. 
Mwenyekiti wa tawi hilo, Hamisi Mpola alitaka wanachama wenzake na wapenzi wa chama kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika shughuli za chama katika ngazi zote.

No comments: