Uongozi wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Lindi, umempongeza Mjumbe wa Halmashauri Kuu
ya Taifa (MNEC) anayewakilisha wilaya ya Lindi Mjini, Mama Salma Kikwete
kutokana na kazi nzuri anazofanya katika kutimiza majukumu yake.
Pongezi hizo
zilitolewa kwa mara ya kwanza na Katibu wa CCM wa Mkoa wa Lindi, Adelina Geffi
alipokuwa akisoma taarifa ya kazi, uhai na Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya
Chama hicho kinachotawala ya mwaka 2010/2015 kwa Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya
ya Wazazi, Abdallah Bulembo aliyekuwa katika ziara ya siku sita mkoani hapa.
Katika taarifa
yake hiyo, Geffi alisema kuwa Mama Salma amenunua gari la kubeba wagonjwa na
kulikabidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo kama mchango wake binafsi kwa ajili
ya huduma hiyo muhimu kwa sekta ya afya.
Mbali na gari
hilo la kubeba wagonjwa ambao ni pamoja na akina mama wenzake wakiwemo
wajawazito, Geffi pia alitaja misaada mingine iliyotolewa na Mama Salma kuwa ni
baiskeli 84 alizonunulia matawi yote 84 ya CCM ya wilaya hiyo anayoiwakilisha
katika vikao vya NEC.
Bulembo
alipokuwa mjini Lindi hapo juzi, jina la Mama Salma lilishangiliwa kwa nderemo
na vifijo na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya hiyo waliokuwa kwenye
kikao chao cha ndani baada ya kutamkwa na Bulembo aliyekuwa mgeni rasmi.
Kutokana na
hali hiyo, Bulembo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM alisema
anampongeza MNEC huyo kwa kutimiza vizuri majukumu yake ya Utekelezaji wa Ilani
ya Uchaguzi ya Mwaka 2010/2015, lakini pia kwa kukifanyia kazi kubwa chama
hicho licha ya kutingwa na shughuli nyingi za kitaifa na kimataifa.
No comments:
Post a Comment