BOSI WA UN ASIFU JITIHADA ZA KIKWETE SEKTA YA AFYA



Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon amesifu jitihada za Rais Jakaya Kikwete na mchango wake mkubwa katika kupigania Afya ya Mama na Mtoto.
Alitoa pongezi hizo juzi wakati alipokuwa akizungumzia juhudi za kumwokoa Mama na Mtoto baada ya Mwaka 2015, mwishoni mwa mkutano wa siku 3 kuhusu Afya ya Mama na Mtoto kama ilivyoainishwa katika Malengo ya Milenia.
Rais Kikwete na Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Harper, kwa  miaka minne  wamekuwa Wenyeviti Wenza wa Kamisheni ya Habari na Uwajibikaji katika masuala ya Afya ya Mama na Mtoto, ambayo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha vifo vya watoto wachanga na mama wajawazito vinapunguzwa  kwa nusu ifikapo mwaka 2015.
"Napenda kumpongeza Rais Kikwete kwa mchango wake mkubwa katika jitihada hizi za kupunguza vifo vya watoto na akina mama. Rais Kikwete na Waziri Harper wamedhihirisha uongozi katika kukuza Afya ya Mama na Mtoto, nawapongeza sana," alisema na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano wa Canada wa kuchangia zaidi katika jitihada hizo.
Pamoja na mafanikio hayo, Rais Kikwete amesema bado jitihada zinahitajika katika kuhakikisha mafanikio haya yanaimarishwa zaidi na kwamba hayapotei.
“Bado tunahitaji wataalamu wa afya wenye ujuzi, vifaa na teknolojia ya kisasa." Amesema na kuongeza kuwa bado zinahitajika juhudi za pamoja katika kusimamia mafanikio yaliyokwisha kupatikana.
Katibu Mkuu huyo wa UN amesema afya ya mama na mtoto ni ajenda muhimu kupigania hata baada ya mwaka 2015 kwani ni muhimu kwa maendeleo.
Rais Kikwete pia alihudhuria chakula cha jioni kilichoandaliwa na wafanya biashara wa Canada na Tanzania ambapo ameelezea umuhimu wa biashara na uwekezaji nchini kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa Tanzania.
Alisema Tanzania inahitaji vitega uchumi zaidi kutoka Canada na hivyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Canada kuja kuwekeza Tanzania.
Rais Kikwete alitarajiwa kuondoka Toronto jana kurejea Dar es Salaam, kupitia Marekani.

No comments: