MAALIM SEIF AKARIBISHA WASHINDANI UCHAGUZI WA CUF



Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amerejesha fomu ya kugombea tena nafasi ya Katibu Mkuu wa chama hicho, na kusisitiza msimamo wake wa kuendelea kuwaunganisha Wazanzibari.
Aidha, amewataka wanachama wengine wenye `ubavu’ wa kuchuana naye katika nafasi hiyo wajitokeze, akisema nafasi anayowania haina mwenyewe, licha ya kuwa ameishikilia kwa muda mrefu, tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwanzoni mwaka 1992.
Akikabidhi fomu yake kwa Katibu wa CUF Wilaya ya Magharibi Unguja, Juma Rajab, Maalim Seif alesema suala la ubaguzi kamwe halitopewa nafasi ndani ya chama hicho.
Aliongeza kuwa, Wazanzibari wote ni wamoja bila ya kujali asili ya mtu anapotokea ndani ya visiwa vya Zanzibar, na kuhimiza umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amerejesha fomu hiyo baada ya kuamua kuingia tena kwenye kinyang’anyiro hicho na kuchukua fomu Ijumaa iliyopita, ambapo alisindikizwa na viongozi wa CUF na wafuasi kadhaa wa chama hicho.

No comments: