MADEREVA WATISHIA KULIPUA MALORI YA MAFUTA


Madereva wa malori  matano yenye shehena za  mafuta yaliyokuwa yakisafirishwa na Kampuni ya Hash Enegy  wamegoma na kutishia kulipua malori hayo na kufunga kizuizi cha Kituo cha Forodha Sirari  wilayani Tarime mkoani  Mara,  kwa madai ya kukwamishwa kwenye kituo hicho kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa. 
Malori hayo ya mafuta yaliyotakiwa kupelekwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yanadaiwa kushindwa kutimiza masharti na kuingiza mafuta na kuyauza nchini kinyemela kwa lengo la kukwepa kodi badala ya DRC. 
Kutokana na kubainika kukiuka masharti hayo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliagiza kurejeshwa Kenya malori hayo ili kufuata taratibu na sheria za kuingia mafuta nchini. 
Malori hayo yana namba  KBR 298 B tela namba ZD 6490; KBP 410 B tela namba ZE 8714; KBP 951 E tela namba ZC 4423; KBK 180 D tela namba ZC 4731 na lori lenye namba KBR 301 B lenye tela namba ZD 8170 yote aina ya Scania. 
Akizungumza na mwandishi katika kituo hicho cha Forodha Sirari  wakati malori hayo yalipofunga kituo hicho kwa saa nne, Meneja wa Kituo cha Forodha  TRA Sirari, Ben Usaje alisema: "Hawa madereva wa malori, tumewaomba waweke dhamana ya fedha taslimu endapo watafikisha mafuta hayo Kongo bila ya kupungua na kukaguliwa huko na maofisa wetu wa DRC na kupewa barua za ukaguzi huko tunawarejeshea fedha zao walizoweka dhamana, lakini wameshindwa masharti ya kuweka dhamana na ndipo wanafunga kizuizi na kuleta vurugu katika maeneo ya forodha".

No comments: