BREAKING NEWS!! GEORGE TYSON AFARIKI DUNIA KWA AJALI YA GARI



Mwongozaji filamu wa siku nyingi nchini na Prodyuza wa kipindi cha runinga cha The Mboni Show, George Tyson (39) amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea jana jioni wakati yeye na wenzake wengine saba wakitokea mjini Dodoma kikazi.
 Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, SACP David Misime, ajali hiyo ilitokea kwenye Kijiji cha Silwa, katika Barabara ya Dodoma – Morogoro majira ya Saa 12:45 jioni ambapo chanzo cha ajali hiyo kwa mujibu wa Kamanda huyo ni mwendo kazi wa gari hilo.
Marehemu Tyson na wenzake walikuwa wakisafiri kwenye gari namba T150 CWA aina ya Toyota Granvia Station Wagon kutoka Dodoma walikokwenda kwa ajili ya shughuli ya kukabidhi madawati kwa shule ya Msingi Chaula ya mjini Dodoma.

Gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Mgeni Shemakame (29) mkazi wa Mburahati, Dar es Salaam ambaye amejeruhiwa, lilipata ajali hiyo iliyokatisha maisha ya Tyson ikiwa ni masaa manne tu tangu waanze safari ya kurejea jijini Dar es Salaam.
Marehemu George Tyson alitamba sana kwenye ulimwengu wa filamu akiwa na kikundi cha Mambo Hayo ambapo alishiriki kikamilifu kwenye uaandaji wa michezo ya kuigiza ya kwenye runinga iliyokuwa ikirushwa na kituo cha televisheni cha ITV.
Marehemu aliwahi kufunga ndoa na mwigizaji maarufu wa kike nchini, Yvonne Cherry ‘Monalisa’ kabla ya kutengana miaka kadhaa iliyopita.
Baadaye, Tyson akajiunga na mwanadada Mboni Masimba katika kuandaa kipindi cha runinga cha Mboni Talk Show ambacho amekitumikia mpaka mauti yalipomfika.
Mungu ailaze roho ya marehemu George Tyson mahali pema peponi, Amina.

No comments: