KAMPUNI YA VODACOM YATENGENEZA AJIRA 400



Kampuni ya simu za mkiononi ya Vodacom imendelea na azma yake ya kuhakikisha inawafaidisha wateja wake kupitia huduma zake, huku wakitengeneza nafasi za ajira kupitia maduka yake yanayoendelea kufunguliwa nchi nzima.
Akizundua duka jipya la Vodacom jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Mauzo ya Rejareja, Upendo Richard alisema dhamira kubwa ya kusambaza maduka ya kampuni hiyo ni kusogeza na kuboresha huduma kwa wateja popote walipo lakini pia kutengeneza nafasi za ajira.
Duka hilo ambalo liko Sinza Afrika Sana ni la 18 kwa wilaya ya Kinondoni pekee na la 79 Tanzania nzima. "Ajira hizi kwa namna moja au nyinigine ni suluhu la upungufu wake nchini na pia hupunguza mzigo kwa serikali katika jitihada za kuhakikisha watu wanajiajiri wenyewe."
Alisema kwa kila duka la Vodacom linalofunguliwa, watu watano mpaka saba huajiriwa kwa nafasi mbalimbali na akasema kuwa takribani watu 400 wameajirwa katika maduka hayo kama  meneja wa duka, uhasibu, wauzaji simu, watoaji ushauri kwa wateja pamoja na wakala wa M-Pesa.
"Wateja wote wa Vodacom sasa wasipate tabu za kwenda maeneo ya mbali kutafuta huduma za kimawasiliano, badala yake watumie duka hili lililopo hapa Sinza Afrika Sana." Alisema  Richard na kuongezea, "Huduma zinazotolewa hapa ni sawa na maduka mengine ili kuweza kutimiza haja zao na kuepukana na usumbufu wa kwenda mbali."
Naye mteja wa kwanza kutumia duka hilo mara baada ya kufunguliwa rasmi, Alfred Joseph, ambaye ni mkazi wa Sinza Afrika Sana ameishukuru Vodacom kwa jitihada zao za kusogeza huduma kwa wateja na kuwapunguzia usumbufu wa kusafiri umbali mrefu.

No comments: