MHE.
PROF. JUMANNE ABDALLAH MAGHEMBE (MB.) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO
NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA MAJI
KWA MWAKA
2014/2015
1.0 UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, leo hii Bunge lako Tukufu limepokea taarifa
ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mheshimiwa Profesa Peter
Mahamudu Msolla, Mbunge wa Kilolo,
kuhusiana na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji. Naomba sasa
kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Kawaida na Maendeleo ya Wizara ya Maji kwa
mwaka 2014/2015.
2.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati hiyo kwa
kupokea na kuchambua Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2013/2014 na
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka 2014/2015. Maoni,
ushauri na maelekezo yaliyotolewa na Kamati yamezingatiwa wakati wa maandalizi ya Bajeti ya Wizara yangu.
3.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dr.
Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuongoza kwa
umahiri mkubwa hatua mbalimbali za mchakato wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba na hatimaye kuteua
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Aidha, napenda kumpongeza Rais wetu kwa kupata Tuzo
ya Heshima ya Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa zaidi katika Maendeleo Barani
Afrika kwa mwaka 2013.
4.
Mheshimiwa Spika,
vilevile nawapongeza Mhe. Samwel Sitta, Mbunge wa Urambo Mashariki kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti
wa Bunge Maalum la Katiba na Mhe. Samia Suluhu
Hassan, Mbunge wa
Makunduchi kuwa Makamu
Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wote wa Bunge hilo kwa kuteuliwa kwao kushiriki
katika mchakato wa kupata Katiba mpya. Watanzania wana matumaini makubwa ya kuwa na Katiba mpya
ambayo itakayozingatia matakwa ya kizazi cha sasa na kijacho.
5.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii, kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge
walioteuliwa kuwa Mawaziri na Manaibu Waziri ili kuziongoza
Wizara mbalimbali. Vilevile, nawapongeza Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wapya wa Kamati
mbalimbali za Kudumu za Bunge waliochaguliwa hivi karibuni. Ni
matumaini yangu kuwa tutaendelea kushirikiana nao katika kutekeleza majukumu
yetu kwa maendeleo ya Taifa letu.
6.
Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu walionitangulia katika kuwapongeza
Waheshimiwa Wabunge wapya Mhe. Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga na Mhe.
Ridhiwani Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze waliochaguliwa kujiunga na Bunge lako Tukufu. Nawatakia heri na mafanikio katika kazi yao hiyo
mpya.
7.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kuchukua fursa hii kumshukuru na kumpongeza Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb) kwa hotuba yake inayotoa mwelekeo wa utekelezaji wa kazi za Serikali. Vilevile, nawapongeza Mawaziri walionitangulia kuwasilisha hoja zao.
8.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ilipokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa, taarifa za vifo vya Waheshimiwa Wabunge wenzetu,
Marehemu William Augustao Mgimwa,
aliyekuwa Waziri wa Fedha na
Mbunge wa Kalenga na Marehemu Saidi
Bwanamdogo, aliyekuwa Mbunge wa
Chalinze. Nachukua nafasi hii
kutoa pole kwako wewe Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu, familia za marehemu,
ndugu na wananchi wa majimbo ya Kalenga na Chalinze kwa misiba hiyo mikubwa.
Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi. Amin.
9.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi,
napenda sasa kuchukua fursa hii kuwasilisha hotuba yangu ya Bajeti
yenye maeneo makuu manne (i) hali ya Sekta ya Maji
nchini; (ii) mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha
2013/2014; (iii) mpango wa bajeti kwa mwaka 2014/2015; na (iv)
shukrani kwa wadau wa Sekta ya Maji na maombi ya fedha kwa mwaka 2014/2015.
Maelezo yatakayotolewa katika maeneo yaliyoainishwa yamezingatia sera na
mikakati ya maendeleo ya kitaifa na kimataifa; sheria, kanuni na miongozo
inayohusiana na Sekta ya Maji; na mgawanyo wa kazi kisekta zinazoongoza
usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini.
2.0 HALI YA SEKTA YA MAJI NCHINI
10.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa
kuzingatia maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka
2010; Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 - 2015/2016); Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa “Tekeleza Sasa
kwa Matokeo Makubwa (Big Results Now - BRN)” na Ahadi za Serikali. Wizara inatekeleza miradi
mbalimbali katika Sekta ya Maji kulingana na Sera ya Maji ya mwaka
2002, Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Maji (2006 – 2015), Sheria na Kanuni za
Maji, na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP).
11.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha hali ya
maisha ya wananchi wake kupitia Sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Maboresho makubwa ya kimfumo na kiutendaji katika sekta zote nchini (Sector
reforms)
yanaendelea kutekelezwa. Aidha, Sekta ya Maji ni moja ya sekta sita zilizopewa
kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya “Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa”
– BRN. Awamu ya Kwanza ya Mpango huo wa miaka mitatu (2013/2014
– 2015/2016)
ni mwelekeo chanya katika kuyafikia
malengo tuliyojiwekea ya kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama,
hususan katika maeneo ya vijijini. Katika
Mpango huo jumla ya miradi 1,810 itakayogharimu kiasi cha shilingi trilioni 1.45 inatarajiwa kujengwa na itakapokamilika
wananchi wapatao milioni 15.4 zaidi watapata huduma ya maji na kufikisha idadi
ya wananchi wanaopata huduma ya majisafi na salama kufikia milioni 30.6 sawa na asilimia 74 ya wakazi wote wa vijijini. Miradi inayotekelezwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta
ya Maji imejumuishwa kwenye Mpango wa BRN ili kuharakisha utekekezaji wa miradi ya maji nchini. Naomba
nikiri kwamba tumepata hamasa kubwa katika utekelezaji wa BRN na nichukue fursa hii niwapongeze Serikali za
Mitaa kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya.
12.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza
Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ambayo ilizinduliwa mwaka 2006/2007 na
kuanza kutekelezwa mwaka 2007/2008. Programu hiyo inatekelezwa katika vipindi
vya miaka mitano mitano hadi mwaka 2025/2026 na imegawanywa katika programu
ndogo nne ambazo ni; Usimamizi na
Uendelezaji wa Rasilimali za Maji, Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira
Vijijini, Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mijini, na Kuimarisha na
Kuzijengea Uwezo Taasisi zinazotekeleza Programu ya Maji. Hadi sasa
hali halisi ya utekelezaji katika Sekta ya Maji imefikia hatua mbalimbali kama
ifuatavyo:-
2.1 RASILIMALI ZA MAJI
13.
Mheshimiwa Spika, Rasilimali tuliyonayo inatumika majumbani, kilimo cha
umwagiliaji, uzalishaji wa nishati, mifugo, uvuvi, viwanda, uchimbaji wa
madini, usafirishaji, utalii, ujenzi pamoja na maendeleo ya miji. Aidha,
Rasilimali za maji zinatumika pia
kwa ajili ya kupokea majitaka yaliyosafishwa na kufikia viwango vinavyokubalika
baada ya matumizi. Usimamizi wa vyanzo vya maji nchini unafuata taratibu za
mipango shirikishi ya usimamizi wa rasilimali za maji kwenye Bodi za Maji za mabonde tisa yaliyopo nchini,
ambapo saba katika hayo
yanahusisha majishirikishi kati ya nchi yetu na nchi jirani.
14.
Mheshimiwa Spika, inakadiriwa kuwa rasilimali za maji juu ya ardhi
zinazofaa kwa matumizi mbalimbali (annual renewable surface water resources) ni wastani wa kilomita za ujazo 87 kwa
mwaka. Aidha, hifadhi ya rasilimali za maji chini ya ardhi inakadiriwa kuwa kilomita
za ujazo 38. Hata hivyo, mtawanyiko na upatikanaji wa rasilimali
hizo nchini hauko sawa katika maeneo yote kutokana na tofauti ya hali ya hewa,
jiografia na jiolojia.
15.
Mheshimiwa Spika, Changamoto kubwa
iliyopo kwenye usimamizi wa rasilimali za maji ni kupungua na kuharibika kwa
vyanzo vya maji kutokana na shughuli za kibinadamu katika maeneo ya vyanzo vya
maji na katika misitu ya hifadhi ya maji (catchments forests and wetlands). Hifadhi hizi zinawezesha upatikanaji wa maji juu
na chini ya ardhi. Takwimu za kitaifa za rasilimali za maji zilizopo zinaonesha
kuwa kiasi cha maji kwa sasa kwa kila mtanzania ni wastani wa mita za ujazo 1,952
kwa mwaka. Endapo hatua madhubuti za utunzaji wa vyanzo vya maji
hazitachukuliwa mapema, kiasi hicho kinatarajiwa kupungua hadi kufikia mita
za ujazo 883 mwaka 2035. Kiwango cha
chini cha mahitaji ya maji kwa kila mtu kwa mwaka kinachokubalika kimataifa ni mita
za ujazo 1,700. Wizara yangu kwa
kushirikiana na wadau wa Sekta ya Maji inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za
kukabiliana na hali hiyo ili nchi yetu isifikie kiwango hicho cha upatikanaji
wa maji kwa kila Mtanzania.
16.
Mheshimiwa Spika, wastani wa mvua katika mabonde ya maji nchini ulikuwa
unatofautiana kutokana na tabia tofauti za hali ya hewa katika maeneo hayo.
Baadhi ya mabonde yalipata mvua kidogo na mengine mvua nyingi kulinganisha na
viwango vya mwaka uliopita kwa mujibu wa taarifa ya mwaka wa kihaidrolojia
(Novemba, 2012 – Oktoba 2013). Kwa ujumla kiasi cha mvua kilikuwa chini ya
wastani katika maeneo mengi ambapo asilimia 67 ya vituo vya mvua vilionesha
kiwango cha mvua chini ya wastani. Kiwango cha mvua katika mabonde sita (6) kati ya tisa (9) ulikuwa kama ifuatavyo:
Bonde la Pangani milimita 720 ikilinganishwa na wastani wa milimita 782 ya mwaka uliopita;
Bonde la Rufiji milimita 1,144 ikilinganishwa na milimita 846.0; Bonde la Wami/Ruvu milimita 979 ikilinganishwa milimita
1,150;
Bonde la Ziwa Tanganyika milimita 895 ikilinganishwa na milimita 705; Bonde la Ziwa
Victoria milimita 968 ikilinganishwa na milimita
1,175;
na katika Bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini wastani wa milimita 730 ikilinganishwa na milimita
917.
17.
Mheshimiwa Spika, kulingana na mvua zilizonyesha katika kipindi hicho,
viwango vya maji kwenye mito pia vimetofautiana kutokana na kiasi cha mvua
pamoja na mitiririko ya maji kuelekea katika mito mbalimbali nchini. Viwango
vya maji katika baadhi ya mito nchini vilikuwa kama ifuatavyo:- Mto Kikuletwa
katika Bonde la Pangani ulikuwa na mita za ujazo 14.66
kwa sekunde ikilinganishwa na kiasi cha mita
za ujazo 21.85 kwa sekunde
kilichopatikana mwaka uliopita; Mto Ruaha Mkuu ulioko Bonde la Rufiji ulikuwa na wastani
wa mita za ujazo 9.93 kwa sekunde ikilinganishwa na mita za ujazo 12.90 kwa sekunde; Mto Wami mita za ujazo 18.69 kwa sekunde
ikilinganishwa na mita za ujazo 89.41 kwa sekunde; na Mto Ruvu mita
za ujazo 36.21 kwa sekunde, ikilinganishwa na wastani wa mita za ujazo 42.90 kwa sekunde. Vilevile,
wastani wa mtiririko wa maji kwenye baadhi ya mito katika bonde la Ziwa
Victoria ulikuwa ni mita za ujazo 66.55 kwa sekunde katika Mto Mara na mita za ujazo 27.46 kwa sekunde kwa Mto
Simiyu ikilinganishwa na mita za ujazo 102.37 na 74.78 kwa sekunde kwa mwaka uliopita katika mito hiyo kwa mtiririko huo.
18.
Mheshimiwa Spika, hali ya maji kwenye baadhi ya mabwawa makubwa
tuliyonayo haikuwa ya kuridhisha japo kulikuwa na ongezeko dogo la kina cha
maji katika mabwawa hayo. Katika Bonde la Pangani bwawa la Nyumba ya Mungu usawa wa maji ulikuwa mita 683.94 juu ya usawa wa bahari,
ikilinganishwa na usawa wa mita 683.20 mwaka uliopita na bwawa la
Mabayani lilikuwa na usawa wa maji wa mita 91.20 ikilinganishwa na mita 91.10
juu ya
usawa wa bahari. Katika mabwawa yaliyopo Bonde la Rufiji, usawa wa maji ulikuwa
kama ifuatavyo; Kihansi (mita 1,144.69), Mtera (mita 691.18) na Kidatu (mita
446.33)
juu ya usawa wa bahari ikilinganishwa na mita 1,145.30 (Kihansi), mita 689.19
(Mtera)
na
mita 444.57 (Kidatu) kwa mwaka uliopita. Kiwango cha maji katika Bwawa la Mtera ambalo
pia hutegemewa na Bwawa la Kidatu katika uzalishaji wa umeme kimeendelea kuwa
chini ya kiwango. Kiwango kinachotakiwa kwa ajili ya kuendesha mitambo ya umeme
katika Bwawa la Mtera ni mita 690.00 juu ya usawa wa bahari.
19.
Mheshimiwa Spika, usawa wa maji katika bwawa la Mindu ni mita 506.45 juu ya usawa wa bahari
ikilinganishwa na mita 506.82 ya mwaka uliopita. Aidha, usawa wa maji katika
Ziwa Victoria ulikuwa mita 1,133.22 juu ya usawa wa bahari
ikilinganishwa na mita 1,133.06 mwaka uliopita, Ziwa Tanganyika lilikuwa wastani
wa mita 774.6 ikilinganishwa na mita 774.3 juu ya usawa wa bahari, na Ziwa Nyasa lilikuwa
na wastani wa mita 474.48 ukilinganisha na mita 475.71 juu ya usawa wa bahari.
20.
Mheshimiwa Spika, kulingana na takwimu hizo, uhaba wa maji umeendelea kuyaathiri maeneo mengi
nchini kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo upungufu wa mvua katika maeneo
mengi hasa yale yanayotegemea mvua za msimu mmoja, kupungua kwa uwezo wa ardhi
kuhifadhi maji wakati yakitiririka kuelekea mitoni kutokana na ukataji miti kwa
wingi na uharibifu wa mazingira,
mabadiliko ya matumizi ya ardhi, athari za mabadiliko ya tabianchi, ongezeko
la shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na kasi kubwa ya
ongezeko la watu. Hata hivyo mvua zilizonyesha mwezi Aprili 2014 ziliongeza
wingi wa maji kwenye mito, mabwawa na maziwa. Katika baadhi ya mito, takwimu
zinaonesha wastani wa mtiririko wa maji uliongezeka kama ifuatavyo:- Mto Mara,
mita za ujazo 260 kwa sekunde, Mto Simiyu mita za ujazo 141.37 kwa sekunde, Mto Wami mita
za ujazo 337.63 kwa sekunde, Mto Rufiji mita za ujazo 800 kwa sekunde na Mto Ruvu ni
zaidi ya mita za ujazo 453 kwa sekunde. Hali hiyo imedhihirika pia katika vina vya
mabwawa ya Mtera mita 693.38 juu ya usawa wa bahari, Nyumba ya Mungu mita 684.25 na Mindu mita 507. Vilevile, vina vya
maji kwenye maziwa nchini vimeongezeka ambapo kwa Ziwa Victoria kilikuwa mita
1133.25, Ziwa Nyasa mita 476.02 na Ziwa Tanganyika mita 775.13 juu ya usawa wa bahari.
Mvua hizo zimeongeza wingi wa maji kwenye vyanzo vya maji katika maeneo
yaliyopata mvua za kutosha.
2.2 HUDUMA YA MAJI VIJIJINI
21.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuwapatia maji safi na salama
wananchi waishio vijijini katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi
yao kama Sera ya Maji ya mwaka 2002 inavyoelekeza. Kwa kushirikiana na
Washirika wa Maendeleo, Serikali za Mitaa, Wananchi, Sekta Binafsi na Wadau
wengine, Serikali inaboresha huduma za maji vijijini kwa kujenga, kupanua na
kukarabati miundombinu ya maji. Jukumu la Wizara ni kutafuta fedha, kuandaa
miongozo ya utekelezaji na kutoa ushauri wa kitaalam. Sekretarieti za Mikoa
husimamia na kutoa ushauri wa kiufundi kwa Halmashauri katika kutekeleza miradi
ya maji vijijini.
22.
Mheshimiwa Spika, uchambuzi wa kina uliofanyika wakati wa matayarisho ya
mpango wa BRN ulibaini vituo vingi vya miradi iliyokamilika kuwa havitoi huduma kutokana
na miradi hiyo kutofanyiwa matengenezo ya mara kwa mara kama inavyotakiwa.
Aidha, baadhi ya miradi, pampu na
vipuri vimeibiwa, au miradi mingine uwezo wa vyanzo vyake umepungua kutokana na
uharibifu wa mazingira katika vyanzo kama vile ukataji miti au kilimo katika
vyanzo hivyo, hii ikiwa ni pamoja na mahitaji ya maji kuongezeka kutokana na
kuongezeka kwa watu ukilinganisha na uwezo wa vyanzo vya miradi hiyo.
2.3 HUDUMA YA MAJI MIJINI
23.
Mheshimiwa Spika, huduma za majisafi na usafi wa mazingira mijini
zinasimamiwa na kutekelezwa na Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira
nchini. Mamlaka hizo zilianzishwa mwaka 1998 chini ya Sheria Na.8 (Water Works Act) ya mwaka 1997, kwa sasa zinasimamiwa
na Sheria Na. 12 ya mwaka 2009 ya Huduma za Majisafi na Usafi
wa Mazingira. Mamlaka hizo za Maji ziko kwenye miji mikuu ya mikoa na wilaya,
miji midogo na miradi ya kitaifa.
24.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka za maji za miji mikuu ya mikoa zinaendeshwa chini
ya usimamizi wa Bodi za Wakurugenzi ambazo huteuliwa na Waziri mwenye dhamana
ya maji kwa kushirikiana na uongozi wa mikoa husika. Lengo la utaratibu huo ni
kuziwezesha Mamlaka hizo zijiendeshe kibiashara na hatimaye kuwa endelevu na
kujitegemea kwa gharama zote za uendeshaji, matengenezo na uwekezaji kutokana
na maduhuli ya mauzo ya maji. Hadi mwezi Machi, 2014 zimeundwa Mamlaka 23 za Miji Mikuu ya Mikoa.
Mamlaka
kati ya hizo yaani Arusha, Dodoma, Iringa, Mbeya, Morogoro, Moshi, Mtwara,
Mwanza, Shinyanga, Tabora, Tanga, Songea na Musoma zipo Daraja ‘A’. Mamlaka hizo zinajitegemea kwa gharama
zote za uendeshaji na matengenezo, ikiwemo mishahara ya watumishi na gharama za
umeme wa kuendesha mitambo ya kusukuma maji na uwekezaji mdogo. Mamlaka nne za Bukoba, Kigoma,
Singida na Sumbawanga ziko Daraja ‘B’ na zinapata ruzuku ya kulipia
sehemu ya gharama za umeme wa kuendesha mitambo. Mamlaka zilizo kwenye Daraja
‘C’ ni Mpanda,
Njombe, Bariadi, Geita, Babati na Lindi ambazo zinaendelea kupata
ruzuku ya mishahara kwa baadhi ya wafanyakazi wake pamoja na kulipia gharama za
umeme wa kuendesha mitambo na uwekezaji.
25.
Mheshimiwa Spika, wastani wa kiwango cha utoaji huduma ya majisafi kwenye
miji mikuu ya mikoa imeendelea kuimarika. Hali hiyo imetokana na ujenzi,
upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya majisafi katika mamlaka zote za maji za
miji mikuu ya mikoa. Hadi mwezi Machi, 2014 upatikanaji wa huduma ya maji
kwenye mamlaka za maji 19 isipokuwa DAWASA na Mamlaka za miji minne ya Mikoa mipya imefikia
wastani wa asilimia 86. Upatikanaji wa huduma ya maji kwa miji minne ya Mpanda,
Njombe, Geita na Bariadi ni wastani wa asilimia 53. Aidha, idadi ya wateja
waliounganishwa kwenye mitandao ya majisafi mijini imeongezeka kutoka wateja 311,478
mwezi
Machi, 2013 hadi kufikia wateja 336,898 ambalo ni ongezeko la asilimia 8.
26.
Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa majisafi kwa Mamlaka zote 23 za miji mikuu ya mikoa
uliongezeka kutoka wastani wa lita milioni 348.76 kwa siku mwezi Machi 2013 hadi
kufikia wastani wa lita milioni 376.07 mwezi Machi 2014. Ufungaji wa
dira za maji umeongezeka hadi kufikia dira za maji 316,018 ukilinganisha na dira
284,861 mwezi Machi 2013, sawa na asilimia 94 ya wateja wote 336,898. Lengo ni kufikia asilimia
100 ya
ufungaji wa dira za maji kwa wateja ifikapo mwezi Desemba 2014. Wastani wa
upotevu wa maji (Non Revenue Water – NRW) kwenye mifumo ya
usambazaji maji umefikia asilimia 38.Upotevu huu wa maji unatokana
na uchakavu wa miundombinu ya usambazaji
wa maji na wizi wa maji. Wastani wa makusanyo ya maduhuli yatokanayo na mauzo ya maji kwa mwezi kwa Mamlaka zote za maji
mijini isipokuwa DAWASCO, yameongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 6.36 (kwa mwezi) mwezi Machi 2014 kutoka
wastani wa shilingi bilioni 5.58, mwezi Machi 2013. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 14. Kuongezeka kwa maduhuli hayo,
kumeziwezesha Mamlaka kuboresha huduma zinazotolewa ikiwa ni pamoja na
kukarabati miundombinu na kugharamia shughuli za uendeshaji. Wizara itaendelea
kuimarisha Mamlaka za maji ili kuongeza maduhuli ziweze kufikia malengo
yaliyoainishwa kwenye Mikataba ya Utendaji kazi waliosaini na Wizara na EWURA.
27.
Mheshimiwa
Spika, miradi nane ya kitaifa ya KASHWASA,
Handeni Trunk Main–HTM, Maswa, Mugango-Kiabakari, Chalinze, Wanging’ombe,
Makonde na Masasi-Nachingwea inasimamiwa na Wizara yangu chini ya kifungu Na. 41 cha Sheria ya Huduma ya
Majisafi na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2009. Aidha, huduma za majisafi kwa
Miji Mikuu ya Wilaya na Miji Midogo hutolewa na Mamlaka za maji za miji hiyo
ambazo husimamiwa na Bodi za Wakurugenzi zinazoteuliwa na Mheshimiwa Waziri
Mkuu na kusimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa. Kwa sasa miradi ya maji ya kitaifa na mamlaka 96 ngazi ya Wilaya na Miji
Midogo zipo daraja C. Wizara
yangu kwa kushirikiana na TAMISEMI inaendelea kuzijengea uwezo Mamlaka hizo ili
zipande daraja kutoka C hadi madaraja ya B na A. Nia yetu ni kuziwezesha
kujiendesha kibiashara na hivyo kupunguza mzigo kwa Serikali.
28.
Mheshimiwa Spika, mmiliki na
msimamizi wa usambazaji wa huduma ya majisafi na uondoaji wa majitaka Jijini Dar-es-Salaam na
Miji ya Kibaha na Bagamoyo ni Dar es Salaam Water
Supply and Sewerage Authority–DAWASA. Serikali kupitia DAWASA iliingia Mkataba
wa kukodisha shughuli za uendeshaji wa huduma ya majisafi na majitaka na Shirika la Usambazaji
Maji Jijini Dar es Salaam (Dar es Salaam Water Supply and Sewerage
Corporation- DAWASCO). Lengo ni kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za utoaji huduma ya majisafi na
majitaka.
29.
Mheshimiwa Spika, idadi ya wakazi wanaopata huduma ya majisafi sasa katika
Jiji la Dar es Salaam ni asilimia 68 kwa wastani wa saa tisa (9) kwa siku. Kati ya hao, asilimia 55 wanapata huduma ya maji
kutoka kwenye mitandao ya mabomba na wanaobaki wanapata huduma ya maji kutoka
kwenye visima, magati na huduma ya magari (water bowsers). Lengo la Serikali ni kuongeza
kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji hadi kufikia asilimia 75 mwezi Juni, 2016. Mahitaji ya maji kwa
hivi sasa ni lita milioni 450 kwa siku ikilinganishwa na uwezo wa mitambo wa
kuzalisha maji lita milioni 300 kwa siku. Hata hivyo, mwezi Machi 2014, uzalishaji
wa maji ulishuka na kufikia wastani wa lita milioni 260 kwa siku. Upungufu huo
wa uzalishaji unatokana na tatizo la kuharibika kwa mara kwa mara kwa mitambo
ya kusukuma maji (pampu kubwa za Ruvu Juu), muda mrefu wa matengenezo,
miundombinu chakavu na hitilafu za umeme. Aidha, mpaka mwezi Machi, 2014 wateja 137,856 walikuwa wameungiwa
huduma ya maji na kufungiwa mita, ikilinganishwa na wateja 118,942 mwezi Machi, 2013, hilo
ni ongezeko la asilimia 16. Ongezeko la wateja limeongeza wastani wa makusanyo ya maduhuli yanayotokana na
mauzo ya maji kutoka shilingi bilioni 3.38 kwa mwezi Machi, 2013 hadi
kufikia shilingi bilioni 3.57 mwezi Machi, 2014. Pamoja na kuwepo kwa changamoto
kubwa inayotokana na uvujaji, uchakavu wa miundombinu, wizi wa maji na
uharibifu unaoweza kutokea wakati wa ukarabati wa miuondombinu ya barabara
huharibu miundombinu ya maji. na kuongeza upotevu wa maji na kupunguza
upatikanaji wa huduma ya maji. Serikali inaendelea kukabiliana na changamoto
hizi na kuzipatia ufumbuzi hatua kwa hatua.
30.
Mheshimiwa Spika, takwimu zilizopo zinaonesha kwamba, huduma ya uondoaji
majitaka ni asilimia 18 kufikia mwezi Machi 2014, ikilinganishwa na malengo ya
MKUKUTA II ya kuongeza kiwango cha huduma ya majitaka kufikia asilimia 22 ifikapo 2015. Miji yenye mitandao ya
majitaka ni Arusha, Moshi, Tanga, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Iringa, Songea,
Tabora, Morogoro na Dar es Salaam. Hali ya huduma ya uondoaji wa majitaka
mijini siyo ya kuridhisha. Aidha, idadi ya wateja waliounganishwa kwenye mtandao wa
majitaka imeongezeka kutoka 21,775 mwezi Machi, 2013 hadi kufikia wateja 22,976 mwezi Machi, 2014.
Pamoja na ongezeko hilo, bado wastani wa huduma ya uondoaji majitaka mijini ni asilimia
18 tu. Hali hiyo inasababishwa
na mwamko mdogo wa wananchi kujiunga kwenye mtandao wa majitaka katika miji
hiyo. Vilevile, miundombinu ya majitaka kwa baadhi ya miji ni chakavu na
inahudumia maeneo machache.
2.4 KUJENGA UWEZO WA TAASISI ZIILIZO CHINI YA PROGRAMU YA MAENDELEO YA SEKTA YA MAJI
31.
Mheshimiwa Spika, kulingana na mahitaji ya rasilimali watu ya
kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji na Mpango wa BRN, Wizara inahitaji wataalam 8,749 kwa kipindi chote cha utekelezaji wa Programu
(2006/2007 hadi 2025) ili kutekeleza
majukumu kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa. Hivi sasa, Sekta ya
Maji ina jumla ya wataalam 1,538. Kwa
mwaka wa kwanza (2013/2014) wa utekelezaji wa Mpango wa BRN, jumla ya wataalam 835 walihitajika kuajiriwa kwenye Sekretarieti za Mikoa
na Halmashauri zote nchini. Kati ya Wataalam hao, wahandisi ni 302 na mafundi sanifu 533. Katika mwaka 2013/2014 Serikali imeiidhinisha ajira
ya wataalamu (wahandisi) 125 wapya
na mafundi sanifu (FTC) 350.
32.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara
yangu ilitekeleza miradi inayohusu usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji,
huduma ya majisafi na usafi wa mazingira vijijini na mijini na masuala
mtambuka. Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2013/2014 na malengo ya
mwaka 2014/2015 kwa Sekta ya Maji unaelezwa katika
sura hii ya Bajeti.
33.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 Wizara
yangu ilisimamia na kuendeleza rasilimali za maji, ikiwemo kuchunguza,
kutathmini na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji nchini pamoja na
rasilimali za majishirikishi (transboundary water resources); na kuimarisha Bodi za
Maji za Mabonde ili zisimamie kikamilifu rasilimali hizo. Kazi nyingine ni
kuandaa mipango shirikishi ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji,
kusanifu na kusimamia ujenzi wa miundombinu ya kipaumbele, yakiwemo mabwawa.
(a)
Mwenendo wa Rasilimali za Maji
34.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuimarisha vituo vya kupima
wingi na ubora wa rasilimali za maji juu na chini ya ardhi ili kuboresha
upatikanaji wa takwimu na upatikanaji wa taarifa sahihi. Katika mwaka
2013/2014, jumla ya vituo 29 vya kupima mtiririko wa maji
mitoni, vituo 14 vya hali ya hewa, vituo sita (6) vya ufuatiliaji maji
chini ya ardhi, vituo vitatu (3) vya kupima maji kwenye
maziwa na vituo saba (7) vya kupima mvua
vilijengwa. Vituo hivyo vipo katika mabonde ya Wami-Ruvu, Pangani, Ziwa Rukwa,
Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na Bonde la Ruvuma na Pwani ya
Kusini. Aidha, ukarabati ulifanyika katika vituo 80 vya kupima mtiririko wa
maji kwenye mito, vituo 18 vya hali ya hewa, vituo viwili (2) vya ufuatiliaji wa maji
chini ya ardhi, vituo vitatu (3) vya kupima maji kwenye
maziwa, vituo vitano (5) vya kupima maji kwenye mabwawa na vituo sita (6) vya kupima mvua. (Jedwali
Na.1)
35.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha upatikanaji
wa takwimu sahihi za hali ya maji nchini, Bodi za Maji za Mabonde zimekusanya
na kuchanganua takwimu za hali ya maji katika vituo mbalimbali. Vituo hivyo
vinajumuisha vituo 203 vya kupima mtiririko wa maji
mitoni, vituo 12 vya kupima usawa wa maji katika maziwa na mabwawa, vituo
122 vya kupima mvua, na vituo 29 vya kupima hali ya
hewa. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kujenga na kukarabati vituo
134 vya kupima mtiririko wa maji mitoni, vituo 17 vya hali ya hewa, vituo
35 vya mvua na vituo 52 vya kupima maji chini ya
ardhi pamoja na kukusanya takwimu kwenye mabonde yote nchini.
36.
Mheshimiwa Spika, takwimu na taarifa zinazokusanywa kutoka kwenye vituo
hivyo husaidia kutambua hali ya maji kwa nyakati tofauti kwenye maeneo mbalimbali
hapa nchini, hivyo kuwezesha maandalizi ya mipango na kutoa maamuzi sahihi ya
ugawaji wa rasilimali za maji kwa matumizi mbalimbali. Aidha, takwimu na
taarifa hizo hutumika katika usanifu na ujenzi wa miundombinu ya miradi ya
maji, mabwawa na madaraja pamoja na utafiti wa mabadiliko ya tabianchi.
(b)
Kuhifadhi wa Mazingira na Vyanzo vya Maji
37.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mikakati ya
kuhifadhi vyanzo vya maji, Wizara yangu imeendelea kuvitambua, kuviwekea mipaka
na kuvitangaza kuwa maeneo tengefu. Katika mwaka wa fedha 2013/2014, jumla ya
vyanzo 153 vilitambuliwa kuwa katika hatari ya kuharibiwa na
kuathiriwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la shughuli za kibinadamu.
Kati ya hivyo, vyanzo 59 vimebainishwa na na kuandaliwa
ili vitangazwe kuwa maeneo tengefu ya vyanzo vya maji. Hadi mwezi Machi 2014,
mapendekezo ya vyanzo saba (7) kati ya vyanzo
vilivyobainishwa katika Bonde la Ziwa Rukwa viko tayari kutangazwa rasmi kuwa
maeneo tengefu. Maeneo hayo ambayo hayakuhitaji fidia ni maeneo ya vyanzo vya
maji chini ya ardhi yaliyoko Chokaa, Kidole, Kiswaga, Matundasi A, Matundasi B,
Mkola na Bwawa la Milala.
38.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2014/2015, Wizara
itaendelea na taratibu za kutangaza vyanzo vya maji vilivyobainishwa kuwa
maeneo tengefu likiwemo Bwawa la Mtera katika Bonde la Rufiji. Vilevile, katika
Bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini vyanzo vya maji vya chemichemi za Mbwinji,
Ndanda, Mwena na Liputu kwenye miteremko ya milima ya Makonde vimewekewa mipaka
kwa ajili ya kuvihifadhi. Uchoraji wa ramani za maeneo husika unaendelea na
utakapokamilika yatatangazwa kuwa maeneo tengefu. Aidha, uwekaji wa mipaka
unaendelea kwenye vyanzo vya maji vya Mitema-Kitangari kwa lengo la
kuvihifadhi. Wizara yangu itaendelea kubaini na kuweka mipaka maeneo mengine ya
vyanzo vya maji ili kuyakinga dhidi ya uharibifu wa mazingira.
39.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana
na wadau mbalimbali wa maji imeandaa Mpango Maalum wa miaka mitano wa Kuhifadhi
na Kutunza Vyanzo vya Maji utakaoanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha
2014/2015. Mpango huo umeainisha maeneo ya utekelezaji ili kuimarisha usimamizi
wa vyanzo vya maji kwa maendeleo endelevu ya sasa na vizazi vijavyo. Mpango huo
utahusisha kutoa elimu kwa umma na kuimarisha ushiriki wa wadau katika shughuli
za uhifadhi, utunzaji na ulinzi wa rasilimali za maji; kujenga uwezo wa wadau
wa sekta ya maji katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji; na kusaidia
shughuli mbadala za kiuchumi ili kupunguza shughuli za kibinadamu kwenye maeneo
ya vyanzo vya maji. Shughuli hizo ni pamoja na ukataji miti, kilimo cha
“vinyungu” na kilimo katika kingo za mito. Wizara kwa kushirikiana na wadau hao
itaendelea kuhakikisha kwamba vyanzo vya maji vinatunzwa na kulindwa.
40.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuimarisha
usimamizi wa rasilimali za maji, hadi mwezi Machi 2014, jumla ya Jumuiya 99 za Watumiaji Maji
ziliundwa. Kati ya hizo Jumuiya 18 zimeundwa katika
kipindi cha mwaka 2013/2014. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaunda
Jumuiya za Watumiaji Maji 20 na Kamati 13 za kulinda misitu katika
vyanzo vya maji (catchment areas) na kuendelea
kuimarisha zilizopo. Taarifa ya tathmini ya athari kwa mazingira
kwa mabwawa sita ya Itobo, Uchama, Nkiniziwa, Leken, Enguikument I na
Enguikument II yaliyopo katika Bonde la Kati imekamilika na kuwasilishwa NEMC kwa hatua zaidi. Kazi
ya tathmini za athari kwa mazingira kwa ajili ya miradi ya mabwawa ya Farkwa na
Ndembera zinaendelea. Vilevile, tathmini ya athari kwa mazingira ya mradi wa
bwawa la Kidunda pamoja na barabara inayoelekea kwenye bwawa inaendelea.
(c)
Kudhibiti Uchafuzi wa Vyanzo vya Maji
41.
Mheshimiwa Spika, udhibiti wa uchafuzi wa vyanzo vya maji ni muhimu
katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji nchini. Katika kutekeleza
jukumu hilo, ukaguzi ulifanyika katika Bonde la Kati kwenye maeneo tisa (9) ya viwanda, migodi 46 na hoteli tatu (3) na katika Bonde la
Pangani, ukaguzi ulifanyika katika mifumo ya utoaji majitaka ya viwanda vitatu (3) na kuangalia utendaji
kazi (performance assessment) wa mabwawa ya majitaka ya
Mamlaka ya Majisafi na Usafi Mazingira, Arusha.
42.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Bodi ya Maji ya Bonde
la Pangani ilikagua maeneo mbalimbali yaliyopo katika Mkoa wa Kilimanjaro ili
kubaini na kuorodhesha shughuli zinazoathiri ubora wa vyanzo vya maji (Inventory
of polluting activities). Maeneo yafuatayo yalibainishwa:- Viwanda vya kahawa,
viwanda vya mkonge, kiwanda cha chokaa, mashamba ya maua, maeneo ya kutengeneza
na kuoshea magari na maeneo ya vyanzo vya maji yanayochafuliwa kwa kuweka
makazi na kutupa taka ngumu.
43.
Mheshimiwa Spika, ukaguzi huo ulibaini baadhi ya viwanda kutokuzingatia
taratibu za utiririshaji wa majitaka kwenda kwenye vyanzo vya maji. Wizara
iliviagiza viwanda hivyo kutengeneza mifumo ya kusafisha majitaka kabla ya
kuyatiririsha kwenda kwenye vyanzo vya maji kwa kuzingatia Sheria Na. 20 ya mwaka 2004 ya
Usimamizi wa Mazingira. Wizara kwa kushirikiana na NEMC itaendelea kufanya
ukaguzi kwenye maeneo ya viwanda na migodi na kuchukua hatua stahiki.
Jedwali Na. 2 linaonesha matokeo ya ukaguzi wa vyanzo vya maji
unaotokana na majitaka kutoka viwandani na migodini.
44.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea na
kuhakikisha vyanzo vipya vya maji vilivyobainishwa vinafanyiwa tathmini na
usanifu ili viweze kujengwa na kuongeza upatikanaji wa maji nchini. Katika
mwaka 2013/2014, Mtaalam Mshauri amekamilisha kazi ya uchunguzi wa kina wa
miamba na ameendelea na kazi ya usanifu kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Farkwa
kwenye Mto Bubu, Wilaya ya Chemba. Mradi huo unatarajiwa kuwapatia maji wakazi
wa Manispaa ya Dodoma pamoja na Miji ya Chamwino, Bahi na Chemba. Aidha, Wizara
inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa Bwawa la Ndembera katika Bonde la Rufiji
litakalotumika kudhibiti mwenendo na mtiririko wa maji katika kipindi cha mwaka
mzima kwenye Mto Ruaha Mkuu. Bwawa hilo pia linatarajiwa kutumika kwa shughuli
za kilimo cha umwagiliaji na kuzalisha umeme. Vilevile, Mtaalam Mshauri
amewasilisha taarifa ya upembuzi yakinifu na anaendelea na kazi ya usanifu wa
kina.
45.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, hatua za awali za ujenzi wa
bwawa la Kidunda zimekamilika ambapo Mtaalam Mshauri anaandaa taarifa ya mwisho
ya usanifu na uandaaji wa zabuni (Final Design Report & Tender Documents). Taratibu za ununuzi
wa Mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya kuelekea kwenye eneo la bwawa
zinatarajiwa kuanza mara baada ya kukamilika kwa mapitio ya Tathmini ya Athari
za Kimazingira na Kijamii (Environmental and Social Impact Assessment-ESIA) na kulipa fidia kwa
watakaoathirika na mradi. Katika mwaka 2014/15, Wizara imetenga fedha za kulipa
fidia, na kujenga barabara.
46.
Mheshimiwa Spika, kwa mradi wa visima vya
kuchunguza mwenendo wa maji chini ya ardhi katika maeneo ya Kimbiji na Mpera,
Wizara yangu ilipanga kuchimba visima nane (8). Hadi mwezi Machi, 2014
visima viwili (2) vya uchunguzi vimekamilika na
kisima cha tatu kinachimbwa na kimefikia mita 200. Inatarajiwa kuwa
kufikia mwezi Novemba, 2014 visima vyote vitakuwa vimekamilika. Katika mwaka
2014/2015 Serikali italipa fidia kwa wananchi watakaoathirika na uchimbaji wa
visima ili kukamilisha mradi wa visima wa Kimbiji na Mpera kama ilivyopangwa.
Baada ya kulipa fidia kwenye eneo la mita 60 kuzunguka kila kisima katika
maeneo ya Kimbiji na Mpera kukamilika, Serikali imekamilisha uhakiki wa fidia
katika maeneo ya Luzando na Kisarawe II na ulipaji wa fidia umeanza kwa eneo
litakapojengwa tanki la Kisarawe II pamoja na kwa eneo la Luzando. Vilevile, uthamini katika maeneo ya
ujenzi wa njia za mabomba za barabara kuelekea kwenye visima umeanza, na maombi
ya kupata Wathamini yamewasilishwa kwenye Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali.
47.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014,
Wizara yangu iliendelea kutafiti maji chini ya ardhi kwa ajili ya kuongeza
upatikanaji wa maji. Utafiti ulibaini maeneo 501 yanayofaa kuchimbwa visima
vya maji katika mabonde ya Rufiji (33), Bonde la Kati (39), Pangani (149), Wami-Ruvu (18), Ziwa Victoria (40), Ziwa Rukwa (73), Ziwa Tanganyika (80) na Ruvuma na Pwani ya
Kusini (69). Wizara yangu pia ilisimamia uchimbaji wa visima vya
utafiti 152 katika mabonde ya Rufiji (40), Bonde la Kati (3), Pangani (4), Ruvuma na Pwani ya Kusini (42) Wami-Ruvu (55), Ziwa Victoria (4) na Ziwa Tanganyika (4). Kwa mwaka 2014/2015,
Serikali itaendelea kutafiti maji chini ya ardhi katika maeneo mengine zaidi.
48.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kushirikiana na Serikali ya
Misri katika utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa uchimbaji wa visima 70; kati ya hivyo,
maandalizi ya uchimbaji wa visima 30 yameanza katika maeneo
ya Wilaya za Kiteto (10), Same (8), Mwanga (1), Bariadi (2) na Itilima (9) ambapo Mkandarasi
amekabidhiwa maeneo ya kazi. Vilevile, Wizara yangu kwa kushirikiana na Serikali
ya Jamhuri ya Watu wa China ilichimba visima 53 kati ya visima 55 vilivyopangwa katika
Wilaya za Kisarawe na Kilosa. Visima 25 vilichimbwa katika
Wilaya ya Kilosa na visima 28 Wilaya ya Kisarawe.
Visima hivyo viko katika hatua za mwisho za ufungaji wa pampu. Katika mwaka
2014/2015, kazi ya uchimbaji wa visima vilivyobaki itakamilishwa katika Wilaya
ya Kisarawe.
49.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu ilisajili kampuni mbili (2) za uchimbaji visima vya
maji kati ya kampuni sita (6) zilizoomba. Kampuni nne
(4) hazikukidhi vigezo kulingana na Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za
Maji Na. 11 ya Mwaka 2009. Uratibu huo unalenga kuhakikisha kwamba taratibu za
kitaalam zinafuatwa ili kuhakikisha visima vina ubora kwa matumizi endelevu.
Hadi mwezi Machi 2014, kampuni binafsi 137 zilikuwa zimesajiliwa.
Aidha, jumla ya visima vya maji 546 vilichimbwa katika
maeneo mbalimbali nchini. Kati ya hivyo, visima 100 vilichimbwa na Wakala
wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) na visima 446 vilichimbwa na kampuni
binafsi.
50.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu kupitia Bodi za
Maji za Mabonde imeendelea kutoa elimu kwa wadau kuhusu umuhimu wa usimamizi
endelevu wa rasilimali za maji, hususan kutoa vibali vya matumizi ya maji na
utiririshaji wa majitaka. Hadi mwezi Machi 2014, jumla ya vibali vipya 586 vilitolewa katika mabonde
ya Pangani (105), Rufiji (92), Wami-Ruvu (112), Ruvuma na Pwani ya
Kusini (21), Bonde la Kati (3), Ziwa Victoria (37), Ziwa Rukwa (66), Ziwa Tanganyika (56) na Ziwa Nyasa (94). Jumla ya maombi 223 yalipokelewa katika
mabonde ya Ziwa Rukwa (19), Ziwa Tanganyika (50), Wami-Ruvu (77), Ziwa Nyasa (60) na Ruvuma na Pwani ya
Kusini (17). Vilevile, usajili wa vibali vya zamani (re-registration) ulifanyika ambapo
vibali 479 kutoka katika mabonde ya Ziwa Nyasa (4), Ziwa Victoria (370) na Wami-Ruvu (105) vilihakikiwa na
kusajiliwa upya kulingana na matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za
Maji Na. 11 ya mwaka 2009..
51.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, vibali 15 vya kutiririsha
majitaka vilitolewa katika mabonde ya Ziwa Victoria (10), Ziwa Rukwa (3) na Pangani (2). Aidha, zoezi la
kuwatambua watumiaji maji kwa matumizi mbalimbali lilifanyika ili waweze
kupatiwa elimu na hatimaye kuweza kufuata taratibu za kisheria za matumizi
endelevu ya maji. Jumla ya watumiaji maji 835 walibainishwa katika
mabonde ya Pangani (513), Ziwa Victoria (27), Ziwa Tanganyika (162), Ziwa Nyasa (24),
Ruvuma na Pwani ya Kusini (19) na Wami-Ruvu (90).
52.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara
yangu iliendelea na utayarishaji wa Mipango itakayo simamia na kuendeleza
Rasilimali za Maji (IWRM&D Plans) na kuwahusisha
wananchi katika mabonde yote tisa. Hadi mwezi Machi 2014, rasimu za mwisho za
mipango katika mabonde ya Ruvuma na Pwani ya Kusini, Bonde la Kati, Ziwa
Tanganyika na Ziwa Nyasa zilifanyiwa marekebisho na Wataalam Washauri baada ya
kupokea maoni na marekebisho kutoka kwa wadau. Wataalam Washauri katika bonde
la Ziwa Rukwa, Pangani na Rufiji wamewasilisha Interim Reports na Wizara imetoa maoni
kuhusu taarifa hizo kwa ajili ya maboresho.
53.
Mheshimiwa Spika, katika Bonde la Wami-Ruvu,
taarifa ya mwisho ya mpango shirikishi wa usimamizi na uendelezaji wa
rasilimali za maji imekamilika na kuwasilishwa wizarani mwezi Desemba, 2013.
Mpango Shirikishi wa Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji katika Ziwa
Victoria upo katika hatua za awali za ukusanyaji wa takwimu na taarifa muhimu
kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika mwaka 2014/2015,
Wizara yangu itaendelea na utayarishaji wa Mpango Shirikishi wa Usimamizi na
Uendelezaji wa Rasilimali za Maji katika Ziwa Victoria. Aidha, Wizara itafanya
tathmini ya athari za kimazingira na kijamii kabla ya utekelezaji wa mipango
iliyoainishwa na (IWRM&D).
(g)
Kuimarisha Bodi za Maji katika Mabonde
54.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuzijengea
uwezo Bodi za Maji za Mabonde kwa kutoa mafunzo kwa watumishi, kujenga ofisi na
kununua vitendea kazi. Katika mwaka 2013/2014,
watumishi 81 wa mabonde nane walipatiwa mafunzo ya muda mfupi na semina
mbalimbali kama ifuatavyo; Bonde la Kati (3), Ziwa Nyasa (8), Pangani (36), Ruvuma na Pwani ya Kusini (6), Wami-Ruvu (2), Ziwa Victoria (10), Rufiji (3) na Bonde la Ziwa Rukwa (13). Mafunzo yalihusu jinsi ya kushirikisha wadau na
jamii katika utunzaji na usimamizi wa rasilimali za maji, usimamizi wa takwimu,
sheria mpya ya ununuzi, mfumo wa maamuzi (Decision Support System - DSS), mifumo ya teknolojia ya Quantum GIS, Google earth and ArcGIS software - conservation
strategies na
usimamizi wa mazingira (Environmental Management System - EMS). Mafunzo hayo yalilenga kuongeza ujuzi na ufanisi
katika utendaji wa kazi.
55.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa jengo jipya la
ofisi ya Bonde la Ziwa Nyasa umekamilika na litakabidhiwa mwezi Julai 2014.
Aidha, ujenzi wa Ofisi za Bodi za Maji za Mabonde ya Ziwa Victoria, Ziwa
Tanganyika na Bonde la Kati umeanza. Taarifa za usanifu wa majengo ya Ofisi za
Bodi za Maji za Mabonde yaliyobaki ya Wami-Ruvu, Ruvuma na Pwani ya Kusini,
Rufiji, Pangani, na Ziwa Rukwa, zimekamilika na kuwasilishwa kwa uhakiki. Kwa
mwaka 2014/2015, taratibu za kuwapata Wakandarasi wa ujenzi wa ofisi zilizobaki
zitakamilika na ujenzi kuanza.
56.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaimarisha Bodi za Maji za Mabonde
ili ziweze kufanya tafiti za rasilimali za maji kwa lengo la kupata ufahamu
zaidi kuhusu rasilimali zetu na katika usimamizi na uendelezaji wake. Wizara
kwa kushirikiana na Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Rukwa imefanya utafiti (Bathymetry) katika Ziwa Rukwa, na Ziwa hilo litakuwa la nne
kufanyiwa utafiti wa aina hiyo hapa nchini baada ya Maziwa ya Victoria,
Tanganyika na Nyasa.
57.
Mheshimiwa Spika, Bodi za Maji za Mabonde
hukusanya maduhuli yatokanayo na ada za matumizi ya maji na kutumia mapato hayo
(retention) katika usimamizi, utunzaji na uendelezaji wa rasilimali
za maji nchini. Hadi mwezi Machi 2014, jumla ya shilingi 1,527,245,592 zilikusanywa. Makusanyo
hayo ni sawa na asilimia 86.34 ya lengo la shilingi
1,768,887,117 zilizopangwa kukusanywa
katika mwaka wa fedha 2013/2014. Katika mwaka 2014/2015,
Bodi za Maji za Mabonde zimelenga kukusanya kiasi cha shilingi 2,576,000,000 kutoka vyanzo
mbalimbali vya mapato ikiwa ni pamoja na ongezeko la Ada ya matumizi ya maji
kama ilivyoainishwa katika Jedwali Na. 3.
58.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa majukumu ya Bodi
za Maji za Mabonde ni kusuluhisha migogoro katika matumizi ya maji kwa
kushirikiana na Jumuiya za Watumiaji Maji na inapobidi vyombo vya sheria
hutumika. Katika mwaka 2013/2014, migogoro 29 ya watumiaji maji ilijitokeza,
ambapo migogoro 21 kati ya hiyo ilisuluhishwa katika Mabonde ya Maji ya
Pangani (5), Wami/Ruvu (10), Ziwa Victoria (2), Rufiji (2) Ziwa Nyasa (1), na Ruvuma na Pwani ya
Kusini (1). Migogoro mingine sita (6) katika Bonde la Kati (4) na Ziwa Victoria (2) ipo katika hatua
mbalimbali za mashauriano nje ya mahakama;. Migogoro miwili (2) iliyobaki katika Bonde
la Pangani iko mahakamani. Katika mwaka 2014/2015, Serikali
itaendelea kusuluhisha migogoro ya watumiaji maji kama itakavyojitokeza na
kutoa elimu ya ugawanaji na utunzaji wa rasilimali za maji.
(j)
Usimamizi wa Rasilimali za Majishirikishi
59.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kushirikiana na nchi nyingine
zinazochangia rasilimali za maji shirikishi kwa kuunda
vyombo vya pamoja na kuimarisha vilivyopo ili kusimamia matumizi endelevu ya
rasilimali hizo. Azma ya ushirikiano huo ni kuhakikisha kunakuwepo na mifumo ya
uwazi na usawa ya uendelezaji na utumiaji wa rasilimali za maji. Mabonde saba
(7) ya maji kati ya tisa (9) yaliyopo nchini
yanavuka mipaka ya nchi yetu na hivyo kuwa na ulazima wa kushirikiana na nchi
nyingine 17 majirani. Nchi hizo ni
Angola, Botswana, Namibia, Zambia, Zimbabwe, Malawi, Msumbiji, Burundi, Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo, Misri, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan, Sudan Kusini,
Uganda na Eritrea. Ushirikiano wa kitaasisi na nchi hizo unatekelezwa kama
ifuatavyo:-
(i) Bonde la Mto Nile
60.
Mheshimiwa Spika, Umoja wa Ushirikiano wa Nchi za Bonde la Mto Nile (Nile
Basin Initiative – NBI) ulianzishwa rasmi mwaka 1999. Umoja huo ni chombo cha
mpito kuelekea kwenye uundwaji wa Kamisheni ya Bonde la Mto Nile. Madhumuni ya
kuanzishwa kwa umoja huo ni kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji, mazingira,
nishati, kilimo, mafunzo na kujenga uwezo kwa taasisi zilizopo katika nchi
husika. Jumla ya nchi 11 zinaunda umoja huo ambazo ni
Burundi, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Misri, Rwanda,
Sudan, Sudan Kusini, Uganda na Tanzania na nchi ya Eritrea ikiwa ni mtazamaji (observer).
61.
Mheshimiwa Spika, Nchi saba za Burundi, Ethiopia,
Uganda, Rwanda, Kenya, Sudan
Kusini na Tanzania zilisaini Mkataba wa Kudumu wa Ushirikiano wa nchi hizo
utakaoanzisha Kamisheni ya Bonde la Mto Nile. Hadi sasa, nchi za Ethiopia na
Rwanda tayari zimeridhia Mkataba huo na Tanzania ipo katika hatua za kukamilisha
taratibu za kuridhia. Aidha, nchi za Misri, Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo zinaendelea na misimamo yao ya kutosaini Mkataba huo. Kulingana na
matakwa ya Mkataba huo, nchi sita (6) zikikamilisha kuridhia
Kamisheni ya Bonde la Mto Nile itaanzishwa. Katika mwaka 2014/2015, nchi ambazo
zilisaini Mkataba huo zitakamilisha taratibu za kuridhia kwa kuzingatia sheria
za nchi zao. Tanzania itaendelea kufuatilia kwa karibu suala hili ambalo ni la
manufaa kwa nchi yetu.
(ii) Mradi wa Hifadhi ya
Mazingira ya Ziwa Victoria
62.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Tanzania kwa
kushirikiana na Serikali za Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda zinatekeleza Awamu
ya Pili ya Mradi wa Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira ya Ziwa Victoria (LVEMP
II). Lengo la mradi ni kuimarisha usimamizi wa pamoja wa
rasilimali za Bonde la Ziwa Victoria kwa kudhibiti uharibifu wa mazingira
katika ziwa hilo. Aidha, nchi yetu inanufaika na mradi huo kwa kuimarisha
Taasisi zinazohusika na hifadhi ya maji na samaki; ukarabati wa mifumo ya
kusafisha majitaka katika miji ya Mwanza, Musoma na Bukoba. Vilevile,
Halmashauri za Wilaya za Maswa, Itilima, Busega, Bariadi, Magu, Meatu, Kwimba,
Sengerema, Geita, Chato, Muleba, Karagwe, Kyerwa na Misenyi zimeingizwa kwenye
awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo.
63.
Mheshimiwa Spika, jumla ya miradi midogo ya kijamii 176 yenye thamani ya Dola
za Marekani milioni 4.5 inatekelezwa katika eneo la mradi. Hadi mwezi Machi
2014, miradi 48 imekamilika na itakabidhiwa kwa jamii. Vilevile, miradi 22 mikubwa ya kijamii yenye
thamani ya Dola za Marekani milioni 5.5 imeanza kutekelezwa
katika Halmashauri za Wilaya za Musoma Mjini, Maswa, Bariadi, Kwimba, Magu,
Meatu na Jiji la Mwanza. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea
kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo na kuhakikisha Wataalam Washauri
wanakamilisha kazi zao ambazo ni pamoja na kuoanisha Sera, Sheria, Kanuni na
Viwango vya utupaji majitaka katika rasilimali za maji zilizopo kwenye Bonde la
Ziwa Victoria.
(iii) Bonde la Mto Mara
64.
Mheshimiwa Spika, Bonde la Mto Mara,
ni moja kati ya mabonde ya mito inayoingiza maji katika Ziwa Victoria na
linahusisha nchi mbili za Kenya (inayomiliki asilimia
65 ya bonde) na Tanzania asilimia 35. Bonde hilo ni
eneo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi pamoja na bayoanuai zilizopo. Utekelezaji
wa miradi na shughuli mbalimbali katika Bonde hilo kikanda unasimamiwa na
Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (Lake Victoria Basin Commission-LVBC). Katika kuimarisha
ushirikiano uliopo katika nchi zetu mbili, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa
Maadhimisho ya “Siku ya Mara” ambayo lengo lake ni kushirikisha Wakazi wa Bonde
hilo katika kulinda, kusimamia na kuendeleza rasilimali asili za Bonde kwa
manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo. Sherehe hizo zilifanyika Mjini Mugumu,
Serengeti ambapo mgeni rasmi alikuwa Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb), Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
65.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2013/2014, Wizara yangu ilianza uratibu wa Mradi wa masuala ya kukabiliana na
mabadiliko ya tabianchi (Planning for Resilience in East Africa through
Policy, Adaptation, Research and Economic Development-PREPARED). Miji iliyopewa
kipaumbele katika utekelezaji wa mradi huo ni Halmashauri za Itilima katika
Mkoa wa Simiyu, Bunda (Mkoa wa Mara) pamoja na Chato (Mkoa wa Geita). Aidha,
taratibu za kuandaa Hati ya Makubaliano (MoU) kwa ajili ya
usimamizi shirikishi wa rasilimali za maji katika ikolojia ya Bonde la Mto Mara
zinaendelea kati ya nchi shirikishi chini ya uratibu wa Nile Basin
Initiatives. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kuratibu
miradi mbalimbali itakayotekelezwa kupitia Mradi wa “PREPARED” ili kusaidia
wananchi wanaoishi maeneo ya Bonde la Mto Mara kukabiliana na athari za
mabadiliko ya tabianchi.
66.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2013/2014, Wizara yangu kwa kupitia Mradi wa Usimamizi na Uendelezaji wa
Rasilimali za Maji katika Bonde la Mto Mara, ulio chini ya Umoja wa Ushirikiano
wa Nchi za Bonde la Mto Nile imeendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa
bwawa la Borenga litakalojengwa kwenye mpaka wa Wilaya za Serengeti na Tarime.
Bwawa hilo ni kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo, nishati ya umeme na
kilimo cha umwagiliaji katika vijiji 16 vilivyopo katika
Wilaya za Butiama, Serengeti na Tarime. Inakadiriwa kuwa hekta 8,340 zitamwagiliwa na
maji kutoka katika bwawa hilo ambalo litakuwa na mita za ujazo milioni 20. Aidha, mradi
unaendelea na uandaaji shirikishi wa mipango ya usimamizi wa hifadhi ya maji
katika sehemu ya Bonde la Mto Mara (Sub Catchment Management Plans) ya Tobora (kilomita
za mraba 364) na Somoche (kilomita za mraba 682). Hifadhi hizo za
maji zipo katika bonde la Mto Mara Wilayani Serengeti. Vilevile, katika mwaka
2013/2014, mradi ulitoa mafunzo ya uendeshaji na matengenezo wa vifaa
vinavyopima wingi wa maji mitoni na ziwani na hali ya hewa (hydro-metereological
equipment) kwa Mafundi Sanifu wa Bonde la Ziwa Victoria. Katika
mwaka 2014/2015, Wizara itakamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi wa
ujenzi wa bwawa la Borenga na kuandaa zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa
ujenzi.
(iv)
Bonde la Mto Zambezi
67.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu iliendelea
kutekeleza Mkataba wa Kamisheni ya Bonde la Mto Zambezi (Zambezi
Watercourse Commission-ZAMCOM) ulioanza kutekelezwa rasmi
kisheria mwaka 2011. Madhumuni ya kuanzisha Kamisheni hiyo ni kusimamia kwa
pamoja rasilimali za maji za Bonde la Mto Zambezi. Jumla ya nchi saba (7) zinatekeleza Mkataba
wa Kamisheni hiyo ambazo ni Angola, Botswana, Msumbiji, Namibia, Zambia,
Zimbabwe na Tanzania. Nchi ya Malawi haijaridhia Mkataba huo hadi sasa. Baada ya Sekretarieti ya
muda (Interim ZAMCOM Secretariat) kumaliza muda wake
tarehe 31 Desemba, 2013, Sekretarieti ya Kudumu ya Kamisheni ya Bonde la Mto
Zambezi imeanza kazi rasmi na Makao Makuu yake yapo Mjini Harare Zimbabwe.
68.
Mheshimiwa Spika, majukumu mengine ya Sekretarieti
ya Kudumu ya ZAMCOM ni kuandaa mikakati ya utekelezaji wa mipango ya
usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji za Bonde la Mto Zambezi kwa
kuzingatia maamuzi ya vikao vya Baraza la Mawaziri wa Maji wa SADC na lile la nchi
wanachama wa ZAMCOM. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea
kuratibu kazi za Kamisheni hiyo zinazofanyika hapa nchini.
(v) Bonde la Mto Ruvuma
69.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji Shirikishi wa
Bonde la Mto Ruvuma unahusisha nchi za Msumbiji na Tanzania na kuratibiwa na
Sekretarieti ya SADC. Mradi huo umeanzishwa ili kuhakikisha rasilimali za
maji za Bonde hilo zinasimamiwa vizuri na kutumiwa kwa manufaa ya nchi hizo
mbili. Hapa nchini mradi unatekelezwa katika Wilaya tano (5) za Mikoa ya Mtwara na
Ruvuma ambazo ni Tandahimba, Nanyumbu, Songea Vijijini, Tunduru na Mbinga.
Katika mwaka 2013/2014, miradi miwili ya kijamii inatekelezwa
katika Wilaya ya Tunduru ambapo jumla ya miche ya miti 5,733 imepandwa katika vijiji
viwili vya Daraja Mbili na Lelolelo kwa ajili ya kuzuia
mmomonyoko wa ardhi na kutunza vyanzo vya maji. Vilevile, mitambo miwili (2) ya gesi asilia
inayotokana na samadi imejengwa katika vijiji vya Nandembo na Majimaji kwa
ajili ya matumizi ya kupikia na kuwashia taa.
70.
Mheshimiwa Spika, katika skimu ya umwagiliaji ya
Namatuhi iliyoko Wilaya ya Songea Vijijini, Mkandarasi anaendelea na kazi ya
ujenzi wa mifereji midogo yenye urefu wa mita 550 na mradi utakamilika
mwezi Juni, 2014. Aidha, uchimbaji wa kisima kirefu cha mita 150 na usambazaji wa maji
katika kijiji cha Mihambwe, Wilaya ya Tandahimba umekamilika. Aidha,
utekelezaji wa mradi wa kusambaza maji katika kijiji cha Mahande, Wilaya ya
Mbinga umekamilika. Kupitia mradi huo wananchi wa vijiji hivyo wamepatiwa
huduma ya maji safi na salama.
71.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu kwa kushirikiana
na taasisi nyingine itakamilisha miradi ya maji ya kijamii, kuelimisha na
kuhamasisha wadau kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji na ufungaji wa vituo vya
hali ya hewa. Jedwali Na. 4 linaonesha orodha ya miradi
inayotekelezwa katika Bonde la Mto Ruvuma.
(vi)
Bonde la Mto Songwe
72.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa
kushirikiana na Serikali ya Malawi inatekeleza Awamu ya Pili ya Programu ya
Kuendeleza Rasilimali za Bonde la Mto Songwe. Awamu hiyo inahusu usanifu wa
kina wa miundombinu ya rasilimali za maji itakayojengwa kwa ajili ya kuzalisha
umeme, kilimo cha umwagiliaji na kuzuia mafuriko. Aidha, mpango unaandaliwa
kuanzisha Kamisheni ya Pamoja ya Kusimamia Programu na kujenga uwezo kwa
watekelezaji wa programu katika ngazi za Halmashauri hadi Taifa. Hadi mwezi
Aprili 2014, Mtaalam Mshauri amekamilisha na kuwasilisha rasimu zifuatazo:-Dira ya Maendeleo ya Programu ya
Kuendeleza Rasilimali za Maji za Bonde la Mto Songwe, upembuzi yakinifu wa
miradi ya kipaumbele na tathmini ya athari za kimazingira na kijamii kuhusu
miradi itakayojengwa. Vilevile, amekamilisha rasimu ya mwisho ya mfumo wa
kitaasisi kwa ajili ya Kamisheni ya Pamoja ya Kusimamia Programu ya Mto Songwe.
Kazi hizo zinatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2015. Mkakati wa elimu na mawasiliano umekamilika na kuanza
kutekelezwa kwenye Halmashauri za Wilaya za Mbeya na Momba kwa upande wa
Tanzania, na kwa upande wa Malawi katika Wilaya za Karonga na Chitipa.
73.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, usanifu wa awali wa mabwawa matatu
(3) katika Bonde la Mto Songwe umekamilika. Lengo la kujenga
mabwawa hayo ni kwa ajili ya kudhibiti mafuriko na kuhamahama kwa mto, matumizi
ya maji majumbani, kilimo cha umwagiliaji na uzalishaji umeme. Jumla ya hekta
5,635 zinatarajiwa kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji ambapo
kwa upande wa Tanzania ni hekta 3,005 na Malawi hekta 2,630. Vilevile, megawati
175 za umeme zinatarajiwa kuzalishwa kutoka bwawa moja (Lower
Dam) litakaloanza kujengwa kati ya mabwawa hayo. Katika mwaka
2014/2015, uandaaji wa muundo wa kitaasisi, usanifu wa kina na makabrasha ya
zabuni utakamilika. Serikali itaendelea kushirikiana na Serikali ya Malawi
kuratibu utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo.
(vii)
Ziwa Tanganyika
74.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kushirikiana kwa karibu na
nchi wanachama wengine wa Mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika ambazo ni
Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia katika usimamizi na
uendelezaji wa rasilimali ya maji ya Ziwa Tanganyika. Tanzania na DRC zinamiliki kwa pamoja asilimia 86 ya Ziwa hilo. Changamoto ya kupungua kwa kina cha
maji ya Ziwa Tanganyika imeathiri sana bandari za Kigoma upande wa Tanzania na
Kalemie, Uvira na Moba zote za DRC. Aidha, chanzo cha maji kwa ajili ya mji wa
Kigoma/Ujiji kiliathirika na kulazimika kuongeza urefu wa bomba kutoka kwenye
banio (intake) umbali wa mita
60 ndani ya
ziwa. Miongoni mwa sababu zinazochangia tatizo la kupungua kwa kina cha maji ni
kubomoka kwa banio la Mto Lukuga ulioko DRC unaotoa maji kutoka Ziwa Tanganyika kupeleka Mto
Kongo.
75.
Mheshimiwa Spika, katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dr.Jakaya Mrisho Kikwete alituma ujumbe maalum mara mbili, mwezi Agosti, 2010
na Machi, 2014 kwa Rais wa DRC, Mhe. Joseph Kabila Kabange kuhusu umuhimu wa Tanzania na DRC kushirikiana (bilaterally) katika kukarabati banio la Mto Lukuga.
76.
Mheshimiwa Spika, kufuatia hatua nilizozitaja, usanifu wa kina wa
banio husika umekamilika mwezi Desemba, 2013 kwa ufadhili wa COMESA. Jumla ya Dola za Marekani milioni 65 zinahitajika kutekeleza miradi ya kudhibiti kupungua
kwa kina cha Ziwa kwa kujenga upya banio hilo. Aidha, Wizara yangu ilimwalika
Waziri wa Maji na Umeme wa DRC kuja Tanzania mwezi Aprili, 2014 kwa lengo la
kujadili namna tutakavyo washirikisha wadau wa
maendeleo ili kupata fedha za kujenga upya
banio hilo. Mkutano wetu ulikuwa wa mafanikio na
kwamba tutaunda timu ya pamoja ya Wataalam kutoka Sekta za Maji, Mazingira na
Usafirishaji kushughulikia changamoto zilizopo. Katika mwaka 2014/2015,
Serikali itajenga ushirikiano imara na nchi za DRC, Zambia na Burundi kuhifadhi
rasilimali za maji ya Bonde la Ziwa Tanganyika.
(viii) Ziwa Chala,
Ziwa Jipe na Mto Umba
77.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu
inaratibu uandaaji wa Mpango Shirikishi wa Usimamizi na Uendelezaji wa
Rasilimali za Maji katika ekolojia ya Maziwa ya Chala na Jipe; na Mto Umba.
Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Kenya na Tanzania
kuhusu utunzaji na uendelezaji wa ekolojia ya maziwa hayo ilisainiwa mwezi
Februari, 2013. Makubaliano hayo yanasisitiza kusimamia na kuendeleza
rasilimali zilizoko katika maeneo hayo ili matumizi yake yawe endelevu, ikiwa
ni pamoja na kulinda mifumo ya ekolojia kwa ustawi wa wananchi wa nchi hizo.
78.
Mheshimiwa Spika, kikao cha pamoja
kati ya Tanzania na Kenya kilifanyika Mjini Taveta mwezi Machi, 2014 na kufikia
makubaliano ya kuandaa mpango wa kitaalam wa kutumia maji ya Ziwa Chala kwa
ajili ya matumizi ya majumbani na kilimo cha umwagiliaji kwa wakazi
wanaozunguka ziwa hilo, kwa kuzingatia kuwa eneo linalozunguka ziwa hilo ni
kame. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kushirikiana na nchi ya
Kenya kutekeleza makubaliano hayo. Lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa miradi ya
kuboresha maisha ya jamii inatekelezwa, hususan miradi ya maji kwa matumizi ya
majumbani. Vilevile, kilimo cha umwagiliaji kitaanza kwa eneo dogo, hatua kwa
hatua kwa kuzingatia usawa wa maji ziwani (trend monitoring).
79.
Mheshimiwa Spika, usimamizi wa rasilimali za maji nchini unahusisha utambuzi na ufuatiliaji
wa wingi na ubora wa maji kutoka katika vyanzo vya maji. Jukumu kuu la Wizara
yangu ni kuhakiki ubora, usafi na usalama wa maji katika vyanzo vya maji
na mitandao ya usambazaji maji
vijijini na mijini kwa lengo la kulinda afya na ustawi wa wananchi. Kama
tunavyofahamu, afya ya wananchi inaweza kuathirika vibaya kama maji
yanayotumika hayakidhi viwango kutokana na kuchafuliwa na mifumo asilia au
shughuli za kibinadamu, hivyo ni muhimu kuwa na takwimu za ubora wa maji
zitakazosaidia kuweka mifumo madhubuti ya kuhifadhi na kudhibiti uchafuzi wa
vyanzo vya maji.
80.
Mheshimiwa Spika, Maabara za maji nchini zinafuatilia na kuchunguza ubora wa maji katika
vyanzo na mitandao ya usambazaji maji. Aidha, maabara hutoa ushauri wa kitaalam
kwa mamlaka za maji, vyombo vya watumiaji maji, Bodi za maji za mabonde,
taasisi na watu binafsi kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango vinavyokubalika
kwa matumizi yaliyokusudiwa. Katika mwaka 2013/2014, Wizara ilipanga kukagua
vyanzo vya maji kwa kuchunguza sampuli 8,000 za maji ili kuhakiki
ubora wake. Vilevile, sampuli 1,000 za majitaka zilipangwa kuchunguzwa kwa lengo la
kuhakiki ubora wake kabla ya kurudishwa kwenye mazingira ili kudhibiti uchafuzi
wa vyanzo vya maji na kuepusha athari za kiafya kwa wananchi na mfumo wa ekolojia.
Takwimu hizo ni muhimu katika kuandaa mikakati ya kudhibiti uchafuzi wa vyanzo
vya maji.
81.
Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Machi, 2014, sampuli 4,673 za maji zilikusanywa na
kuhakikiwa ubora wake. Kati ya hizo, sampuli 3,200 ni za maji kwa ajili ya matumizi
ya majumbani; sampuli 382 kwa matumizi ya viwandani; sampuli 712 ni za kuratibu mwenendo
wa ubora wa maji katika vyanzo (mito, chemichemi, maziwa na mabwawa); sampuli
341 za
utafiti; na sampuli 38 kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji. Jedwali Na. 5 linaonesha mwelekeo wa
sampuli za maji zilizokusanywa na kuchunguzwa ubora wake kuanzia mwaka 2009/2010 hadi Machi, 2014.
(a)
Ubora wa Maji kwa Matumizi ya Majumbani
82.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, wananchi wote wa vijijini na mijini wanatakiwa
kutumia maji safi na salama ili kulinda afya zao kwa ustawi wa maendeleo ya
kiuchumi na kijamii. Sheria ya Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Na.
12 ya mwaka 2009 inavitaka vyombo
vinavyohusika na huduma hii kuhakikisha maji yanayosambazwa yana ubora
unaokubalika. Matokeo ya uchunguzi wa sampuli 2,880 sawa na asilimia 90 yameonesha kuwa maji hayo
yalikidhi viwango vinavyokubalika. Sampuli 320, maji yake hayakukidhi viwango
kutokana na uwepo wa kiwango kikubwa cha chumvichumvi, madini-chuma (iron),
manganese na fluoride. Maji yaliyoonekana kuwa na madini-chuma na manganese, ushauri ulitolewa maji
hayo yawekwe katika hali ya kuongezewa hewa ya Oxgen (aeration) ambayo huwezesha
madini chuma kutuama kama masimbi, au kutafuta vyanzo mbadala. Kwa vyanzo vilivyobainika
kuwa na kiwango kikubwa cha madini ya fluoride, hatua zimeanza kuchukuliwa
kutafuta vyanzo mbadala vya kukidhi mahitaji pamoja na kutumia teknolojia ya
kuondoa madini ya fluoride kwenye maji ya kunywa na kupikia. Aidha, ushauri ulitolewa
wa kutumia madawa ya kutibu maji yanayokidhi viwango na kukagua mitambo ya
kusafisha maji mara kwa mara kwa kuzingatia mabadiliko ya ubora wa maji
yanayotokana na misimu ya mwaka. Jedwali Na. 6 linaonesha maeneo ambayo maji
hayakukidhi viwango vinavyokubalika.
83.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutekeleza Mpango wa Usalama wa Maji (Water Safety Plan) kwa maeneo mbalimbali nchini. Mpango huo una lengo la kuboresha shughuli za
usimamizi wa ubora wa maji kwa mamlaka za maji na vyombo vya watumiaji maji
vijijini (COWSOs) kuanzia kwenye chanzo cha maji hadi kwa mtumiaji.
(b)
Ubora wa Maji kwa Matumizi ya Viwanda
84.
Mheshimiwa Spika, shughuli za viwanda zinahitaji maji yanayokidhi viwango vya ubora kwa lengo
la kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa au kusindikwa zinakidhi viwango. Kwa
kuzingatia hilo, jumla ya sampuli 382 kutoka viwanda mbalimbali vya
kuzalisha bidhaa zilikusanywa na kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara. Kati ya
hizo, sampuli 358 zilitoka viwanda vya samaki katika Miji ya Bukoba,
Musoma, Tanga, Mafia, Mwanza na Dar es Salaam na matokeo ya uchunguzi huo
yalionesha maji kukidhi viwango vya kimataifa. Sampuli 24 kutoka viwanda vya
sukari-Kagera, saruji na Pepsi Mkoani Mbeya zilichunguzwa na matokeo kuonesha
kuwa maji yana ubora unaokubalika kwa matumizi yaliyokusudiwa.
(c)
Kuratibu Mwenendo wa Ubora wa Maji katika Vyanzo
85.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Mradi wa Hifadhi ya Mazingira
ya Ziwa Victoria (LVEMP) hufuatilia mwenendo wa ubora wa maji na udhibiti wa
ongezeko la magugu maji katika Ziwa Victoria. Hadi mwezi Machi, 2014, kwa
upande wa Tanzania ufuatiliaji (cruise monitoring) kwenye vituo 28 ulifanyika na jumla ya
sampuli 334 zilikusanywa na kuchunguzwa. Matokeo yalionesha kuwa
hali ya uwepo wa virutubisho vya nitrate na phosphorus kwenye vituo vya
pembezoni mwa ziwa bado ni mkubwa kutokana na shughuli za kibinadamu
ikilinganishwa na vituo vya katikati ya ziwa ambapo hali ya wingi wa virutubisho
inapungua. Aidha, sampuli za maji katika mabonde ya Wami-Ruvu (124), Ziwa Tanganyika (56), Ziwa Rukwa (41), Rufiji (27), Bonde la Kati (86),
Pangani
(8),
Ziwa Nyasa (8) na Pwani ya Kusini (28) zilipimwa kwa ajili ya kutoa takwimu zinazotumika katika
usimamizi wa rasilimali za maji. Matokeo yalionesha maji kutoka kwenye vyanzo
hivyo kuwa na ubora unaokubalika kwa ustawi wa viumbe hai na kuendelezwa kwa
matumizi mbalimbali.
(d)
Ubora wa Maji kwa ajili ya Umwagiliaji na Utafiti
86.
Mheshimiwa Spika, maji yanayotumika kwa ajili ya umwagiliaji yanatakiwa
kukidhi viwango vya ubora kutegemeana na aina ya udongo na aina ya mazao
yanayomwagiliwa ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao hayo. Hadi mwezi
Machi 2014, sampuli 38 za maji kwa ajili ya umwagiliaji kutoka maeneo ya
Kiloka, Mikindo (Morogoro), Mlowa, Matali (Iringa), Matiganjola, Kivavi,
Igongolo (Njombe), Litapwasi, Peramiho (Ruvuma) na Kibiti (Pwani).
zilichunguzwa na kuonesha kukidhi ubora kwa matumizi yaliyokusudiwa. Aidha,
Wizara hupima sampuli za maji kwa ajili ya shughuli za utafiti kutoka kwenye
taasisi na watu binafsi. Sampuli 341 za maji zilipokelewa na
kuchunguzwa na ushauri ulitolewa kulingana na mahitaji ya utafiti.
(e)
Ubora wa Majitaka Yanayorudishwa kwenye Mazingira
87.
Mheshimiwa Spika, moja ya sababu za uchafuzi wa
vyanzo vya maji ni majitaka yanayozalishwa viwandani na majumbani. Hadi mwezi
Machi 2014, sampuli 630 za majitaka kutoka kwenye mabwawa ya majitaka
ya Miji ya Dodoma, Morogoro, Mwanza, Dar es Salaam, Tanga na Iringa; na kutoka viwanda vya sukari, samaki, nguo, bia na tumbaku zilikusanywa na
kuchunguzwa. Kati ya hizo sampuli 120 zilichunguzwa kuangalia uwezo wa mifumo ya kusafisha
majitaka na uchunguzi wa sampuli 510
ulilenga kuhakiki ubora wa majitaka yanayorudishwa kwenye mazingira. Matokeo yalionesha kuwa asilimia 85 yana ubora usiosababisha uchafuzi wa vyanzo vya maji na ushauri wa kitaalam wa
kuboresha utendaji wa mabwawa na mitambo ya kusafisha majitaka ulitolewa kwa
taasisi husika.
88.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea itaimarisha usimamizi na
ufuatiliaji wa ubora wa maji kwenye vyanzo kwa ajili ya matumizi ya majumbani,
viwandani, kilimo na mazingira. Katika kutekeleza majukumu hayo, sampuli 8,000 za maji na sampuli 1,000 za majitaka
zitakusanywa na kuchunguzwa. Takwimu zitakazopatikana zitatumika kushauri hatua
za kuchukua kabla ya kutumia maji kutoka kwenye chanzo husika. Aidha, takwimu
hizo zitawezesha utekelezaji wa Mkakati wa Kusimamia Ubora wa Maji na Kudhibiti
Uchafuzi wa Maji (Water Quality Management and Pollution Control Strategy) ambapo moja ya shughuli zilizoainishwa ni ufuatiliaji wa mwenendo wa
kiwango cha madini tembo (heavy metals)
aina ya zebaki (mercury), arsenic, urani (uranium) na cyanide katika vyanzo vya maji kwenye maeneo ya migodi.
(f)
Ubora wa Madawa ya Kusafisha na Kutibu Maji
89.
Mheshimiwa Spika, ni wajibu wetu kuhakiki madawa ya kutibu na
kusafisha maji ili kuthibitisha ubora wake katika kupata maji safi na salama.
Jumla ya sampuli 50 za madawa ya kusafisha na
kutibu maji kutoka Morogoro, Tanga,
Chalinze na DAWASCO zilihakikiwa ubora wake. Kati
ya sampuli hizo, sampuli za shabu (Aluminium Sulphate) zilikuwa 16, sodium
bicarbonate nne (4) na Polyaluminium Chloride (15) ambazo hutumika
kusafisha maji; na Calcium Hypochlorite (15) inayotumika kuua vijidudu. Matokeo yalionesha kuwa sampuli 33 zilikuwa na viwango vinavyokubalika na ushauri wa kitaalam ulitolewa
kuhusu matumizi sahihi ya madawa hayo. Sampuli 17
ambazo ni za Calcium Hypochlorite nne (4), Aluminium Sulphate
sita (6)
na Polyaluminium Chloride saba
(7) zilibainika kuwa na viambata hafifu
visivyotosheleza kutibu maji katika kiwango kinachotakiwa. Katika mwaka
2014/2015, Wizara yangu itaendelea kuhakiki ubora wa madawa na kukagua ufanisi
wa mitambo ya kusafisha na kutibu maji pamoja na kutoa ushauri wa kitaalam kwa
vyombo vinavyotoa huduma ya majisafi vijijini na mijini.
(g)
Uondoaji wa Madini ya Fluoride katika Maji ya Kunywa na Kupikia
90.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya mwaka 2013/2014
nililielezea Bunge lako Tukufu kuwa Wizara yangu imeandaa mkakati wa usambazaji
wa teknolojia ya uondoaji madini ya fluoride
katika maji ya kunywa na kupikia kwa kutumia mkaa wa mifupa ya ng'ombe (bone char). Hadi Machi, 2014, tanuru mbili (2) zenye uwezo wa kuchoma tani nne (4) za
mifupa ya ng’ombe kwa mara moja zimejengwa na majaribio ya kubaini ufanisi wa
uchomaji katika matanuru hayo yanaendelea. Vilevile, mould kwa ajili ya kuzalisha mitambo ya kuondoa madini ya fluoride katika maji ya kunywa na kupikia kwa ngazi ya kaya imenunuliwa na
uzalishaji wa mitambo 1,000 kwa ajili ya kuisambaza
kwenye kaya za maeneo yenye vyanzo vya maji yenye kiwango kikubwa cha fluoride unaendelea kufanyika. Lengo ni kuhamasisha wananchi kutumia teknolojia
ya mkaa wa mifupa ya ng’ombe ili kuondoa madini ya fluoride katika maji ya kunywa na kupikia na hivyo kupunguza athari hasa kwa
watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
91.
Mheshimiwa Spika, mwezi Novemba 2013, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,
Mifugo na Maji ilitembelea Kituo cha Utafiti wa Fluoride kilichopo Ngurdoto
Mkoani Arusha na jamii inayotumia vifaa vya kuondolea madini hayo katika maji
ya kunywa vilivyobuniwa na kituo hicho. Lengo la ziara hiyo, lilikuwa kutoa
fursa kwa Kamati hiyo ya Bunge kutathmini utafiti unaofanyika na kupata taarifa
ya hatua iliyofikiwa ya matumizi ya teknolojia ya chengachenga za mkaa wa
mifupa ya ng’ombe (Bonechar filter media). Matumizi ya
teknolojia ya kuondoa madini ya Fluoride imetumika kwa zaidi ya miaka mitatu sasa katika ngazi
ya kaya katika kaya 22 kwenye maeneo ya Ngaramtoni (9), Kijenge (1), Leganga (1), Kiwawa (1), Ngongongare (6), Arusha Mjini (1), Njiro (2) na Olasiti (1), Mkoani Arusha. Vilevile, kwa ngazi ya jamii 11, Mkoa wa Arusha na jamii moja (1) maeneo ya Mwando, Mkoa wa Singida. Katika mwaka 2014/2015,
Serikali itaendelea na mkakati wa usambazaji wa teknolojia ya mkaa wa mifupa ya
ng’ombe na kutayarisha ramani (fluoride mapping) itakayoainisha maeneo yenye
kiwango kikubwa cha fluoride katika maji ili kuyatambua maeneo hayo wakati wa
kuibua miradi ya maji.
(h)
Maabara za Maji kupata Ithibati (Accreditation)
92.
Mheshimiwa Spika,
vigezo vinavyotumika kwa taasisi zinazohusika na vipimo na uchunguzi wa
kimaabara kutambulika kimataifa ni kupata Ithibati (Accreditation). Kupatikana kwa Ithibati kutawezesha Maabara zetu kutambulika
kimataifa na hivyo, kukidhi miongozo ya Sheria Na. 11 ya mwaka 2009 ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji, Sheria Na.12 ya mwaka 2009 ya Huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira na Sheria
Na. 20 ya mwaka 2004 ya Usimamizi wa Mazingira. Maabara
ya Maji Mwanza imekamilisha uandaaji wa mwongozo wa utendaji kazi (Quality
Manual) na kuwasilisha kwa taasisi inayosimamia shughuli
hizo kimataifa (SADCAS) kwa ajili ya kufanyiwa
tathmini. Lengo la Wizara yangu ni kuziwezesha maabara zote kukidhi vigezo vya
kupata Ithibati na hivyo kuwa na maabara zenye viwango.
93.
Mheshimiwa Spika,
hatua hiyo inawezesha maabara zetu kushiriki kwenye majaribio ya kujipima uwezo
wa utendaji kazi za kimaabara (Laboratory Performance Evaluation or
Proficiency Testing) yanayoandaliwa na taasisi za
kimataifa. Majaribio hayo hufanyika kila mwaka na kwa mwaka 2013/2014 majaribio
yaliyofanywa ni:-
(i)
Mwezi Julai 2013, Maabara saba (7) za Iringa, Mwanza, Arusha, Morogoro, Mbeya, Tanga na Maabara Kuu Dar es
Salaam zilishiriki katika jaribio la kujipima uwezo linaloratibiwa na Southern
Africa Development Community Measurement Traceability (SADCMET).
(ii) Mwezi Agosti 2013, Maabara tisa (9) za
Mwanza, Iringa, Mbeya, Tanga, Arusha, Dodoma, Mtwara, Bukoba na Maabara Kuu Dar
es Salaam zilishiriki katika jaribio la kujipima uwezo chini ya Programu ya Global
Environmental Monitoring System/Water (GEMS/Water).
Tathmini ya matokeo ya
majaribio hayo imeonesha kuwa maabara zilizoshiriki zimefanya vizuri kwa
wastani wa asilimia 65 kwa vielelezo vya kemikali na
asilimia 92 ya upimaji wa vimelea vya vijidudu (bacteria) kwenye maji. Tathmini hiyo inaonesha kuwa maabara zinaongeza ufanisi
katika utendaji kimaabara baada ya kujengewa uwezo wa kupatiwa vitendea kazi. Jedwali
Na. 7 linaonesha matokeo ya majaribio ya kujipima uwezo
wa maabara za maji kwa ajili ya kupata ithibati.
94.
Mheshimiwa Spika,
Wizara yangu inaendelea na ukarabati wa Maabara Kuu ya Wizara na maabara za
mikoa. Uboreshaji huo utaongeza ufanisi katika utendaji kazi na hivyo kutoa
huduma yenye tija zaidi. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuzijengea
uwezo maabara zake kwa kuweka mazingira mazuri kwa wataalam kufanya kazi za
uchunguzi katika hali bora na salama kama inavyoelekezwa kwenye viwango vya
kimataifa (ISO 17025).
95.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika utangulizi wa hotuba hii, Sekta
ya Maji ni moja kati ya sekta sita (6) zinazotekeleza mpango maalum wa “Tekeleza Sasa
kwa Matokeo Makubwa” (Big Results Now) ulioandaliwa na Serikali chini
ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dr. Jakaya
Mrisho Kikwete. Katika Sekta ya Maji, tathmini ya BRN juu ya hali ya huduma ya maji
vijijini iliyofanyika mwezi Februari, 2013 ilibaini hali ya upatikanaji wa
huduma ya maji kushuka kutoka asilimia 57.8 hadi kufikia asilimia 40. Sababu za kushuka kwa
huduma hiyo ni pamoja na kuharibika kwa baadhi ya miundombinu ya maji
kulikosababishwa na ukosefu wa matengenezo ya mara kwa mara ya miundombinu
hiyo. Utekelezaji wa mpango wa BRN ulioanza rasmi mwezi Julai 2013,
umeboresha kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji vijijini hadi kufikia asilimia 49 mwezi Machi 2014. Lengo
ni kufikia asilimia 74 ifikapo mwezi Juni 2016. Mpango huo unaelekeza maeneo
manne (4) ya utekelezaji ambayo ni ujenzi wa miradi mipya (new construction), ukarabati wa miradi
chakavu (rehabilitation), upanuzi wa miradi iliyopo (extension) na uendeshaji na
matengenezo (operation and maintenance).
96.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa miradi mipya unahusisha miradi ya vijiji 10 kwa kila Halmashauri
pamoja na miradi ya kimkakati (strategic projects). Miradi ya upanuzi na
ukarabati inahusisha utekelezaji wa miradi ya matokeo ya haraka kutoka kwenye
vyanzo vya mabwawa, visima virefu, vyanzo vidogo vya juu ya ardhi, miradi ya
kitaifa na miradi inayohitaji matengenezo. Aidha, uendeshaji na matengenezo unahusu kuvijengea uwezo
vyombo vya watumiaji maji na
ukusanyaji wa taarifa za utekelezaji wa miradi.
97.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inashirikiana na Ofisi ya Waziri
Mkuu–TAMISEMI kusimamia utekelezaji wa BRN kulingana na mipango na
vipaumbele kama ilivyoainishwa kwa kila Halmashauri. Katika kuhakikisha miradi
ya maji vijijini inatekelezwa kwa haraka na ufanisi, Wizara imepeleka wataalam
wazoefu katika Sekretarieti za Mikoa ili kuwajengea uwezo Wahandisi wa Mikoa na
Halmashauri. Vilevile, Wizara imeondoa vibali (No-Objection) ili kupunguza muda wa
ununuzi wa Wataalam Washauri na Wakandarasi. Hatua nyingine ni kuhusu ujenzi wa
miradi kuanza hata kama fedha zote za mradi hazijaifikia Halmashauri na hata
kama michango ya wananchi haijakamilika. Michango hiyo inatumika wakati wa
uendeshaji wa miradi baada ya ujenzi kukamilika.
98.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu ilikasimiwa shilingi
bilioni 236 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji vijijini. Aidha, kiasi kingine cha shillingi
bilioni 108 kilikasimiwa kupitia mafungu ya mikoa kwa ajili ya Halmashauri,
OWM-TAMISEMI na Wizara zinazoshiriki katika kutekeleza kampeni ya kitaifa ya
usafi wa mazingira vijijini. Hadi kufikia Machi 2014, Serikali imezipatia
Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa shilingi 137,904,598,951 kwa ajili ya
utekelezaji na usimamizi wa mradi wa maji wa vijiji 10 kwa kila Halmashauri.
Vilevile, jumla ya shilingi 10,610,746,989 zimeelekezwa kwenye miradi
mingine ya maji vijijini kama vile miradi ya yenye kuleta matokeo ya haraka,
ujenzi wa mabwawa, vijiji 100 kutoka bomba la KASHWASA, Same-Mwanga-Korogwe na
gharama za ziada za usimamizi na ufuatiliaji wa miradi. Jedwali Na. 8 linaonesha mgao wa fedha
zilizotumwa kwenye Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa.
99.
Mheshimiwa Spika, kwa kutumia fedha hizo, jumla ya miradi ya maji 248
yenye jumla ya vituo vya kuchotea maji 10,560 imejengwa kwenye Halmashauri 98 na kunufaisha vijiji
270. Juhudi hizo zimeongeza idadi ya wakazi vijijini wanaopata huduma ya maji
safi na salama kutoka wakazi 15,200,000 mwezi Juni, 2013 hadi kufikia
wakazi 17,840,000, sawa na ongezeko la wakazi 2,640,000 . Ongezeko hilo
limeboresha huduma ya upatikanaji wa maji vijijini kutoka asilimia 40 hadi kufikia asilimia
49.
Lengo la Serikali kulingana na Mpango huo, ni kuwapatia huduma ya maji wananchi
milioni 22 waishio vijijini ifikapo mwezi Juni 2014. Hata hivyo uwezekano wa kufikia
lengo hilo unaendelea kufifia kutokana na upatikanaji wa fedha mdogo.
3.2.3 Mpango wa BRN kwa mwaka 2014/2015
100.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2014/2015,
Wizara yangu imepanga kuendelea kutekeleza miradi ya maji vijijni chini ya
Mpango wa BRN. Kazi zitakazotekelezwa ni ujenzi na upanuzi wa miradi ya maji pamoja na
ukarabati wa miundombinu ya maji. Fedha zilizopangwa kutumika ni shilingi
bilioni 270.97, ambapo shilingi bilioni 166.81 ni fedha za ndani na shilingi
bilioni 104.16 ni fedha za nje. Fedha hizo zitatekeleza miradi kwenye vijiji 1,239 na itakapokamilika
itakuwa na vituo 28,031 vya kuchotea maji
vitakavyohudumia jumla ya wakazi 7,007,628 wanaoishi vijijini.
(a)
Ujenzi wa Miradi Mipya
(i)
Ujenzi wa Miradi ya Vijiji 10 kwa kila
Halmashauri
101.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inatekeleza Mradi wa Maji wa Vijiji 10
ambapo katika mwaka 2013/2014, vijiji 1,538 vilipangwa kupatiwa huduma ya
maji. Hata hivyo, wakati wa utekelezaji vijiji 17 zaidi viliongezwa na kufikia
jumla ya vijiji 1,555. Mradi huo ukikamilika, vituo 32,274 vya kuchotea maji vyenye uwezo wa
kuhudumia wananchi wapatao 8,068,500 vitakuwa vimejengwa kwenye Halmashauri
167
kati ya Halmashauri 168 nchini. Vijiji vya Halmashauri iliyobaki ya Manispaa ya
Musoma vitapata huduma ya maji kutoka katika mradi wa maji na usafi wa
mazingira unaoendelea kutekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira
Mjini Musoma.
102.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mpango huo wa vijiji 10, miradi ya maji
766 kwenye
vijiji 830 imeendelea kutekelezwa katika Halmashauri zote nchini. Hadi mwezi Machi
2014, kati ya miradi hiyo, miradi 228 kwa ajili ya vijiji 247 imekamilika. Kukamilika
kwa miradi hiyo kumeongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama
kwa wakazi 2,398,500 zaidi waishio vijijini. Aidha, miradi 538 kwenye vijiji 583 itakayokuwa na vituo
9,630
yenye uwezo wa kuhudumia watu 2,407,500 inaendelea kujengwa; mikataba
ya ujenzi wa miradi 707 kwa ajili ya vijiji 725 itakayokuwa na vituo 13,050 vyenye uwezo wa
kuhudumia watu 3,262,500 imesainiwa.
103. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015,
Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 148.12 kujenga miradi ya maji
ya vijiji 10 kwenye vijiji 725 katika Halmashauri 167 ambapo jumla ya vituo 13,050 vya kuchotea maji vinatarajiwa kujengwa vyenye
uwezo wa kuhudumia wakazi wapatao 3,262,500.
(ii) Miradi ya Kimkakati
Mradi wa Maji Masoko
104.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji Masoko unaojengwa katika Wilaya ya Rungwe
ulisimama baada ya Halmashauri kusitisha Mkataba wa Mkandarasi aliyeshindwa
kutekeleza kazi kulingana na viwango vya usanifu. Kazi za mradi huo zinahusisha
ujenzi wa banio la maji, chujio la maji, matanki matatu (3) ya kuhifadhia maji
yenye ujazo wa lita 90,000 kila moja, vituo 122 vya kuchotea maji, ununuzi wa
pampu na ulazaji wa mabomba. Mradi unalenga kunufaisha wakazi 15,158 wa vijiji 15 vya Bulongwe, Igembe, Ngaseke, Ntandabala, Lupando,
Bujesi, Lufumbi, Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifwa, Ikama, Itagata, Nsanga na
Nsyasya. Awali mradi huo ulikadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi
4,754,773,420. Gharama ya kazi zilizofanyika ni shilingi 1,713,445,750. Hata hivyo, hadi
Mkataba unasitishwa Mkandarasi huyo alikuwa amelipwa kiasi cha shilingi
1,269,851,102.
105.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha
2014/2015, Serikali itaendelea kukamilisha Mradi wa Maji wa Masoko kwa vipande
(lots) kwa kadri fedha zitakavyopatikana. Hii ni kutokana na gharama za
kukamilisha mradi huo zinazotolewa na wakandarasi kuwa mara mbili zaidi ya
gharama zilizokadiriwa kwenye usanifu wa mradi. Mradi huo utajengwa na
Halmashauri kwa kutumia Wakandarasi wadogo na ujenzi utasimamiwa na Wataalam wa
Wizara wakishirikiana na Wataalam wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mbeya na Wataalam
wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ili kuharakisha upatikanaji wa huduma ya
maji kwa wakazi wa Masoko.
106. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo
inatekeleza mradi wa Same-Mwanga-Korogwe unaolenga kupeleka maji
katika miji ya Mwanga na Same. Mchango wa BADEA wa Dola za Marekani milioni 10, OFID Dola
za Marekani milioni 12 na Serikali Dola
za Marekani milioni 13.76 zitatumika
kujenga sehemu ya mradi kutoka kwenye chanzo katika bwawa la Nyumba
ya Mungu, mtambo wa kutibu maji eneo la Njia Panda na kulaza
bomba kubwa la milimita 900 au inchi
35 hadi kwenye
matanki ya kituo cha kusukuma maji Kisangara. Tangazo la
kupata Mkandarasi kwa ajili ya kazi hiyo limetolewa tarehe 1 Mei, 2014
na Mkandarasi anategemewa kuanzia kazi mwezi Agosti, 2014.
107. 106. Mheshimiwa Spika, Mkataba wa kupata fedha (Financing Agreement) kati ya Serikali na Kuwait Fund (Dola za Marekani milioni 34), Saud Fund (Dola za Marekani milioni 25), BADEA (Dola za
Marekani milioni 12) na OFID (Dola za Marekani milioni 15) utasainiwa mwezi Septemba, 2014. Fedha hizi ni za
kujenga sehemu ya mradi kutoka Kisangara hadi Mwanga na Same kupitia kwenye
matanki mawili yenye ujazo lita
milioni 7.5
kila moja eneo la Kiverenge. Mkandarasi anategemewa
kupatikana na kuanza kazi mwezi Machi, 2015. Mradi huu
utakapokamilika utahudumia wananchi 456, 931.
108.
Mheshimiwa Spika, katika awamu ya pili, Washirika wa Maendeleo
walioahidi kutoa fedha ni Kuwait Fund Dola za Marekani milioni 34,
Saudi
Fund
Dola za Marekani milioni 25, BADEA Dola za Marekani milioni 12 na OFID Dola za Marekani milioni 15.
Fedha
hizo zinatarajiwa kupatikana mwezi Septemba, 2014 na ujenzi wa awamu ya pili
utaanza mwezi Machi, 2015.
Mradi wa Maji Vijijini katika
Mkoa wa Tabora
109.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Japan
inatekeleza mradi wa maji katika vijiji 20 kwenye Wilaya zote saba za Mkoa wa Tabora.
Mradi una awamu mbili; awamu ya kwanza ilianza mwezi Septemba, 2009 na
kukamilika mwezi Machi, 2014. Awamu ya pili imeanza kutekelezwa mwezi Aprili,
2014 na inatarajiwa kukamilika mwaka 2016. Katika awamu ya kwanza, kazi
zilizotekelezwa ni pamoja na kukarabati visima virefu na vifupi 46 vya pampu za mkono
katika Wilaya sita; kuandaa Mpango Mahsusi wa Maji Vijijini kwa Mkoa unaoanisha maeneo
ya kipaumbele ya kutekeleza miradi ya maji; kufanya upembuzi yakinifu na
usanifu wa miradi ya maji katika vijiji 20; na kuandaa makadirio ya
gharama za ujenzi pamoja na makabrasha ya zabuni.
110.
Mheshimiwa Spika, awamu ya pili ya mradi imeanza kutekelezwa mwezi Aprili,
2014 na itaendelea hadi mwaka 2016. Mradi ukikamilika utanufaisha zaidi ya
wananchi 45,000. Kampuni ya KONOIKE ya Japan imepewa kazi ya kutekeleza mradi kwa gharama ya Yeni
za Kijapan 1,560,000,000 sawa na shilingi bilioni 25. Awamu hiyo inahusisha
kazi zifuatazo:-
i.
Ujenzi wa miradi minne (4) ya usambazaji maji katika vijiji vinne (4) vya Isanga (Nzega),
Mpumbuli na Mabama (Uyui) na Kakola (Manispaa ya Tabora);
ii.
Ujenzi wa visima virefu 114 vya pampu za mkono katika Wilaya saba za Mkoa katika vijiji
vya Busomeke na Kalemela (Igunga); Isanga, Kitangili, Makomelo na Wela (Nzega);
Kasandalala, Usunga na Mpombwe (Sikonge); Mabama, Ufuluma na Mpumbuli (Uyui);
Kakola, Misha na Kalumwa (Manispaa ya Tabora); na vijiji vya Imalamakoye,
Kapilula, Kalembela, Kiloleni na Usungwa katika Wilaya ya Urambo/Kaliua; na
Mafunzo kwa Wataalam wa Maji
kuhusu uendeshaji na matengenezo ya miradi na mafunzo kwa vitendo kuhusu
matumizi ya vifaa vya utafiti wa maji chini ya ardhi.
(iii) Mradi wa Maji na usafi wa Mazingira Mkoa wa Kigoma
(Water and Sanitation Kigoma Region Project - WaSKiP)
111.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Ubelgiji imekubali kushirikiana na
Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi ya maji vijijini katika Mkoa wa
Kigoma. Miradi hiyo itaongeza upatikanaji wa maji safi na salama vijijini na inatarajiwa
kugharimu shilingi bilioni 20.6 .
Kati ya hizo shilingi bilioni 18.13
sawa na Euro milioni 8 zitatolewa
na Serikali ya Ubelgiji wakati shilingi bilioni 2.44 zitatolewa na Serikali ya Tanzania. Mradi huu
utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2014/2015. Kwa mwaka
huu wa fedha, kiasi cha shilingi milioni 90.63 ambacho kitatolewa na Serikali ya Ubelgiji
kimetengwa ili kuwezesha kufanya mapitio ya master plan ya mkoa, kutayarisha mpango wa utekelezaji, kupata
orodha ya vijiji vitakayotekelezwa (identification study) na kufanya usanifu. Ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha
2015/16.
(iv)
Miradi yenye Matokeo ya Haraka (Quickwins)
Mradi wa Maji Vijiji 100 Kandokando ya Bomba la Ziwa Victoria
hadi Kahama-Shinyanga
112.
Mheshimiwa Spika, Wizara inatekeleza Mradi wa Maji wa vijiji 100 vilivyoko kandokando ya
bomba kuu kutoka Ziwa Victoria hadi Kahama-Shinyanga. Hadi mwezi Machi, 2014
upimaji na usanifu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika vijiji 31 vilivyoko Halmashauri
za Wilaya za Msalala na Shinyanga Vijijini umekamilika. Ujenzi wa miradi katika
vijiji vinne vya Magobeko, Nyashimbi, Kakulu na Butegwa katika Halmashauri ya Wilaya ya
Msalala umeanza. Taratibu za kuwapata wakandarasi wa ujenzi wa miradi katika
vijiji vingine zinaendelea.
113.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015, Wizara itakamilisha usanifu kwenye
vijiji vingine vilivyobaki kufikia vijiji 100 na ujenzi wa miradi katika vijiji
40
utakamilika ifikapo mwezi Juni, 2015. Utekelezaji huo utagharimu kiasi cha shilingi 2,586,819,387 na matarajio ni kuwa na
vituo 664 vya kuchotea maji vitakavyohudumia zaidi ya wananchi 115,430. Jedwali Na. 9 linaonesha utekelezaji wa miradi
ya maji katika vijiji 40 kandokando ya bomba kuu la maji toka Ziwa Victoria
hadi Kahama-Shinyanga.
Mradi wa Maji Bungu
114.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali kwa kushirikiana na
Shirika la World Vision iliendelea na kazi za upanuzi na ukarabati wa mradi wa
maji wa Bungu katika Wilaya ya Korogwe. Hadi mwezi Machi, 2014, jumla ya vituo
22 vya
kuchotea maji vimejengwa na kukarabatiwa katika vijiji vya Bungu, Manka na
Msasa ambapo wakazi 6,909 wanapata huduma ya
maji. Vilevile, bomba kuu lenye urefu wa
kilomita 10.4 kutoka chanzo cha
maji kilichopo Sakare hadi kitongoji cha Sinai limejengwa; na mtandao wa
kusambaza maji kutoka tanki la Gare hadi kijiji cha Msasa wenye urefu wa kilomita
4 umekamilika. Aidha, mtandao wa
kusambaza maji katika kijiji cha Manka wenye urefu wa kilomita 6 umekamilika na matanki mawili yenye ujazo wa lita 90,000 kila moja yamejengwa katika vijiji vya Manka na
Gare.
115.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi huo utaendelea katika mwaka wa fedha
wa 2014/2015 ambapo tanki lenye ujazo wa lita 90,000 litajengwa katika
kijiji cha Sinai na mtandao wa mabomba utajengwa katika vijiji vya Bungu-Msiga,
Ngulu, Kwemshai na Mlungui. Mradi huo utakapokamilika jumla ya wakazi 18,460 wa vijiji saba (7) vilivyokusudiwa vya Bungu, Bungu Msiga, Kwamshai, Ngulu, Mlungui, Msasa
na Manka watanufaika na huduma ya maji safi na salama.
Mradi wa Ntomoko katika
Halmashauri za Kondoa na Chemba
116.
Mheshimiwa Spika, kati ya
vijiji 18 vinavyohudumiwa na
mradi wa maji wa Ntomoko, ujenzi wa miundombinu katika vijiji vinne (4) vya Jenjeluse, Goima, Mtakuja na Mlongia upo katika
hatua mbalimbali za utekelezaji ambazo ni asilimia 88 kwa kijiji cha Jenjeluse, Goima asilimia 62, Mtakuja asilimia 8 na Mlongia asilimia 20. Wakandarasi kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu
ya maji katika vijiji 10 vya
Makirinya, Kirere cha Ng’ombe, Lusangi, Hamai, Songolo, Madaha, Churuku,
Kimkima, Jinjo na Jangalo wamepatikana na utafiti kwa ajili ya kuchimba visima
katika vijiji vya Igunga, Itolwa, Mapango na Chandama umekamilika. Halmashauri
husika zimekubaliana kuwa mikataba iliyoingiwa na Wilaya mama ya Kondoa
ihamishiwe Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ili kuongeza ufanisi wa usimamizi.
Mradi wa Chiwambo
117.
Mheshimiwa Spika, huduma ya maji katika mradi wa Chiwambo, Wilaya ya
Masasi imekuwa duni kutokana na kuchakaa kwa miundombinu. Katika kuboresha
huduma ya maji kwenye maeneo hayo, Wizara inakarabati miundombinu ya maji
ikihusisha ulazaji wa bomba kuu la kilomita 11 kutoka kwenye chanzo cha maji
cha chemchemi ya Lulindi hadi kwenye matanki ya kijiji cha Nagaga, kukarabati
bomba lenye kipenyo cha milimita 110 kutoka Nagaga hadi Chiungutwa
umbali wa kilomita 16 na kukarabati bomba lenye kipenyo cha milimita 110 kutoka Nagaga hadi
Mitesa umbali wa kilomita 10. Vilevile, ukarabati na upanuzi wa mradi huo
unahusisha ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 50, ujenzi wa matanki 10 ya kuhifadhi maji na
vituo 78 vya kuchotea maji. Kukamilika kwa mradi huu kutanufaisha wakazi wapato 32,570 wanaoishi katika kata
saba za Lulindi, Mbuyuni, Namalenga, Nachungutwa, Sindano, Mchauru na
Lupumbulu.
118.
Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Machi 2014, kazi ya kulaza bomba kuu la kilomita
11
kutoka kwenye chanzo cha maji hadi kwenye matanki ya Nagaga umefikia kilomita
9.7.
Aidha, bomba la milimita 200 limelazwa umbali wa kilomita mbili kutoka kwenye chanzo
hadi matanki ya Nagaga ili kuongeza wingi wa maji katika eneo la mradi. Bomba
la milimita 110 la urefu wa kilomita mbili limelazwa kutoka Nagaga kwenda Chiungutwa na
kutoka Nagaga kwenda Mitesa limelazwa kwa umbali wa kilomita 1.5. Ujenzi wa matanki mawili kwenye eneo la mradi
umeanza na ukarabati wa matanki manne unaendelea. Vituo 11 vya kuchotea maji
vimejengwa. Mikataba kwa ajili ya kazi za ujenzi wa miundombinu ya kusambaza
maji kwenye vijiji vyote vya mradi huo imesainiwa.
(v) Usambazaji wa Maji
kutoka kwenye Mabwawa na Miradi ya Matokeo ya Haraka
119.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, jumla ya shilingi bilioni 45.74 zitatumika kwa ajili ya
kuendelea kutekeleza miradi inayotarajiwa kuleta matokeo ya haraka. Miradi hiyo
itahusisha ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji kutoka kwenye
mabwawa, visima virefu na vyanzo vingine vinavyoweza kusambaza maji kwenye
vijiji zaidi ya kimoja. Katika miradi hiyo, jumla ya vituo 4,808 vya kuchotea maji
vitajengwa kwa ajili ya kuhudumia wananchi 1,253,101.
120.
Mheshimiwa Spika, kati ya shilingi bilioni 45.74 kiasi cha shilingi
bilioni 10.18 zitatumika upande wa usambazaji maji kutoka kwenye mabwawa kwenye vijiji
30
vitakavyokuwa na vituo vya kuchotea maji 993 vyenye uwezo wa kuhudumia watu 257,166. Mradi utatumia vyanzo
vya maji kutoka mabwawa 10 ya Mti Mmoja
(Monduli), Looderkes (Simanjiro), Salama Kati (Bunda), Nyambori (Rorya), Kawa
(Nkasi), Mihama (Nzega), Ulyanyama (Sikonge), Kwa Maligwa (Kilindi), Masuguru
(Bagamoyo) na Nkoma (Itilima). Aidha, shilingi bilioni 35.56 zilizobaki zitatumika kutekeleza miradi yenye kuleta
matokeo ya haraka iliyoainishwa kwa kutumia vyanzo vingine vya maji ikiwa ni
visima virefu na vyanzo vya juu ya ardhi. Katika mwaka 2014/2015, Wizara
itaendelea kushirikiana na OWM-TAMISEMI katika kujenga uwezo wa Halmashauri na
Sekretarieti za Mikoa ili kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo. (Majedwali
Na. 10.1 na 10.2) yanaonesha mchanganuo wa fedha zilizopangwa kutumwa kwenye Halmashauri na
Sekretarieti za Mikoa kwa mwaka 2014/2015.
(vi)
Ukarabati na Upanuzi wa Miradi ya Kitaifa
121.
Mheshimiwa Spika, Mpango wa BRN umeainisha miradi mitatu ya
kitaifa itakayokarabatiwa na kupanuliwa mifumo ya usambazaji kwa kipindi cha
miaka mitatu. Miradi itakayohusika ni:-
i.
Mradi wa kitaifa wa Makonde ambao utahusisha vijiji vya Wilaya za Newala,
Tandahimba na Mtwara Vijijini;
ii.
Mradi wa maji wa Wanging’ombe utakaohusisha uunganishaji wa vijiji vilivyo
kandokando ya bomba kuu hadi Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya; na
iii.
Handeni Trunk Main (HTM) utakaohusisha Wilaya za Handeni, Korogwe na
Kilindi.
Katika mwaka 2014/2015
Serikali itatumia kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya upanuzi na
ukarabati wa miradi hiyo. Kati ya fedha hizo, mradi wa maji wa Makonde umepangiwa
shilingi milioni 800, Wanging’ombe shilingi milioni 300 na HTM shilingi
milioni 500.
122.
Mheshimiwa Spika, ili miradi ya maji iwe endelevu na kutoa huduma iliyokusudiwa, Serikali
imeweka taratibu zitakazohakikisha kuwa miradi hiyo inakuwa endelevu ikiwa ni
pamoja na kuunda wa Vyombo vya Watumiaji Maji (COWSOs), kuongeza idadi ya
wataalam kwenye miradi, na kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa skimu za miradi ya
maji.
3.2.4
Ujenzi wa Miradi Mingine ya Maji
Vijijini
123.
Mheshimiwa Spika, Serikali inashirikiana na mashirika na taasisi zisizo
za kiserikali kujenga miradi ya maji katika juhudi za kuboresha na kuongeza
upatikanaji wa huduma ya maji vijijini.
(i) Uvunaji wa Maji ya
Mvua
124.
Mheshimiwa Spika, uvunaji wa maji ya mvua ni muhimu sana kwa nchi
yetu kutokana na hali duni ya upatikanaji wa maji hasa maeneo kame ya vijijini.
Halmashauri zinatekeleza agizo
la Serikali la kuandaa mpango wa miaka mitano na kutunga sheria ndogo
zinazohakikisha kuwa michoro ya nyumba zote zinazojengwa zinajumuisha mifumo ya
miundombinu ya kuvuna maji ya mvua kabla ya kuidhinishwa ujenzi wake. Hadi
mwezi Machi, 2014 Serikali kupitia Halmashauri imejenga jumla ya matanki 675 ya uvunaji wa maji kwenye maeneo mbalimbali
zikiwemo taasisi kama shule, zahanati na taasisi nyingine.
(ii) Ujenzi wa Mabwawa
125.
Mheshimiwa Spika, yapo maeneo hapa nchini yenye ukame na kutokuwa na
vyanzo vya maji vya uhakika juu ya ardhi na visima vingi vilivyochimbwa kukosa
maji. Aidha, maeneo mengine yana vyanzo vyenye uwezo mdogo sana wa kutoa maji.
Hali hiyo imeilazimu Wizara kujenga na kukarabati mabwawa kwenye maeneo hayo
ili kuwapatia wananchi huduma endelevu ya maji. Ujenzi huu unahusu mabwawa ya:-
(a)
Bwawa la
Sasajila
126.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa bwawa
la Sasajila lililopo wilayani Chamwino, mkoa wa Dodoma ulisimama kutokana na
Mkandarasi wa awali kuondoka eneo la mradi kinyume na Mkataba. Kwa sababu hiyo,
Wizara imeajiri Mkandarasi mwingine ambaye ameanza kazi mwezi Novemba, 2013. Hadi mwezi
Machi, 2014 ujenzi wa bwawa umefikia asilimia 62.5. Katika mwaka 2014/2015, kazi za
ujenzi zilizobaki zitakamilishwa.
(b)
Bwawa la Iguluba
127.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa bwawa la Iguluba, Halmashauri ya Wilaya ya
Iringa Vijijini, ulikamilika kulingana na kazi zilizoainishwa kwenye Mkataba.
Hata hivyo, ukaguzi uliofanyika ulibaini ongezeko la kazi ambazo hazikuwemo
kwenye mkataba huo. Kazi ambazo hazijakamilika ni kujenga crest weir, miundombinu ya mawe
kuzuia mmomonyoko wa udongo; kupanda nyasi upande wa nje wa tuta na kupanga
mawe upande wa ndani wa tuta, ujenzi wa miundombinu ya kutolea maji kwenye
bwawa na ujenzi wa sand traps 3 za kupokea mchanga na kuondoa
mchanga ndani ya Bwawa. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itakamilisha kazi za
ziada zilizojitokeza.
(c)
Mabwawa ya Habiya, Seke
Ididi na Matwiga
128.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza kutekeleza ujenzi wa mabwawa ya Habiya (Itilima, Simiyu), Seke
Ididi (Kishapu, Shinyanga) na Matwiga (Chunya, Mbeya) ambayo ujenzi wake ulisimama
baada ya Wakandarasi husika kushindwa kazi na kuondoka kwenye maeneo ya miradi.
Hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kusitisha mikataba ya
Wakandarasi hao baada ya kwenda kinyume na mikataba. Wakala wa Uchimbaji Visima
na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) ameteuliwa kukamilisha ujenzi wa mabwawa hayo. Mikataba
ya kukamilisha ujenzi wa mabwawa hayo imesainiwa tarehe 28.2.2014 na ujenzi utaanza mwezi Juni, 2014 baada ya
msimu wa mvua.
(d)
Bwawa la Kawa
129.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Bwawa
la Kawa (Nkasi, Rukwa) umefikia asilimia
95. Mkandarasi aliyekuwa akiendelea
na ujenzi wa bwawa hilo aliondoka eneo la mradi. Aidha, Wizara imeajiri
Mkandarasi mwingine kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji kutoka katika
bwawa kupeleka maji katika vijiji vya
Nkundi, Kalundi na Fyengerezya. Ujenzi wa mradi huo umesimama kwa muda ili kupisha
usanifu wa kituo cha kutibu maji. Hadi mwezi Machi, 2014 ujenzi wa miundombinu
hiyo ulikuwa umefikia asilimia 20. Vilevile, Wizara inajadiliana na Mkandarasi huyo
ili akamilishe kazi ya ujenzi wa bwawa zilizoachwa na Mkandarasi wa awali.
Mradi huo ukikamilika jumla ya wananchi 13,500 watanufaika na huduma ya maji.
(e)
Bwawa la Wegero
130.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Bwawa la
Wegero (Butiama, Mara) ulikamilika mwaka 2010 kwa mujibu wa mkataba wa awali.
Hata hivyo kuongezeka kwa shughuli za kijamii hasa kilimo katika eneo
linalozunguka bwawa kumesababisha bwawa hilo kujaa tope katika muda mfupi na
kushindwa kutumika ipasavyo. Wizara ilifanya upimaji mwezi Novemba, 2013, na
kuonekana kuwa bwawa linaweza kufanyiwa ukarabati ili kuongeza wingi wa maji
kwa mita za ujazo 32,000. Kazi hiyo zitafanyika katika mwaka wa fedha
2014/2015.
(f)
Bwawa la Mwanjoro
131.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa bwawa la Mwanjoro (Meatu, Simiyu)
umekamilika kwa asilimia 78. Ujenzi
huo kwa sasa umesimama baada ya Mkandarasi kuondoka eneo la kazi kinyume na
Mkataba. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaajiri Mkandarasi mwingine ili
kukamilisha kazi zilizobaki.
(g)
Bwawa la Kidete
132. Mheshimiwa Spika, Bwawa la Kidete (Kilosa, Morogoro) lilijengwa
kabla ya Uhuru kwa lengo la kuthibiti mafuriko kwenye eneo la Reli ya Kati.
Bwawa hilo lilibomoka kutokana na mafuriko ya mwaka 2003, hivyo kuilazimu
Serikali kulijenga upya. Gharama ya ujenzi ilikadiriwa kuwa shilingi bilioni
4.48.
Ujenzi umesimama kutokana na matatizo ya
kimkataba ambayo yanashughulikiwa ili ujenzi uweze kukamilishwa katika mwaka
2014/2015.
3.2.5
Uendeshaji na Matengenezo
133.
Mheshimiwa Spika, ili kupata takwimu sahihi zinazohusiana na huduma ya maji
vijijini, Wizara yangu imetekeleza mradi wa kuainisha vituo vya kuchotea maji
vijijini unaotumia mfumo wa kompyuta. Kuainishwa kwa vituo hivyo kumewezesha
kufahamika kwa usahihi zaidi takwimu za uendeshaji wa miundombinu na kuandaa
ramani za vituo vya maji (water point mapping). Takwimu zilizopatikana
zinawezesha Halmashauri kufahamu hali ya upatikanaji wa maji katika vijiji.
134.
Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Machi, 2014 takwimu za vituo 88,913 vya kuchotea maji katika
Halmashauri 168 zimekusanywa. Aidha, Wizara imetoa mafunzo maalum ya utumiaji
wa vifaa kwa ajili ya kutoa na kuboresha taarifa (data up-dating) ya vituo vya kuchotea
maji kwa wahandisi wote wa Sekretarieti za mikoa; na wahandisi wa maji wa
Wilaya, mafundi sanifu na wasajili wa vyombo vya watumia maji wa Halmashauri
zote nchini. Mafunzo hayo yalitolewa kwenye vituo vinne (4) vya Moshi, Mbeya,
Mwanza na Morogoro na kukamilika mwezi Aprili 2014. Katika mwaka 2014/2015,
Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri zote za Wilaya itaendelea
kuboresha mfumo wa ukusanyaji takwimu kwa kutoa mafunzo, kununua vifaa na
matumizi ya teknolojia mpya kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa taarifa
sahihi na kwa wakati.
(ii) Uundaji na Usajili wa Vyombo vya Watumiaji Maji
135. Mheshimiwa Spika, kulingana na Kifungu Na. 31 cha Sheria Na. 12 ya mwaka 2009 ya
Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, Halmashauri zinaelekezwa kusajili
vyombo vya watumiaji maji (COWSOs)
ili kuhakikisha kuwa uendeshaji na usimamizi wa miradi ya maji unafanyika kwa
mujibu wa sheria. Wizara yangu, imetoa miongozo ya usajili ikiwemo uteuzi wa
Wasajili katika Halmashauri na namna vyombo vitakavyoendeshwa. Kupitia sheria
na miongozo hiyo, wananchi wanawajibika kuunda vyombo hivyo na kuvisajili
rasmi.
136.
Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Machi, 2014,
idadi ya vyombo vya watumiaji maji vilivyosajiliwa kisheria imefikia 373 kutoka vyombo 147 ya mwaka uliopita. Aidha, Wizara yangu imetoa mafunzo
mbalimbali kwa Halmashauri kwa ajili ya vyombo hivyo ikiwa ni pamoja na mafunzo
ya uendeshaji, utunzaji wa fedha, matengenezo madogo madogo ya mradi na njia
mbalimbali za utoaji wa taarifa za maendeleo ya mradi. Katika mwaka 2014/2015,
Serikali itaendelea kutoa mafunzo, kuhimiza uundwaji zaidi wa vyombo vya
watumiaji maji na kusisitiza wasajili kuongeza kasi ya usajili kwa miradi
iliyopo na mingine itakayojengwa. Vilevile, Halmashauri zinatakiwa ziandae
mipango kazi ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kuanzisha na kusajili vyombo na
kutoa taarifa ya utekelezaji wa mipango hiyo kila robo mwaka.
3.3 HUDUMA YA MAJISAFI NA USAFI WA MAZINGIRA MIJINI
137.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali, ilitekeleza Programu ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mijini
kujenga,kukarabati na kupanua mifumo ya majisafi na majitaka pamoja na
kuzijengea uwezo Mamlaka za maji mijini. Lengo la utekelezaji huo ni kuwapatia
wananchi wengi zaidi huduma nzuri katika Jiji la Dar es Salaam, miji mikuu ya
mikoa, miji mikuu ya wilaya, miji midogo, na miradi ya maji ya kitaifa.
3.3.1 Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mijini
(a) Miradi ya Maji ya
Kukidhi Mahitaji ya Muda wa Kati katika Miji Saba
138.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la
Ufaransa (AFD), Serikali ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya inatekeleza miradi ya kukidhi
mahitaji ya maji katika miji saba ya Bukoba, Musoma, Lindi, Kigoma, Sumbawanga,
Mtwara na Babati.
139.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa miradi ya Majisafi na Usafi wa Mazingira
katika Manispaa za Musoma na Bukoba unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na
Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) unaendelea. Hadi mwezi Machi,
2014 utekelezaji wa miradi hiyo ambayo inagharimu kiasi cha Shilingi bilioni 68.2 umefikia asilimia 50 kwa Manispaa ya Musoma na asilimia 40 kwa Bukoba. Kazi
zinazotekelezwa ni kujenga mitambo ya kusafisha na kusukuma maji pamoja na
kulaza mabomba ya usambazaji wa maji katika miji hiyo. Miradi hiyo inatarajiwa
kukamilika mwezi Desemba, 2014.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa
kushirikiana na Serikali ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya imeanza
utekelezaji wa miradi katika Miji ya Lindi, Kigoma na Sumbawanga yenye gharama
ya Euro milioni 62.59. Wakandarasi wanaendelea na ujenzi wa miradi hiyo na
wanatazamiwa kukamilisha kazi mwezi Aprili, 2015. Utekelezaji wa miradi hiyo
unahusu uchimbaji wa visima, ujenzi wa mabanio, ujenzi wa matanki, ulazaji wa
bomba kuu na mabomba ya usambazaji, ujenzi wa chujio na ujenzi wa vituo vya
kuchotea maji.
140.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali ya Ujerumani kupitia KfW ilitenga Euro milioni 8.72 kwa ajili ya ujenzi wa
mradi wa majisafi na usafi wa mazingira katika Miji ya Mtwara na Babati chini ya programu ya Millenium
Development Goal Initiative (MDGI-EU). Kufuatia kumalizika kwa upembuzi yakinifu
imebainika kuwa fedha hizo hazitatosha kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo.
Wizara yangu inakamilisha taratibu za kumtafuta Mtaalam Mshauri kwa ajili ya
usimamizi wa utekelezaji wa Mradi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa miji hiyo ambaye
ataainisha kazi ambazo zitafanyika kulingana na kiasi cha fedha kilichopo huku
Serikali ikiendelea na kutafuta jibu la muda mrefu katika Miji hiyo.
(b) Miradi ya Maji ya
Kukidhi Mahitaji ya Muda Mrefu
(i)
Mradi wa Maji Tabora
141.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu ilitekeleza mradi wa
ukarabati wa miundombinu ya maji na
maboresho ya kituo cha maji cha Igombe Mjini Tabora kwa gharama ya Dola za Marekani
milioni 4.84. Mradi huo unatekelezwa kwa kushirikiana na Serikali ya Uswisi kupitia Shirika lake
la Maendeleo (SECO). Hadi mwezi Machi, 2014, mradi umekamilika kwa asilimia
96 na
unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa ifikapo mwezi Juni, 2014. Aidha, ukarabati na upanuzi wa chujio la maji katika kituo
cha Igombe Mjini Tabora unaogharamiwa na Mfuko wa Pamoja wa Sekta ya Maji unaendelea
kwa kufunga pampu kubwa mpya tatu na kulaza bomba kuu la urefu wa mita 240 kutoka bwawani hadi kwenye chujio. Mradi huo
unatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2015. Kukamilika kwa mradi huo
kutawapatia wakazi wa Manispaa ya Tabora Maji ya kutosha hadi mwaka 2032.
(ii)
Mradi wa Maji Mjini Dodoma
142.
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha kiwango cha upatikanaji wa huduma ya
majisafi na usafi wa mazingira katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Wizara yangu
inatekeleza mradi wa ujenzi wa kuongeza majisafi. Mradi huo unahusisha ujenzi
wa kituo cha kusukuma majisafi kwenda Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na ujenzi wa matanki matatu (3) ya ujazo wa lita milioni
12.
Aidha, mradi wa ujenzi wa mfumo wa uondoaji majitaka unaogharimu shilingi bilioni 27.7 unaendelea. Mradi huo
unajumuisha ujenzi wa mtandao wa kukusanya majitaka wenye urefu wa kilomita
32 na
ujenzi wa mabwawa ya kutibu majitaka.
Hadi mwezi Machi, 2014 utekelezaji wa kazi za mradi wote umefikia asilimia
54, na
unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2014. Kukamilika kwa mradi huo kutaondoa
kero ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na kufurika kwa majitaka katika
maeneo mbalimbali ya chuo.
143.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea na juhudi za kuwapatia wananchi
wa Manispaa ya Dodoma majisafi na salama kwa kuendeleza Mradi ulioanza mwezi
Desemba 2012, unaotekelezwa kwa kushirikiana na Serikali ya Korea Kusini kwa
gharama ya shilingi bilioni 49.62. Hadi mwezi Machi 2014, visima 15 vimekarabatiwa kati ya visima
21 vilivyopangwa
na visima vipya viwili (2) vimechimbwa kati ya visima vitatu (3). Kwa ujumla utekelezaji
wa
mradi umefikia asilimia 35. Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Januari, 2015 na utaongeza kiwango cha
utoaji huduma kutoka asilimia 87 hadi kufikia asilimia 90.
144.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na mahitaji makubwa ya maji yanayotokana na ongezeko la
watu pamoja na shughuli za kiuchumi na kijamii katika Manispaa ya Dodoma,
Serikali imeajiri Mtaalam Mshauri kwa ajili ya kusanifu Bwawa la Farkwa na
tayari amewasilisha taarifa ya awali ya usanifu (interim report I) imewasilishwa na
anaendelea na usanifu. Pia, bwawa hilo litakuwa chanzo cha maji kwa Miji ya Kondoa, Chamwino, Chemba na
Bahi ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya maji katika miji hiyo. Gharama za
usanifu wa bwawa hilo ni shilingi bilioni 1.6. Usanifu huo unaotarajiwa
kukamilika mwezi Desemba, 2014 utaonesha gharama halisi za ujenzi wa bwawa hilo
pamoja na kiwango cha maji kitakachopatikana.
(iii)
Mradi wa Maji Jijini Arusha
145.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeanza kutekeleza mradi
wa kuboresha huduma ya majisafi katika Jiji la Arusha. Utekelezaji huo unahusu
uchimbaji wa kisima kirefu na ujenzi wa
tanki la maji katika maeneo ya kata ya Moshono. Hadi mwezi Machi 2014, uchimbaji wa
kisima umefikia asilimia 75 na kinatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2014. Ujenzi wa
tanki lenye ujazo wa lita milioni 2.5 umeanza na unatarajiwa kujengwa
na kukamilika mwezi Desemba, 2014. Mradi
huo utakapokamilika utahudumia wakazi wapatao 28,124 wa Kata za Moshono na Engutoto.
(iv)
Mradi wa Maji Mjini Singida
146.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya
Kiarabu (BADEA) pamoja na Mfuko wa Maendeleo wa Nchi zinazozalisha Mafuta (OPEC Fund
for International Development-OFID) ilikamilisha ujenzi wa mradi wa uboreshaji wa
miundombinu ya majisafi Mjini Singida. Ujenzi huo ulihusu uchimbaji wa visima
virefu 10, kati ya hivyo visima saba (7) vilikamilika na tayari vinatumika katika maeneo ya
Mwankoko viwili (2) na Irao vitano (5). Visima vitatu (3) kati ya 10 havikuwa na maji ya
kutosha. Aidha, kazi za ujenzi wa matanki mawili (2) katika maeneo ya Airport; kulaza bomba kuu la
maji hadi kwenye matanki; na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji katika eneo
la Mandewa zilikamilika. Mradi huo uligharimu shilingi bilioni 32.53. Kukamilika kwa mradi
huo kumeongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 8 kwa siku kwa sasa hadi
kufikia lita milioni 17.76 na utakidhi asilimia 100 ya mahitaji ya wakazi wa Mji wa
Singida.
(v)
Mradi wa Maji Morogoro Mjini
147.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi wa kupanua na kuboresha upatikanaji
wa majisafi katika Manispaa ya Morogoro unaendelea. Hadi mwezi Machi 2014, kazi
zilizotekelezwa ni pamoja na kukarabati matanki matatu (3), ulazaji wa bomba kuu
la maji la urefu wa kilomita 1.8, kupanua chujio la maji la Mafiga na kujenga mtambo
wa kusafisha maji wa Mambogo. Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 92 na unatarajiwa
kukamilika mwezi Juni, 2014. Mradi huo unatekelezwa na Serikali kwa
kushirikiana na Shirika la MCC la Marekani na utagharimu shilingi bilioni 10. Kukamilika kwa mradi
huo kutaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 23 kwa siku za sasa hadi
lita milioni 33.
(vi)
Mradi wa Maji Songea Mjini
148.
Mheshimiwa Spika, kazi ya ukarabati wa chanzo cha Mto Ruhira, Mjini
Songea imeanza mwezi Aprili, 2014. Kazi hiyo ni kujenga banio la maji (weir) ili kukabiliana na
upungufu wa maji wakati wa kiangazi. Gharama ya kukamilisha mradi ni Shilingi bilioni 2.6. Katika mwaka 2014/2015, Wizara
yangu itaendelea na utekelezaji wa mradi huo ambao utakapokamilika unatarajiwa
kuongeza uhifadhi wa maji kutoka lita milioni 3.4 za sasa hadi kufikia lita milioni
6.5 wakati
wa kiangazi.
(vii)
Mradi wa Kutoa Maji Mto Ruvuma Kupeleka Mtwara-Mikindani
149.
Mheshimiwa Spika, Kutokana na ongezeko la shughuli za kiuchumi katika
Manispaa ya Mtwara, Serikali inaendelea kutafuta vyanzo vingine
vitakavyohudumia Manispaa hiyo. Katika mwaka 2013/2014 Serikali illingia
mkataba na Mhandisi Mshauri kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi
mpya wa kutoa maji mto Ruvuma kwenda Manispaa ya Mtwara na vijiji vitakavyopitiwa
na bomba kuu. Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2014 na ujenzi
utaanza mwaka wa fedha 2014/2015 ambapo Serikali imetenga shilingi milioni 800
kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huu.
(viii)
Mradi wa Maji katika Miji ya Geita, Sengerema na Nansio
150.
Mheshimiwa Spika, awamu ya pili ya Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa
Ziwa Victoria (LVWATSAN II) unatekelezwa katika miji 15 iliyoko kwenye nchi tano (5) za Jumuiya ya Afrika
Mashariki kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Kwa upande wa nchi
yetu mradi unatekelezwa katika Miji ya Geita, Sengerema na Nansio kwa gharama
ya Dola za Marekani milioni 30.4 na unasimamiwa na Mamlaka ya
Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA).
151.
Mheshimiwa Spika, kazi zinazoendelea kutekelezwa ni za vipindi vya muda
mfupi na muda mrefu ambazo ni kujenga na kuboresha miundombinu ya majisafi,
mifumo ya utoaji wa huduma ya usafi wa mazingira, mitaro ya maji ya mvua na
kuzijengea uwezo Mamlaka za maji za Miji ya Geita, Sengerema na Nansio. Mtaalam
Mshauri wa kusanifu na kusimamia kazi za ujenzi wa mradi huo amewasilisha
taarifa ya usanifu wa mradi.
152.
Mheshimiwa Spika, kazi ambazo tayari zimetekelezwa chini ya mpango wa muda
mfupi ni ununuzi wa magari matano (5) na kugawiwa kwa mamlaka za maji
za Geita (1), Sengerema (1), Nansio (1) na kwa MWAUWASA (2); ununuzi wa pikipiki nane
(8) kwa
Geita (3), Sengerema (3) na Nansio (2); ununuzi wa trekta na tela zake
tisa (9) kwa Geita (3), Sengerema (3) na Nansio (3); Ununuzi wa magari
makubwa ya majitaka matano (5) kwa Geita (2), Sengerema (2) na Nansio (1); na ununuzi wa magari
madogo ya majitaka matatu (3) kwa Geita (1), Sengerema (1) na Nansio (1). Aidha, mamlaka hizo
zimegawiwa vifaa vya kukusanyia taka ngumu vikiwemo kontena na toroli, Geita (40), Sengerema (37) na Nansio (27). Mkandarasi wa ujenzi
wa miundombinu ya maji amepatikana na Mikataba ya ujenzi wa miradi hiyo
itasainiwa kabla ya mwezi Agosti, 2014 na ujenzi utakamilika mwezi Desemba,
2015.
(ix)
Mradi wa Maji
kutoka Ziwa Victoria Unaotekelezwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) kwa Kushirikiana na Serikali
153.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kushirikiana na Mgodi
wa Dhahabu wa Geita (Geita Gold Mining Limited – GGML) wamekamilisha kazi ya
ujenzi wa chanzo, chujio la maji, kulaza bomba kuu na tanki moja lenye ujazo wa
lita milioni 1.2 kwa gharama za Dola za Marekani milioni 5.4, fedha ambazo zimetolewa na GGML. Katika mwaka
2014/2015, kazi ya ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji itatekelezwa na mradi utagharimu kiasi cha Dola za Marekani
milioni 1.4 kati ya hizo mchango wa
Serikali ni Dola za Marekani 400,000 na GGML ni Dola za Marekani
milioni 1. Maandalizi ya Hati ya
Makubaliano (Limited Distribution Network Agreement) kati ya Wizara yangu, GGML, Halmashauri ya Geita
na Mamlaka ya Majisafi Geita yapo kwenye hatua za mwisho na inatarajiwa
kusainiwa baada ya ridhaa ya Mwanasheria Mkuu. Mradi huo utakapokamilika utazalisha lita milioni
4.8 za
maji kwa siku na kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 3.5 hadi asilimia 40. Aidha mwaka wa fedha
2014/2015 Serikali imetenga Shilingi billioni 2.5 kwa ajili ya kupanua mtandao
wa usambazaji maji katika mji wa Geita.
154.
Mheshimiwa Spika, mradi wa maji ya mtiririko wa Ihako unaofadhiliwa na UN
HABITAT kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliibuliwa
kutokana na uhaba wa maji uliokuwepo katika miji ya Muleba na Mutukula. Kwa
upande wa Muleba, mradi umelengwa kutekelezwa katika awamu mbili. Awamu ya
Kwanza ulihusisha ujenzi wa chanzo cha Ihako chenye uwezo wa kuzalisha maji lita
544,000 kwa siku; tanki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 680,000; ulazaji wa bomba kuu
lenye urefu wa kilomita 10.1; na ujenzi wa vituo 19 vya kuchotea maji. Awamu ya kwanza ya
utekelezaji wa mradi huo umekamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 1.39.
155.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015. Wizara yangu itakamilisha
utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huu kwa kulaza mabomba ya usambazaji maji
yenye urefu wa kilomita 21.5; uchimbaji wa kisima kirefu na kufunga pampu.
Mradi huo ukikamilika utahudumia zaidi ya wakazi 29,000 ambapo kwa sasa mradi
unahudumia wakazi wapatao 11,563 na kati ya hao wakazi 10,063 ni wa mji wa Muleba na 1,500 ni wa vijiji vya Bwata,
Kamishango, Kabare na Katanga.
156.
Mheshimiwa Spika, katika mji wa Mtukula, kazi zilizokamilika ni ulazaji wa
bomba kuu lenye urefu wa kilomita 2.1, kulaza mabomba ya kusambaza
maji lenye urefu wa kilomita 5.3, uchimbaji wa visima viwili (2), ujenzi wa vituo 16 vya kuchotea maji na
ujenzi wa tanki la ujazo wa lita
120,000. Gharama za mradi ni shilingi milioni 653.29. Kazi zilizobaki ni kupeleka
umeme kwenye visima viwili (2) na ufungaji wa pampu. Mradi huo utakapokamilika
utahudumiwa wakazi wapatao 5,000 wa mji wa Mtukula.
(x)
Miradi Mipya
katika Eneo la Ziwa Victoria
157.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European
Investment Bank-EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (French
Development Agency-AFD) itatekeleza mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji pamoja na usafi wa
mazingira katika Jiji la Mwanza, pamoja na Miji ya Musoma, Bukoba, Magu,
Misungwi na Lamadi. Katika utekelezaji wa mradi huo, jumla ya Euro milioni
104.5
zitatumika ambapo Serikali itatoa Euro milioni 14.5, EIB na AFD kwa pamoja watatoa
jumla ya Euro milioni 90. Mikataba ya kifedha ilisainiwa tarehe 23/12/2013 na
tarehe 5/03/2014 hivyo fedha ziko tayari. Hatua za manunuzi zimeanza na Mtaalam
Mshauri anatarajiwa kupatikana mwezi Juni, 2014.
158.
Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa mradi huo kutaongeza upatikanaji wa huduma
ya maji kutoka asilimia 35 hadi asilimia 90 kwa Mji wa Magu; asilimia 5 hadi asilimia 90 kwa Mji wa Lamadi; na asilimia
45 hadi
asilimia 90 kwa Mji wa Misungwi. Aidha, katika Jiji la Mwanza mradi unategemewa
kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi katika maeneo ya miinuko sambamba
na kuboresha usafi wa mazingira kwenye maeneo hayo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
vyoo katika shule za msingi na maeneo ya vituo vya mabasi.
159.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 Wizara yangu iliendelea kutekeleza
miradi ya majitaka kwa Miji ya Bukoba na Musoma. Usanifu na uandaaji wa makabrasha vya zabuni kwa mifumo ya majitaka
unaendelea na mkataba wa kupata fedha (loan agreement) za kutekeleza miradi hiyo kati ya Serikali na AFD utasainiwa mwezi Mei, 2014. Ujenzi wa miradi utaanza
baada ya kukamilika kwa taratibu za zabuni na kumpata Mkandarasi. Miradi ikikamilika
itahudumia asilimia 15 ya wakazi wa Bukoba na asilimia 20 ya wakazi Mji wa Musoma.
(xi) Miradi ya Majisafi na
Usafi wa Mazingira katika Miji Inayozunguka Ziwa Tanganyika
160.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji na
Usafi wa Mazingira kwa eneo la Ziwa Tanganyika (LT-WATSAN) unatekelezwa katika nchi za Zambia, Burundi,
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Tanzania, na kusimamiwa na Shirika
la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT). Kwa upande wa Tanzania, mradi unatekelezwa katika miji ya Kigoma,
Kasulu, Mpanda, Namanyere, Uvinza na Kasanga. Mradi huo ulifanyiwa upembuzi
yanikifu mwaka 2011, hata hivyo, utekelezaji wake haukuanza kutokana na
kutopatikana kwa fedha. Kwa sasa gharama za utekelezaji zimeongezeka
ikilinganishwa na makadirio ya awali, hivyo, nchi wanachama walielekezwa
wapitie upya gharama za ujenzi ili kupata gharama halisi za sasa. Baada ya
mapitio, gharama hizo kwa Tanzania zimekadiriwa kuwa Dola za Marekani
milioni 39.18, ambazo zimepangwa
kama ifuatavyo:- Mji wa Kigoma ni Dola za Marekani milioni 19.10; Kasulu Dola za
Marekani milioni 5.39; Mpanda Dola za Marekani milioni 4.33; Namanyere Dola za
Marekani milioni 3.79; Uvinza milioni 3.01 na Kasanga milioni 3.56. Kazi zinazotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na
usambazaji wa majisafi na usafi wa mazingira, ujenzi wa mifereji ya maji ya
mvua na uondoaji wa taka ngumu pamoja na kuzijengea uwezo taasisi husika. Wafadhili wa mradi huo wanatarajiwa kupatikana baada
ya majadiliano yetu katika Kikao cha Mawaziri wa Maji wa nchi zetu kilichofanyika Mjini Bujumbura, mwezi
Aprili, 2014
3.3.2 Uboreshaji wa Huduma ya Maji katika Miji Mikuu ya Mikoa Mipya
161.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha huduma ya majisafi katika miji mikuu ya mikoa mipya ya
Mpanda, Njombe na Bariadi. Miradi inayoendelea kutekelezwa katika miji hiyo
ni:-
(i)
Mji wa Mpanda
162.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inatarajia kutumia shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji kwa kujenga miradi mbalimbali katika Mji wa
Mpanda. Katika mwaka 2013/2014 Serikali imetuma kiasi cha shilingi bilioni
1.5 kwa
ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika mji huo. Kazi zinazoendelea
kutekelezwa ni pamoja na kulaza bomba kutoka maeneo ya Ikolongo hadi Kazima
urefu wa kilomita 13.6;
ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita
milioni moja; nyumba mbili za watumishi Ikolongo na Kazima na kufungwa solar
panel;
ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji
urefu wa kilomita 48 yenye
kipenyo cha milimita 110 maeneo
ya Kawajense, Kazima, Nsemulwa, Ilembo na Makanyagio; na ununuzi wa dira za
maji 4,000 na viungio vyake.
163.
Mheshimiwa Spika, hadi mwezi
Machi 2014, utekelezaji wa kazi hizo, ni kama ifuatavyo:-
i. Mtaro wa urefu wa kilomita 12.4 umechimbwa kati ya kilomita 13.6 na kulaza bomba urefu wa kilomita 1.3. Kazi hizo zinatarajiwa kukamilika mwezi Agosti,
2014;
ii. Ujenzi wa nyumba mbili na tanki la maji lenye ujazo lita milioni moja umeanza na kazi hii itakamilika mwezi Agosti, 2014;
na
iii. Ununuzi wa viungio kwa ajili ya ufungaji wa dira za
maji umekamilika. Aidha, ununuzi wa vifaa vyote vya mradi unatarajiwa
kukamilika mwezi Agosti, 2014.
Mradi
utakapokamilika utaongeza kiasi cha lita milioni tano za maji kwa siku. Vilevile, idadi ya watu wapatao 50,000 watanufaika na huduma hiyo ambapo upatikanaji wa maji
utaongezeka kutoka asilimia 38.8
ya sasa hadi kufikia asilimia 72.
Katika mwaka 2014/2015, Serikali imetenga shillingi billioni 3 kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa mradi kutoka
chanzo cha maji cha mtiririko Ikolongo II awamu ya pili utakaoongeza upatikanaji
wa maji kutoka asilimia 72 hadi asilimia
82.
(ii)
Mji wa Njombe
164.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 Serikali imetuma kiasi cha shilingi
bilioni 1.2 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji katika Mji wa Njombe. Kazi
zinazoendelea kufanyika ni ujenzi wa intake ya maji na kulaza bomba kuu la maji
kwa gharama ya shilingi bilioni 1.75 na ujenzi wa matanki matatu ya lita 135,000 kila moja kwa gharama
ya shilingi milioni 321. Kazi zote zinatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2014. Mradi
huo ukikamilika, kiasi cha maji kitaongezeka kutoka lita milioni 3.66 hadi lita milioni 5.77 kwa siku. Wananchi
watakaonufaika na mradi wataongezeka kutoka 20,734 hadi 32,734. Na mradi utakidhi
mahitaji ya maji toka asilimia 41 za sasa na kufikia asilimia 58. Katika mwaka 2014/2015 mradi huu
utapanuliwa ili ufikie asilimia 79 ya mahitaji ya Mji wa Njombe. Kiasi cha shilingi bilioni 3.5 kimetengwa kwa kazi
hiyo.
(iii)
Mji wa Bariadi
165.
Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kutekelezwa katika Mji wa Bariadi ni
kuchimba visima sita na kufunga pampu; kujenga tanki la maji lenye ujazo wa lita
45,000;
kupanua mtandao wa maji; kukarabati tanki la Somanda; kuunganisha umeme kwa
ajili ya visima vya Somanda, Sanungu, Isanzu na Kidinda; na kujenga ofisi ya
mamlaka ya maji. Mradi huo utagharimu shilingi bilioni 2. Hadi mwezi Machi 2014,
mtaro wenye urefu wa kilomita 6.8 kati ya kilomita 7.6 umechimbwa na ulazaji wa
mabomba yenye urefu wa kilomita 2.1 umekamilika kati ya kilomita
7.6 zilizopangwa.
Nguzo za umeme tayari zimefika katika eneo la ujenzi. Katika mwaka 2013/2014,
Wizara imetuma shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya utekelezaji wa
kazi hizo. Mradi ukikamilika, kiasi cha maji kitaongezeka kutoka lita
861,000 hadi lita 1,560,000 kwa siku na huduma ya upatikanaji maji itaimarika kutoka
asilimia 17 hadi asilimia 30. Katika mwaka 2014/15 Serikali imetenga shilingi
bilioni 3.5 ili kuendelea na ujenzi na
upanuzi wa mradi wa maji wa Mji wa Bariadi kutoka asilimia 30 kufikia asilimia 75 ya mahitaji ya kila
siku.
3.3.3 Usanifu wa Miradi ya Majisafi na Majitaka
166. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2014/2015, Serikali itaendelea na usanifu wa kina na kuandaa vitabu vya zabuni
kwa miradi ya maji katika miji midogo na miji mikuu ya Wilaya za Biharamulo,
Muleba, Ngara, Karagwe, Chato na Bunazi (Kagera). Mtaalam Mshauri ameajiriwa
tarehe 27/12/2013 na anaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu. Taratibu za
kuwapata Wataalam Washauri katika mji wa Kakonko (Kigoma) na Miji ya Namanyere,
Chala na Laela (Rukwa) zinaendelea. Kwa upande wa Miji ya Manyoni na Kiomboi
(Singida), Mtaalam Mshauri ameanza kazi tarehe 21/08/2013 na anatarajiwa
kukamilisha mwezi Juni, 2014. Usanifu unaendelea kwa miradi ya maji ya Miji ya
Mombo, Songe, Lushoto, Kasela, Korogwe na Handeni Trunk Main - HTM katika Mkoa wa
Tanga; na mradi wa kutoa maji Mto Ugala hadi Miji ya Urambo na Kaliua. Katika
Mkoa wa Tabora. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea
na utekelezaji wa miradi hiyo.
3.3.4 Miradi ya Maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka katika Miji Mbalimbali
167.
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya ujenzi wa miradi ya maji kutoka Ziwa
Victoria kupeleka katika miji mbalimbali yanaendelea. Mradi wa kupeleka maji katika
Miji ya Bariadi, Mwanhuzi, Lagangabilili na Maswa utakapokamilika
utanufaisha vijiji 40 vilivyo umbali wa kilomita 12 kandokando ya bomba kuu
kutoka kwenye Ziwa Victoria. Katika mwaka 2014/2015, kiasi cha shilingi
bilioni 3.5 zimepangwa kwa ajili ya mradi huo, na upembuzi yakinifu utaanza mwezi Mei,
2014. Kwa upande wa Miji ya Magu kwenda Kwimba, mradi utakapokamilika utahudumia
vijiji na miji ya njiani litakapopita bomba kuu ikiwemo miji midogo ya Sumve na
Malya na kiasi
cha shilingi bilioni 4 zimepangwa kutumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi
huo. Vilevile, Miji ya Kagongwa, Isaka hadi Tinde itapata huduma ya maji kutoka
bomba kuu
la Kahama-Shinyanga kutoka Ziwa Victoria. Katika mwaka 2014/2015, Wizara
yangu imepanga kutumia kiasi cha shilingi bilioni 8 kwa ajili ya utekelezaji wa
mradi huo.
166. Mheshimiwa
Spika, mradi wa upanuzi wa mtandao wa bomba kuu la maji la Mamlaka
ya Maji ya KASHWASA kutoka tanki la maji lililopo katika kijiji cha Mhalo kwenda
katika Mji wa Ngudu unatekelezwa na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2014.
Mradi huu unasimamiwa na Mamlaka ya KASHWASA. Kazi zilizokamilika hadi sasa ni uchimbaji wa mtaro na kulaza
bomba kutoka kijiji cha Runere hadi Mjini Ngudu umbali wa kilomita 24.6; na ukarabati wa tanki
la maji lililopo Ngudu; na chemba
13 kati
ya 75 zimejengwa.
Mradi upo katika hatua nzuri ya utekelezaji, ambapo majaribio ya kupeleka maji
kutoka Mhalo hadi Runere yamefanyika. Maandalizi ya kazi za majaribio ya
kupeleka maji kutoka Runere hadi Ngudu yanaendelea.
3.3.5 Mradi wa Maji wa Chalinze
168.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu iliendelea na utekelezaji wa awamu ya pili
ya mradi wa maji Chalinze, utakaotoa huduma ya majisafi katika vijiji 47 vya mikoa ya Pwani (42) na Morogoro (5). Mradi huo
unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na BADEA, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa
China na Mfuko wa Pamoja wa Sekta ya Maji, utawanufaisha wakazi 197,684 wa Wilaya tatu za Bagamoyo, Kibaha na
Morogoro. Wizara yangu inaendelea kutekeleza awamu hiyo ya mradi inayotegemewa
kukamilika mwezi Septemba, 2014. Jedwali Na. 11 linaonesha viwango vya
utekelezaji wa sehemu mbalimbali za mradi huo.
169.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2013/2014, Serikali iliingia Mkataba na Mtaalam Mshauri ili kufanya mapitio ya
usanifu na kusimamia utekelezaji wa mradi wa Chalinze awamu ya tatu
utakaogharimu Dola za Marekani milioni 49. Kazi hiyo ilianza mwezi Agosti, 2013 na inatarajiwa
kukamilika mwezi Juni, 2014. Katika mwaka 2014/2015 Serikali itaanza ujenzi wa
mradi baada ya kumpata Mkandarasi. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2016.
Kazi zitakazotekelezwa ni ukarabati wa chanzo, kujenga matanki ya kuhifadhia
maji katika vijiji 20, kupanua mitandao ya bomba kuu na bomba la usambazaji,
kujenga tanki kubwa la kuhifadhi maji katika Mlima Mazizi na kujenga vituo vya
kuchotea maji katika maeneo ambayo hayakufikiwa na ujenzi wa awamu za I na II.
3.3.6 Miradi katika Jiji la Dar es Salaam
170.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliendelea
kutekeleza miradi mbalimbali iliyopangwa ili kuboresha upatikanaji wa huduma ya
maji katika Jiji la Dar es Salaam. Hadi mwezi Machi, 2014 miradi inayoendelea
kutekelezwa ni kama ifuatavyo:-
(a) Ujenzi wa Bwawa la
Kidunda
171.
Mheshimiwa Spika, Mtaalam Mshauri aliyepewa kazi ya
kutathmini athari za kimazingira na kijamii (ESIA) zitakazotokana na ya ujenzi wa
barabara kuelekea eneo la ujenzi wa bwawa la Kidunda
amewasilisha rasimu ya mwisho ya kazi hiyo tarehe 24 Februari, 2014. Serikali imekamilisha
taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi wa
barabara kuelekea kwenye eneo la bwawa na ujenzi unatarajiwa kuanza mara baada
ya kukamilika tathmini ya ESIA na ulipaji fidia kwa watakaoathirika na mradi.
172.
Mheshimiwa Spika, upande wa malipo ya fidia, Mthamini wa Serikali amekamilisha mapitio ya uthamini ili kuongeza
thamani ya fidia baada ya kuchelewa malipo. Kulingana na Sheria ya Ardhi Na.
4 ya mwaka 1999, thamani ya fidia imeongezeka kwa asilimia
8. Vitabu vipya vimetayarishwa na rasimu ziliwasilishwa
tarehe 28/2/2014. Taratibu za kupata fedha
za kulipia fidia hiyo ambayo ni shilingi bilioni 7.9 zinaendelea. Katika mwaka 2014/2015, Serikali imepanga kutumia kiasi
cha shilingi bilioni 7.0 kwa ajili ya
maandalizi na ulipaji wa fidia.
Aidha, Wizara inaendelea na juhudi za
kutafuta fedha za ujenzi wa bwawa na hivi sasa yapo mashauriano kati ya Benki
ya Uwekezaji ya Afrika Kusini ikishirikiana na Benki ya Rasilimali ya Tanzania,
na Benki ya Dunia kwa ajili ya kupata fedha za ujenzi wa bwawa hilo.
(b) Visima Virefu vya
Kimbiji na Mpera
173.
Mheshimiwa Spika, mradi wa visima virefu vya Kimbiji na Mpera unahusisha
uchimbaji wa visima 20 vya uzalishaji na visima vinane (8) vya kubaini mwenendo wa
rasilimali za maji chini ya ardhi. Hadi mwezi Machi, 2014 Mtaalam Mshauri wa
kusimamia kazi ya uchimbaji wa visima 20 vya Kimbiji na Mpera ametoa
maoni yaliyowasilishwa na Mkandarasi kuhusu uagizaji vifaa vya kuchimbia visima
pamoja na mabomba (casings and screens) yatakayotumika katika
uchimbaji wa visima hivyo. Mkandarasi anaendelea kukamilisha maandalizi ya vitendea kazi na mabomba (equipment mobilization) na
anategemewa kuanza kazi mwezi Juni, 2014. Uchimbaji wa visima hivyo unatarajiwa
kukamilika mwezi Novemba, 2014.
174.
Mheshimiwa Spika, mkandarasi wa uchimbaji wa visima virefu vinane (8) vya uchunguzi wa
mwenendo wa maji chini ya ardhi amekamilisha uchimbaji wa visima viwili (2) eneo la Mwasonga na Mkuranga. Majaribio ya uwingi (output) wa maji katika visima hivyo na matokeo ya vipimo vya ubora wa maji
yameonesha dalili za kuwa na maji mengi yenye ubora unaofaa kwa matumizi ya
binadamu. Kwa sasa Mkandarasi anachimba kisima cha
tatu eneo la Kibada na amefikia mita 200 kati
ya mita 600. Aidha, Mtaalam Mshauri anayetathmini athari za kimazingira na kijamii (ESIA) amewasilisha rasimu ya
tatu ya taarifa ya ESIA tarehe 24/3/2014 na kupelekwa Benki ya Dunia tarehe
26/03/2014 kwa ajili ya kuridhiwa.
175.
Mheshimiwa Spika, baada ya ulipaji wa fidia kwenye eneo la mita 60 kuzunguka kila kisima
katika maeneo ya Kimbiji na Mpera kukamilika, Serikali ilikamilisha uhakiki wa
fidia katika maeneo ya Luzando na
Kisarawe II. Ulipaji wa fidia kwa eneo litakapojengwa tanki la Kisarawe II
ulianza tarehe 20/8/2013 na kwa
eneo la Luzando tarehe 29/10/2013. Vilevile, uthamini katika maeneo ya ujenzi wa njia za mabomba na barabara kuelekea
kwenye visima umeanza, na maombi ya kupata Wathamini kutoka Ofisi ya Mthamini
Mkuu wa Serikali yamewasilishwa. Kwa sasa Mtaalam Mshauri anakamilisha usanifu
wa kazi hiyo. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kutekeleza mradi
wa kuchimba visima katika eneo la Kimbiji na Mpera.
(c) Upanuzi wa
Mtambo wa Ruvu Juu
176. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na
changamoto ya ukuaji wa kasi wa Miji ya Mlandizi, Kibaha na Jiji la Dar es
Salaam, Wizara yangu kwa kushirikiana na Serikali ya India inajenga na kupanua mtambo wa
kuzalisha maji Ruvu Juu na ulazaji wa bomba kuu kutoka Mlandizi hadi Kimara
kuanzia tarehe 15/02/2014. Mradi huo unatarajiwa kukamilika baada ya
miezi 18. Mradi utakapokamilika utagharimu Dola za
Marekani milioni 39.7 kwa ajili ya upanuzi wa
mtambo na Dola za Marekani milioni 59.3
kwa ulazaji wa bomba kuu. Kukamilika kwa upanuzi wa mradi kutaongeza uzalishaji wa
maji kutoka lita milioni 82 hadi lita milioni 196 kwa siku. Aidha, wananchi
wanaoishi kwenye maeneo ya Jiji ambayo miundombinu ya usambazaji maji
ilikarabatiwa na haikuwa na maji kwa kipindi kirefu watapata huduma hiyo.
(d) Upanuzi wa Mradi wa Maji wa
Ruvu Chini
177.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali kwa kushirikiana na MCC, imekamilisha upanuzi
wa mradi wa maji wa Ruvu Chini. Kwa sasa Mkandarasi anafanya majaribio ya
mitambo. Hadi mwezi Machi 2014, kazi ya ulazaji wa bomba kuu kutoka mitambo ya
Ruvu Chini hadi kwenye matanki ya Chuo Kikuu cha Ardhi lenye urefu wa kilomita
55.93 imekamilika
kwa asilimia
62.87
sawa na kilomita 35.16. Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2014.
Aidha, kazi ya ujenzi wa kingo za Mto Ruvu katika eneo la Kidogozero
ulikamilika mwezi Novemba, 2013 na umekabidhiwa kwa DAWASA, kwa sasa Mkandarasi
yuko kwenye kipindi cha uangalizi (defects liability period).
(e) Ukarabati na Upanuzi
wa Mfumo wa Kusambaza Majisafi
178.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Mfumo wa Kusambaza
Majisafi kati ya Jiji la Dar es Salaam na Mji wa Bagamoyo unahusisha kuunganisha
wateja kutoka Tegeta hadi Mpiji na Mpiji hadi Bagamoyo. Mradi huo
unajumuisha ulazaji wa mabomba ya urefu wa kilomita 732 ya kusambaza maji
yatakayounganisha wateja 24,400 na kujenga magati 30 kati ya Bagamoyo
na Tegeta. Mtaalam Mshauri atakayesanifu na kusimamia ujenzi amepatikana. Kwa sasa
Mtaalam Mshauri huyo anaandaa nyaraka za zabuni za ujenzi wa mradi (pre-qualification
document) na tayari amewasilisha rasimu ya kwanza ya nyaraka za kuwatafuta
Wakandarasi watakaoshiriki zabuni. Aidha, kwa mradi wa kuunganisha mabomba ya
usambazaji maji ya urefu wa kilomita 300 kwenye eneo la Mbezi hadi
Kiluvya uliendelea kutekelezwa. Jumla ya wateja 10,000 wataunganishwa na
magati 30 yatajengwa. Kazi hiyo inahusu miradi ya mabomba madogo madogo na
kuunganisha wateja kwenye eneo kati ya Mbezi hadi Kiluvya. Mtaalam Mshauri
anaandaa nyaraka za zabuni.
179.
Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuboresha hali ya huduma ya maji katika
Jiji la Dar es Salaam ili iwe endelevu, Wizara yangu imefikia makubaliano ya
awali na Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) ili kuwekeza kwenye mradi wa
ukarabati na upanuzi wa mfumo wa usambazaji maji katika Jiji la Dar es Salaam.
Kwa sasa Mtaalam Mshauri ameanza kazi ya upembuzi yakinifu na kuandaa makadirio
ya gharama za mradi ili zitumike kutayarisha Mkataba wa kifedha. Pamoja na
majadiliano yanayoendelea na TIB, Kampuni za AVIC International na China Machinery
and Engineering Corporation kutoka nchini China zimeonesha nia ya kufadhili baadhi ya
miradi ikiwemo upanuzi wa miundombinu ya majitaka. Wizara yangu inaendelea na
taratibu za awali za kufikia mikataba ya kifedha.
(f) Miradi Mingine ya
Kuboresha Huduma ya Maji Jijini Dar es Salaam
180.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la
Ubelgiji (BTC) na Umoja wa Nchi za Ulaya imekamilisha miradi tisa (9) kati ya miradi 15 ya kujenga mifumo ya
usambazaji maji katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam. Kazi zilizokamilika ni
pamoja na kuchimba visima 14; na kujenga vituo 194 vya kuchotea maji na matanki
15 ya
kuhifadhia maji. Miradi sita (6) iliyobaki katika maeneo ya Tabata Darajani, Minazi
mirefu, Kinyerezi, Mwanamtoti, Yombo Dovya - Msakala na Tandale inatarajiwa
kukamilika mwezi Juni, 2014 baada ya kuwasha mitambo na kupima msukumo wa maji
(pressure test). Vilevile, mradi huo umejenga vyoo
bora 21 vya mfano katika maeneo
ya jumuiya (shule 6 za msingi,
zahanati 4, soko 1 na katika Ofisi za Serikali za Mitaa 10). Vyoo hivyo vimejengwa kwa lengo la watu kujifunza
jinsi ya kujenga vyoo bora katika makazi yao. Pamoja na ujenzi wa vyoo hivyo
vipya, mradi umekarabati vyoo vya zamani katika shule tisa (9). Vilevile,
mradi umetoa elimu ya maji, afya na usafi wa mazingira kwa wananchi na
wanafunzi wa shule husika katika eneo la mradi. Jedwali Na. 12 linaonesha utekelezaji wa uchimbaji wa visima katika
maeneo mbalimbali ya mradi Jijini Dar es Salaam
181.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliendelea
kutekeleza miradi ya uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali ya Jiji la
Dar es Salaam ili kupunguza kero ya maji wakati wa kusubiri utekelezaji wa
Mradi Maalum wa Kuboresha Upatikanaji wa Huduma ya Majisafi na Uondoaji
Majitaka katika Jiji la Dar es Salaam. Hadi mwezi Machi 2014, DAWASA imechimba visima 44 kati ya visima 46 vilivyopangwa. Kati ya
visima hivyo, visima 21 vimekamilika na kuanza kutumika. Visima nane (8) vipo Kimara, katika
maeneo ya Mavurunza
A, Kilungule A, Kilungule B, King’ongo I, King'ongo II, King'ongo III, Saranga
I na Saranga II; Visima vitano (5) vipo Keko/Chang’ombe maeneo ya Keko Magurumbasi, Keko Mwanga A, Chang’ombe A,
Unubini na Chang’ombe Toroli; na visima vitatu (3) vipo Sandali katika maeneo ya Sandali,
Mpogo na Mwembe Ladu. Vilevile, visima vingine viwili (2) vilivyokamilika vinatumika Mburahati maeneo ya Mburahati National Housing
na Shule ya Msingi
Muungano; na kisima kimoja kimoja katika maeneo ya Mwaninga-Kigamboni, Kipunguni na FFU yaliyoko Ukonga. Katika
mwaka 2014/2015, DAWASA itaendelea na kazi ya ufungaji wa pampu ili kukamilisha
visima vilivyobaki.
(g) Mradi wa Maji ya
Bomba kwenda Mloganzila
182. Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza
ujenzi wa Kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Udaktari na Sayansi Shirikishi katika
eneo la Mloganzila. Ili
kurahisisha ujenzi, Wizara yangu inajenga mradi wa Bomba la Maji kwenda eneo la
upanuzi. Katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu imekamilisha usanifu wa mradi,
ununuzi wa mabomba na pampu, ukarabati wa tanki la zamani kwenye kituo cha
kusukumia maji na ujenzi wa mnara wa tanki jipya
litakalopokea maji kutoka kwenye chanzo cha Ruvu Juu. Kazi zote zilikamilika mwezi Oktoba, 2013. Uchimbaji wa mtaro wenye urefu wa kilomita 1.94 umekamilika ambapo
mabomba yenye urefu wa kilomita 1.0 yamelazwa. Kazi ya kulaza
mabomba yenye urefu wa kilomita 0.94 zilizobaki inaendelea na
mradi utakamilika mwezi Juni, 2014.
3.3.7 Huduma ya Maji katika Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo na Miradi ya Kitaifa
(a) Miradi ya Maji katika
Miji ya Kibiti na Kibaigwa
183.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ilikamilisha ujenzi wa miradi ya maji katika
Miji ya Kibiti na Kibaigwa katika mwaka 2013/2014. Mradi wa Kibiti ambao
uligharimu shilingi bilioni 5.3 ulizinduliwa rasmi tarehe 5/10/2013 na Mhe. Dr.
Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mradi huo unatoa
huduma kwa wakazi wapatao 29,931 wa Kata mbili za Kibiti na Mtawanya. Aidha,
mradi wa Kibaigwa uliogharimu shilingi bilioni 2.27 ulizinduliwa na Mhe. Mizengo
Kayanza Peter Pinda (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa
Maadhimisho ya Wiki ya Maji tarehe 17/3/2014. Kukamilika kwa mradi huo
kumewezesha asilimia 90 ya wananchi wa Kibaigwa kupata maji safi na salama
ukilinganisha na asilimia 48 kabla ya mradi.
(b) Miradi ya Maji katika
Miji ya Kisarawe, Ikwiriri, Kilosa, Turiani, Mahenge, Mvomero na Gairo
184.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza miradi ya maji katika Mji wa Kisarawe,
Wizara imekamilisha uchimbaji wa visima vitano (5) katika maeneo ya Kwala, Mtunani,
Chole-Samvula, Yombo-Lukinga I na Yombo-Lukinga II. Aidha, Wizara imeendelea na
ujenzi wa miradi ya maji katika miji midogo ya Ikwiriri, Kilosa, Turiani,
Mahenge, Mvomero na Gairo. Hadi mwezi Machi 2014, ujenzi wa miradi ya maji
katika miji hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kama ifuatavyo:-
Ikwiriri asilimia 100, Kilosa asilimia 80, Turiani asilimia 77, Mahenge asilimia 77, Mvomero asilimia 81
na Gairo
asilimia 86. Miradi hiyo inatarajiwa kukamilika mwaka 2014/2015.
(c) Miradi ya Maji
Masasi/Nachingwea na Bunda
185. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014,
Wizara yangu imekamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji wa Masasi-Nachingwea. Mradi huo
umekamilika mwezi Julai, 2013 na unahudumia Miji ya Masasi na Nachingwea pamoja
na vijiji vya Likwachu na Chinongwe vilivyopo Wilaya ya Ruangwa na vijiji vya
Chiumbati Shuleni na Chiumbati Miembeni vilivyopo Wilaya ya Nachingwea. Kazi ya
kuunganisha wateja na ufungaji wa dira za maji inaendelea. Hadi mwezi Machi,
2014 jumla ya wateja 2,972 wameunganishwa kwenye mtandao wa majisafi.
Vilevile, huduma kwa wakazi wasio na maji majumbani inatolewa kwenye magati
68
yaliyojengwa maeneo mbalimbali ya Miji ya Masasi na Nachingwea.
186. Mheshimiwa Spika, katika Mji wa Bunda,
hadi mwezi Machi, 2014 Mkandarasi amekamilisha kazi ya ukarabati wa matanki mawili (2) kati ya matanki
matatu (3) yenye ujazo wa lita
225,000 kila moja. Vilevile, ujenzi wa
Ofisi ya Mtaalam Mshauri na ununuzi wa magari mawili umekamilika. Kazi ya
ulazaji wa bomba inaendelea na imefikia asilimia 40, ambapo kilomita 9.3 kati ya kilomita
25.4 zimekamilika.
Katika mwaka 2014/2015 ujenzi huo utaendelea na kutumia shilingi bilioni 3 kukamilisha ulazaji wa bomba na kujenga
mfumo wa kusambaza maji katika Mji wa Bunda.
(d) Mradi wa Maji
Orkesumet
187.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Nchi
za Kiarabu (BADEA) na OFID inatarajia kujenga mradi wa majisafi utakaohudumia
Mji wa Orkesumet. Katika utekelezaji wa mradi huo, BADEA watatoa Dola za
Marekani milioni 8, OFID Dola za Marekani milioni 8 na Serikali Dola za Marekani milioni 2.4. Mtaalam Mshauri
anaendelea na kufanya mapitio (review) ya usanifu uliofanywa hapo
awali na kutayarisha vitabu vya zabuni kwa ajili ya kumtafuta Mkandarasi wa
ujenzi. Hadi mwezi Machi, 2014 Mtaalam Mshauri ameshawasilisha taarifa ya
mapitio ya usanifu wa kina (detail design review), kwa ajili ya kuhakikiwa.
Katika mwaka 2014/2015, ujenzi wa mradi huo utaanza baada ya kumpata Mkandarasi.
(e) Mradi wa Uboreshaji
wa Huduma ya Majisafi Muheza
188.
Mheshimiwa Spika, katika
kupunguza kero ya upatikanaji wa majisafi na salama katika Mji wa Muheza,
Wizara yangu imetuma shilingi milioni 350 ili kuboresha miundombinu ya maji ya visima virefu vitatu (3) maeneo ya soko la Michungwani, NHC-tank na Kwasemwaiko. Kazi zinazoendelea kutekelezwa ni
ununuzi na ufungaji wa pampu na viungio vyake, ujenzi wa chemba mbili (2) na vituo viwili (2) vya kuchotea maji, uchimbaji mtaro, ulazaji wa
mabomba na ununuzi wa vifaa vya ujenzi na umeme. Ujenzi huo ukikamilika kwenye
kisima cha NHC-tank kitakuwa na
uwezo wa kusukuma maji lita 2,000
kwa saa (saa 22 kwa siku), kisima cha Kwasemwaiko kikikamilika kitasukuma maji lita
2,500 kwa saa (saa 22 kwa siku).
(f)
Mradi wa Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi Karatu
189.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali ilitekeleza mradi wa maji wa dharura katika Mji wa
Karatu unaogharimu Shilingi milioni
930. Mradi huo umezinduliwa rasmi tarehe 22/04/2014 na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete. Kazi zilizokamilika hadi sasa ni ujenzi wa tanki moja lenye ujazo wa lita 225,000;
ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa kilomita 2.9;
ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji yenye urefu wa kilomita 4.4; ujenzi wa vituo 12 vya kuchotea maji; ujenzi wa njia kuu ya umeme yenye
urefu wa kilomita 1.2; na ufungaji wa transfoma na pampu. Kazi hizo
zimegharimu shilingi milioni 609.9 na
kuongeza
upatikanaji wa maji kwa kiasi cha lita 720,000 kwa siku na hivyo kufikia asilimia
34.5 ya
mahitaji ya maji kwa Mji wa Karatu. Katika mwaka 2014/2015, Wizara
yangu imepanga kutumia shilingi milioni 250 kuendelea kutekeleza kazi
zilizobaki ambazo ni pamoja na:- Ujenzi wa tanki moja lenye ujazo wa
lita 225,000; ulazaji wa mabomba ya usambazaji wa maji yenye
urefu wa kilomita 3.8; na
uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba ya kupeleka maji eneo la G-lambo.
(g) Miradi ya Maji ya
Miji Midogo
190.
Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga shilingi bilioni 17.1 kwa ajili ya kukarabati
na kupanua miundombinu ya maji katika miji mikuu ya wilaya na miji midogo 46. Fedha hizo zitatumika
kutekeleza miradi inayoendelea na ambayo italeta ahueni kubwa ya maji kwa
wakazi wa Miji hiyo. Miradi hiyo
imeorodheshwa kwenye Jedwali Na. 13 linaonesha mchanganuo wa fedha
zitakazotumwa kwenye Mamlaka za Miji Mikuu ya Wilaya na Miji Midogo.
(h) Mradi wa Maji Longido
191.
Mheshimiwa Spika, Mji wa Longido unakadiriwa kuwa na wakazi 21,000 na mifugo ipatayo 13,000. Mahitaji ya maji kwa
sasa ni wastani wa lita milioni 1.2 kwa siku wakati uzalishaji wa
maji kwa siku ni wastani wa lita 240,000. Utafiti uliofanyika awali umeonesha
kuwa maeneo ya karibu na Mji hayana vyanzo vya maji vinavyoweza kutosheleza
mahitaji ya maji kwa Mji huo. Kutokana na hali hiyo, Wizara yangu imefanya
utafiti wa kina na kubaini kuwa chanzo pekee ambacho kitatosheleza mahitaji ni
Mto Meru. Katika mwaka 2014/2015, Wizara imetenga shilingi bilioni 3 kutekeleza mradi wa
kutoa maji Mto Meru hadi Mji wa Longido ili kutatua tatizo la maji katika Mji
huo.
3.3.8 Miradi ya Maji ya Kitaifa
192.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na upungufu wa maji katika Miradi ya
Kitaifa na kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma katika maeneo ya miradi
hiyo, Wizara yangu ilituma shilingi milioni 870 kwa ajili ya ununuzi wa pampu, mabomba na ukarabati wa
miundombinu ya maji. Mgao wa fedha ulikuwa kama ifuatavyo:- Handeni Trunk
Main - HTM shilingi milioni 50, Makonde shilingi milioni 60, Maswa
shilingi milioni 200,
Mugango-Kiabakari shilingi milioni 250, Wanging’ombe shilingi milioni 50, Chalinze shilingi milioni 60, Masasi-Nachingwea shilingi milioni 150, na KASHWASA
shilingi milioni 50. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu imepanga kutumia
jumla ya shilingi bilioni 11.6
kukarabati miundombinu ya maji katika miradi hiyo ili kuhakikisha wananchi
wanapata huduma iliyo bora na endelevu.
193.
Mheshimiwa
Spika, katika mwaka 2014/2015, Wizara
yangu itaajiri Mtaalam Mshauri wa kufanya mapitio ya usanifu na usimamizi wa
mradi wa miundombinu ya maji katika Mradi wa Kitaifa Mugango-Kiabakari na
vijiji vilivyopo umbali wa kilomita 12 kando ya bomba kuu. Mradi huo
utatekelezwa na Serikali kwa
kushirikiana na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA) na Mfuko wa Maendeleo wa Saudia (Saudi Fund for
Development - SFD) kwa gharama ya Dola
za Marekani milioni 30.69. Kazi
zitakazotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa chanzo, ujenzi wa mtambo wa kusafisha
na kusukuma maji, kujenga matanki matatu, kulaza mabomba kutoka Mugango hadi
Kiabakari na Butiama urefu wa kilomita 32, kukarabati mitambo ya kusukuma maji ya Kiabakari na kulaza mabomba ya
mtandao wa usambazaji maji Butiama hadi Bisalye. Kukamilika kwa mradi huo
kutanufaisha wananchi wapatao 80,000 katika eneo hilo.
3.3.9 Kuzijengea Uwezo Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Mijini
194.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu imeendelea
kuzijengea uwezo Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Mijini ili ziongeze
ufanisi katika utoaji wa huduma kwenye maeneo yao. Ujenzi wa ofisi za Mamlaka
za maji za Miji ya Utete na Mpwapwa umekamilika. Ujenzi wa ofisi ya Mamlaka ya
Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Babati unaendelea na unatarajiwa
kukamilika mwezi Juni, 2014. Katika Mamlaka ya maji Tunduma, ujenzi wa ofisi
utakamilika mwezi Novemba, 2014. Aidha, katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu
itaendelea kuziimarisha mamlaka za maji ngazi ya mikoa, wilaya, miji midogo na
miradi ya kitaifa kwa kuzijengea mazingira mazuri zaidi ya kazi ili zitoe
huduma bora kwa wananchi.
195.
Mheshimiwa Spika, ili kuijengea uwezo miradi ya kitaifa na mamlaka za
maji za daraja B na C, Wizara yangu imetoa jumla ya shilingi milioni 435 kwa ajili ya kulipia
sehemu ya ankara za umeme wa mitambo ya kuzalisha maji. Katika mwaka 2014/2015
Wizara yangu, itaendelea kuchangia gharama za uendeshaji wa miradi ya kitaifa
na Mamlaka za daraja B na C ili hatimaye ziweze kujiendesha zenyewe na hivyo
kuipunguzia Serikali mzigo wa kuchangia gharama hizo.
196.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuwekeza
kwenye miundombinu ya maji na kuzijengea uwezo Mamlaka za maji za ngazi ya
wilaya, miji midogo na miradi ya kitaifa ili kuboresha huduma ya majisafi na
usafi wa mazingira katika maeneo ya mamlaka hizo.
197.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu imeendelea kuisimamia Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ili iweze kutekeleza majukumu
yake kama yalivyoainishwa kwenye Kifungu Na. 414 cha Sheria Na.11 ya EWURA ya mwaka 2001. Sheria
hiyo inaitaka EWURA kudhibiti utoaji wa huduma kwenye Sekta za umeme, mafuta
ya petroli, gesi asilia, majisafi na majitaka nchini. Kwa mujibu wa sheria
hiyo, EWURA ina majukumu ya kutoa leseni, kusimamia utekelezaji wa masharti ya leseni,
kudhibiti ubora na ufanisi wa utoaji huduma, kutathmini na kupitisha bei za
huduma na kutatua migogoro baina ya watoa huduma na wateja wao. Kwa upande wa
sekta ya Maji, EWURA imeendelea na udhibiti wa huduma za maji zinazotolewa na Mamlaka za Maji 129 nchini. Kati ya Mamlaka
hizo, 23 ni za miji mikuu ya mikoa, 96 za miji mikuu ya wilaya na miji midogo, DAWASA,
DAWASCO na miradi ya maji minane (8) ya kitaifa.
198.
Mheshimiwa Spika, EWURA iliendelea kutathmini na kuidhinisha bei za huduma ya maji kwa mamlaka mbalimbali za majisafi
na usafi wa mazingira nchini. Katika mwaka 2013/2014, EWURA iliidhinisha bei mpya
za huduma
za maji kwa mamlaka 23 za maji za Babati, Moshi, Musoma, Kilwa Masoko,
Kahama, Arusha, Bariadi, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, KASHWASA, Kigoma,
Lindi, Mbeya, Morogoro, Mpanda, Mtwara, Mwanza, Shinyanga, Singida, Songea,
Tabora na Tanga. Mabadiliko ya bei hizo yanatokana na kuongezeka kwa gharama za
uendeshaji hususan gharama ya umeme. Aidha, EWURA, ilipokea na kupitia Mipango ya
Kibiashara (Business Plans) ya miaka mitatu kutoka mamlaka za maji za Miji ya
Kisarawe, Songea na Mtwara. Mamlaka zilizobaki zinaendelea kutekeleza mipango
yao ya kibiashara.
199.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, EWURA ilitoa taarifa ya
utendaji wa Mamlaka za Maji kwa mwaka 2012/13. Taarifa hiyo inaonesha kuwa
mamlaka za maji zimepiga hatua katika ufungaji wa dira za maji, kuongezeka kwa
idadi ya wateja wa majisafi na majitaka na ukusanyaji wa maduhuli. Aidha,
katika mwaka 2013/2014, jumla ya malalamiko 12 yalipokelewa EWURA. Malalamiko hayo
yalihusu ankara za majisafi na majitaka zilizokosewa, ukosefu wa maji, kukatiwa
huduma ya maji kimakosa na huduma hafifu kwa wateja (poor customer service). Kati ya malalamiko
yaliyowasilishwa, sita (6) yamepatiwa ufumbuzi na sita (6) yaliyobaki yapo katika
hatua mbalimbali za utatuzi.
200.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 EWURA imeendelea kusimamia Sekta
Ndogo za Umeme, Petroli na Gesi Asilia, hususan katika masuala ya kusimamia
ubora wa huduma ya umeme, kukagua miundombinu ya umeme, gesi asili na mafuta
ili kuhakikisha ubora na usalama wa huduma hizo. EWURA imeendelea kuandaa
kanuni na taratibu zinazovutia
uwekezaji na kutoa leseni mbili (2) kwa wawekezaji wa miradi midogo
midogo isiyozidi Megawati 10 (makampuni ya Mapembasi ya Njombe na Bwelui ya
Mbeya). Katika Sekta ndogo ya Petroli jumla ya leseni 15 kwa ajili ya wauzaji wa
jumla wa mafuta ya petroli zilitolewa. Vilevile, leseni 19 kwa ajili ya wauzaji wa
rejareja wa mafuta hayo zilitolewa. Aidha, EWURA imeendelea kukagua miundombinu
ya kuchakata, kusafirisha na kusambaza gesi asilia na kubainika kuwa ni salama
kwa matumizi na mazingira.
201.
Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha udhibiti wa huduma ya majisafi na uondoaji wa majitaka
inayotolewa na mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira nchini, katika mwaka
2014/2015 vipaumbele vifuatavyo vitazingatiwa:-
(i)
Kuhimiza uwekezaji kwa mamlaka za maji kwa kuandaa miongozo ya jinsi ya
kushirikisha sekta binafsi katika utoaji wa huduma za majisafi na majitaka;
(ii)
Kuendelea kufuatilia utendaji wa mamlaka za maji nchini kwa kuchambua na
kuhakiki taarifa za utendaji kazi na kukagua miundombinu na utendaji wa mamlaka
za maji;
(iii)
Kuandaa miongozo ya viwango vya ubora wa huduma zinazotolewa na mamlaka za
maji;
(iv)
Kuendelea kufuatilia utekelezaji wa mipango yao ya kibiashara (Business
Plans)
kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na EWURA;
(v)
Kuandaa na kutekeleza mipango ya kuhimiza ubora wa huduma wa mamlaka za
maji katika miji midogo, miji mikuu ya wilaya na miradi ya kitaifa; na
(vi)
Kuandaa na kutekeleza hatua zitakazosaidia kupunguza gharama za kuunganisha
huduma za maji kwa wateja.
202.
Mheshimiwa Spika, EWURA ni mamlaka ya udhibiti wa Sekta kuu mbili za
Nishati na Maji. Ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi, nimeiagiza
EWURA iendeleze ushirikiano wa karibu na kupokea na kutekeleza miongozo
inayotolewa na Wizara zinazosimamia Sekta hizo kulingana na Sheria zilizopo.
203.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu la Chuo cha Maendeleo na
Usimamizi wa Maji la kujenga uwezo wa kitaalam wa fani za ufundi zinazohitajika
kwenye Sekta ya Maji, Chuo kilidahili wanafunzi 412 wa mwaka wa kwanza wa Stashahada (water
technicians) na wanafunzi 69 wa Shahada ya Kwanza ya Uhandisi wa Rasilimali za
Maji na Umwagiliaji (Bachelor of Engineering in Water Resources and Irrigation). Udahili huo umeongeza idadi ya wanafunzi wote kufikia 1,020 ikilinganishwa na 757 mwaka
2012/2013.
204.
Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Novemba
2013, wanafunzi 144 walihitimu
mafunzo katika fani za ufundi sanifu wa mifumo ya usambazaji wa majisafi na usafi
wa mazingira (80), utafutaji wa
maji chini ya ardhi na uchimbaji wa visima vya maji (Hydrogeology and water
well drilling) (22), haidrolojia na hali ya hewa (26) na teknolojia ya maabara ya uchunguzi wa ubora wa
maji (Water Quality Laboratory technology) wanafunzi (16). Katika
jitihada za kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike kujiunga na fani za ufundi,
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)
ilifadhili wanafunzi 52 wa kike
katika kozi za kuwawezesha kujiunga na masomo ya stashahada. Hii imewezesha
kuongeza udahili wa wanafunzi wa kike kutoka 67 mwaka 2012/2013 hadi 79 katika mwaka 2013/2014.
205.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Chuo kimeendelea kutoa ushauri juu ya
ubora wa maji kwa wateja 136
waliowasilisha sampuli za maji na kupima pamoja na kushauri juu ya upatikanaji
wa maji ardhini katika maeneo ya
Makambako (Njombe), Ilula (Iringa); Kiwalani, Kibamba na Kigamboni (Dar
es Salaam); Gairo (Morogoro);
Sikonge (Tabora), Korogwe (Tanga) na Makongo (Pwani). Aidha, washiriki 135 walipewa mafunzo ya muda mfupi katika fani
mbalimbali zinazohusu Sekta ya Maji.
206.
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya utoaji wa mafunzo,
Chuo kimesaini mikataba ya ununuzi wa vifaa ikiwa ni pamoja na samani na
vitendea kazi vya maabara za hydraulics, ubora wa maji, usambazaji maji, hali ya hewa, na udongo. Katika
kukabiliana na upungufu wa watumishi, Chuo kiliajiri watumishi wanane (8) na watumishi 70 walipatiwa mafunzo ya masuala ya ununuzi. Katika mwaka 2014/2015 chuo
kitaendelea kutoa mafunzo katika ngazi ya Stashahada (Water Technician) kwa wanafunzi 1,056, sambamba na mafunzo ya ngazi ya Shahada kwa
wanafunzi 135. Mafunzo ya muda
mfupi kwa washiriki 300
yatatolewa. Vilevile, Chuo kitafanya utafiti na kutoa ushauri katika masuala
yanayohusu Sekta ya Maji. Ili kukabiliana na upungufu wa ofisi na madarasa,
Chuo kitakarabati majengo yaliyopo na kuanza ujenzi wa jengo la ghorofa sita
lenye madarasa, maabara, maktaba na kumbi za mikutano.
207.
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) uliendelea na uchimbaji wa visima virefu katika
maeneo mbalimbali nchini. Hadi mwezi Machi, 2014 visima virefu 100 vilikamilika na ifikapo mwezi Juni, 2014 visima vingine 150 vinatarajiwa kuchimbwa katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, uchunguzi wa maji chini ya ardhi kwa ajili ya
uchimbaji visima virefu umekamilika katika maeneo 184 na ifikapo mwezi Juni, 2014 maeneo 244 yatachunguzwa. Jedwali Na. 14 linaloonesha orodha ya visima vilivyochimbwa na DDCA katika mwaka 2013/2014.
208.
Mheshimiwa Spika, Wakala umekamilisha mradi wa ujenzi wa mnara wa
kubeba tanki la kuhifadhi maji na ujenzi wa miundombinu ya maji katika ghala la
kuhifadhi madawa MSD-Kizota
(Dodoma). Vilevile, Wakala unaendelea kutekeleza kazi ya ujenzi wa tanki la
kuhifadhi maji NHC-Kibada (Kigamboni, Dar es Salaam) kazi ambayo imefikia asilima
90. Kazi hiyo itakamilika ifikapo
mwezi Juni, 2014. Kazi ya upembuzi yakinifu wa miradi ya mabwawa katika maeneo manne
(4) ya bwawa la Aviv Estate Wilayani Songea, bwawa la Saadani National Park Wilayani Pangani, bwawa la Pande Game Reserve Wilayani Bagamoyo na bwawa la Mfilisi (Mbegesela)
Wilayani Kilosa nayo imekamilika. Ujenzi wa bwawa la umwagiliaji la Aviv
Estate – Lipokera, Songea
utakamilika ifikapo mwezi Juni, 2014. Aidha, ukarabati wa mabwawa matatu (3)
ya Seke Ididi Wilayani Kishapu,
Habiya Wilayani Itilima na Matwiga Wilayani Chunya umeanza. Katika mwaka
2014/2015, Wizara yangu itaendelea na mpango wa kuujengea uwezo Wakala kwa
kununua mitambo mbalimbali ya uchimbaji visima na ujenzi wa mabwawa ili
kuongeza kasi ya kuchunguza maji chini ya ardhi, uchimbaji wa visima na ujenzi
wa mabwawa nchini. Wizara imeiagiza Wakala kuandaa mkakati wa kujitegemea (Exit
Strategy), lengo likiwa ni kuwa na
Wakala wenye weledi mkubwa na pia inayojitegemea katika kugharamia shughuli
zake zote.
209.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Bohari Kuu ya Maji
inaendelea kununua, kuhifadhi na
kusambaza vifaa na madawa ya kusafisha na kutibu maji kwenye Halmashauri mbalimbali, Mamlaka za Maji na Miradi ya
Kitaifa. Katika mwaka 2013/2014, vifaa mbalimbali vilisambazwa vikiwemo pampu
za maji, mabomba na viungio vyake. Aidha, Bohari Kuu ya Maji imekamilisha
ujenzi wa uzio na ukarabati wa ghala la kuhifadhi vifaa vya ujenzi. Wizara
yangu katika mwaka 2014/2015, itaendelea kuijengea uwezo Bohari Kuu ya Maji ili
iweze kununua vifaa vya ujenzi wa
miradi ya maji kwa wingi (Bulk Purchase) na kurahisisha upatikanaji wa vifaa hivyo katika Halmashauri, Mamlaka
za Maji na Miradi ya Kitaifa ili kwenda sambamba na Mpango wa “Tekeleza Sasa
kwa Matokeo Makubwa”. Aidha, nimeiagiza Bohari Kuu ya Maji kubuni
Miradi ya Ubia (Public Private Partnership-PPP) ili kupunguza utegemezi wake kwa Serikali.
3.5 MASUALA
MTAMBUKA
210.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2013/2014, Wizara imeendelea kutoa ushauri wa kisheria na elimu
kuhusu utekelezaji wa sheria mbalimbali na hatua za kuchukua dhidi ya ukiukwaji
wa sheria hizo. Elimu na ushauri umetolewa katika ngazi ya Wizara, Bodi za Maji
za Mabonde, Mamlaka za Maji, Halmashauri, Vyombo vya Watumiaji Maji na Wadau wa
Sekta ya Maji kupitia mikutano, kongamano, warsha na mafunzo mbalimbali. Jumla
ya nakala 478 za Sheria Na.11 ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji na Sheria Na.12 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira za mwaka
2009 na kanuni zake zimesambazwa. Aidha, mikataba 110 zikiwemo Randama za Makubaliano (MoU) zilipitiwa na kutolewa ushauri wa kisheria.
211.
Mheshimiwa Spika, Wizara ilikamilisha utayarishaji wa kanuni saba
(7) za Sheria za Maji ambazo ni:-
Usalama wa Mabwawa (The Water Resources Management (Dam Safety) Regulations,
2013), iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 237 la
tarehe 02/08/2013; Usambazaji wa Maji (The Water Supply Regulations 2013) na Mfuko wa Taifa wa Uwekezaji wa Maji (The
National Water Investment Fund Regulations 2013),
Gazeti la Serikali Na.
236 la tarehe 02/08/2013; Usimamizi
wa Maji chini ya Ardhi (The Ground Water (Exploration and Drilling)
Licensing Regulations, 2013), Gazeti
la Serikali Na. 219 la tarehe 02/07/2013; Uunganishaji wa Mamlaka za Maji
(Water Supply and Sanitation (Clustering
of Water Authorities) Regulations, 2013) Gazeti la Serikali Na
437 la tarehe 06/12/2013; Uteuzi na Sifa za Wajumbe wa
Bodi (EWURA (Appointment and Qualifications of Board Members) Regulations
2013), Gazeti la Serikali
Na 255 la tarehe 23/8/2013; Uteuzi na Ukomo wa Wajumbe wa Baraza la Ushauri la
Watumiaji (EWURA
(Appointment and Tenure of Members of the Consumer Consultative Council)
Regulations, 2013) Gazeti la
Serikali Na 256 la tarehe 23/8/2013; na Baraza la Ushauri kwa Serikali (EWURA (Government Consultative
Council) Regulations 2013), Gazeti
la Serikali Na. 254 la tarehe 30/08/2013. Nakala 95 za Kanuni hizo
zilisambazwa kwa jamii na pia zinapatikana kupitia tovuti ya Wizara ya Maji (www.maji.go.tz).
212.
Mheshimiwa Spika, utayarishaji wa rasimu ya kanuni za Bodi ya Leseni (The
Water Supply and Sanitation (Licensing Board) 2014) umekamilika. Rasimu ya tafsiri za Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na.11 ya mwaka 2009 na Sheria ya Huduma za Maji na Usafi
wa Mazingira Na. 12 ya mwaka 2009
kwa lugha ya Kiswahili zimekamilika na kuwasilishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali kwa ajili ya kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali.
213.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto za kisheria katika
utekelezaji wa Sheria za Maji, Wizara imetayarisha rasimu za marekebisho (amendment) ya Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na.11 ya mwaka 2009, Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa
Mazingira Na. 12 ya mwaka 2009 na
Sheria ya DAWASA Na. 20 ya mwaka
2001. Maoni ya wadau yanaendelea kukusanywa na kufanyiwa kazi. Katika mwaka
2014/2015, Wizara itaendelea
kutoa ushauri wa kisheria kuhusu utekelezaji wa sheria za maji na kuendelea
kutayarisha kanuni sita za sheria za maji.
214.
Mheshimiwa Spika, uanzishwaji wa Mfuko wa Maji (National Water
Investment Fund) unalenga kuongeza
fedha za uwekezaji katika Sekta ya Maji kwa mujibu wa Sheria Na. 12 ya mwaka 2009 ya Huduma ya Maji na Usafi wa
Mazingira. Katika kufanikisha azma hiyo, Wizara yangu imekamilisha Kanuni za
uendeshaji wa Mfuko wa Maji (National Water Investment Fund Regulations,
2013) na kuzichapisha kwenye Gazeti
la Serikali Na. 236 la tarehe 02/08/2013, na zimeanza kutumika. Maandalizi ya kuuwezesha Mfuko
kuanza kazi yamekamilika na kwa mwaka 2013/2014 Serikali ilitenga kiasi cha shilingi
milioni 100 kama kianzio (seed
money) kwa ajili ya Mfuko. Serikali
itaendelea kuutunisha Mfuko huo kwa kubaini vyanzo vingine vya mapato ikiwa ni
pamoja na ada na tozo mbalimbali.
215.
Mheshimiwa Spika, elimu na taarifa kuhusu maendeleo ya Sekta ya Maji
ni muhimu kwa jamii kama njia mojawapo ya kuelezea masuala ya usimamizi na
uendelezaji wa miradi ya maji nchini. Katika mwaka 2013/2014, Wizara iliendelea
kutoa elimu kwa wananchi kupitia maonesho, warsha, tovuti na vyombo mbalimbali
vya habari. Vilevile, mwezi Agosti 2013, Wizara yangu
ilishiriki kikamilifu katika maonesho ya Kilimo ya Nanenane yaliyofanyika
Nzuguni Mjini Dodoma ambapo vipeperushi, majarida na machapisho mbalimbali
yanayohusu shughuli zinazotekelezwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya
Maji vilisambazwa kwa jamii. Pia, elimu ya Sera ya Maji kwa lugha nyepesi
ilitolewa kwa wananchi kupitia majarida na santuri za maigizo ili kuifahamu
mipango na mikakati ya Wizara. Aidha, katika Maadhimisho ya Wiki ya Maji
yaliyofanyika kitaifa Mkoani Dodoma mwezi Machi, 2014, Wizara yangu ilitoa
jumla ya machapisho 5,000 na
vipindi saba (7) vya redio na
luninga.
216.
Mheshimiwa Spika, Wizara ilitoa vipindi maalum kupitia vyombo vya
habari kuhusiana na hali ya maji Mkoani Dodoma; mradi wa maji wa kitaifa wa
Masasi-Nachingwea; upanuzi wa mradi wa maji wa Ruvu Chini; mradi wa maji wa
Kahama-Shinyanga; na kituo cha utafiti cha kuondoa madini ya fluoride kwenye maji kilichopo Ngurdoto, Mkoani Arusha.
Vipindi hivyo vililenga katika kufafanua na kuelimisha jamii katika masuala
mbalimbali ya Sekta ya Maji. Pia, makala mbalimbali zilitolewa magazetini na
kwenye mitandao ya kijamii ya mawasiliano kuelezea kazi mbalimbali
zinazotekelezwa na Wizara. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea
kuelimisha wananchi na kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu Sekta ya Maji;
kuandaa na kutangaza vipindi katika luninga na redio; na kuboresha tovuti ya
Wizara ili wananchi wengi zaidi waitumie.
217.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu imeendelea kuimarisha matumizi ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuboresha utoaji wa huduma na
utendaji kazi. Uimarishaji wa matumizi ya TEHAMA ulihusu masuala yafuatayo:-
(i)
Kuboresha mfumo wa kielektroniki wa takwimu na taarifa (Water Sector Management Information system) ili kusaidia masuala
ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mipango na miradi kwenye Sekta ya
Maji (scaling up/out MIS to cover M&E functions – physical aspects). Vilevile, mafunzo ya mfumo huo yametolewa kwa watumishi 40 kutoka Makao
Makuu ya Wizara, 72 kutoka Halmashauri za Wilaya mpya, nane (8) Mikoa mipya, 62 Mamlaka za Majisafi na Majitaka na watumishi 18 wa Bodi
za Maji za Mabonde. Matumizi ya mfumo huo yameboresha usimamizi wa fedha za
utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji;
(ii)
Matumizi ya mfumo wa
kielektroniki wa ukusanyaji wa takwimu na utambuzi wa vituo vya kuchotea maji
vijijini (Water point mapping)
kwa kutumia TEHAMA (www.wpm.maji.go.tz). Hadi mwezi Machi 2014, mafunzo ya mfumo huo
yametolewa kwa watumishi 50
kutoka Makao Makuu ya Wizara, Wahandisi wa Maji 155 wa Halmashauri, Wahandisi wa maji 26 kwenye Sekretarieti za Mikoa, Wasajili 163 wa Vyombo vya Watumiaji Maji kwenye Halmashauri na
Maafisa Maji wa Mabonde watatu (3);
(iii)
Kuendeleza juhudi za
Serikali za utekelezaji wa Serikali Mtandao (e-Government) kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (e-Government
Agency) katika utayarishaji wa
mikakati ya kutekeleza ‘Open Data.’
Mikakati hiyo itahusisha kujenga uwezo wa Wizara na
Taasisi katika matumizi ya Serikali Mtandao ili kutoa taarifa mbalimbali za
utekelezaji wa miradi ya maji na matumizi ya fedha kwa uwazi zaidi.
218.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kuimarisha matumizi ya
TEHAMA katika ukusanyaji na uchambuzi wa kina wa takwimu pamoja na kutathmini
hali halisi ya upatikanaji wa maji vijijini. Tathmini ya hali halisi itafanyika
baada ya kukamilisha ukusanyaji wa takwimu na utayarishaji wa ramani za vituo
vya kuchotea maji vijijini (Water Point Mapping). Aidha, Wizara itaendeleza
juhudi za kujenga uwezo wa Halmashauri za Wilaya na Sektretarieti ya Mikoa
katika kutumia mfumo huo.
219.
Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zitakazotekelezwa ni pamoja na:- kuimarisha mfumo wa
kielektroniki wa takwimu na taarifa ili kusaidia masuala ya ufuatiliaji na
tathmini; kutekeleza Mpango wa ‘Open
Data’ ili kuwezesha utoaji wa
takwimu na taarifa za Sekta ya Maji kwa uwazi. Lengo ni kurahisisha ushiriki wa
wananchi na wadau katika kuendeleza Sekta ya Maji nchini kwa kuzingatia maeneo
ambayo yataonekana kuwa na mapungufu zaidi ya huduma za maji; kujenga uwezo wa
Wizara na Taasisi katika matumizi ya TEHAMA ili kuboresha huduma ndani ya Sekta
ya Maji.
220.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuzingatia umuhimu wa kuwepo
kwa uwiano wa kijinsia baina ya
wanawake na wanaume katika ngazi za
uongozi na maamuzi. Katika mwaka 2013/2014, asilimia ya wanawake katika
vyombo vya maamuzi kwenye ngazi ya Wizara na Taasisi zake ni zaidi ya asilimia
30 kama
ifuatavyo:- Wizara (asilimia 39), Bodi ya Taifa ya Maji (asilimia 33), Bodi za Mabonde ya
Maji (asilimia 34), Bodi za Mamlaka za Maji Mijini (asilimia 31), na Bodi za Wakala (asilimia
50).
Pia, kwa upande wa vyombo vya watumia maji, suala la
ushiriki wa wanawake kwa asilimia 50 linaendelea kuzingatiwa kulingana na mwongozo uliotolewa na Wizara.
221.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu imeshirikiana na
wadau wa masuala ya jinsia (Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto; TGNP; na TaGLA) kutoa mafunzo kwa
watumishi kwa awamu ili kujenga uwezo wa uongozi katika kusimamia na kutekeleza
masuala ya jinsia. Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani
(GIZ) inaandaa Mkakati na Mwongozo wa masuala ya jinsia ambao utatumika katika
kupanga mipango madhubuti na kubaini changamoto zinazohusu jinsia mahala pa kazi
na kuzipatia ufumbuzi. Katika
mwaka 2014/2015, Wizara itaandaa benki ya takwimu ya masuala ya jinsia kwa
lengo la kuwa na takwimu sahihi za
ushiriki unaozingatia jinsia
katika mipango, ufuatiliaji na usimamizi wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.
222.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu imetoa elimu
kuhusu UKIMWI kwa watumishi 580 wa
Wizara. Kati ya hao, watumishi 160
walipata ushauri nasaha na kukubali kupima VVU kwa hiari ili kujua afya zao.
Aidha, Dawati la UKIMWI la Wizara lilishiriki katika maonesho ya Wiki ya Maji
yaliyofanyika kitaifa Mjini Dodoma kuanzia tarehe 16 - 22/3/2014 kwa kutoa
elimu, ushauri nasaha pamoja na upimaji wa hiari kwa jamii. Katika mwaka
2014/2015, kwa kuzingatia
maelekezo ya Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Wizara yangu itaandaa Mpango wa Ukimwi Mahali pa Kazi
(HIV Plan at Work Place) kwa
kutekeleza yafuatayo:- kutathmini hali ya UKIMWI katika Wizara; kutoa mafunzo
elekezi kwa waelimisha rika na watumishi kwa ujumla; kutenga bajeti ya masuala
ya ukimwi; kuandaa mpango wa mafunzo utakaoonesha aina ya mafunzo
yatakayotolewa; na kuzingatia mahitaji halisi ya watumishi wanaoishi na VVU
kama yalivyoainishwa katika sheria ya kazi na mwongozo wa utumishi wa umma.
Aidha, Wizara yangu imeendelea kutoa lishe kamili kwa watumishi wake 10 waliojiweka wazi kuwa wanaishi na VVU.
223.
Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Aprili 2014, Wizara imepokea watumishi 22 kutoka Sekretarieti ya Ajira. Kati ya hao, Mhasibu
Msaidizi mmoja (1), Wahaidrolojia
watatu (3), Wakemia wanne (4), Mhudumu wa Afya mmoja (1), Mafundi Sanifu sita (6) katika fani ya ujenzi, wawili (2) fani ya haidrolojia na watano (5) wa
fani ya haidrojiolojia. Katika mwaka 2014/2015, Wizara inatarajia kuwapandisha
vyeo watumishi 367 na kuwaajiri
watumishi wapya 429 wa kada
mbalimbali. Aidha, Wizara inaendelea kufuatilia kibali cha ajira mbadala kwa
ajili ya kujaza nafasi 28 zilizo
wazi za watumishi wa kada mbalimbali waliostaafu, waliofariki au kuacha kazi.
224.
Mheshimiwa Spika, mwezi Januari, 2014 watumishi 42 walipatiwa mafunzo elekezi kuhusu utumishi wa umma.
Vilevile, mwezi Februari na mwezi Aprili 2014, Wizara kwa kushirikiana na
Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) ilitoa mafunzo kwa viongozi 36 wa Wizara pamoja na Maafisa
Watendaji Wakuu wa taasisi zilizo chini yake kwa ajili ya kuimarisha uongozi na utendaji kazi. Katika mwaka
2014/2015, Wizara yangu itaendelea kutekeleza mpango wa kuwapatia watumishi
mafunzo ya muda mrefu na ya muda mfupi ili kukidhi sifa za miundo ya kada zao
na kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi. Mafunzo hayo yatatolewa kwa
kuzingatia Mpango wa Mafunzo wa Wizara.
(h)
Mapambano Dhidi ya Rushwa
225.
Mheshimiwa Spika, tathmini ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya
maji katika maeneo mbalimbali nchini imeonesha kupungua kwa malalamiko ya
kushuka kwa maadili kutokana na vitendo vya rushwa na watumishi wasiokuwa
waaminifu kuhujumu miradi na miundombinu ya maji. Mwanzoni mwa mwezi Machi
2014, Wizara yangu kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi
ilitoa mafunzo ya maadili kwa viongozi wote wa Wizara na taasisi zake za EWURA,
DAWASA, DAWASCO, DDCA, Bohari Kuu ya
Maji na Chuo cha Maji. Katika mwaka 2014/2015, mafunzo ya aina hiyo
yanatarajiwa kutolewa kwa watumishi wengine wa Wizara ili kujenga uelewa wa
pamoja.
(i)
Uratibu wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji
226. Mheshimiwa Spika, Wizara inatekeleza Sera ya Maji ya Mwaka 2002 ambayo
imeweka mfumo madhubuti na endelevu wa kusimamia na kuendeleza rasilimali za
maji nchini. Hii ni pamoja na kuandaa na kutekeleza taratibu za kisheria na
kuweka muundo wa kitaasisi wenye uwezo wa kutekeleza Sera. Muundo huo
unaohusisha ushirikishwaji wa Wadau wa Sekta ya Maji katika hatua mbalimbali za
utekelezaji ikiwa ni pamoja na kubuni, kupanga, kusanifu, kujenga, kusimamia,
kuendesha na matengenezo miradi ya maji pamoja na kuchangia gharama za huduma
za maji. Sera hiyo inatekelezwa kupitia Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Maji
(2006-2015) na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (2006-2025).
227. Mheshimiwa Spika, Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (Water Sector
Development Programme – WSDP) ni ya kipindi cha
miaka 18 kuanzia mwaka 2006 hadi 2025.
Awamu ya kwanza ya miaka mitano ya utekelezaji wa Programu
ilianza mwezi Julai, 2007 na ilipangwa kukamilika mwezi Juni, 2012. Ili
kukamilisha miradi iliyopangwa, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa
Maendeleo iliamua kuongeza muda wa utekelezaji wa awamu ya kwanza kutoka Juni,
2012 hadi Juni, 2014. Kulingana na Hati ya Makubaliano kati ya Serikali na
Washirika wa Maendeleo, Wizara yangu imeendelea kuandaa taarifa za utekelezaji
wa Programu na kuratibu maandalizi ya mikutano ya majadiliano kati ya Serikali,
Washirika wa Maendeleo na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayohusiana na Sekta
ya Maji.
228.
Mheshimiwa Spika, lengo la
uratibu wa Programu ni kuhakikisha kuwa Programu ya Maji inatekelezwa kulingana
na makubaliano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo ikiwemo kuhakikisha
kuwa taarifa za utekelezaji na taarifa za matumizi ya fedha zinaandaliwa kwa
wakati. Pia, kuhakikisha kuwa ushirikiano wa kiutendaji unakuwepo muda wote wa
utekelezaji wa Programu kati ya Wizara ya Maji na OWM-TAMISEMI, Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Fedha na
Wizara nyingine ambazo ni watumiaji wakubwa wa maji, mfano, Wizara ya Nishati
na Madini na Wizara ya Kilimo. Aidha, ushirikiano wa kiutendaji kati ya ngazi
ya Wizara hizo, Sekretarieti za Mikoa, Halmashauri, Bodi za Maji za Mabonde,
Mamlaka za Maji Mijini na Miradi ya Kitaifa unakuwepo muda wote wa utekelezaji
ili kuhakikisha kuwa viwango na kasi ya utekelezaji kwa kuzingatia thamani ya
fedha inayotumika vinafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu. Katika mwaka
2014/2015, Wizara yangu itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kutoa taarifa
mbalimbali za utekelezaji wa Programu na kuratibu majadiliano baina ya wadau wa
sekta.
(j)
Maandalizi ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Pili
229. Mheshimiwa Spika, tathmini ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Programu
iliyohusisha wadau wa Sekta ya Maji ilifanyika mwezi Februari hadi Mei, 2013.
Tathmini hiyo ilipitia maeneo yote yanayohitaji maboresho kwa ajili ya Awamu ya
Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (2014/2015 – 2018/2019).
Mapendekezo hayo yalihusu kuimarishwa kwa mipango shirikishi ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji; mipango ya ujenzi wa miradi ya maji katika miji mikuu ya wilaya na
miji midogo na kuboresha huduma za maji katika miji mikuu ya mikoa; na mipango ya ujenzi wa miradi ya maji vijijini
inayohusisha uwekezaji, ukarabati, upanuzi, ujenzi wa miradi mipya na
uendeshaji na matengenezo ya miradi katika Halmashauri. Pia, tathmini
ilibainisha umuhimu wa kuzijengea uwezo taasisi zinazotekeleza Programu ikiwa
ni pamoja na kuongeza wigo wa kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira kwa
kuhusisha maeneo yote ya vijijini na kwenye taasisi za huduma za jamii zikiwemo
shule na vituo vya huduma ya afya kwa kushirikiana na sekta nyingine.
230. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imepokea maoni na ushauri kutoka kwa Wadau
kuboresha rasimu ya awamu ya pili ya Programu. Kikosi-kazi kimekamilisha kazi
hiyo na kitabu cha awamu ya pili ya Programu kipo tayari kutumika kama mwongozo
wa mipango ya utekelezaji na bajeti ya kila mwaka kuanzia 2014/2015 hadi mwaka
2018/2019.
231.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika mwaka 2013/2014, Sekta ya Maji
imeendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali. Changamoto hizo na hatua zinazochukuliwa ili kukabiliana nazo ni kama
ifuatavyo:-
(a)
Kuongezeka kwa
Mahitaji ya Maji Yasiyowiana na Uwekezaji kwenye Miradi ya Sekta ya Maji
232.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inakabiliwa na changamoto ya kuongezeka kwa
idadi ya watu, hususan mijini. Miji hiyo inakua kwa kasi kubwa sana wakati
miundombinu ya kusambaza maji imeendelea kubaki ile ya zamani. Idadi ya watu
mijini imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 4.5 ambapo kwa vijijini ni asilimia
2.3 kwa
mwaka. Kwa Jiji la Dar es Salaam idadi ya watu inakua kwa wastani wa asilimia
5.6 kwa
mwaka. Ongezeko hilo la watu linasababisha mahitaji makubwa ya maji yasiyowiana
na uwezo wa Serikali kuwekeza kwenye miundombinu ya maji. Aidha, kwa upande wa
vijijini upungufu wa huduma ya maji umesababishwa na uwekezaji mdogo wa
miundombinu ya maji katika baadhi ya maeneo nchini. Sababu nyingine ni
kuharibika kwa miundombinu ya maji pamoja na vituo vya kuchotea maji
vilivyojengwa.
233.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo, Wizara yangu
imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji kwa kukarabati, kupanua na kujenga
miradi mipya mijini na vijijini. Kwa upande wa uboreshaji wa huduma za maji
mijini, ujenzi wa miradi ya maji unaendelea katika miji mikuu ya mikoa na
wilaya, miji midogo pamoja na miradi ya kitaifa. Katika Jiji la Dar es Salaam
upanuzi wa mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu, ujenzi wa bomba
kuu kutoka Bagamoyo hadi kwenye matanki ya Chuo Kikuu cha Ardhi, uchimbaji wa
visima vya Kimbiji na Mpera na ujenzi wa Bwawa la Kidunda unaendelea. Aidha,
kwa upande wa vijijini, Serikali imeendelea kukarabati na kujenga miradi ya
kipaumbele ambayo inatoa huduma kwa wananchi wengi zaidi ikiwa ni pamoja na
kuendelea kwa ujenzi wa mradi wa maji wa vijiji 10 kila Halmashauri.
234.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji kwenye maeneo haya niliyoyaainisha kwa kiasi
kikubwa umeathiriwa na uhaba mkubwa wa fedha. Uhaba huu unatokana na kukasimiwa bajeti ndogo ambayo haikidhi mahitaji
ya uwekezaji katika miundombinu ya maji. Fedha inayotolewa kwa ajili ya
utekelezaji wa miradi ya maji huwa ni kidogo ikilinganishwa na kiasi kinachokasimiwa.
Kwa miaka mitatu mfululizo fedha za maendeleo za ndani zilizotolewa kwa Fungu
la Wizara ya Maji zilikuwa ni kidogo kulinganisha na fedha zilizokasimiwa.
235.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa
fedha 2011/2012, fedha zilizokasimiwa zilikuwa ni shilingi 41,565,045,000 na kiasi kilichotolewa ni shilingi 24,746,549,522 ambayo ni pungufu kwa asilimia 40.5. Kwa mwaka 2012/2013 jumla ya shilingi
140,015,967,000 zilikasimiwa ambapo
fedha zilizotolewa zilikuwa ni shilingi 104,000,000,000 ambayo ni pungufu kwa asilimia 25.7; na kwa mwaka 2013/2014, kiasi cha shilingi 312,066,164,000 zilikasimiwa na kiasi kilichopatikana hadi mwezi Machi, 2014 ni shilingi
bilioni 86sawa na upungufu wa asilimia 72.4. Jedwali Na. 15 linaonesha mwenendo wa upatikanaji wa fedha za ndani za maendeleo tangu
kuanza kwa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.
236.
Mheshimiwa Spika, Serikali
hujenga miradi ya maji vijijini na baada ya kukamilika huikabidhi kwa wananchi
kwa ajili ya kuiendesha. Uendeshaji na usimamizi wa miradi hiyo umekuwa ni
changamoto kubwa kwa maeneo mengi vijijini kutokana na kutokuwa na taaluma na
uwezo wa kugharamia matengenezo pindi miradi inapoharibika. Kwa hali hiyo,
miradi mingi vijijini imeshindwa kutoa huduma kama ilivyokusudiwa na kupunguza
kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji safi kwa wananchi. Kukabiliana na
changamoto hiyo, Halmashauri zimeelekezwa kuunda na kusajili vyombo vya
watumiaji maji kwenye miradi ya maji vijijini ili kuwepo na usimamizi wa karibu
katika kuendesha miradi hiyo. Aidha, vyombo hivyo vimejengewa uwezo wa mafunzo
kuhusu usimamizi na utunzaji wa fedha zinazotokana na mauzo ya maji; na
uendeshaji na matengenezo ya miradi ili kuifanya huduma hiyo kuwa endelevu.
237.
Mheshimiwa Spika, ongezeko la mahitaji ya huduma ya maji halilingani
na upatikanaji wa vifaa na vitendea kazi vya kutekeleza miradi ya maji na
hivyo, kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati. Kutokana na hali hiyo,
Wizara inajadiliana na Wadau mbalimbali walioonesha nia ya kuwekeza kwenye
miradi ya maji na usafi wa mazingira ili kutekeleza miradi hiyo kupitia ubia
baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partinership - PPP). Hadi sasa usanifu unaendelea kwa miradi ya PPP ikiwemo uvunaji wa maji ya bahari (desalination
project) kwa ajili ya Jiji la Dar es
Salaam na Handeni Trunk Main - HTM.
Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kushawishi wawekezaji wengi
zaidi ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji na usafi wa mazingira
kupitia PPP.
238.
Mheshimiwa
Spika, hatua zinazoendelea
kuchukuliwa kukabiliana na uhaba wa fedha ni pamoja na Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kutafuta fedha zaidi kutoka Washirika wa
Maendeleo, na kuhakikisha kuwa fedha zinazokasimiwa zinatolewa kama
zilivyopangwa na kwa wakati. Hadi mwezi Machi 2014, Washirika wa Maendeleo
wameahidi kuongeza jumla ya Dola za Marekani milioni 73 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Sekta ya Maji.
Wizara inaendelea kujadiliana na Washirika wa Maendeleo ili watoe fedha
walizoahidi kulingana na makubaliano.
(b)
Kupungua kwa
rasilimali za maji
239.
Mheshimiwa Spika, upungufu wa rasilimali za maji nchini ni miongoni mwa
changamoto zinazoikabili Sekta ya Maji na kusababisha maeneo mengi kukumbwa na uhaba wa maji. Miongoni mwa sababu za
upungufu huo ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, uvamizi katika vyanzo vya maji
kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, uchafuzi wa vyanzo vya maji na matumizi
holela ya maji.
240.
Mheshimiwa Spika, athari za mabadiliko ya tabianchi katika rasilimali za maji ni pamoja na kutotabirika
kwa urahisi majira ya mwaka na mtawanyiko wa mvua. Hali hii husababisha mvua
kunyesha kwa uchache au wingi na hivyo kusababisha maeneo kuwa kame na wakati
mwingine kukumbwa na mafuriko. Matukio yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi
yanaathiri vyanzo vya maji pamoja na miundombinu yake.
241.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko
ya tabianchi, Wizara yangu imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo
kuwekeza katika ujenzi na uendelezaji wa vyanzo vya maji na kuhifadhi maeneo
oevu. Hatua hizo zinalenga kuboresha upatikanaji wa maji kwa kipindi chote cha
mwaka. Aidha, Wizara yangu imeandaa mipango shirikishi ya uendelezaji na
usimamizi wa rasilimali za maji kwa Bodi za Maji za Mabonde kama njia mojawapo
ya kukabiliana na athari za mabadaliko ya tabianchi. Utekelezaji wa mipango
hiyo, unahusisha sekta na wadau mbalimbali nchini katika kupanga na kutumia
rasilimali za maji kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
242.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeandaa mpango mkakati wa kutekeleza
Mkakati wa Taifa wa Mabadiliko ya Tabianchi ili kutekeleza shughuli za
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika Sekta ya Maji. Vilevile, kupitia
Jukwaa la Majadiliano ya athari za mabadiliko ya tabianchi katika Sekta ya
Maji, Wizara yangu imekuwa ikishirikiana na taasisi za kiserikali na zisizo za
kiserikali pamoja na wadau wa sekta katika utambuzi wa mbinu za kukabiliana na
athari hizo kupitia taarifa za shughuli zinazotekelezwa na wadau hao na tafiti
mbalimbali zinazofanyika nchini kuhusiana na athari za mabadiliko ya tabianchi
kwenye Sekta ya Maji. Pia, Serikali inaendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii
juu ya teknolojia ya uvunaji na uhifadhi wa maji ya mvua katika ngazi ya kaya
ili kuongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi.
243.
Mheshimiwa Spika, uvamizi na uchafuzi wa vyanzo vya maji umechangia kwa
kiasi kikubwa upungufu katika vyanzo vya maji nchini. Hali hii imechangiwa na
ukosefu wa mipango endelevu ya matumizi bora ya ardhi na hivyo maeneo mengi ya
vyanzo vya maji kutumika katika shughuli za uzalishaji mali hususan kilimo.
Shughuli hizo zisizozingatia matumizi bora ya ardhi zimesababisha vyanzo vingi
kuharibiwa na kuchafuliwa hatimaye kupoteza wingi na ubora wa maji. Vilevile,
kumekuwa na matumizi yasiyozingatia vibali vya matumizi vinavyotolewa na
mamlaka husika na hivyo kusababisha upungufu wa rasilimali hiyo adimu kwa
watumiaji wengine na kusababisha migogoro ya mara kwa mara katika maeneo
mbalimbali nchini.
244.
Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeendelea kuviimarisha vyombo vya
kisheria vya usimamizi wa rasilimali za maji ili viweze kusimamia sheria,
kanuni na miongozo iliyowekwa. Vyombo hivyo vinaendelea kutekeleza majukumu yao
na kuhakikisha rasilimali za maji zilizopo maeneo husika zinagawanywa na
kutumiwa kwa mujibu wa sheria. Aidha, maeneo ya vyanzo vya maji yamebainishwa
na utaratibu wa kuyawekea mipaka unaendelea ili kulinda maeneo hayo
yasiharibiwe na kuchafuliwa na shughuli mbalimbali za binadamu.
(c)
Kiwango Kikubwa
cha Upotevu wa Maji
245.
Mheshimiwa Spika, miongoni mwa changamoto ambazo Mamlaka za maji katika miji mikuu
ya mikoa, wilaya, miji midogo pamoja na miradi ya Kitaifa inazokabiliana nazo
ni kiwango kikubwa cha upotevu wa maji (NRW). Hali hii inasababisha kutofikiwa kwa malengo ya
makusanyo ya maduhuli na hivyo kuathiri utekelezaji wa shughuli za uendeshaji
kutokana na uhaba wa fedha. Kwa mamlaka za miji mikuu ya mikoa isipokuwa DAWASCO, makadirio ya kiwango cha maji yasiyolipiwa kwa
kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2011/2012 hadi 2013/2014 yanaonesha mamlaka
hizo zinapoteza wastani wa zaidi ya shilingi milioni 30 kwa kila mamlaka kwa mwaka, sawa na asilimia 34.2
ya upotevu wa maji. Kwa upande wa DAWASCO, wastani
wa upotevu wa maji kwa kipindi hicho ni asilimia 52 ambapo ni sawa na shilingi bilioni 50. Upotevu huo wa maji unatokana na sababu zifuatazo:-
(i)
Uchakavu wa Miundombinu
246. Mheshimiwa Spika, mamlaka nyingi za maji bado zina miundombinu ambayo
ilijengwa miaka mingi iliyopita, hali hiyo imesababisha miundombinu hiyo
kuzidiwa uwezo na msukumo mkubwa wa maji yanayotoka kwenye mitambo na
kusababisha kuwepo kwa upotevu mkubwa wa maji. Vilevile, uwekezaji wa
miundombinu ya maji katika baadhi ya miradi mipya hususan miradi ambayo
uwekezaji wake ulilenga bomba kuu pekee na kuacha miundombinu ya usambazaji.
Uwekezaji wa aina hiyo umesababisha mabomba ya zamani ya usambazaji kushindwa
kuhimili msukumo mkubwa wa maji
kutoka mradi mpya na kusababisha kupasuka mara kwa mara kwa mabomba hayo.
Upasukaji huo umeongeza upotevu mkubwa wa maji. Mfano wa matokeo hayo ya
uwekezaji ni kwenye mradi mpya wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira,
Iringa ambayo upotevu wake wa maji ulifikia asilimia 60 baada ya kukamilika kwa mradi.
247.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inachukua hatua za kukarabati miundombinu ya maji katika mamlaka mbalimbali na
kuhakikisha wakati wa kuanzisha miradi ya uzalishaji maji, usanifu unazingatia
mfumo wa mabomba ya usambazaji maji. Vilevile, Wizara imeziagiza mamlaka hizo
kuviimarisha vitengo vya matengenezo ili viweze kukarabati mitandao ya maji kwa
wakati pindi mivujo inapojitokeza.
(ii) Wizi wa Maji
248. Mheshimiwa
Spika, upotevu wa maji umeendelea kuwa changamoto kubwa kwenye Mamlaka za maji
mijini kutokana na baadhi ya wateja wasiokuwa waaminifu kujipatia huduma ya
maji kinyume na taratibu (by-pass, and illegal connection). Aidha,
udanganyifu wa wateja kuchezea dira za maji ili kubana matumizi ya maji nao
umechangia upotevu huo.
249.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka za maji kwa
kushirikiana na Manispaa za miji husika zimeweka mikakati ya kufuatilia wizi
huo wa maji. Vilevile, Wizara kwa kuzingatia matakwa ya Sheria Na. 12 ya mwaka 2009 ya
Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira pamoja na Kanuni zake, inazitaka
mamlaka hizo kutumia wanasheria wao na vyombo vingine vya usalama kufuatilia
wizi wa maji na hujuma kwenye miundombinu ya maji. Kwa sasa Wanasheria wa Wizara, DAWASA na DAWASCO wanaendelea na taratibu za kuziboresha sheria hizo ili kuzipa nguvu
katika utekelezaji wake. Aidha, Kikosi Kazi cha kufuatilia na kubaini wezi wa
maji katika Jiji la Dar es salaam kimeundwa na kinaendelea na kazi hiyo kwa
ufanisi. Hadi mwezi Machi 2014, jumla ya watu 107 walituhumiwa kuwa ni wezi wa maji na wamefikishwa
mahakamani na kesi zao ziko kwenye hatua mbalimbali za kisheria.
(iii) Hujuma
kwenye Miundombinu ya Maji
250.
Mheshimiwa Spika, miundombinu ya usambazaji wa maji na uondoaji
majitaka imeendela kuhujumiwa kutokana na kushamiri kwa biashara ya chuma chakavu. Biashara hiyo imeleta athari kubwa
katika maendeleo ya Sekta ya Maji ambapo wahujumu hao wamefikia hatua ya
kuharibu mitandao ya usambazaji majisafi na majitaka kwa kuiba mabomba ya
majisafi, mifuniko ya majitaka, pampu, dira na viungio mbalimbali vya mabomba
ya maji na hatimaye kuuza vifaa hivyo kama vyuma chakavu. Kutokana na hujuma
hizo, kero ya uhaba wa maji kwa wananchi imeongezeka na pia kusababisha
uchafuzi na uharibifu wa mazingira.
251.
Mheshimiwa Spika, hatua zinazochukuliwa ni
pamoja na kutoa elimu kwa wananchi
kupitia vyombo mbalimbali vya habari juu ya utunzaji wa miundombinu ya maji na
kusisitiza ulinzi shirikishi wa miundombinu hiyo. Aidha, Mamlaka zinashirikiana
na Sekretarieti za Mikoa, Serikali za Mitaa pamoja na Jeshi la Polisi kudhibiti
biashara hiyo ya chuma chakavu. Hatua hiyo imesaidia kukamatwa kwa watuhumiwa
na kufikishwa katika vyombo vya Sheria katika Mikoa ya Dodoma, Tabora, Mbeya,
Moshi na Dar es Salaam na kesi zao ziko katika hatua mbalimbali za kusikilizwa.
Kuanzia mwaka 2010 hadi mwezi Machi, 2014 hasara iliyopatikana kwa Mamlaka za
majisafi mijini kutokana na kuibiwa kwa mitandao ya usambazaji maji inakadiriwa
kufikia kiasi cha shilingi bilioni 1.5 ambapo DAWASA pekee ni shilingi
milioni 700.
(d) Upungufu wa Wataalam
katika Sekta ya Maji
252.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Maji inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wataalam 7,211, unaotokana na Serikali
kutoajiri kwa muda mrefu, kuongezeka kwa idadi ya Mikoa, Wilaya, Halmashauri
pamoja na kustaafu kwa baadhi ya watumishi. Idadi ya wataalam wanaohitajika
kwenye Sekta ya Maji katika ngazi ya Wizara, Sekretarieti za Mikoa na
Halmashauri ni 8,749. Wataalam waliopo kwenye Sekta ya Maji ni 1,538. Mchanganuo wa mahitaji
ya Wataalam wa kada mbalimbali katika Sekta ya Maji umeainishwa katika Jedwali
Na. 16.
253.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo, Wizara
yangu iliomba kibali cha ajira Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma
mwezi Desemba, 2013. Napenda kuwajulisha Waheshimiwa Wabunge kwamba mnamo mwezi
Machi, 2014 Ofisi hiyo imetoa kibali cha nafasi 475 kwa ajili ya kuajiri Wahandisi wa maji 125 na Mafundi Sanifu 350
ambao watafanya kazi kwenye miradi ya maji iliyopo kwenye Halmashauri. Hatua za
kuajiri wataalam hao zinaendelea kufanywa na Wizara yangu kwa kushirikiana na
Sekretarieti ya Ajira.
254.
Mheshimiwa Spika, usimamizi wa mikataba inayosainiwa na Wakandarasi ni muhimu katika
kuhakikisha miradi ya maji inajengwa na kukamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa. Hata
hivyo, kutokana na upungufu wa wataalam katika Sekta ya Maji, usimamizi wa
mikataba hiyo umekuwa hafifu na kusababisha miradi mingi kuchelewa na kwa
wakati mwingine, kujengwa chini ya viwango na kutumia gharama kubwa. Katika
kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maji, Wizara imewasilisha
maombi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili kuajiri kwa mkataba
Wataalam wa maji wenye uzoefu kwa ajili ya kuwajengea uwezo Wataalam wapya
watakaoajiriwa. Vilevile, baadhi ya wahandisi wazoefu kutoka Wizarani
wamehamishiwa kwenye Sekretarieti za Mikoa ili kuongeza uwezo wa usimamizi na
ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maji kwenye Halmashauri mbalimbali
nchini.
(e)
Upatikanaji wa
Taarifa Sahihi na kwa Wakati kutoka kwa Watekelezaji
255.
Mheshimiwa Spika, katika kuratibu utekelezaji wa miradi ya maji
kumekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa taarifa sahihi kutoka kwa
watekelezaji wa miradi hiyo hususan Halmashauri. Aidha, taarifa hizo zimekuwa
hazifiki kwa wakati na hivyo kuchelewesha maamuzi na utekelezaji wa miradi
inayofuata. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali imeanza kutumia Mfumo
wa Taarifa za Mikataba ya Miradi na Fedha (Management Information System -
MIS) ambapo mafunzo maalum
yametolewa kwa watekelezaji wa miradi ya maji. Serikali pia, inaandaa mfumo wa
kompyuta kwa ajili ya kuweka kumbukumbu za hali ya vituo vya kuchotea maji (water
point mapping system) utakaounganishwa kwenye Halmashauri zote kwa ajili ya
kuweka na kuboresha kumbukumbu.
(f)
Mawasiliano kati
ya Wizara na Wadau wa Sekta ya Maji
256.
Mheshimiwa
Spika, kumekuwepo mawasiliano hafifu
baina ya Wizara na wadau wengine wanaotekeleza miradi ya majisafi na usafi wa
mazingira tangu kuanza kwa awamu ya kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya
Maji. Hali hii inasababisha pamoja na mambo mengine, upatikanaji wa taarifa
sahihi kuwa mgumu na ucheleweshaji wa utoaji wa maamuzi ya utekelezaji.
Mathalan, kwa kipindi kirefu upatikanaji wa taarifa za matumizi ya fedha za
utekelezaji wa Programu zimekuwa hazipatikani kwa usahihi na kwa wakati
kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu ya uhakika ya mawasiliano katika baadhi
ya maeneo nchini.
257.
Mheshimiwa Spika, vilevile, kutokuwepo kwa mawasiliano ya karibu kati
ya Sekta ya Maji na Sekta nyingine imesababisha utekelezaji wa miradi ya maji
kukwama au kucheleweshwa kwa muda mrefu. Tumeshuhudia utekelezaji wa miradi
kama vile ujenzi wa mabomba makuu ya maji kuchelewa kujengwa kutokana na
matakwa ya kuomba vibali vya kukatiza katika hifadhi za barabara na zuio za
kimahakama. Vilevile, upatikanaji wa vibali au kumalizika kwa kesi za mahakama
kunachukua muda mrefu na hivyo kuathiri utekelezaji wa miradi ya maji
kukamilika katika muda uliopangwa. Hali hiyo mara nyingi inawavunja moyo
wananchi kwa kukosa huduma ya maji pamoja na Washirika wetu wa maendeleo
wanaochangia miradi ya maji, hivyo kupunguza michango yao ya uwekezaji katika
Sekta ya Maji.
258.
Mheshimiwa Spika, vilevile, kumekuwepo na mawasiliano hafifu na wadau wengine wanaotoa mchango wa
kuendeleza utoaji wa huduma ya maji ikiwa ni pamoja na Mashirika yasiyo ya
Kiserikali, Mashirika ya Dini na Watu Binafsi. Upungufu huo umesababisha Wizara
kukosa taarifa za miradi ya maji inayotekelezwa na wadau hao ili kujua hali
halisi ya huduma ya upatikanaji wa maji kwenye maeneo husika.
259.
Mheshimiwa Spika, hatua zinazochukuliwa katika kukabiliana na
changamoto hiyo ni pamoja na kuimarisha mawasiliano na wadau hao kwa
kuwashirikisha katika vikao mbalimbali vinavyojadili masuala ya Sekta ya Maji
ili kubadilishana uzoefu na kupanga mikakati ya pamoja kukabiliana na
changamoto zilizopo. Aidha, Wizara inaendelea kuboresha Mfumo wa Menejimenti ya
Taarifa na Takwimu za Sekta ya Maji. Mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa
taarifa sahihi na kwa wakati.
260.
Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyofikiwa katika kuendeleza Sekta ya Maji
yametokana na michango inayoendelea kutolewa na Wadau mbalimbali, hivyo napenda
sasa kutumia fursa hii kuwashukuru wale wote waliochangia na kutuwezesha
kufanikisha majukumu ya sekta. Naamini kuwa mafanikio yaliyopatikana katika mwaka
2013/2014 ni kutokana na jitihada za pamoja, ushirikiano na misaada ya kifedha
na kitaalam kutoka kwa Washirika wa Maendeleo, ikiwa ni pamoja na nchi
wahisani, mashirika ya misaada ya kimataifa, taasisi zisizo za kiserikali,
mashirika ya kidini na taasisi za kifedha. Napenda kuzishukuru nchi rafiki
zikiwemo Serikali za Ujerumani, Uholanzi, Uingereza, Marekani, Japan, Ufaransa,
China, Uswisi, Ubeligiji, Ireland, Korea ya Kusini, Sweden, Denmark, Norway,
India na Misri.
261.
Mheshimiwa Spika, napenda pia, kuzishukuru taasisi za fedha za kimataifa na
mashirika ya kimaendeleo kwa misaada ya fedha na ushirikiano wa kitaalam katika
kufanikisha utekelezaji wa majukumu na malengo ya Wizara yangu. Taasisi hizo ni
pamoja na:- Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Maendeleo ya
Ujerumani (KfW), Benki ya Maendeleo ya Ufaransa (AFD), Benki ya Uwekezaji ya
Umoja wa Ulaya (EIB), Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Afrika (BADEA), Mfuko wa Maendeleo wa Nchi Zinazozalisha Mafuta (OPEC
Fund for International Development-OFID), Mfuko wa Maendeleo wa Saudia (SFD), Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Marekani
la Changamoto za Milenia (MCC), Shirika la Misaada ya Maendeleo la Norway (NORAD),
Taasisi
ya Maendeleo ya Uingereza (DFID), Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), Mpango wa Umoja wa
Mataifa wa Maendeleo (UNDP), Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA), Mpango wa Umoja wa
Mataifa wa Makazi Duniani (UN HABITAT), Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Misaada ya Maendeleo la Sweden (SIDA), Shirika la Misaada ya
Maendeleo la Canada (CIDA), Shirika la Misaada ya Maendeleo la Denmark (DANIDA), na Shirika la Misaada
la Marekani (USAID).
262.
Mheshimiwa Spika, aidha, michango ya mashirika ya kidini imeongeza hamasa
katika kuyafikia malengo tuliyojiwekea. Hivyo, napenda kuyashukuru mashirika
hayo ya kidini ambayo ni:- World Islamic League, Shirika la Ahmadiya Muslim
Jamaat Tanzania, Islamic Foundation, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Kanisa la
Kilutheri la Ujerumani, Baraza Kuu la Waislam Tanzania, Kanisa Katoliki
Tanzania, Kanisa la Kianglikana Tanzania, Catholic Agency for Overseas Aid
and Development (CARITAS), Adventist Development Relief Agency (ADRA), Norwegian
Church Aid na Livingwater International. Pia, nazishukuru taasisi zisizo za kiserikali za Tanzania
Water and Sanitation Network (TAWASANET); Wahamasishaji wa Maji, Maendeleo
na Afya (WAMMA); Southern Highlands Participatory Organizasition (SHIPO); WaterAid; World Vision; Plan International; Concern Worldwide; Netherlands
Volunteers Services (SNV); Shirika la Kimataifa la Kuhifadhi Uasili na Mali Asili (IUCN); World Wide Fund for Nature (WWF); African Medical
Research Foundation (AMREF); Clinton HIV Aids Initiative (CHAI); Bill and Melinda
Gates Foundation; na wale wote ambao wameendelea kuisaidia Wizara ya Maji kufanikisha
malengo yake.
263.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee kabisa naomba nitumie fursa hii
kutoa shukurani zangu za dhati kwa Mhe.
Amos Gabriel Makalla (Mb), Naibu Waziri wa Maji; Mhandisi Bashir Juma Mrindoko, Katibu Mkuu; Mhandisi Mbogo Futakamba, Naibu Katibu Mkuu; Wakurugenzi wote na Wakuu wa
Vitengo; Maafisa na Watendaji Wakuu wa Mashirika, Wakala na Taasisi zilizo
chini ya Wizara yangu; na Wataalam na Watumishi wote kwa ushirikiano wanaonipatia
pamoja na kujituma kwao katika kusimamia utekelezaji wa majukumu tuliyopewa.
264. Mheshimiwa Spika, Napenda nimshukuru sana Mhe. Dr. Mhandisi Bilinith
Saatano Mahenge (Mb) na ambaye tulianza kazi
hii ya kuwapelekea maji watanzania kwa nguvu mpya. Leo ninayo furaha kumpongeza Dr. Binilith S. Mahenge (Mb)
kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira). Napenda
pia nimshukuru aliyekuwa Katibu Mkuu, Mhandisi Christopher Nestory Sayi ambaye amestaafu kwa heshima. Ni matumaini yangu kuwa
huko waliko kwa sasa wataendelea kuwa mabalozi wazuri wa Sekta ya Maji.
265.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba sasa kutoa hoja kwamba
Bunge lako tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 520,906,475,000 kwa
ajili ya matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka 2014/2015, ili Wizara iweze kutekeleza
majukumu na malengo yaliyoelezwa katika hotuba hii. Kati ya fedha hizo, Matumizi
ya Kawaida
ni shilingi 30,899,443,000 ambapo shilingi 15,384,999,000 ni Mishahara ya Watumishi (PE),
na shilingi 15,514,444,000 ni fedha za Matumizi
Mengineyo (OC). Jumla ya Bajeti ya Maendeleo ni shilingi 490,007,032,000
ambapo
kati ya fedha hizo shilingi 312,066,164,000
ni
fedha za ndani na shilingi 177,940,868,000 ni fedha za nje.
266.
Mheshimiwa Spika, naomba tena nitoe shukurani zangu kwako na kwa
Waheshimiwa Wabunge kwa kunisikiliza. Hotuba hii pia inapatikana katika Tovuti
ya Wizara kwa anwani: www.maji.go.tz.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
5 comments:
What's up to every body, it's my first go to see of this web site; this weblpog
contains remarkable and genuinely fine data
designed for readers.
Woah! I'm really enjoying the template/theme of this blog.
It's simple, yet effective. A lot of times it's tough to get that "perfect balance" between superb usability and visual appeal.
I must say that you've done a very good job with this.
In addition, the blog lkads super quick for me on Chrome.
Outstanding Blog!
Thanks a bunch for sharing this with all people you really recognise what you're
speaking about! Bookmarked. Kindly also seek adviuce from
my website =). We could have a link trade arranggement among us
Heya i'm for the first time here. I found this board and I find It really useful & it helped me out a lot.
I hope to gijve something back and aid others likke
you aided me.
whoah this weblog is fantastic i really lik studying your posts.
Keep upp the great work! You realize, a llot off persons are looking around for this info, you could help them greatly.
Post a Comment