BAJETI YA WIZARA YA MAJI

MHE. PROF. JUMANNE ABDALLAH MAGHEMBE (MB.) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA MAJI
KWA MWAKA 2014/2015

1.0          UTANGULIZI


1.             Mheshimiwa Spika, leo hii Bunge lako Tukufu limepokea taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mheshimiwa Profesa Peter Mahamudu Msolla, Mbunge wa Kilolo, kuhusiana na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji. Naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Kawaida na Maendeleo ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2014/2015.

2.             Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati hiyo kwa kupokea na kuchambua Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2013/2014 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka 2014/2015. Maoni, ushauri na maelekezo yaliyotolewa na Kamati yamezingatiwa wakati wa maandalizi ya Bajeti ya Wizara yangu.

3.             Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuongoza kwa umahiri mkubwa hatua mbalimbali za mchakato wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba na hatimaye kuteua Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Aidha, napenda kumpongeza Rais wetu kwa kupata Tuzo ya Heshima ya Kiongozi Mwenye Mchango Mkubwa zaidi katika Maendeleo Barani Afrika kwa mwaka 2013.

4.             Mheshimiwa Spika, vilevile nawapongeza Mhe. Samwel Sitta, Mbunge wa Urambo Mashariki kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mbunge wa Makunduchi kuwa Makamu Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wote wa Bunge hilo kwa kuteuliwa kwao kushiriki katika mchakato wa kupata Katiba mpya. Watanzania wana matumaini makubwa ya kuwa na Katiba mpya ambayo itakayozingatia matakwa ya kizazi cha sasa na kijacho.

5.             Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii, kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge walioteuliwa kuwa Mawaziri na Manaibu Waziri ili kuziongoza Wizara mbalimbali. Vilevile, nawapongeza Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wapya wa Kamati mbalimbali za Kudumu za Bunge waliochaguliwa hivi karibuni. Ni matumaini yangu kuwa tutaendelea kushirikiana nao katika kutekeleza majukumu yetu kwa maendeleo ya Taifa letu.

6.             Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu walionitangulia katika kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wapya Mhe. Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga na Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze waliochaguliwa kujiunga na Bunge lako Tukufu. Nawatakia heri na mafanikio katika kazi yao hiyo mpya.

7.             Mheshimiwa Spika, napenda pia kuchukua fursa hii kumshukuru na kumpongeza Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb) kwa hotuba yake inayotoa mwelekeo wa utekelezaji wa kazi za Serikali. Vilevile, nawapongeza Mawaziri walionitangulia kuwasilisha hoja zao.

8.             Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ilipokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa, taarifa za vifo vya Waheshimiwa Wabunge wenzetu, Marehemu William Augustao Mgimwa, aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mbunge wa Kalenga na Marehemu Saidi Bwanamdogo, aliyekuwa Mbunge wa Chalinze. Nachukua nafasi hii kutoa pole kwako wewe Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu, familia za marehemu, ndugu na wananchi wa majimbo ya Kalenga na Chalinze kwa misiba hiyo mikubwa. Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi. Amin.

9.             Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, napenda sasa kuchukua fursa hii kuwasilisha hotuba yangu ya Bajeti yenye maeneo makuu manne (i) hali ya Sekta ya Maji nchini; (ii) mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014; (iii) mpango wa bajeti kwa mwaka 2014/2015; na (iv) shukrani kwa wadau wa Sekta ya Maji na maombi ya fedha kwa mwaka 2014/2015. Maelezo yatakayotolewa katika maeneo yaliyoainishwa yamezingatia sera na mikakati ya maendeleo ya kitaifa na kimataifa; sheria, kanuni na miongozo inayohusiana na Sekta ya Maji; na mgawanyo wa kazi kisekta zinazoongoza usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini.


2.0          HALI YA SEKTA YA MAJI NCHINI


10.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010; Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 - 2015/2016); Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa “Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa (Big Results Now - BRN)” na Ahadi za Serikali. Wizara inatekeleza miradi mbalimbali katika Sekta ya Maji kulingana na Sera ya Maji ya mwaka 2002, Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Maji (2006 – 2015), Sheria na Kanuni za Maji, na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP).

11.          Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha hali ya maisha ya wananchi wake kupitia Sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Maboresho makubwa ya kimfumo na kiutendaji katika sekta zote nchini (Sector reforms) yanaendelea kutekelezwa. Aidha, Sekta ya Maji ni moja ya sekta sita zilizopewa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya “Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa” – BRN. Awamu ya Kwanza ya Mpango huo wa miaka mitatu (2013/2014 – 2015/2016) ni mwelekeo chanya katika kuyafikia malengo tuliyojiwekea ya kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama, hususan katika maeneo ya vijijini. Katika Mpango huo jumla ya miradi 1,810 itakayogharimu kiasi cha shilingi trilioni 1.45 inatarajiwa kujengwa na itakapokamilika wananchi wapatao milioni 15.4 zaidi watapata huduma ya maji na kufikisha idadi ya wananchi wanaopata huduma ya majisafi na salama kufikia milioni 30.6 sawa na asilimia 74 ya wakazi wote wa vijijini. Miradi inayotekelezwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji imejumuishwa kwenye Mpango wa BRN ili kuharakisha utekekezaji wa miradi ya maji nchini. Naomba nikiri kwamba tumepata hamasa kubwa katika utekelezaji wa BRN na nichukue fursa hii niwapongeze Serikali za Mitaa kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya.

12.          Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ambayo ilizinduliwa mwaka 2006/2007 na kuanza kutekelezwa mwaka 2007/2008. Programu hiyo inatekelezwa katika vipindi vya miaka mitano mitano hadi mwaka 2025/2026 na imegawanywa katika programu ndogo nne ambazo ni; Usimamizi  na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji, Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini, Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mijini, na Kuimarisha na Kuzijengea Uwezo Taasisi zinazotekeleza Programu ya Maji. Hadi sasa hali halisi ya utekelezaji katika Sekta ya Maji imefikia hatua mbalimbali kama ifuatavyo:-


2.1            RASILIMALI ZA MAJI


13.          Mheshimiwa Spika, Rasilimali tuliyonayo inatumika majumbani, kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji wa nishati, mifugo, uvuvi, viwanda, uchimbaji wa madini, usafirishaji, utalii, ujenzi pamoja na maendeleo ya miji. Aidha, Rasilimali za  maji zinatumika pia kwa ajili ya kupokea majitaka yaliyosafishwa na kufikia viwango vinavyokubalika baada ya matumizi. Usimamizi wa vyanzo vya maji nchini unafuata taratibu za mipango shirikishi ya usimamizi wa rasilimali za maji kwenye Bodi za Maji za mabonde tisa yaliyopo nchini, ambapo saba katika hayo yanahusisha majishirikishi kati ya nchi yetu na nchi jirani.

14.          Mheshimiwa Spika, inakadiriwa kuwa rasilimali za maji juu ya ardhi zinazofaa kwa matumizi mbalimbali (annual renewable surface water resources) ni wastani wa kilomita za ujazo 87 kwa mwaka. Aidha, hifadhi ya rasilimali za maji chini ya ardhi inakadiriwa kuwa kilomita za ujazo 38. Hata hivyo, mtawanyiko na upatikanaji wa rasilimali hizo nchini hauko sawa katika maeneo yote kutokana na tofauti ya hali ya hewa, jiografia na jiolojia.
15.          Mheshimiwa Spika, Changamoto kubwa iliyopo kwenye usimamizi wa rasilimali za maji ni kupungua na kuharibika kwa vyanzo vya maji kutokana na shughuli za kibinadamu katika maeneo ya vyanzo vya maji na katika misitu ya hifadhi ya maji (catchments forests and wetlands). Hifadhi hizi zinawezesha upatikanaji wa maji juu na chini ya ardhi. Takwimu za kitaifa za rasilimali za maji zilizopo zinaonesha kuwa kiasi cha maji kwa sasa kwa kila mtanzania ni wastani wa mita za ujazo 1,952 kwa mwaka. Endapo hatua madhubuti za utunzaji wa vyanzo vya maji hazitachukuliwa mapema, kiasi hicho kinatarajiwa kupungua hadi kufikia mita za ujazo 883 mwaka 2035. Kiwango cha chini cha mahitaji ya maji kwa kila mtu kwa mwaka kinachokubalika kimataifa ni mita za ujazo 1,700. Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Maji inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na hali hiyo ili nchi yetu isifikie kiwango hicho cha upatikanaji wa maji kwa kila Mtanzania.

16.          Mheshimiwa Spika, wastani wa mvua katika mabonde ya maji nchini ulikuwa unatofautiana kutokana na tabia tofauti za hali ya hewa katika maeneo hayo. Baadhi ya mabonde yalipata mvua kidogo na mengine mvua nyingi kulinganisha na viwango vya mwaka uliopita kwa mujibu wa taarifa ya mwaka wa kihaidrolojia (Novemba, 2012 – Oktoba 2013). Kwa ujumla kiasi cha mvua kilikuwa chini ya wastani katika maeneo mengi ambapo asilimia 67 ya vituo vya mvua vilionesha kiwango cha mvua chini ya wastani. Kiwango cha mvua katika mabonde sita (6) kati ya tisa (9) ulikuwa kama ifuatavyo: Bonde la Pangani milimita 720 ikilinganishwa na wastani wa milimita 782 ya mwaka uliopita; Bonde la Rufiji milimita 1,144 ikilinganishwa na milimita 846.0; Bonde la Wami/Ruvu milimita 979 ikilinganishwa milimita 1,150; Bonde la Ziwa Tanganyika milimita 895 ikilinganishwa na milimita 705; Bonde la Ziwa Victoria  milimita 968 ikilinganishwa na milimita 1,175; na katika Bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini wastani wa milimita 730 ikilinganishwa na milimita 917.

17.          Mheshimiwa Spika, kulingana na mvua zilizonyesha katika kipindi hicho, viwango vya maji kwenye mito pia vimetofautiana kutokana na kiasi cha mvua pamoja na mitiririko ya maji kuelekea katika mito mbalimbali nchini. Viwango vya maji katika baadhi ya mito nchini vilikuwa kama ifuatavyo:- Mto Kikuletwa katika Bonde la Pangani ulikuwa na mita za ujazo 14.66 kwa sekunde ikilinganishwa na kiasi cha mita za ujazo 21.85 kwa sekunde kilichopatikana mwaka uliopita; Mto Ruaha Mkuu ulioko Bonde la Rufiji ulikuwa na wastani wa mita za ujazo 9.93 kwa sekunde ikilinganishwa na mita za ujazo 12.90 kwa sekunde; Mto Wami mita za ujazo 18.69 kwa sekunde ikilinganishwa na mita za ujazo 89.41 kwa sekunde; na Mto Ruvu mita za ujazo 36.21 kwa sekunde, ikilinganishwa na wastani wa mita za ujazo 42.90 kwa sekunde. Vilevile, wastani wa mtiririko wa maji kwenye baadhi ya mito katika bonde la Ziwa Victoria ulikuwa ni mita za ujazo 66.55 kwa sekunde katika Mto Mara na mita za ujazo 27.46 kwa sekunde kwa Mto Simiyu ikilinganishwa na mita za ujazo 102.37 na 74.78 kwa sekunde kwa mwaka uliopita katika mito hiyo kwa mtiririko huo.

18.          Mheshimiwa Spika, hali ya maji kwenye baadhi ya mabwawa makubwa tuliyonayo haikuwa ya kuridhisha japo kulikuwa na ongezeko dogo la kina cha maji katika mabwawa hayo. Katika Bonde la Pangani bwawa la Nyumba ya Mungu usawa wa maji ulikuwa mita 683.94 juu ya usawa wa bahari, ikilinganishwa na usawa wa mita 683.20 mwaka uliopita na bwawa la Mabayani lilikuwa na usawa wa maji wa mita 91.20 ikilinganishwa na mita 91.10 juu ya usawa wa bahari. Katika mabwawa yaliyopo Bonde la Rufiji, usawa wa maji ulikuwa kama ifuatavyo; Kihansi (mita 1,144.69), Mtera (mita 691.18) na Kidatu (mita 446.33) juu ya usawa wa bahari ikilinganishwa na mita 1,145.30 (Kihansi), mita 689.19 (Mtera) na mita 444.57 (Kidatu) kwa mwaka uliopita. Kiwango cha maji katika Bwawa la Mtera ambalo pia hutegemewa na Bwawa la Kidatu katika uzalishaji wa umeme kimeendelea kuwa chini ya kiwango. Kiwango kinachotakiwa kwa ajili ya kuendesha mitambo ya umeme katika Bwawa la Mtera ni mita 690.00 juu ya usawa wa bahari.

19.          Mheshimiwa Spika, usawa wa maji katika bwawa la Mindu ni mita 506.45 juu ya usawa wa bahari ikilinganishwa na mita 506.82 ya mwaka uliopita. Aidha, usawa wa maji katika Ziwa Victoria ulikuwa mita 1,133.22 juu ya usawa wa bahari ikilinganishwa na mita 1,133.06 mwaka uliopita, Ziwa Tanganyika lilikuwa wastani wa mita 774.6 ikilinganishwa na mita 774.3 juu ya usawa wa bahari, na Ziwa Nyasa lilikuwa na wastani wa mita 474.48 ukilinganisha na mita 475.71 juu ya usawa wa bahari.

20.          Mheshimiwa Spika, kulingana na takwimu hizo, uhaba wa maji umeendelea kuyaathiri maeneo mengi nchini kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo upungufu wa mvua katika maeneo mengi hasa yale yanayotegemea mvua za msimu mmoja, kupungua kwa uwezo wa ardhi kuhifadhi maji wakati yakitiririka kuelekea mitoni kutokana na ukataji miti kwa wingi na uharibifu wa mazingira,  mabadiliko ya matumizi ya ardhi, athari za mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na kasi kubwa ya ongezeko la watu. Hata hivyo mvua zilizonyesha mwezi Aprili 2014 ziliongeza wingi wa maji kwenye mito, mabwawa na maziwa. Katika baadhi ya mito, takwimu zinaonesha wastani wa mtiririko wa maji uliongezeka kama ifuatavyo:- Mto Mara, mita za ujazo 260 kwa sekunde, Mto Simiyu mita za ujazo 141.37 kwa sekunde, Mto Wami mita za ujazo 337.63 kwa sekunde, Mto Rufiji mita za ujazo 800 kwa sekunde na Mto Ruvu ni zaidi ya mita za ujazo 453 kwa sekunde. Hali hiyo imedhihirika pia katika vina vya mabwawa ya Mtera mita 693.38 juu ya usawa wa bahari, Nyumba ya Mungu mita 684.25 na Mindu mita 507. Vilevile, vina vya maji kwenye maziwa nchini vimeongezeka ambapo kwa Ziwa Victoria kilikuwa mita 1133.25, Ziwa Nyasa mita 476.02 na Ziwa Tanganyika mita 775.13 juu ya usawa wa bahari. Mvua hizo zimeongeza wingi wa maji kwenye vyanzo vya maji katika maeneo yaliyopata mvua za kutosha.


2.2            HUDUMA YA MAJI VIJIJINI


21.          Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuwapatia maji safi na salama wananchi waishio vijijini katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao kama Sera ya Maji ya mwaka 2002 inavyoelekeza. Kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo, Serikali za Mitaa, Wananchi, Sekta Binafsi na Wadau wengine, Serikali inaboresha huduma za maji vijijini kwa kujenga, kupanua na kukarabati miundombinu ya maji. Jukumu la Wizara ni kutafuta fedha, kuandaa miongozo ya utekelezaji na kutoa ushauri wa kitaalam. Sekretarieti za Mikoa husimamia na kutoa ushauri wa kiufundi kwa Halmashauri katika kutekeleza miradi ya maji vijijini.

22.          Mheshimiwa Spika, uchambuzi wa kina uliofanyika wakati wa matayarisho ya mpango wa BRN ulibaini vituo vingi vya miradi iliyokamilika kuwa havitoi huduma kutokana na miradi hiyo kutofanyiwa matengenezo ya mara kwa mara kama inavyotakiwa. Aidha, baadhi  ya miradi, pampu na vipuri vimeibiwa, au miradi mingine uwezo wa vyanzo vyake umepungua kutokana na uharibifu wa mazingira katika vyanzo kama vile ukataji miti au kilimo katika vyanzo hivyo, hii ikiwa ni pamoja na mahitaji ya maji kuongezeka kutokana na kuongezeka kwa watu ukilinganisha na uwezo wa vyanzo vya miradi hiyo.


2.3            HUDUMA YA MAJI MIJINI


23.          Mheshimiwa Spika, huduma za majisafi na usafi wa mazingira mijini zinasimamiwa na kutekelezwa na Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini. Mamlaka hizo zilianzishwa mwaka 1998 chini ya Sheria Na.8 (Water Works Act) ya mwaka 1997, kwa sasa zinasimamiwa na Sheria Na. 12 ya mwaka 2009 ya Huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira. Mamlaka hizo za Maji ziko kwenye miji mikuu ya mikoa na wilaya, miji midogo na miradi ya kitaifa.


24.          Mheshimiwa Spika, Mamlaka za maji za miji mikuu ya mikoa zinaendeshwa chini ya usimamizi wa Bodi za Wakurugenzi ambazo huteuliwa na Waziri mwenye dhamana ya maji kwa kushirikiana na uongozi wa mikoa husika. Lengo la utaratibu huo ni kuziwezesha Mamlaka hizo zijiendeshe kibiashara na hatimaye kuwa endelevu na kujitegemea kwa gharama zote za uendeshaji, matengenezo na uwekezaji kutokana na maduhuli ya mauzo ya maji. Hadi mwezi Machi, 2014 zimeundwa Mamlaka 23 za Miji Mikuu ya Mikoa. Mamlaka kati ya hizo yaani Arusha, Dodoma, Iringa, Mbeya, Morogoro, Moshi, Mtwara, Mwanza, Shinyanga, Tabora, Tanga, Songea na Musoma zipo Daraja ‘A’. Mamlaka hizo zinajitegemea kwa gharama zote za uendeshaji na matengenezo, ikiwemo mishahara ya watumishi na gharama za umeme wa kuendesha mitambo ya kusukuma maji na uwekezaji mdogo. Mamlaka nne za Bukoba, Kigoma, Singida na Sumbawanga ziko Daraja ‘B’ na zinapata ruzuku ya kulipia sehemu ya gharama za umeme wa kuendesha mitambo. Mamlaka zilizo kwenye Daraja ‘C’ ni Mpanda, Njombe, Bariadi, Geita, Babati na Lindi ambazo zinaendelea kupata ruzuku ya mishahara kwa baadhi ya wafanyakazi wake pamoja na kulipia gharama za umeme wa kuendesha mitambo na uwekezaji.

25.          Mheshimiwa Spika, wastani wa kiwango cha utoaji huduma ya majisafi kwenye miji mikuu ya mikoa imeendelea kuimarika. Hali hiyo imetokana na ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya majisafi katika mamlaka zote za maji za miji mikuu ya mikoa. Hadi mwezi Machi, 2014 upatikanaji wa huduma ya maji kwenye mamlaka za maji 19 isipokuwa DAWASA na Mamlaka za miji minne ya Mikoa mipya imefikia wastani wa asilimia 86. Upatikanaji wa huduma ya maji kwa miji minne ya Mpanda, Njombe, Geita na Bariadi ni wastani wa asilimia 53. Aidha, idadi ya wateja waliounganishwa kwenye mitandao ya majisafi mijini imeongezeka kutoka wateja 311,478 mwezi Machi, 2013 hadi kufikia wateja 336,898 ambalo ni ongezeko la asilimia 8.

26.          Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa majisafi kwa Mamlaka zote 23 za miji mikuu ya mikoa uliongezeka kutoka wastani wa lita milioni 348.76 kwa siku mwezi Machi 2013 hadi kufikia wastani wa lita milioni 376.07 mwezi Machi 2014. Ufungaji wa dira za maji umeongezeka hadi kufikia dira za maji 316,018 ukilinganisha na dira 284,861 mwezi Machi 2013, sawa na asilimia 94 ya wateja wote 336,898. Lengo ni kufikia asilimia 100 ya ufungaji wa dira za maji kwa wateja ifikapo mwezi Desemba 2014. Wastani wa upotevu wa maji (Non Revenue Water – NRW) kwenye mifumo ya usambazaji maji umefikia asilimia 38.Upotevu huu wa maji unatokana  na uchakavu wa miundombinu ya usambazaji wa maji na wizi wa maji. Wastani wa makusanyo ya maduhuli yatokanayo na mauzo ya maji kwa mwezi kwa Mamlaka zote za maji mijini isipokuwa DAWASCO, yameongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 6.36 (kwa mwezi) mwezi Machi 2014 kutoka wastani wa shilingi bilioni 5.58, mwezi Machi 2013. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 14. Kuongezeka kwa maduhuli hayo, kumeziwezesha Mamlaka kuboresha huduma zinazotolewa ikiwa ni pamoja na kukarabati miundombinu na kugharamia shughuli za uendeshaji. Wizara itaendelea kuimarisha Mamlaka za maji ili kuongeza maduhuli ziweze kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye Mikataba ya Utendaji kazi waliosaini na Wizara na EWURA.


27.          Mheshimiwa Spika, miradi nane ya kitaifa ya KASHWASA, Handeni Trunk Main–HTM, Maswa, Mugango-Kiabakari, Chalinze, Wanging’ombe, Makonde na Masasi-Nachingwea inasimamiwa na Wizara yangu chini ya kifungu Na. 41 cha Sheria ya Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2009. Aidha, huduma za majisafi kwa Miji Mikuu ya Wilaya na Miji Midogo hutolewa na Mamlaka za maji za miji hiyo ambazo husimamiwa na Bodi za Wakurugenzi zinazoteuliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu na kusimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwa sasa miradi ya maji ya kitaifa na mamlaka 96 ngazi ya Wilaya na Miji Midogo zipo daraja C. Wizara yangu kwa kushirikiana na TAMISEMI inaendelea kuzijengea uwezo Mamlaka hizo ili zipande daraja kutoka C hadi madaraja ya B na A. Nia yetu ni kuziwezesha kujiendesha kibiashara na hivyo kupunguza mzigo kwa Serikali.


28.          Mheshimiwa Spika, mmiliki na msimamizi wa usambazaji wa huduma ya majisafi na uondoaji wa majitaka Jijini Dar-es-Salaam na Miji ya Kibaha na Bagamoyo ni Dar es Salaam Water Supply and Sewerage Authority–DAWASA. Serikali kupitia DAWASA iliingia Mkataba wa kukodisha shughuli za uendeshaji wa huduma ya majisafi na majitaka na Shirika la Usambazaji Maji Jijini Dar es Salaam (Dar es Salaam Water Supply and Sewerage Corporation- DAWASCO). Lengo ni kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za utoaji huduma ya majisafi na majitaka.

29.          Mheshimiwa Spika, idadi ya wakazi wanaopata huduma ya majisafi sasa katika Jiji la Dar es Salaam ni asilimia 68 kwa wastani wa saa tisa (9) kwa siku. Kati ya hao, asilimia 55 wanapata huduma ya maji kutoka kwenye mitandao ya mabomba na wanaobaki wanapata huduma ya maji kutoka kwenye visima, magati na huduma ya magari (water bowsers). Lengo la Serikali ni kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji hadi kufikia asilimia 75 mwezi Juni, 2016. Mahitaji ya maji kwa hivi sasa ni lita milioni 450 kwa siku ikilinganishwa na uwezo wa mitambo wa kuzalisha maji lita milioni 300 kwa siku. Hata hivyo, mwezi Machi 2014, uzalishaji wa maji ulishuka na kufikia wastani wa lita milioni 260 kwa siku. Upungufu huo wa uzalishaji unatokana na tatizo la kuharibika kwa mara kwa mara kwa mitambo ya kusukuma maji (pampu kubwa za Ruvu Juu), muda mrefu wa matengenezo, miundombinu chakavu na hitilafu za umeme. Aidha, mpaka mwezi Machi, 2014 wateja 137,856 walikuwa wameungiwa huduma ya maji na kufungiwa mita, ikilinganishwa na wateja 118,942 mwezi Machi, 2013, hilo ni ongezeko la asilimia 16. Ongezeko la wateja limeongeza wastani wa makusanyo ya maduhuli yanayotokana na mauzo ya maji kutoka shilingi bilioni 3.38 kwa mwezi Machi, 2013 hadi kufikia shilingi bilioni 3.57 mwezi Machi, 2014. Pamoja na kuwepo kwa changamoto kubwa inayotokana na uvujaji, uchakavu wa miundombinu, wizi wa maji na uharibifu unaoweza kutokea wakati wa ukarabati wa miuondombinu ya barabara huharibu miundombinu ya maji. na kuongeza upotevu wa maji na kupunguza upatikanaji wa huduma ya maji. Serikali inaendelea kukabiliana na changamoto hizi na kuzipatia ufumbuzi hatua kwa hatua.


30.          Mheshimiwa Spika, takwimu zilizopo zinaonesha kwamba, huduma ya uondoaji majitaka ni asilimia 18 kufikia mwezi Machi 2014, ikilinganishwa na malengo ya MKUKUTA II ya kuongeza kiwango cha huduma ya majitaka kufikia asilimia 22 ifikapo 2015. Miji yenye mitandao ya majitaka ni Arusha, Moshi, Tanga, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Iringa, Songea, Tabora, Morogoro na Dar es Salaam. Hali ya huduma ya uondoaji wa majitaka mijini siyo ya kuridhisha. Aidha, idadi ya wateja waliounganishwa kwenye mtandao wa majitaka imeongezeka kutoka 21,775 mwezi Machi, 2013 hadi kufikia wateja 22,976 mwezi Machi, 2014. Pamoja na ongezeko hilo, bado wastani wa huduma ya uondoaji majitaka mijini ni asilimia 18 tu. Hali hiyo inasababishwa na mwamko mdogo wa wananchi kujiunga kwenye mtandao wa majitaka katika miji hiyo. Vilevile, miundombinu ya majitaka kwa baadhi ya miji ni chakavu na inahudumia maeneo machache.



2.4         KUJENGA UWEZO WA TAASISI ZIILIZO CHINI YA PROGRAMU YA MAENDELEO YA SEKTA YA MAJI


31.          Mheshimiwa Spika, kulingana na mahitaji ya rasilimali watu ya kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji na Mpango wa BRN, Wizara inahitaji wataalam 8,749 kwa kipindi chote cha utekelezaji wa Programu (2006/2007 hadi 2025) ili kutekeleza majukumu kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa. Hivi sasa, Sekta ya Maji ina jumla ya wataalam 1,538. Kwa mwaka wa kwanza (2013/2014) wa utekelezaji wa Mpango wa BRN, jumla ya wataalam 835 walihitajika kuajiriwa kwenye Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri zote nchini. Kati ya Wataalam hao, wahandisi ni 302 na mafundi sanifu 533. Katika mwaka 2013/2014 Serikali imeiidhinisha ajira ya wataalamu (wahandisi) 125 wapya na mafundi sanifu (FTC) 350.



32.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu ilitekeleza miradi inayohusu usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji, huduma ya majisafi na usafi wa mazingira vijijini na mijini na masuala mtambuka. Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2013/2014 na malengo ya mwaka 2014/2015 kwa Sekta ya Maji unaelezwa katika sura hii ya Bajeti.





33.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 Wizara yangu ilisimamia na kuendeleza rasilimali za maji, ikiwemo kuchunguza, kutathmini na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji nchini pamoja na rasilimali za majishirikishi (transboundary water resources); na kuimarisha Bodi za Maji za Mabonde ili zisimamie kikamilifu rasilimali hizo. Kazi nyingine ni kuandaa mipango shirikishi ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji, kusanifu na kusimamia ujenzi wa miundombinu ya kipaumbele, yakiwemo mabwawa.


(a)           Mwenendo wa Rasilimali za Maji

34.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuimarisha vituo vya kupima wingi na ubora wa rasilimali za maji juu na chini ya ardhi ili kuboresha upatikanaji wa takwimu na upatikanaji wa taarifa sahihi. Katika mwaka 2013/2014, jumla ya vituo 29 vya kupima mtiririko wa maji mitoni, vituo 14 vya hali ya hewa, vituo sita (6) vya ufuatiliaji maji chini ya ardhi, vituo vitatu (3) vya kupima maji kwenye maziwa na vituo saba (7) vya kupima mvua vilijengwa. Vituo hivyo vipo katika mabonde ya Wami-Ruvu, Pangani, Ziwa Rukwa, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na Bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini. Aidha, ukarabati ulifanyika katika vituo 80 vya kupima mtiririko wa maji kwenye mito, vituo 18 vya hali ya hewa, vituo viwili (2) vya ufuatiliaji wa maji chini ya ardhi, vituo vitatu (3) vya kupima maji kwenye maziwa, vituo vitano (5) vya kupima maji kwenye mabwawa na vituo sita (6) vya kupima mvua. (Jedwali Na.1)

35.          Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha upatikanaji wa takwimu sahihi za hali ya maji nchini, Bodi za Maji za Mabonde zimekusanya na kuchanganua takwimu za hali ya maji katika vituo mbalimbali. Vituo hivyo vinajumuisha vituo 203 vya kupima mtiririko wa maji mitoni, vituo 12 vya kupima usawa wa maji katika maziwa na mabwawa, vituo 122 vya kupima mvua, na vituo 29 vya kupima hali ya hewa. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kujenga na kukarabati vituo 134 vya kupima mtiririko wa maji mitoni, vituo 17 vya hali ya hewa, vituo 35 vya mvua na vituo 52 vya kupima maji chini ya ardhi pamoja na kukusanya takwimu kwenye mabonde yote nchini.

36.          Mheshimiwa Spika, takwimu na taarifa zinazokusanywa kutoka kwenye vituo hivyo husaidia kutambua hali ya maji kwa nyakati tofauti kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini, hivyo kuwezesha maandalizi ya mipango na kutoa maamuzi sahihi ya ugawaji wa rasilimali za maji kwa matumizi mbalimbali. Aidha, takwimu na taarifa hizo hutumika katika usanifu na ujenzi wa miundombinu ya miradi ya maji, mabwawa na madaraja pamoja na utafiti wa mabadiliko ya tabianchi.

(b)           Kuhifadhi wa Mazingira na Vyanzo vya Maji

37.          Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mikakati ya kuhifadhi vyanzo vya maji, Wizara yangu imeendelea kuvitambua, kuviwekea mipaka na kuvitangaza kuwa maeneo tengefu. Katika mwaka wa fedha 2013/2014, jumla ya vyanzo 153 vilitambuliwa kuwa katika hatari ya kuharibiwa na kuathiriwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la shughuli za kibinadamu. Kati ya hivyo, vyanzo 59 vimebainishwa na na kuandaliwa ili vitangazwe kuwa maeneo tengefu ya vyanzo vya maji. Hadi mwezi Machi 2014, mapendekezo ya vyanzo saba (7) kati ya vyanzo vilivyobainishwa katika Bonde la Ziwa Rukwa viko tayari kutangazwa rasmi kuwa maeneo tengefu. Maeneo hayo ambayo hayakuhitaji fidia ni maeneo ya vyanzo vya maji chini ya ardhi yaliyoko Chokaa, Kidole, Kiswaga, Matundasi A, Matundasi B, Mkola na Bwawa la Milala.

38.          Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea na taratibu za kutangaza vyanzo vya maji vilivyobainishwa kuwa maeneo tengefu likiwemo Bwawa la Mtera katika Bonde la Rufiji. Vilevile, katika Bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini vyanzo vya maji vya chemichemi za Mbwinji, Ndanda, Mwena na Liputu kwenye miteremko ya milima ya Makonde vimewekewa mipaka kwa ajili ya kuvihifadhi. Uchoraji wa ramani za maeneo husika unaendelea na utakapokamilika yatatangazwa kuwa maeneo tengefu. Aidha, uwekaji wa mipaka unaendelea kwenye vyanzo vya maji vya Mitema-Kitangari kwa lengo la kuvihifadhi. Wizara yangu itaendelea kubaini na kuweka mipaka maeneo mengine ya vyanzo vya maji ili kuyakinga dhidi ya uharibifu wa mazingira.

39.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maji imeandaa Mpango Maalum wa miaka mitano wa Kuhifadhi na Kutunza Vyanzo vya Maji utakaoanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2014/2015. Mpango huo umeainisha maeneo ya utekelezaji ili kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya maji kwa maendeleo endelevu ya sasa na vizazi vijavyo. Mpango huo utahusisha kutoa elimu kwa umma na kuimarisha ushiriki wa wadau katika shughuli za uhifadhi, utunzaji na ulinzi wa rasilimali za maji; kujenga uwezo wa wadau wa sekta ya maji katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji; na kusaidia shughuli mbadala za kiuchumi ili kupunguza shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya vyanzo vya maji. Shughuli hizo ni pamoja na ukataji miti, kilimo cha “vinyungu” na kilimo katika kingo za mito. Wizara kwa kushirikiana na wadau hao itaendelea kuhakikisha kwamba vyanzo vya maji vinatunzwa na kulindwa.

40.          Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji, hadi mwezi Machi 2014, jumla ya Jumuiya 99 za Watumiaji Maji ziliundwa. Kati ya hizo Jumuiya 18 zimeundwa katika kipindi cha mwaka 2013/2014. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaunda Jumuiya za Watumiaji Maji 20 na Kamati 13 za kulinda misitu katika vyanzo vya maji (catchment areas) na kuendelea kuimarisha zilizopo. Taarifa ya tathmini ya athari kwa mazingira kwa mabwawa sita ya Itobo, Uchama, Nkiniziwa, Leken, Enguikument I na Enguikument II yaliyopo katika Bonde la Kati imekamilika na kuwasilishwa NEMC kwa hatua zaidi. Kazi ya tathmini za athari kwa mazingira kwa ajili ya miradi ya mabwawa ya Farkwa na Ndembera zinaendelea. Vilevile, tathmini ya athari kwa mazingira ya mradi wa bwawa la Kidunda pamoja na barabara inayoelekea kwenye bwawa inaendelea.

(c)           Kudhibiti Uchafuzi wa Vyanzo vya Maji

41.          Mheshimiwa Spika, udhibiti wa uchafuzi wa vyanzo vya maji ni muhimu katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji nchini. Katika kutekeleza jukumu hilo, ukaguzi ulifanyika katika Bonde la Kati kwenye maeneo tisa (9) ya viwanda, migodi 46 na hoteli tatu (3) na katika Bonde la Pangani, ukaguzi ulifanyika katika mifumo ya utoaji majitaka ya viwanda vitatu (3) na kuangalia utendaji kazi (performance assessment) wa mabwawa ya majitaka ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi Mazingira, Arusha.

42.          Mheshimiwa Spika, vilevile, Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani ilikagua maeneo mbalimbali yaliyopo katika Mkoa wa Kilimanjaro ili kubaini na kuorodhesha shughuli zinazoathiri ubora wa vyanzo vya maji (Inventory of polluting activities). Maeneo yafuatayo yalibainishwa:- Viwanda vya kahawa, viwanda vya mkonge, kiwanda cha chokaa, mashamba ya maua, maeneo ya kutengeneza na kuoshea magari na maeneo ya vyanzo vya maji yanayochafuliwa kwa kuweka makazi na kutupa taka ngumu.

43.          Mheshimiwa Spika, ukaguzi huo ulibaini baadhi ya viwanda kutokuzingatia taratibu za utiririshaji wa majitaka kwenda kwenye vyanzo vya maji. Wizara iliviagiza viwanda hivyo kutengeneza mifumo ya kusafisha majitaka kabla ya kuyatiririsha kwenda kwenye vyanzo vya maji kwa kuzingatia Sheria Na. 20 ya mwaka 2004 ya Usimamizi wa Mazingira. Wizara kwa kushirikiana na NEMC itaendelea kufanya ukaguzi kwenye maeneo ya viwanda na migodi na kuchukua hatua stahiki. Jedwali Na. 2 linaonesha matokeo ya ukaguzi wa vyanzo vya maji unaotokana na majitaka kutoka viwandani na migodini.


44.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea na kuhakikisha vyanzo vipya vya maji vilivyobainishwa vinafanyiwa tathmini na usanifu ili viweze kujengwa na kuongeza upatikanaji wa maji nchini. Katika mwaka 2013/2014, Mtaalam Mshauri amekamilisha kazi ya uchunguzi wa kina wa miamba na ameendelea na kazi ya usanifu kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Farkwa kwenye Mto Bubu, Wilaya ya Chemba. Mradi huo unatarajiwa kuwapatia maji wakazi wa Manispaa ya Dodoma pamoja na Miji ya Chamwino, Bahi na Chemba. Aidha, Wizara inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa Bwawa la Ndembera katika Bonde la Rufiji litakalotumika kudhibiti mwenendo na mtiririko wa maji katika kipindi cha mwaka mzima kwenye Mto Ruaha Mkuu. Bwawa hilo pia linatarajiwa kutumika kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji na kuzalisha umeme. Vilevile, Mtaalam Mshauri amewasilisha taarifa ya upembuzi yakinifu na anaendelea na kazi ya usanifu wa kina.

45.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, hatua za awali za ujenzi wa bwawa la Kidunda zimekamilika ambapo Mtaalam Mshauri anaandaa taarifa ya mwisho ya usanifu na uandaaji wa zabuni (Final Design Report & Tender Documents). Taratibu za ununuzi wa Mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya kuelekea kwenye eneo la bwawa zinatarajiwa kuanza mara baada ya kukamilika kwa mapitio ya Tathmini ya Athari za Kimazingira na Kijamii (Environmental and Social Impact Assessment-ESIA) na kulipa fidia kwa watakaoathirika na mradi. Katika mwaka 2014/15, Wizara imetenga fedha za kulipa fidia, na kujenga barabara.

46.          Mheshimiwa Spika, kwa mradi wa visima vya kuchunguza mwenendo wa maji chini ya ardhi katika maeneo ya Kimbiji na Mpera, Wizara yangu ilipanga kuchimba visima nane (8). Hadi mwezi Machi, 2014 visima viwili (2) vya uchunguzi vimekamilika na kisima cha tatu kinachimbwa na kimefikia mita 200. Inatarajiwa kuwa kufikia mwezi Novemba, 2014 visima vyote vitakuwa vimekamilika. Katika mwaka 2014/2015 Serikali italipa fidia kwa wananchi watakaoathirika na uchimbaji wa visima ili kukamilisha mradi wa visima wa Kimbiji na Mpera kama ilivyopangwa. Baada ya kulipa fidia kwenye eneo la mita 60 kuzunguka kila kisima katika maeneo ya Kimbiji na Mpera kukamilika, Serikali imekamilisha uhakiki wa fidia katika maeneo ya Luzando na Kisarawe II na ulipaji wa fidia umeanza kwa eneo litakapojengwa tanki la Kisarawe II pamoja na kwa eneo la Luzando.  Vilevile, uthamini katika maeneo ya ujenzi wa njia za mabomba za barabara kuelekea kwenye visima umeanza, na maombi ya kupata Wathamini yamewasilishwa kwenye Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali.

47.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliendelea kutafiti maji chini ya ardhi kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa maji. Utafiti ulibaini maeneo 501 yanayofaa kuchimbwa visima vya maji katika mabonde ya Rufiji (33), Bonde la Kati (39), Pangani (149), Wami-Ruvu (18), Ziwa Victoria (40), Ziwa Rukwa (73), Ziwa Tanganyika (80) na Ruvuma na Pwani ya Kusini (69). Wizara yangu pia ilisimamia uchimbaji wa visima vya utafiti 152 katika mabonde ya Rufiji (40), Bonde la Kati (3), Pangani (4), Ruvuma na Pwani ya Kusini (42) Wami-Ruvu (55), Ziwa Victoria (4) na Ziwa Tanganyika (4). Kwa mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kutafiti maji chini ya ardhi katika maeneo mengine zaidi.

48.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kushirikiana na Serikali ya Misri katika utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa uchimbaji wa visima 70; kati ya hivyo, maandalizi ya uchimbaji wa visima 30 yameanza katika maeneo ya Wilaya za Kiteto (10), Same (8), Mwanga (1), Bariadi (2) na Itilima (9) ambapo Mkandarasi amekabidhiwa maeneo ya kazi. Vilevile, Wizara yangu kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ilichimba visima 53 kati ya visima 55 vilivyopangwa katika Wilaya za Kisarawe na Kilosa. Visima 25 vilichimbwa katika Wilaya ya Kilosa na visima 28 Wilaya ya Kisarawe. Visima hivyo viko katika hatua za mwisho za ufungaji wa pampu. Katika mwaka 2014/2015, kazi ya uchimbaji wa visima vilivyobaki itakamilishwa katika Wilaya ya Kisarawe.

49.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu ilisajili kampuni mbili (2) za uchimbaji visima vya maji kati ya kampuni sita (6) zilizoomba. Kampuni nne (4) hazikukidhi vigezo kulingana na  Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya Mwaka 2009. Uratibu huo unalenga kuhakikisha kwamba taratibu za kitaalam zinafuatwa ili kuhakikisha visima vina ubora kwa matumizi endelevu. Hadi mwezi Machi 2014, kampuni binafsi 137 zilikuwa zimesajiliwa. Aidha, jumla ya visima vya maji 546 vilichimbwa katika maeneo mbalimbali nchini. Kati ya hivyo, visima 100 vilichimbwa na Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) na visima 446 vilichimbwa na kampuni binafsi.


50.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu kupitia Bodi za Maji za Mabonde imeendelea kutoa elimu kwa wadau kuhusu umuhimu wa usimamizi endelevu wa rasilimali za maji, hususan kutoa vibali vya matumizi ya maji na utiririshaji wa majitaka. Hadi mwezi Machi 2014, jumla ya vibali vipya 586 vilitolewa katika mabonde ya Pangani (105), Rufiji (92), Wami-Ruvu (112), Ruvuma na Pwani ya Kusini (21), Bonde la Kati (3), Ziwa Victoria (37), Ziwa Rukwa (66), Ziwa Tanganyika (56) na Ziwa Nyasa (94). Jumla ya maombi 223 yalipokelewa katika mabonde ya Ziwa Rukwa (19), Ziwa Tanganyika (50), Wami-Ruvu (77), Ziwa Nyasa (60) na Ruvuma na Pwani ya Kusini (17). Vilevile, usajili wa vibali vya zamani (re-registration) ulifanyika ambapo vibali 479 kutoka katika mabonde ya Ziwa Nyasa (4), Ziwa Victoria (370) na Wami-Ruvu (105) vilihakikiwa na kusajiliwa upya kulingana na matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya mwaka 2009..

51.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, vibali 15 vya kutiririsha majitaka vilitolewa katika mabonde ya Ziwa Victoria (10), Ziwa Rukwa (3) na Pangani (2). Aidha, zoezi la kuwatambua watumiaji maji kwa matumizi mbalimbali lilifanyika ili waweze kupatiwa elimu na hatimaye kuweza kufuata taratibu za kisheria za matumizi endelevu ya maji. Jumla ya watumiaji maji 835 walibainishwa katika mabonde ya Pangani (513), Ziwa Victoria (27), Ziwa Tanganyika (162), Ziwa Nyasa (24), Ruvuma na Pwani ya Kusini (19) na Wami-Ruvu (90).

(f)            Mipango ya Uendelezaji wa Rasilimali za Maji

52.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliendelea na utayarishaji wa Mipango itakayo simamia na kuendeleza Rasilimali za Maji (IWRM&D Plans) na kuwahusisha wananchi katika mabonde yote tisa. Hadi mwezi Machi 2014, rasimu za mwisho za mipango katika mabonde ya Ruvuma na Pwani ya Kusini, Bonde la Kati, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa zilifanyiwa marekebisho na Wataalam Washauri baada ya kupokea maoni na marekebisho kutoka kwa wadau. Wataalam Washauri katika bonde la Ziwa Rukwa, Pangani na Rufiji wamewasilisha Interim Reports na Wizara imetoa maoni kuhusu taarifa hizo kwa ajili ya maboresho.

53.          Mheshimiwa Spika, katika Bonde la Wami-Ruvu, taarifa ya mwisho ya mpango shirikishi wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji imekamilika na kuwasilishwa wizarani mwezi Desemba, 2013. Mpango Shirikishi wa Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji katika Ziwa Victoria upo katika hatua za awali za ukusanyaji wa takwimu na taarifa muhimu kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea na utayarishaji wa Mpango Shirikishi wa Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji katika Ziwa Victoria. Aidha, Wizara itafanya tathmini ya athari za kimazingira na kijamii kabla ya utekelezaji wa mipango iliyoainishwa na (IWRM&D).

(g)           Kuimarisha Bodi za Maji katika Mabonde

54.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuzijengea uwezo Bodi za Maji za Mabonde kwa kutoa mafunzo kwa watumishi, kujenga ofisi na kununua vitendea kazi. Katika mwaka 2013/2014, watumishi 81 wa mabonde nane walipatiwa mafunzo ya muda mfupi na semina mbalimbali kama ifuatavyo; Bonde la Kati (3), Ziwa Nyasa (8), Pangani (36), Ruvuma na Pwani ya Kusini (6), Wami-Ruvu (2), Ziwa Victoria (10), Rufiji (3) na Bonde la Ziwa Rukwa (13). Mafunzo yalihusu jinsi ya kushirikisha wadau na jamii katika utunzaji na usimamizi wa rasilimali za maji, usimamizi wa takwimu, sheria mpya ya ununuzi, mfumo wa maamuzi (Decision Support System - DSS), mifumo ya teknolojia ya Quantum GIS, Google earth and ArcGIS software - conservation strategies na usimamizi wa mazingira (Environmental Management System - EMS). Mafunzo hayo yalilenga kuongeza ujuzi na ufanisi katika utendaji wa kazi.

55.          Mheshimiwa Spika, ujenzi wa jengo jipya la ofisi ya Bonde la Ziwa Nyasa umekamilika na litakabidhiwa mwezi Julai 2014. Aidha, ujenzi wa Ofisi za Bodi za Maji za Mabonde ya Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Bonde la Kati umeanza. Taarifa za usanifu wa majengo ya Ofisi za Bodi za Maji za Mabonde yaliyobaki ya Wami-Ruvu, Ruvuma na Pwani ya Kusini, Rufiji, Pangani, na Ziwa Rukwa, zimekamilika na kuwasilishwa kwa uhakiki. Kwa mwaka 2014/2015, taratibu za kuwapata Wakandarasi wa ujenzi wa ofisi zilizobaki zitakamilika na ujenzi kuanza.

56.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaimarisha Bodi za Maji za Mabonde ili ziweze kufanya tafiti za rasilimali za maji kwa lengo la kupata ufahamu zaidi kuhusu rasilimali zetu na katika usimamizi na uendelezaji wake. Wizara kwa kushirikiana na Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Rukwa imefanya utafiti (Bathymetry) katika Ziwa Rukwa, na Ziwa hilo litakuwa la nne kufanyiwa utafiti wa aina hiyo hapa nchini baada ya Maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.


57.          Mheshimiwa Spika, Bodi za Maji za Mabonde hukusanya maduhuli yatokanayo na ada za matumizi ya maji na kutumia mapato hayo (retention) katika usimamizi, utunzaji na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini. Hadi mwezi Machi 2014, jumla ya shilingi 1,527,245,592 zilikusanywa. Makusanyo hayo ni sawa na asilimia 86.34 ya lengo la shilingi 1,768,887,117 zilizopangwa kukusanywa katika mwaka wa fedha 2013/2014. Katika mwaka 2014/2015, Bodi za Maji za Mabonde zimelenga kukusanya kiasi cha shilingi 2,576,000,000 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwa ni pamoja na ongezeko la Ada ya matumizi ya maji kama ilivyoainishwa katika Jedwali Na. 3.


58.          Mheshimiwa Spika, miongoni mwa majukumu ya Bodi za Maji za Mabonde ni kusuluhisha migogoro katika matumizi ya maji kwa kushirikiana na Jumuiya za Watumiaji Maji na inapobidi vyombo vya sheria hutumika. Katika mwaka 2013/2014, migogoro 29 ya watumiaji maji ilijitokeza, ambapo migogoro 21 kati ya hiyo ilisuluhishwa katika Mabonde ya Maji ya Pangani (5), Wami/Ruvu (10), Ziwa Victoria (2), Rufiji (2) Ziwa Nyasa (1), na Ruvuma na Pwani ya Kusini (1). Migogoro mingine sita (6) katika Bonde la Kati (4) na Ziwa Victoria (2) ipo katika hatua mbalimbali za mashauriano nje ya mahakama;. Migogoro miwili (2) iliyobaki katika Bonde la Pangani iko mahakamani. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kusuluhisha migogoro ya watumiaji maji kama itakavyojitokeza na kutoa elimu ya ugawanaji na utunzaji wa rasilimali za maji.

(j)             Usimamizi wa Rasilimali za Majishirikishi

59.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kushirikiana na nchi nyingine zinazochangia rasilimali za maji shirikishi kwa kuunda vyombo vya pamoja na kuimarisha vilivyopo ili kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali hizo. Azma ya ushirikiano huo ni kuhakikisha kunakuwepo na mifumo ya uwazi na usawa ya uendelezaji na utumiaji wa rasilimali za maji. Mabonde saba (7) ya maji kati ya tisa (9) yaliyopo nchini yanavuka mipaka ya nchi yetu na hivyo kuwa na ulazima wa kushirikiana na nchi nyingine 17 majirani. Nchi hizo ni Angola, Botswana, Namibia, Zambia, Zimbabwe, Malawi, Msumbiji, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Misri, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan, Sudan Kusini, Uganda na Eritrea. Ushirikiano wa kitaasisi na nchi hizo unatekelezwa kama ifuatavyo:-

(i)    Bonde la Mto Nile

60.          Mheshimiwa Spika, Umoja wa Ushirikiano wa Nchi za Bonde la Mto Nile (Nile Basin Initiative – NBI) ulianzishwa rasmi mwaka 1999. Umoja huo ni chombo cha mpito kuelekea kwenye uundwaji wa Kamisheni ya Bonde la Mto Nile. Madhumuni ya kuanzishwa kwa umoja huo ni kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji, mazingira, nishati, kilimo, mafunzo na kujenga uwezo kwa taasisi zilizopo katika nchi husika. Jumla ya nchi 11 zinaunda umoja huo ambazo ni Burundi, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Misri, Rwanda, Sudan, Sudan Kusini, Uganda na Tanzania na nchi ya Eritrea ikiwa ni mtazamaji (observer).

61.          Mheshimiwa Spika, Nchi saba za Burundi, Ethiopia, Uganda, Rwanda, Kenya,  Sudan Kusini na Tanzania zilisaini Mkataba wa Kudumu wa Ushirikiano wa nchi hizo utakaoanzisha Kamisheni ya Bonde la Mto Nile. Hadi sasa, nchi za Ethiopia na Rwanda tayari zimeridhia Mkataba huo na Tanzania ipo katika hatua za kukamilisha taratibu za kuridhia. Aidha, nchi za Misri, Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinaendelea na misimamo yao ya kutosaini Mkataba huo. Kulingana na matakwa ya Mkataba huo, nchi sita (6) zikikamilisha kuridhia Kamisheni ya Bonde la Mto Nile itaanzishwa. Katika mwaka 2014/2015, nchi ambazo zilisaini Mkataba huo zitakamilisha taratibu za kuridhia kwa kuzingatia sheria za nchi zao. Tanzania itaendelea kufuatilia kwa karibu suala hili ambalo ni la manufaa kwa nchi yetu.

(ii)  Mradi wa Hifadhi ya Mazingira ya Ziwa Victoria

62.          Mheshimiwa Spika, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali za Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda zinatekeleza Awamu ya Pili ya Mradi wa Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira ya Ziwa Victoria (LVEMP II). Lengo la mradi ni kuimarisha usimamizi wa pamoja wa rasilimali za Bonde la Ziwa Victoria kwa kudhibiti uharibifu wa mazingira katika ziwa hilo. Aidha, nchi yetu inanufaika na mradi huo kwa kuimarisha Taasisi zinazohusika na hifadhi ya maji na samaki; ukarabati wa mifumo ya kusafisha majitaka katika miji ya Mwanza, Musoma na Bukoba. Vilevile, Halmashauri za Wilaya za Maswa, Itilima, Busega, Bariadi, Magu, Meatu, Kwimba, Sengerema, Geita, Chato, Muleba, Karagwe, Kyerwa na Misenyi zimeingizwa kwenye awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo.

63.          Mheshimiwa Spika, jumla ya miradi midogo ya kijamii 176 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 4.5 inatekelezwa katika eneo la mradi. Hadi mwezi Machi 2014, miradi 48 imekamilika na itakabidhiwa kwa jamii. Vilevile, miradi 22 mikubwa ya kijamii yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 5.5 imeanza kutekelezwa katika Halmashauri za Wilaya za Musoma Mjini, Maswa, Bariadi, Kwimba, Magu, Meatu na Jiji la Mwanza. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo na kuhakikisha Wataalam Washauri wanakamilisha kazi zao ambazo ni pamoja na kuoanisha Sera, Sheria, Kanuni na Viwango vya utupaji majitaka katika rasilimali za maji zilizopo kwenye Bonde la Ziwa Victoria.

(iii) Bonde la Mto Mara

64.          Mheshimiwa Spika, Bonde la Mto Mara, ni moja kati ya mabonde ya mito inayoingiza maji katika Ziwa Victoria na linahusisha nchi mbili za Kenya (inayomiliki asilimia 65 ya bonde) na Tanzania asilimia 35. Bonde hilo ni eneo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi pamoja na bayoanuai zilizopo. Utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali katika Bonde hilo kikanda unasimamiwa na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (Lake Victoria Basin Commission-LVBC). Katika kuimarisha ushirikiano uliopo katika nchi zetu mbili, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya “Siku ya Mara” ambayo lengo lake ni kushirikisha Wakazi wa Bonde hilo katika kulinda, kusimamia na kuendeleza rasilimali asili za Bonde kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo. Sherehe hizo zilifanyika Mjini Mugumu, Serengeti ambapo mgeni rasmi alikuwa Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

65.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu ilianza uratibu wa Mradi wa masuala ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (Planning for Resilience in East Africa through Policy, Adaptation, Research and Economic Development-PREPARED). Miji iliyopewa kipaumbele katika utekelezaji wa mradi huo ni Halmashauri za Itilima katika Mkoa wa Simiyu, Bunda (Mkoa wa Mara) pamoja na Chato (Mkoa wa Geita). Aidha, taratibu za kuandaa Hati ya Makubaliano (MoU) kwa ajili ya usimamizi shirikishi wa rasilimali za maji katika ikolojia ya Bonde la Mto Mara zinaendelea kati ya nchi shirikishi chini ya uratibu wa Nile Basin Initiatives. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kuratibu miradi mbalimbali itakayotekelezwa kupitia Mradi wa “PREPARED” ili kusaidia wananchi wanaoishi maeneo ya Bonde la Mto Mara kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

66.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu kwa kupitia Mradi wa Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji katika Bonde la Mto Mara, ulio chini ya Umoja wa Ushirikiano wa Nchi za Bonde la Mto Nile imeendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa bwawa la Borenga litakalojengwa kwenye mpaka wa Wilaya za Serengeti na Tarime. Bwawa hilo ni kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo, nishati ya umeme na kilimo cha umwagiliaji katika vijiji 16 vilivyopo katika Wilaya za Butiama, Serengeti na Tarime. Inakadiriwa kuwa hekta 8,340 zitamwagiliwa na maji kutoka katika bwawa hilo ambalo litakuwa na mita za ujazo milioni 20. Aidha, mradi unaendelea na uandaaji shirikishi wa mipango ya usimamizi wa hifadhi ya maji katika sehemu ya Bonde la Mto Mara (Sub Catchment Management Plans) ya Tobora (kilomita za mraba 364) na Somoche (kilomita za mraba 682). Hifadhi hizo za maji zipo katika bonde la Mto Mara Wilayani Serengeti. Vilevile, katika mwaka 2013/2014, mradi ulitoa mafunzo ya uendeshaji na matengenezo wa vifaa vinavyopima wingi wa maji mitoni na ziwani na hali ya hewa (hydro-metereological equipment) kwa Mafundi Sanifu wa Bonde la Ziwa Victoria. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itakamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi wa ujenzi wa bwawa la Borenga na kuandaa zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa ujenzi.

(iv)         Bonde la Mto Zambezi

67.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu iliendelea kutekeleza Mkataba wa Kamisheni ya Bonde la Mto Zambezi (Zambezi Watercourse Commission-ZAMCOM) ulioanza kutekelezwa rasmi kisheria mwaka 2011. Madhumuni ya kuanzisha Kamisheni hiyo ni kusimamia kwa pamoja rasilimali za maji za Bonde la Mto Zambezi. Jumla ya nchi saba (7) zinatekeleza Mkataba wa Kamisheni hiyo ambazo ni Angola, Botswana, Msumbiji, Namibia, Zambia, Zimbabwe na Tanzania. Nchi ya Malawi haijaridhia Mkataba huo hadi sasa. Baada ya Sekretarieti ya muda (Interim ZAMCOM Secretariat) kumaliza muda wake tarehe 31 Desemba, 2013, Sekretarieti ya Kudumu ya Kamisheni ya Bonde la Mto Zambezi imeanza kazi rasmi na Makao Makuu yake yapo Mjini Harare Zimbabwe.

68.          Mheshimiwa Spika, majukumu mengine ya Sekretarieti ya Kudumu ya ZAMCOM ni kuandaa mikakati ya utekelezaji wa mipango ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji za Bonde la Mto Zambezi kwa kuzingatia maamuzi ya vikao vya Baraza la Mawaziri wa Maji wa SADC na lile la nchi wanachama wa ZAMCOM. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kuratibu kazi za Kamisheni hiyo zinazofanyika hapa nchini.

(v)  Bonde la Mto Ruvuma

69.          Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji Shirikishi wa Bonde la Mto Ruvuma unahusisha nchi za Msumbiji na Tanzania na kuratibiwa na Sekretarieti ya SADC. Mradi huo umeanzishwa ili kuhakikisha rasilimali za maji za Bonde hilo zinasimamiwa vizuri na kutumiwa kwa manufaa ya nchi hizo mbili. Hapa nchini mradi unatekelezwa katika Wilaya tano (5) za Mikoa ya Mtwara na Ruvuma ambazo ni Tandahimba, Nanyumbu, Songea Vijijini, Tunduru na Mbinga. Katika mwaka 2013/2014, miradi miwili ya kijamii inatekelezwa katika Wilaya ya Tunduru ambapo jumla ya miche ya miti 5,733 imepandwa katika vijiji viwili vya Daraja Mbili na Lelolelo kwa ajili ya kuzuia mmomonyoko wa ardhi na kutunza vyanzo vya maji. Vilevile, mitambo miwili (2) ya gesi asilia inayotokana na samadi imejengwa katika vijiji vya Nandembo na Majimaji kwa ajili ya matumizi ya kupikia na kuwashia taa.

70.          Mheshimiwa Spika, katika skimu ya umwagiliaji ya Namatuhi iliyoko Wilaya ya Songea Vijijini, Mkandarasi anaendelea na kazi ya ujenzi wa mifereji midogo yenye urefu wa mita 550 na mradi utakamilika mwezi Juni, 2014. Aidha, uchimbaji wa kisima kirefu cha mita 150 na usambazaji wa maji katika kijiji cha Mihambwe, Wilaya ya Tandahimba umekamilika. Aidha, utekelezaji wa mradi wa kusambaza maji katika kijiji cha Mahande, Wilaya ya Mbinga umekamilika. Kupitia mradi huo wananchi wa vijiji hivyo wamepatiwa huduma ya maji safi na salama.

71.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu kwa kushirikiana na taasisi nyingine itakamilisha miradi ya maji ya kijamii, kuelimisha na kuhamasisha wadau kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji na ufungaji wa vituo vya hali ya hewa. Jedwali Na. 4 linaonesha orodha ya miradi inayotekelezwa katika Bonde la Mto Ruvuma.

(vi)         Bonde la Mto Songwe

72.          Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Malawi inatekeleza Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Rasilimali za Bonde la Mto Songwe. Awamu hiyo inahusu usanifu wa kina wa miundombinu ya rasilimali za maji itakayojengwa kwa ajili ya kuzalisha umeme, kilimo cha umwagiliaji na kuzuia mafuriko. Aidha, mpango unaandaliwa kuanzisha Kamisheni ya Pamoja ya Kusimamia Programu na kujenga uwezo kwa watekelezaji wa programu katika ngazi za Halmashauri hadi Taifa. Hadi mwezi Aprili 2014, Mtaalam Mshauri amekamilisha na kuwasilisha rasimu zifuatazo:-Dira ya Maendeleo ya Programu ya Kuendeleza Rasilimali za Maji za Bonde la Mto Songwe, upembuzi yakinifu wa miradi ya kipaumbele na tathmini ya athari za kimazingira na kijamii kuhusu miradi itakayojengwa. Vilevile, amekamilisha rasimu ya mwisho ya mfumo wa kitaasisi kwa ajili ya Kamisheni ya Pamoja ya Kusimamia Programu ya Mto Songwe. Kazi hizo zinatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2015. Mkakati wa elimu na mawasiliano umekamilika na kuanza kutekelezwa kwenye Halmashauri za Wilaya za Mbeya na Momba kwa upande wa Tanzania, na kwa upande wa Malawi katika Wilaya za Karonga na Chitipa.

73.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, usanifu wa awali wa mabwawa matatu (3) katika Bonde la Mto Songwe umekamilika. Lengo la kujenga mabwawa hayo ni kwa ajili ya kudhibiti mafuriko na kuhamahama kwa mto, matumizi ya maji majumbani, kilimo cha umwagiliaji na uzalishaji umeme. Jumla ya hekta 5,635 zinatarajiwa kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji ambapo kwa upande wa Tanzania ni hekta 3,005 na Malawi hekta 2,630. Vilevile, megawati 175 za umeme zinatarajiwa kuzalishwa kutoka bwawa moja (Lower Dam) litakaloanza kujengwa kati ya mabwawa hayo. Katika mwaka 2014/2015, uandaaji wa muundo wa kitaasisi, usanifu wa kina na makabrasha ya zabuni utakamilika. Serikali itaendelea kushirikiana na Serikali ya Malawi kuratibu utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo.

(vii)        Ziwa Tanganyika

74.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kushirikiana kwa karibu na nchi wanachama wengine wa Mamlaka ya Bonde la Ziwa Tanganyika ambazo ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali ya maji ya Ziwa Tanganyika. Tanzania na DRC zinamiliki kwa pamoja asilimia 86 ya Ziwa hilo. Changamoto ya kupungua kwa kina cha maji ya Ziwa Tanganyika imeathiri sana bandari za Kigoma upande wa Tanzania na Kalemie, Uvira na Moba zote za DRC. Aidha, chanzo cha maji kwa ajili ya mji wa Kigoma/Ujiji kiliathirika na kulazimika kuongeza urefu wa bomba kutoka kwenye banio (intake) umbali wa mita 60 ndani ya ziwa. Miongoni mwa sababu zinazochangia tatizo la kupungua kwa kina cha maji ni kubomoka kwa banio la Mto Lukuga ulioko DRC unaotoa maji kutoka Ziwa Tanganyika kupeleka Mto Kongo.

75.          Mheshimiwa Spika, katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dr.Jakaya Mrisho Kikwete alituma ujumbe maalum mara mbili, mwezi Agosti, 2010 na Machi, 2014 kwa Rais wa DRC, Mhe. Joseph Kabila Kabange kuhusu umuhimu wa Tanzania na DRC kushirikiana (bilaterally) katika kukarabati banio la Mto Lukuga.

76.          Mheshimiwa Spika, kufuatia hatua nilizozitaja, usanifu wa kina wa banio husika umekamilika mwezi Desemba, 2013 kwa ufadhili wa COMESA. Jumla ya Dola za Marekani milioni 65 zinahitajika kutekeleza miradi ya kudhibiti kupungua kwa kina cha Ziwa kwa kujenga upya banio hilo. Aidha, Wizara yangu ilimwalika Waziri wa Maji na Umeme wa DRC kuja Tanzania mwezi Aprili, 2014 kwa lengo la kujadili namna tutakavyo washirikisha wadau wa maendeleo ili kupata fedha za kujenga upya banio hilo. Mkutano wetu ulikuwa wa mafanikio na kwamba tutaunda timu ya pamoja ya Wataalam kutoka Sekta za Maji, Mazingira na Usafirishaji kushughulikia changamoto zilizopo. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itajenga ushirikiano imara na nchi za DRC, Zambia na Burundi kuhifadhi rasilimali za maji ya Bonde la Ziwa Tanganyika.

(viii)      Ziwa Chala, Ziwa Jipe na Mto Umba

77.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaratibu uandaaji wa Mpango Shirikishi wa Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji katika ekolojia ya Maziwa ya Chala na Jipe; na Mto Umba. Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Kenya na Tanzania kuhusu utunzaji na uendelezaji wa ekolojia ya maziwa hayo ilisainiwa mwezi Februari, 2013. Makubaliano hayo yanasisitiza kusimamia na kuendeleza rasilimali zilizoko katika maeneo hayo ili matumizi yake yawe endelevu, ikiwa ni pamoja na kulinda mifumo ya ekolojia kwa ustawi wa wananchi wa nchi hizo.

78.          Mheshimiwa Spika, kikao cha pamoja kati ya Tanzania na Kenya kilifanyika Mjini Taveta mwezi Machi, 2014 na kufikia makubaliano ya kuandaa mpango wa kitaalam wa kutumia maji ya Ziwa Chala kwa ajili ya matumizi ya majumbani na kilimo cha umwagiliaji kwa wakazi wanaozunguka ziwa hilo, kwa kuzingatia kuwa eneo linalozunguka ziwa hilo ni kame. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kushirikiana na nchi ya Kenya kutekeleza makubaliano hayo. Lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa miradi ya kuboresha maisha ya jamii inatekelezwa, hususan miradi ya maji kwa matumizi ya majumbani. Vilevile, kilimo cha umwagiliaji kitaanza kwa eneo dogo, hatua kwa hatua kwa kuzingatia usawa wa maji ziwani (trend monitoring).


79.          Mheshimiwa Spika, usimamizi wa rasilimali za maji nchini unahusisha utambuzi na ufuatiliaji wa wingi na ubora wa maji kutoka katika vyanzo vya maji. Jukumu kuu la Wizara yangu ni kuhakiki ubora, usafi na usalama wa maji katika vyanzo vya maji na  mitandao ya usambazaji maji vijijini na mijini kwa lengo la kulinda afya na ustawi wa wananchi. Kama tunavyofahamu, afya ya wananchi inaweza kuathirika vibaya kama maji yanayotumika hayakidhi viwango kutokana na kuchafuliwa na mifumo asilia au shughuli za kibinadamu, hivyo ni muhimu kuwa na takwimu za ubora wa maji zitakazosaidia kuweka mifumo madhubuti ya kuhifadhi na kudhibiti uchafuzi wa vyanzo vya maji.

80.          Mheshimiwa Spika, Maabara za maji nchini zinafuatilia na kuchunguza ubora wa maji katika vyanzo na mitandao ya usambazaji maji. Aidha, maabara hutoa ushauri wa kitaalam kwa mamlaka za maji, vyombo vya watumiaji maji, Bodi za maji za mabonde, taasisi na watu binafsi kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango vinavyokubalika kwa matumizi yaliyokusudiwa. Katika mwaka 2013/2014, Wizara ilipanga kukagua vyanzo vya maji kwa kuchunguza sampuli 8,000 za maji ili kuhakiki ubora wake. Vilevile, sampuli 1,000 za majitaka zilipangwa kuchunguzwa kwa lengo la kuhakiki ubora wake kabla ya kurudishwa kwenye mazingira ili kudhibiti uchafuzi wa vyanzo vya maji na kuepusha athari za kiafya kwa wananchi na mfumo wa ekolojia. Takwimu hizo ni muhimu katika kuandaa mikakati ya kudhibiti uchafuzi wa vyanzo vya maji.

81.          Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Machi, 2014, sampuli 4,673 za maji zilikusanywa na kuhakikiwa ubora wake. Kati ya hizo, sampuli 3,200 ni za maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani; sampuli 382 kwa matumizi ya viwandani; sampuli 712 ni za kuratibu mwenendo wa ubora wa maji katika vyanzo (mito, chemichemi, maziwa na mabwawa); sampuli 341 za utafiti; na sampuli 38 kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji. Jedwali Na. 5 linaonesha mwelekeo wa sampuli za maji zilizokusanywa na kuchunguzwa ubora wake kuanzia mwaka 2009/2010 hadi Machi, 2014.

(a)           Ubora wa Maji kwa Matumizi ya Majumbani

82.          Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza hapo awali, wananchi wote wa vijijini na mijini wanatakiwa kutumia maji safi na salama ili kulinda afya zao kwa ustawi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Sheria ya Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Na. 12  ya mwaka 2009 inavitaka vyombo vinavyohusika na huduma hii kuhakikisha maji yanayosambazwa yana ubora unaokubalika. Matokeo ya uchunguzi wa sampuli 2,880 sawa na asilimia 90 yameonesha kuwa maji hayo yalikidhi viwango vinavyokubalika. Sampuli 320, maji yake hayakukidhi viwango kutokana na uwepo wa kiwango kikubwa cha chumvichumvi, madini-chuma (iron), manganese na fluoride. Maji yaliyoonekana kuwa na madini-chuma na manganese, ushauri ulitolewa maji hayo yawekwe katika hali ya kuongezewa hewa ya Oxgen (aeration) ambayo huwezesha madini chuma kutuama kama masimbi, au kutafuta vyanzo mbadala. Kwa vyanzo vilivyobainika kuwa na kiwango kikubwa cha madini ya fluoride, hatua zimeanza kuchukuliwa kutafuta vyanzo mbadala vya kukidhi mahitaji pamoja na kutumia teknolojia ya kuondoa madini ya fluoride kwenye maji ya kunywa na kupikia. Aidha, ushauri ulitolewa wa kutumia madawa ya kutibu maji yanayokidhi viwango na kukagua mitambo ya kusafisha maji mara kwa mara kwa kuzingatia mabadiliko ya ubora wa maji yanayotokana na misimu ya mwaka. Jedwali Na. 6 linaonesha maeneo ambayo maji hayakukidhi viwango vinavyokubalika.

83.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutekeleza Mpango wa Usalama wa Maji (Water Safety Plan) kwa maeneo mbalimbali nchini. Mpango huo una lengo la kuboresha shughuli za usimamizi wa ubora wa maji kwa mamlaka za maji na vyombo vya watumiaji maji vijijini (COWSOs) kuanzia kwenye chanzo cha maji hadi kwa mtumiaji.

(b)           Ubora wa Maji kwa Matumizi ya Viwanda

84.          Mheshimiwa Spika, shughuli za viwanda zinahitaji maji yanayokidhi viwango vya ubora kwa lengo la kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa au kusindikwa zinakidhi viwango. Kwa kuzingatia hilo, jumla ya sampuli 382 kutoka viwanda mbalimbali vya kuzalisha bidhaa zilikusanywa na kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara. Kati ya hizo, sampuli 358 zilitoka viwanda vya samaki katika Miji ya Bukoba, Musoma, Tanga, Mafia, Mwanza na Dar es Salaam na matokeo ya uchunguzi huo yalionesha maji kukidhi viwango vya kimataifa. Sampuli 24 kutoka viwanda vya sukari-Kagera, saruji na Pepsi Mkoani Mbeya zilichunguzwa na matokeo kuonesha kuwa maji yana ubora unaokubalika kwa matumizi yaliyokusudiwa.

(c)           Kuratibu Mwenendo wa Ubora wa Maji katika Vyanzo

85.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Mradi wa Hifadhi ya Mazingira ya Ziwa Victoria (LVEMP) hufuatilia mwenendo wa ubora wa maji na udhibiti wa ongezeko la magugu maji katika Ziwa Victoria. Hadi mwezi Machi, 2014, kwa upande wa Tanzania ufuatiliaji (cruise monitoring) kwenye vituo 28 ulifanyika na jumla ya sampuli 334 zilikusanywa na kuchunguzwa. Matokeo yalionesha kuwa hali ya uwepo wa virutubisho vya nitrate na phosphorus kwenye vituo vya pembezoni mwa ziwa bado ni mkubwa kutokana na shughuli za kibinadamu ikilinganishwa na vituo vya katikati ya ziwa ambapo hali ya wingi wa virutubisho inapungua. Aidha, sampuli za maji katika mabonde ya Wami-Ruvu (124), Ziwa Tanganyika (56), Ziwa Rukwa (41), Rufiji (27), Bonde la Kati (86), Pangani (8), Ziwa Nyasa (8) na Pwani ya Kusini (28) zilipimwa kwa ajili ya kutoa takwimu zinazotumika katika usimamizi wa rasilimali za maji. Matokeo yalionesha maji kutoka kwenye vyanzo hivyo kuwa na ubora unaokubalika kwa ustawi wa viumbe hai na kuendelezwa kwa matumizi mbalimbali.

(d)           Ubora wa Maji kwa ajili ya Umwagiliaji na Utafiti

86.          Mheshimiwa Spika, maji yanayotumika kwa ajili ya umwagiliaji yanatakiwa kukidhi viwango vya ubora kutegemeana na aina ya udongo na aina ya mazao yanayomwagiliwa ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao hayo. Hadi mwezi Machi 2014, sampuli 38 za maji kwa ajili ya umwagiliaji kutoka maeneo ya Kiloka, Mikindo (Morogoro), Mlowa, Matali (Iringa), Matiganjola, Kivavi, Igongolo (Njombe), Litapwasi, Peramiho (Ruvuma) na Kibiti (Pwani). zilichunguzwa na kuonesha kukidhi ubora kwa matumizi yaliyokusudiwa. Aidha, Wizara hupima sampuli za maji kwa ajili ya shughuli za utafiti kutoka kwenye taasisi na watu binafsi. Sampuli 341 za maji zilipokelewa na kuchunguzwa na ushauri ulitolewa kulingana na mahitaji ya utafiti.

(e)           Ubora wa Majitaka Yanayorudishwa kwenye Mazingira

87.          Mheshimiwa Spika, moja ya sababu za uchafuzi wa vyanzo vya maji ni majitaka yanayozalishwa viwandani na majumbani. Hadi mwezi Machi 2014, sampuli 630 za majitaka kutoka kwenye mabwawa ya majitaka ya Miji ya Dodoma, Morogoro, Mwanza, Dar es Salaam, Tanga na Iringa; na kutoka viwanda vya sukari, samaki, nguo, bia na tumbaku zilikusanywa na kuchunguzwa. Kati ya hizo sampuli 120 zilichunguzwa kuangalia uwezo wa mifumo ya kusafisha majitaka na uchunguzi wa sampuli 510 ulilenga kuhakiki ubora wa majitaka yanayorudishwa kwenye mazingira. Matokeo yalionesha kuwa asilimia 85 yana ubora usiosababisha uchafuzi wa vyanzo vya maji na ushauri wa kitaalam wa kuboresha utendaji wa mabwawa na mitambo ya kusafisha majitaka ulitolewa kwa taasisi husika.

88.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea itaimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa ubora wa maji kwenye vyanzo kwa ajili ya matumizi ya majumbani, viwandani, kilimo na mazingira. Katika kutekeleza majukumu hayo, sampuli 8,000 za maji na sampuli 1,000 za majitaka zitakusanywa na kuchunguzwa. Takwimu zitakazopatikana zitatumika kushauri hatua za kuchukua kabla ya kutumia maji kutoka kwenye chanzo husika. Aidha, takwimu hizo zitawezesha utekelezaji wa Mkakati wa Kusimamia Ubora wa Maji na Kudhibiti Uchafuzi wa Maji (Water Quality Management and Pollution Control Strategy) ambapo moja ya shughuli zilizoainishwa ni ufuatiliaji wa mwenendo wa kiwango cha madini tembo (heavy metals) aina ya zebaki (mercury), arsenic, urani (uranium) na cyanide katika vyanzo vya maji kwenye maeneo ya migodi.

(f)            Ubora wa Madawa ya Kusafisha na Kutibu Maji

89.          Mheshimiwa Spika, ni wajibu wetu kuhakiki madawa ya kutibu na kusafisha maji ili kuthibitisha ubora wake katika kupata maji safi na salama. Jumla ya sampuli 50 za madawa ya kusafisha na kutibu maji kutoka Morogoro, Tanga, Chalinze na DAWASCO zilihakikiwa ubora wake. Kati ya sampuli hizo, sampuli za shabu (Aluminium Sulphate) zilikuwa 16, sodium bicarbonate nne (4) na Polyaluminium Chloride (15) ambazo hutumika kusafisha maji; na Calcium Hypochlorite (15) inayotumika kuua vijidudu. Matokeo yalionesha kuwa sampuli 33 zilikuwa na viwango vinavyokubalika na ushauri wa kitaalam ulitolewa kuhusu matumizi sahihi ya madawa hayo. Sampuli 17 ambazo ni za Calcium Hypochlorite nne (4), Aluminium Sulphate sita (6) na Polyaluminium Chloride saba (7) zilibainika kuwa na viambata hafifu visivyotosheleza kutibu maji katika kiwango kinachotakiwa. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kuhakiki ubora wa madawa na kukagua ufanisi wa mitambo ya kusafisha na kutibu maji pamoja na kutoa ushauri wa kitaalam kwa vyombo vinavyotoa huduma ya majisafi vijijini na mijini.



(g)           Uondoaji wa Madini ya Fluoride katika Maji ya Kunywa na Kupikia

90.          Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu ya mwaka 2013/2014 nililielezea Bunge lako Tukufu kuwa Wizara yangu imeandaa mkakati wa usambazaji wa teknolojia ya uondoaji madini ya fluoride katika maji ya kunywa na kupikia kwa kutumia mkaa wa mifupa ya ng'ombe (bone char). Hadi Machi, 2014, tanuru mbili (2) zenye uwezo wa kuchoma tani nne (4) za mifupa ya ng’ombe kwa mara moja zimejengwa na majaribio ya kubaini ufanisi wa uchomaji katika matanuru hayo yanaendelea. Vilevile, mould kwa ajili ya kuzalisha mitambo ya kuondoa madini ya fluoride katika maji ya kunywa na kupikia kwa ngazi ya kaya imenunuliwa na uzalishaji wa mitambo 1,000 kwa ajili ya kuisambaza kwenye kaya za maeneo yenye vyanzo vya maji yenye kiwango kikubwa cha fluoride unaendelea kufanyika. Lengo ni kuhamasisha wananchi kutumia teknolojia ya mkaa wa mifupa ya ng’ombe ili kuondoa madini ya fluoride katika maji ya kunywa na kupikia na hivyo kupunguza athari hasa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

91.          Mheshimiwa Spika, mwezi Novemba 2013, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilitembelea Kituo cha Utafiti wa Fluoride kilichopo Ngurdoto Mkoani Arusha na jamii inayotumia vifaa vya kuondolea madini hayo katika maji ya kunywa vilivyobuniwa na kituo hicho. Lengo la ziara hiyo, lilikuwa kutoa fursa kwa Kamati hiyo ya Bunge kutathmini utafiti unaofanyika na kupata taarifa ya hatua iliyofikiwa ya matumizi ya teknolojia ya chengachenga za mkaa wa mifupa ya ng’ombe (Bonechar filter media). Matumizi ya teknolojia ya kuondoa madini ya Fluoride imetumika kwa zaidi ya miaka mitatu sasa katika ngazi ya kaya katika kaya 22 kwenye maeneo ya Ngaramtoni (9), Kijenge (1), Leganga (1), Kiwawa (1), Ngongongare (6), Arusha Mjini (1), Njiro (2) na Olasiti (1), Mkoani Arusha. Vilevile, kwa ngazi ya jamii 11, Mkoa wa Arusha na jamii moja (1) maeneo ya Mwando, Mkoa wa Singida. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea na mkakati wa usambazaji wa teknolojia ya mkaa wa mifupa ya ng’ombe na kutayarisha ramani (fluoride mapping) itakayoainisha maeneo yenye kiwango kikubwa cha fluoride katika maji ili kuyatambua maeneo hayo wakati wa kuibua miradi ya maji.

(h)           Maabara za Maji kupata Ithibati (Accreditation)

92.          Mheshimiwa Spika, vigezo vinavyotumika kwa taasisi zinazohusika na vipimo na uchunguzi wa kimaabara kutambulika kimataifa ni kupata Ithibati (Accreditation). Kupatikana kwa Ithibati kutawezesha Maabara zetu kutambulika kimataifa na hivyo, kukidhi miongozo ya Sheria Na. 11 ya mwaka 2009 ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji, Sheria Na.12 ya mwaka 2009 ya Huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira na Sheria Na. 20 ya mwaka 2004 ya Usimamizi wa Mazingira. Maabara ya Maji Mwanza imekamilisha uandaaji wa mwongozo wa utendaji kazi (Quality Manual) na kuwasilisha kwa taasisi inayosimamia shughuli hizo kimataifa (SADCAS) kwa ajili ya kufanyiwa tathmini. Lengo la Wizara yangu ni kuziwezesha maabara zote kukidhi vigezo vya kupata Ithibati na hivyo kuwa na maabara zenye viwango.

93.          Mheshimiwa Spika, hatua hiyo inawezesha maabara zetu kushiriki kwenye majaribio ya kujipima uwezo wa utendaji kazi za kimaabara (Laboratory Performance Evaluation or Proficiency Testing) yanayoandaliwa na taasisi za kimataifa. Majaribio hayo hufanyika kila mwaka na kwa mwaka 2013/2014 majaribio yaliyofanywa ni:-

(i)        Mwezi Julai 2013, Maabara saba (7) za Iringa, Mwanza, Arusha, Morogoro, Mbeya, Tanga na Maabara Kuu Dar es Salaam zilishiriki katika jaribio la kujipima uwezo linaloratibiwa na Southern Africa Development Community Measurement Traceability (SADCMET).

(ii)       Mwezi Agosti 2013, Maabara tisa (9) za Mwanza, Iringa, Mbeya, Tanga, Arusha, Dodoma, Mtwara, Bukoba na Maabara Kuu Dar es Salaam zilishiriki katika jaribio la kujipima uwezo chini ya Programu ya Global Environmental Monitoring System/Water (GEMS/Water).

Tathmini ya matokeo ya majaribio hayo imeonesha kuwa maabara zilizoshiriki zimefanya vizuri kwa wastani wa asilimia 65 kwa vielelezo vya kemikali na asilimia 92 ya upimaji wa vimelea vya vijidudu (bacteria) kwenye maji. Tathmini hiyo inaonesha kuwa maabara zinaongeza ufanisi katika utendaji kimaabara baada ya kujengewa uwezo wa kupatiwa vitendea kazi. Jedwali Na. 7 linaonesha matokeo ya majaribio ya kujipima uwezo wa maabara za maji kwa ajili ya kupata ithibati.

94.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea na ukarabati wa Maabara Kuu ya Wizara na maabara za mikoa. Uboreshaji huo utaongeza ufanisi katika utendaji kazi na hivyo kutoa huduma yenye tija zaidi. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuzijengea uwezo maabara zake kwa kuweka mazingira mazuri kwa wataalam kufanya kazi za uchunguzi katika hali bora na salama kama inavyoelekezwa kwenye viwango vya kimataifa (ISO 17025).




95.          Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika utangulizi wa hotuba hii, Sekta ya Maji ni moja kati ya sekta sita (6) zinazotekeleza mpango maalum wa “Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa” (Big Results Now) ulioandaliwa na Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete. Katika Sekta ya Maji, tathmini ya BRN juu ya hali ya huduma ya maji vijijini iliyofanyika mwezi Februari, 2013 ilibaini hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kushuka kutoka asilimia 57.8 hadi kufikia asilimia 40. Sababu za kushuka kwa huduma hiyo ni pamoja na kuharibika kwa baadhi ya miundombinu ya maji kulikosababishwa na ukosefu wa matengenezo ya mara kwa mara ya miundombinu hiyo. Utekelezaji wa mpango wa BRN ulioanza rasmi mwezi Julai 2013, umeboresha kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji vijijini hadi kufikia asilimia 49 mwezi Machi 2014. Lengo ni kufikia asilimia 74 ifikapo mwezi Juni 2016. Mpango huo unaelekeza maeneo manne (4) ya utekelezaji ambayo ni ujenzi wa miradi mipya (new construction), ukarabati wa miradi chakavu (rehabilitation), upanuzi wa miradi iliyopo (extension) na uendeshaji na matengenezo (operation and maintenance).

96.          Mheshimiwa Spika, ujenzi wa miradi mipya unahusisha miradi ya vijiji 10 kwa kila Halmashauri pamoja na miradi ya kimkakati (strategic projects). Miradi ya upanuzi na ukarabati inahusisha utekelezaji wa miradi ya matokeo ya haraka kutoka kwenye vyanzo vya mabwawa, visima virefu, vyanzo vidogo vya juu ya ardhi, miradi ya kitaifa na miradi inayohitaji matengenezo. Aidha, uendeshaji na matengenezo unahusu kuvijengea uwezo vyombo vya watumiaji maji na ukusanyaji wa taarifa za utekelezaji wa miradi.


97.          Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI kusimamia utekelezaji wa BRN kulingana na mipango na vipaumbele kama ilivyoainishwa kwa kila Halmashauri. Katika kuhakikisha miradi ya maji vijijini inatekelezwa kwa haraka na ufanisi, Wizara imepeleka wataalam wazoefu katika Sekretarieti za Mikoa ili kuwajengea uwezo Wahandisi wa Mikoa na Halmashauri. Vilevile, Wizara imeondoa vibali (No-Objection) ili kupunguza muda wa ununuzi wa Wataalam Washauri na Wakandarasi. Hatua nyingine ni kuhusu ujenzi wa miradi kuanza hata kama fedha zote za mradi hazijaifikia Halmashauri na hata kama michango ya wananchi haijakamilika. Michango hiyo inatumika wakati wa uendeshaji wa miradi baada ya ujenzi kukamilika.

98.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu ilikasimiwa shilingi bilioni 236 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji vijijini. Aidha, kiasi kingine cha shillingi bilioni 108 kilikasimiwa kupitia mafungu ya mikoa kwa ajili ya Halmashauri, OWM-TAMISEMI na Wizara zinazoshiriki katika kutekeleza kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira vijijini. Hadi kufikia Machi 2014, Serikali imezipatia Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa shilingi 137,904,598,951 kwa ajili ya utekelezaji na usimamizi wa mradi wa maji wa vijiji 10 kwa kila Halmashauri. Vilevile, jumla ya shilingi 10,610,746,989 zimeelekezwa kwenye miradi mingine ya maji vijijini kama vile miradi ya yenye kuleta matokeo ya haraka, ujenzi wa mabwawa, vijiji 100 kutoka bomba la KASHWASA, Same-Mwanga-Korogwe na gharama za ziada za usimamizi na ufuatiliaji wa miradi. Jedwali Na. 8 linaonesha mgao wa fedha zilizotumwa kwenye Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa.

99.          Mheshimiwa Spika, kwa kutumia fedha hizo, jumla ya miradi ya maji 248 yenye jumla ya vituo vya kuchotea maji 10,560 imejengwa kwenye Halmashauri 98 na kunufaisha vijiji 270. Juhudi hizo zimeongeza idadi ya wakazi vijijini wanaopata huduma ya maji safi na salama kutoka wakazi 15,200,000 mwezi Juni, 2013 hadi kufikia wakazi 17,840,000, sawa na ongezeko la wakazi 2,640,000 . Ongezeko hilo limeboresha huduma ya upatikanaji wa maji vijijini kutoka asilimia 40 hadi kufikia asilimia 49. Lengo la Serikali kulingana na Mpango huo, ni kuwapatia huduma ya maji wananchi milioni 22 waishio vijijini ifikapo mwezi Juni 2014. Hata hivyo uwezekano wa kufikia lengo hilo unaendelea kufifia kutokana na upatikanaji wa fedha mdogo.

3.2.3 Mpango wa BRN kwa mwaka 2014/2015

100.      Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2014/2015, Wizara yangu imepanga kuendelea kutekeleza miradi ya maji vijijni chini ya Mpango wa BRN. Kazi zitakazotekelezwa ni ujenzi na upanuzi wa miradi ya maji pamoja na ukarabati wa miundombinu ya maji. Fedha zilizopangwa kutumika ni shilingi bilioni 270.97, ambapo shilingi bilioni 166.81 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 104.16 ni fedha za nje. Fedha hizo zitatekeleza miradi kwenye vijiji 1,239 na itakapokamilika itakuwa na vituo 28,031 vya kuchotea maji vitakavyohudumia jumla ya wakazi 7,007,628 wanaoishi vijijini.



(a)           Ujenzi wa Miradi Mipya

(i)    Ujenzi wa Miradi ya Vijiji 10 kwa kila Halmashauri

101.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inatekeleza Mradi wa Maji wa Vijiji 10 ambapo katika mwaka 2013/2014, vijiji 1,538 vilipangwa kupatiwa huduma ya maji. Hata hivyo, wakati wa utekelezaji vijiji 17 zaidi viliongezwa na kufikia jumla ya vijiji 1,555. Mradi huo ukikamilika, vituo 32,274 vya kuchotea maji vyenye uwezo wa kuhudumia wananchi wapatao 8,068,500 vitakuwa vimejengwa kwenye Halmashauri 167 kati ya Halmashauri 168 nchini. Vijiji vya Halmashauri iliyobaki ya Manispaa ya Musoma vitapata huduma ya maji kutoka katika mradi wa maji na usafi wa mazingira unaoendelea kutekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Musoma.

102.      Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mpango huo wa vijiji 10, miradi ya maji 766 kwenye vijiji 830 imeendelea kutekelezwa katika Halmashauri zote nchini. Hadi mwezi Machi 2014, kati ya miradi hiyo, miradi 228 kwa ajili ya vijiji 247 imekamilika. Kukamilika kwa miradi hiyo kumeongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi 2,398,500 zaidi waishio vijijini. Aidha, miradi 538 kwenye vijiji 583 itakayokuwa na vituo 9,630 yenye uwezo wa kuhudumia watu 2,407,500 inaendelea kujengwa; mikataba ya ujenzi wa miradi 707 kwa ajili ya vijiji 725 itakayokuwa na vituo 13,050 vyenye uwezo wa kuhudumia watu 3,262,500 imesainiwa.

103.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 148.12 kujenga miradi ya maji ya vijiji 10 kwenye vijiji 725 katika Halmashauri 167 ambapo jumla ya vituo 13,050 vya kuchotea maji vinatarajiwa kujengwa vyenye uwezo wa kuhudumia wakazi wapatao 3,262,500.

(ii)  Miradi ya Kimkakati

Mradi wa Maji Masoko

104.      Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji Masoko unaojengwa katika Wilaya ya Rungwe ulisimama baada ya Halmashauri kusitisha Mkataba wa Mkandarasi aliyeshindwa kutekeleza kazi kulingana na viwango vya usanifu. Kazi za mradi huo zinahusisha ujenzi wa banio la maji, chujio la maji, matanki matatu (3) ya kuhifadhia maji yenye ujazo wa lita 90,000 kila moja, vituo 122 vya kuchotea maji, ununuzi wa pampu na ulazaji wa mabomba. Mradi unalenga kunufaisha wakazi 15,158 wa vijiji 15 vya Bulongwe, Igembe, Ngaseke, Ntandabala, Lupando, Bujesi, Lufumbi, Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifwa, Ikama, Itagata, Nsanga na Nsyasya. Awali mradi huo ulikadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi 4,754,773,420. Gharama ya kazi zilizofanyika ni shilingi 1,713,445,750. Hata hivyo, hadi Mkataba unasitishwa Mkandarasi huyo alikuwa amelipwa kiasi cha shilingi 1,269,851,102.

105.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali itaendelea kukamilisha Mradi wa Maji wa Masoko kwa vipande (lots) kwa kadri fedha zitakavyopatikana. Hii ni kutokana na gharama za kukamilisha mradi huo zinazotolewa na wakandarasi kuwa mara mbili zaidi ya gharama zilizokadiriwa kwenye usanifu wa mradi. Mradi huo utajengwa na Halmashauri kwa kutumia Wakandarasi wadogo na ujenzi utasimamiwa na Wataalam wa Wizara wakishirikiana na Wataalam wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mbeya na Wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ili kuharakisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa Masoko.

106.      Mheshimiwa Spika, Serikali kwa  kushirikiana na Washirika wa Maendeleo  inatekeleza mradi wa Same-Mwanga-Korogwe unaolenga kupeleka maji katika miji ya Mwanga na Same.  Mchango wa BADEA wa  Dola za Marekani milioni 10, OFID Dola za Marekani milioni 12 na Serikali Dola za Marekani milioni 13.76  zitatumika kujenga sehemu ya mradi kutoka kwenye chanzo katika bwawa la  Nyumba ya Mungu, mtambo wa kutibu maji eneo la Njia Panda na  kulaza bomba kubwa la milimita 900 au inchi 35 hadi  kwenye matanki  ya kituo cha kusukuma maji  Kisangara. Tangazo la kupata Mkandarasi kwa ajili ya kazi hiyo limetolewa tarehe 1 Mei, 2014 na Mkandarasi anategemewa kuanzia kazi mwezi Agosti, 2014.

107.      106. Mheshimiwa Spika, Mkataba wa kupata fedha (Financing Agreement) kati ya Serikali na Kuwait Fund (Dola za Marekani milioni 34), Saud Fund (Dola za Marekani milioni 25), BADEA (Dola za Marekani milioni 12) na OFID (Dola za Marekani milioni 15) utasainiwa mwezi Septemba, 2014. Fedha hizi ni za kujenga sehemu ya mradi kutoka Kisangara hadi Mwanga na Same kupitia kwenye matanki mawili yenye ujazo  lita milioni 7.5 kila  moja eneo la Kiverenge.  Mkandarasi anategemewa kupatikana  na kuanza kazi mwezi  Machi, 2015.  Mradi huu utakapokamilika utahudumia wananchi 456, 931.

108.      Mheshimiwa Spika, katika awamu ya pili, Washirika wa Maendeleo walioahidi kutoa fedha ni Kuwait Fund Dola za Marekani milioni 34, Saudi Fund Dola za Marekani milioni 25, BADEA Dola za Marekani milioni 12 na OFID Dola za Marekani milioni 15. Fedha hizo zinatarajiwa kupatikana mwezi Septemba, 2014 na ujenzi wa awamu ya pili utaanza mwezi Machi, 2015.
Mradi wa Maji Vijijini katika Mkoa wa Tabora

109.      Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Japan inatekeleza mradi wa maji katika vijiji 20 kwenye Wilaya zote saba za Mkoa wa Tabora. Mradi una awamu mbili; awamu ya kwanza ilianza mwezi Septemba, 2009 na kukamilika mwezi Machi, 2014. Awamu ya pili imeanza kutekelezwa mwezi Aprili, 2014 na inatarajiwa kukamilika mwaka 2016. Katika awamu ya kwanza, kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kukarabati visima virefu na vifupi 46 vya pampu za mkono katika Wilaya sita; kuandaa Mpango Mahsusi wa Maji Vijijini kwa Mkoa unaoanisha maeneo ya kipaumbele ya kutekeleza miradi ya maji; kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ya maji katika vijiji 20; na kuandaa makadirio ya gharama za ujenzi pamoja na makabrasha ya zabuni.

110.      Mheshimiwa Spika, awamu ya pili ya mradi imeanza kutekelezwa mwezi Aprili, 2014 na itaendelea hadi mwaka 2016. Mradi ukikamilika utanufaisha zaidi ya wananchi 45,000. Kampuni ya KONOIKE ya Japan imepewa kazi ya kutekeleza mradi kwa gharama ya Yeni za Kijapan 1,560,000,000 sawa na shilingi bilioni 25. Awamu hiyo inahusisha kazi zifuatazo:-

  i.              Ujenzi wa miradi minne (4) ya usambazaji maji katika vijiji vinne (4) vya Isanga (Nzega), Mpumbuli na Mabama (Uyui) na Kakola (Manispaa ya Tabora);

ii.              Ujenzi wa visima virefu 114 vya pampu za mkono katika Wilaya saba za Mkoa katika vijiji vya Busomeke na Kalemela (Igunga); Isanga, Kitangili, Makomelo na Wela (Nzega); Kasandalala, Usunga na Mpombwe (Sikonge); Mabama, Ufuluma na Mpumbuli (Uyui); Kakola, Misha na Kalumwa (Manispaa ya Tabora); na vijiji vya Imalamakoye, Kapilula, Kalembela, Kiloleni na Usungwa katika Wilaya ya Urambo/Kaliua; na

Mafunzo kwa Wataalam wa Maji kuhusu uendeshaji na matengenezo ya miradi na mafunzo kwa vitendo kuhusu matumizi ya vifaa vya utafiti wa maji chini ya ardhi.

(iii) Mradi wa Maji na usafi wa Mazingira Mkoa wa Kigoma (Water and Sanitation Kigoma Region Project - WaSKiP)

111.      Mheshimiwa Spika, Serikali ya Ubelgiji imekubali kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi ya maji vijijini katika Mkoa wa Kigoma. Miradi hiyo itaongeza upatikanaji wa maji safi na salama vijijini na inatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 20.6 . Kati ya hizo shilingi bilioni 18.13 sawa na Euro milioni 8 zitatolewa na Serikali ya Ubelgiji wakati shilingi bilioni 2.44 zitatolewa na Serikali ya Tanzania. Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2014/2015. Kwa mwaka huu wa fedha, kiasi cha shilingi milioni 90.63 ambacho kitatolewa na Serikali ya Ubelgiji kimetengwa ili kuwezesha kufanya mapitio ya master plan ya mkoa, kutayarisha mpango wa utekelezaji, kupata orodha ya vijiji vitakayotekelezwa (identification study) na kufanya usanifu. Ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2015/16.

(iv)         Miradi yenye Matokeo ya Haraka (Quickwins)

 Mradi wa Maji Vijiji 100 Kandokando ya Bomba la Ziwa Victoria hadi Kahama-Shinyanga

112.      Mheshimiwa Spika, Wizara inatekeleza Mradi wa Maji wa vijiji 100 vilivyoko kandokando ya bomba kuu kutoka Ziwa Victoria hadi Kahama-Shinyanga. Hadi mwezi Machi, 2014 upimaji na usanifu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika vijiji 31 vilivyoko Halmashauri za Wilaya za Msalala na Shinyanga Vijijini umekamilika. Ujenzi wa miradi katika vijiji vinne vya Magobeko, Nyashimbi, Kakulu na Butegwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala umeanza. Taratibu za kuwapata wakandarasi wa ujenzi wa miradi katika vijiji vingine zinaendelea.

113.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015, Wizara itakamilisha usanifu kwenye vijiji vingine vilivyobaki kufikia vijiji 100 na ujenzi wa miradi katika vijiji 40 utakamilika ifikapo mwezi Juni, 2015. Utekelezaji huo utagharimu kiasi cha shilingi 2,586,819,387 na matarajio ni kuwa na vituo 664 vya kuchotea maji vitakavyohudumia zaidi ya wananchi 115,430. Jedwali Na. 9 linaonesha utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji 40 kandokando ya bomba kuu la maji toka Ziwa Victoria hadi Kahama-Shinyanga.

Mradi wa Maji Bungu

114.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la World Vision iliendelea na kazi za upanuzi na ukarabati wa mradi wa maji wa Bungu katika Wilaya ya Korogwe. Hadi mwezi Machi, 2014, jumla ya vituo 22 vya kuchotea maji vimejengwa na kukarabatiwa katika vijiji vya Bungu, Manka na Msasa ambapo wakazi 6,909 wanapata huduma ya maji. Vilevile, bomba kuu lenye urefu wa kilomita 10.4 kutoka chanzo cha maji kilichopo Sakare hadi kitongoji cha Sinai limejengwa; na mtandao wa kusambaza maji kutoka tanki la Gare hadi kijiji cha Msasa wenye urefu wa kilomita 4 umekamilika. Aidha, mtandao wa kusambaza maji katika kijiji cha Manka wenye urefu wa kilomita 6 umekamilika na matanki mawili yenye ujazo wa lita 90,000 kila moja yamejengwa katika vijiji vya Manka na Gare.

115.      Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi huo utaendelea katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 ambapo tanki lenye ujazo wa lita 90,000 litajengwa katika kijiji cha Sinai na mtandao wa mabomba utajengwa katika vijiji vya Bungu-Msiga, Ngulu, Kwemshai na Mlungui. Mradi huo utakapokamilika jumla ya wakazi 18,460 wa vijiji saba (7) vilivyokusudiwa vya Bungu, Bungu Msiga, Kwamshai, Ngulu, Mlungui, Msasa na Manka watanufaika na huduma ya maji safi na salama.

Mradi wa Ntomoko katika Halmashauri za Kondoa na Chemba

116.      Mheshimiwa Spika, kati ya vijiji 18 vinavyohudumiwa na mradi wa maji wa Ntomoko, ujenzi wa miundombinu katika vijiji vinne (4) vya Jenjeluse, Goima, Mtakuja na Mlongia upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambazo ni asilimia 88 kwa kijiji cha Jenjeluse, Goima asilimia 62, Mtakuja asilimia 8 na Mlongia asilimia 20. Wakandarasi kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya maji katika vijiji 10 vya Makirinya, Kirere cha Ng’ombe, Lusangi, Hamai, Songolo, Madaha, Churuku, Kimkima, Jinjo na Jangalo wamepatikana na utafiti kwa ajili ya kuchimba visima katika vijiji vya Igunga, Itolwa, Mapango na Chandama umekamilika. Halmashauri husika zimekubaliana kuwa mikataba iliyoingiwa na Wilaya mama ya Kondoa ihamishiwe Halmashauri ya Wilaya ya Chemba ili kuongeza ufanisi wa usimamizi.

Mradi wa Chiwambo

117.      Mheshimiwa Spika, huduma ya maji katika mradi wa Chiwambo, Wilaya ya Masasi imekuwa duni kutokana na kuchakaa kwa miundombinu. Katika kuboresha huduma ya maji kwenye maeneo hayo, Wizara inakarabati miundombinu ya maji ikihusisha ulazaji wa bomba kuu la kilomita 11 kutoka kwenye chanzo cha maji cha chemchemi ya Lulindi hadi kwenye matanki ya kijiji cha Nagaga, kukarabati bomba lenye kipenyo cha milimita 110 kutoka Nagaga hadi Chiungutwa umbali wa kilomita 16 na kukarabati bomba lenye kipenyo cha milimita 110 kutoka Nagaga hadi Mitesa umbali wa kilomita 10. Vilevile, ukarabati na upanuzi wa mradi huo unahusisha ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 50, ujenzi wa matanki 10 ya kuhifadhi maji na vituo 78 vya kuchotea maji. Kukamilika kwa mradi huu kutanufaisha wakazi wapato 32,570 wanaoishi katika kata saba za Lulindi, Mbuyuni, Namalenga, Nachungutwa, Sindano, Mchauru na Lupumbulu.

118.      Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Machi 2014, kazi ya kulaza bomba kuu la kilomita 11 kutoka kwenye chanzo cha maji hadi kwenye matanki ya Nagaga umefikia kilomita 9.7. Aidha, bomba la milimita 200 limelazwa umbali wa kilomita mbili kutoka kwenye chanzo hadi matanki ya Nagaga ili kuongeza wingi wa maji katika eneo la mradi. Bomba la milimita 110 la urefu wa kilomita mbili limelazwa kutoka Nagaga kwenda Chiungutwa na kutoka Nagaga kwenda Mitesa limelazwa kwa umbali wa kilomita 1.5. Ujenzi wa matanki mawili kwenye eneo la mradi umeanza na ukarabati wa matanki manne unaendelea. Vituo 11 vya kuchotea maji vimejengwa. Mikataba kwa ajili ya kazi za ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji kwenye vijiji vyote vya mradi huo imesainiwa.




(v)  Usambazaji wa Maji kutoka kwenye Mabwawa na Miradi ya Matokeo ya Haraka

119.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, jumla ya shilingi bilioni 45.74 zitatumika kwa ajili ya kuendelea kutekeleza miradi inayotarajiwa kuleta matokeo ya haraka. Miradi hiyo itahusisha ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji kutoka kwenye mabwawa, visima virefu na vyanzo vingine vinavyoweza kusambaza maji kwenye vijiji zaidi ya kimoja. Katika miradi hiyo, jumla ya vituo 4,808 vya kuchotea maji vitajengwa kwa ajili ya kuhudumia wananchi 1,253,101.

120.      Mheshimiwa Spika, kati ya shilingi bilioni 45.74 kiasi cha shilingi bilioni 10.18 zitatumika upande wa usambazaji maji kutoka kwenye mabwawa kwenye vijiji 30 vitakavyokuwa na vituo vya kuchotea maji 993 vyenye uwezo wa kuhudumia watu 257,166. Mradi utatumia vyanzo vya maji kutoka mabwawa 10 ya Mti Mmoja (Monduli), Looderkes (Simanjiro), Salama Kati (Bunda), Nyambori (Rorya), Kawa (Nkasi), Mihama (Nzega), Ulyanyama (Sikonge), Kwa Maligwa (Kilindi), Masuguru (Bagamoyo) na Nkoma (Itilima). Aidha, shilingi bilioni 35.56 zilizobaki zitatumika kutekeleza miradi yenye kuleta matokeo ya haraka iliyoainishwa kwa kutumia vyanzo vingine vya maji ikiwa ni visima virefu na vyanzo vya juu ya ardhi. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kushirikiana na OWM-TAMISEMI katika kujenga uwezo wa Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa ili kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo. (Majedwali Na. 10.1 na 10.2) yanaonesha mchanganuo wa fedha zilizopangwa kutumwa kwenye Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa kwa mwaka 2014/2015.



(vi)         Ukarabati na Upanuzi wa Miradi ya Kitaifa

121.      Mheshimiwa Spika, Mpango wa BRN umeainisha miradi mitatu ya kitaifa itakayokarabatiwa na kupanuliwa mifumo ya usambazaji kwa kipindi cha miaka mitatu. Miradi itakayohusika ni:-

      i.         Mradi wa kitaifa wa Makonde ambao utahusisha vijiji vya Wilaya za Newala, Tandahimba na Mtwara Vijijini;

     ii.         Mradi wa maji wa Wanging’ombe utakaohusisha uunganishaji wa vijiji vilivyo kandokando ya bomba kuu hadi Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya; na

   iii.         Handeni Trunk Main (HTM) utakaohusisha Wilaya za Handeni, Korogwe na Kilindi.

Katika mwaka 2014/2015 Serikali itatumia kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa miradi hiyo. Kati ya fedha hizo, mradi wa maji wa Makonde umepangiwa shilingi milioni 800, Wanging’ombe shilingi milioni 300 na HTM shilingi milioni 500.

122.      Mheshimiwa Spika, ili miradi ya maji iwe endelevu na kutoa huduma iliyokusudiwa, Serikali imeweka taratibu zitakazohakikisha kuwa miradi hiyo inakuwa endelevu ikiwa ni pamoja na kuunda wa Vyombo vya Watumiaji Maji (COWSOs), kuongeza idadi ya wataalam kwenye miradi, na kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa skimu za miradi ya maji.

3.2.4 Ujenzi wa Miradi Mingine ya Maji Vijijini

123.      Mheshimiwa Spika, Serikali inashirikiana na mashirika na taasisi zisizo za kiserikali kujenga miradi ya maji katika juhudi za kuboresha na kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji vijijini.

(i)    Uvunaji wa Maji ya Mvua

124.      Mheshimiwa Spika, uvunaji wa maji ya mvua ni muhimu sana kwa nchi yetu kutokana na hali duni ya upatikanaji wa maji hasa maeneo kame ya vijijini. Halmashauri zinatekeleza agizo la Serikali la kuandaa mpango wa miaka mitano na kutunga sheria ndogo zinazohakikisha kuwa michoro ya nyumba zote zinazojengwa zinajumuisha mifumo ya miundombinu ya kuvuna maji ya mvua kabla ya kuidhinishwa ujenzi wake. Hadi mwezi Machi, 2014 Serikali kupitia Halmashauri imejenga jumla ya matanki 675 ya uvunaji wa maji kwenye maeneo mbalimbali zikiwemo taasisi kama shule, zahanati na taasisi nyingine.

(ii)  Ujenzi wa Mabwawa

125.      Mheshimiwa Spika, yapo maeneo hapa nchini yenye ukame na kutokuwa na vyanzo vya maji vya uhakika juu ya ardhi na visima vingi vilivyochimbwa kukosa maji. Aidha, maeneo mengine yana vyanzo vyenye uwezo mdogo sana wa kutoa maji. Hali hiyo imeilazimu Wizara kujenga na kukarabati mabwawa kwenye maeneo hayo ili kuwapatia wananchi huduma endelevu ya maji. Ujenzi huu unahusu mabwawa ya:-

(a)      Bwawa la Sasajila

126.      Mheshimiwa Spika, ujenzi wa bwawa la Sasajila lililopo wilayani Chamwino, mkoa wa Dodoma ulisimama kutokana na Mkandarasi wa awali kuondoka eneo la mradi kinyume na Mkataba. Kwa sababu hiyo, Wizara imeajiri Mkandarasi mwingine ambaye ameanza kazi mwezi Novemba, 2013. Hadi mwezi Machi, 2014 ujenzi wa bwawa umefikia asilimia 62.5. Katika mwaka 2014/2015, kazi za ujenzi zilizobaki zitakamilishwa.

(b)      Bwawa la Iguluba

127.      Mheshimiwa Spika, ujenzi wa bwawa la Iguluba, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, ulikamilika kulingana na kazi zilizoainishwa kwenye Mkataba. Hata hivyo, ukaguzi uliofanyika ulibaini ongezeko la kazi ambazo hazikuwemo kwenye mkataba huo. Kazi ambazo hazijakamilika ni kujenga crest weir, miundombinu ya mawe kuzuia mmomonyoko wa udongo; kupanda nyasi upande wa nje wa tuta na kupanga mawe upande wa ndani wa tuta, ujenzi wa miundombinu ya kutolea maji kwenye bwawa na ujenzi wa sand traps   3 za kupokea mchanga na kuondoa mchanga ndani ya Bwawa. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itakamilisha kazi za ziada zilizojitokeza.

(c)      Mabwawa ya Habiya, Seke Ididi na Matwiga

128.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza kutekeleza ujenzi wa mabwawa ya Habiya (Itilima, Simiyu), Seke Ididi (Kishapu, Shinyanga) na Matwiga (Chunya, Mbeya) ambayo ujenzi wake ulisimama baada ya Wakandarasi husika kushindwa kazi na kuondoka kwenye maeneo ya miradi. Hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kusitisha mikataba ya Wakandarasi hao baada ya kwenda kinyume na mikataba. Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) ameteuliwa kukamilisha ujenzi wa mabwawa hayo. Mikataba ya kukamilisha ujenzi wa mabwawa hayo imesainiwa tarehe 28.2.2014 na ujenzi utaanza mwezi Juni, 2014 baada ya msimu wa mvua.


(d)      Bwawa la Kawa

129.      Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Bwawa la Kawa (Nkasi, Rukwa) umefikia asilimia 95. Mkandarasi aliyekuwa akiendelea na ujenzi wa bwawa hilo aliondoka eneo la mradi. Aidha, Wizara imeajiri Mkandarasi mwingine kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji kutoka katika bwawa kupeleka maji katika vijiji vya Nkundi, Kalundi na Fyengerezya. Ujenzi wa mradi huo umesimama kwa muda ili kupisha usanifu wa kituo cha kutibu maji. Hadi mwezi Machi, 2014 ujenzi wa miundombinu hiyo ulikuwa umefikia asilimia 20. Vilevile, Wizara inajadiliana na Mkandarasi huyo ili akamilishe kazi ya ujenzi wa bwawa zilizoachwa na Mkandarasi wa awali. Mradi huo ukikamilika jumla ya wananchi 13,500 watanufaika na huduma ya maji.

(e)      Bwawa la Wegero

130.      Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Bwawa la Wegero (Butiama, Mara) ulikamilika mwaka 2010 kwa mujibu wa mkataba wa awali. Hata hivyo kuongezeka kwa shughuli za kijamii hasa kilimo katika eneo linalozunguka bwawa kumesababisha bwawa hilo kujaa tope katika muda mfupi na kushindwa kutumika ipasavyo. Wizara ilifanya upimaji mwezi Novemba, 2013, na kuonekana kuwa bwawa linaweza kufanyiwa ukarabati ili kuongeza wingi wa maji kwa mita za ujazo 32,000. Kazi hiyo zitafanyika katika mwaka wa fedha 2014/2015.

(f)        Bwawa la Mwanjoro

131.      Mheshimiwa Spika, ujenzi wa bwawa la Mwanjoro (Meatu, Simiyu) umekamilika kwa asilimia 78. Ujenzi huo kwa sasa umesimama baada ya Mkandarasi kuondoka eneo la kazi kinyume na Mkataba. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaajiri Mkandarasi mwingine ili kukamilisha kazi zilizobaki.

(g)      Bwawa la Kidete

132.      Mheshimiwa Spika, Bwawa la Kidete (Kilosa, Morogoro) lilijengwa kabla ya Uhuru kwa lengo la kuthibiti mafuriko kwenye eneo la Reli ya Kati. Bwawa hilo lilibomoka kutokana na mafuriko ya mwaka 2003, hivyo kuilazimu Serikali kulijenga upya. Gharama ya ujenzi ilikadiriwa kuwa shilingi bilioni 4.48. Ujenzi umesimama kutokana na matatizo ya kimkataba ambayo yanashughulikiwa ili ujenzi uweze kukamilishwa katika mwaka 2014/2015.

3.2.5     Uendeshaji na Matengenezo


133.      Mheshimiwa Spika, ili kupata takwimu sahihi zinazohusiana na huduma ya maji vijijini, Wizara yangu imetekeleza mradi wa kuainisha vituo vya kuchotea maji vijijini unaotumia mfumo wa kompyuta. Kuainishwa kwa vituo hivyo kumewezesha kufahamika kwa usahihi zaidi takwimu za uendeshaji wa miundombinu na kuandaa ramani za vituo vya maji (water point mapping). Takwimu zilizopatikana zinawezesha Halmashauri kufahamu hali ya upatikanaji wa maji katika vijiji.

134.      Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Machi, 2014 takwimu za vituo 88,913 vya kuchotea maji katika Halmashauri 168 zimekusanywa. Aidha, Wizara imetoa mafunzo maalum ya utumiaji wa vifaa kwa ajili ya kutoa na kuboresha taarifa (data up-dating) ya vituo vya kuchotea maji kwa wahandisi wote wa Sekretarieti za mikoa; na wahandisi wa maji wa Wilaya, mafundi sanifu na wasajili wa vyombo vya watumia maji wa Halmashauri zote nchini. Mafunzo hayo yalitolewa kwenye vituo vinne (4) vya Moshi, Mbeya, Mwanza na Morogoro na kukamilika mwezi Aprili 2014. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri zote za Wilaya itaendelea kuboresha mfumo wa ukusanyaji takwimu kwa kutoa mafunzo, kununua vifaa na matumizi ya teknolojia mpya kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati.

(ii)  Uundaji na Usajili wa Vyombo vya Watumiaji Maji

135.      Mheshimiwa Spika, kulingana na Kifungu Na. 31 cha Sheria Na. 12 ya mwaka 2009 ya Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, Halmashauri zinaelekezwa kusajili vyombo vya watumiaji maji (COWSOs) ili kuhakikisha kuwa uendeshaji na usimamizi wa miradi ya maji unafanyika kwa mujibu wa sheria. Wizara yangu, imetoa miongozo ya usajili ikiwemo uteuzi wa Wasajili katika Halmashauri na namna vyombo vitakavyoendeshwa. Kupitia sheria na miongozo hiyo, wananchi wanawajibika kuunda vyombo hivyo na kuvisajili rasmi.

136.      Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Machi, 2014, idadi ya vyombo vya watumiaji maji vilivyosajiliwa kisheria imefikia 373 kutoka vyombo 147 ya mwaka uliopita. Aidha, Wizara yangu imetoa mafunzo mbalimbali kwa Halmashauri kwa ajili ya vyombo hivyo ikiwa ni pamoja na mafunzo ya uendeshaji, utunzaji wa fedha, matengenezo madogo madogo ya mradi na njia mbalimbali za utoaji wa taarifa za maendeleo ya mradi. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea kutoa mafunzo, kuhimiza uundwaji zaidi wa vyombo vya watumiaji maji na kusisitiza wasajili kuongeza kasi ya usajili kwa miradi iliyopo na mingine itakayojengwa. Vilevile, Halmashauri zinatakiwa ziandae mipango kazi ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kuanzisha na kusajili vyombo na kutoa taarifa ya utekelezaji wa mipango hiyo kila robo mwaka.


3.3            HUDUMA YA MAJISAFI NA USAFI WA MAZINGIRA MIJINI


137.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ilitekeleza Programu ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mijini kujenga,kukarabati na kupanua mifumo ya majisafi na majitaka pamoja na kuzijengea uwezo Mamlaka za maji mijini. Lengo la utekelezaji huo ni kuwapatia wananchi wengi zaidi huduma nzuri katika Jiji la Dar es Salaam, miji mikuu ya mikoa, miji mikuu ya wilaya, miji midogo, na miradi ya maji ya kitaifa.

3.3.1 Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mijini


(a)      Miradi ya Maji ya Kukidhi Mahitaji ya Muda wa Kati katika Miji Saba

138.      Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Serikali ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya inatekeleza miradi ya kukidhi mahitaji ya maji katika miji saba ya Bukoba, Musoma, Lindi, Kigoma, Sumbawanga, Mtwara na Babati.

139.      Mheshimiwa Spika, ujenzi wa miradi ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Manispaa za Musoma na Bukoba unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) unaendelea. Hadi mwezi Machi, 2014 utekelezaji wa miradi hiyo ambayo inagharimu kiasi cha Shilingi bilioni 68.2 umefikia asilimia 50 kwa Manispaa ya Musoma na asilimia 40 kwa Bukoba. Kazi zinazotekelezwa ni kujenga mitambo ya kusafisha na kusukuma maji pamoja na kulaza mabomba ya usambazaji wa maji katika miji hiyo. Miradi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2014.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya imeanza utekelezaji wa miradi katika Miji ya Lindi, Kigoma na Sumbawanga yenye gharama ya Euro milioni 62.59. Wakandarasi wanaendelea na ujenzi wa miradi hiyo na wanatazamiwa kukamilisha kazi mwezi Aprili, 2015. Utekelezaji wa miradi hiyo unahusu uchimbaji wa visima, ujenzi wa mabanio, ujenzi wa matanki, ulazaji wa bomba kuu na mabomba ya usambazaji, ujenzi wa chujio na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji.

140.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali ya Ujerumani kupitia KfW ilitenga Euro milioni 8.72 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa majisafi na usafi wa mazingira katika Miji ya Mtwara na Babati chini ya programu ya Millenium Development Goal Initiative (MDGI-EU). Kufuatia kumalizika kwa upembuzi yakinifu imebainika kuwa fedha hizo hazitatosha kwa ajili ya ujenzi wa miradi hiyo. Wizara yangu inakamilisha taratibu za kumtafuta Mtaalam Mshauri kwa ajili ya usimamizi wa utekelezaji wa Mradi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa miji hiyo ambaye ataainisha kazi ambazo zitafanyika kulingana na kiasi cha fedha kilichopo huku Serikali ikiendelea na kutafuta jibu la muda mrefu katika Miji hiyo.





(b)      Miradi ya Maji ya Kukidhi Mahitaji ya Muda Mrefu

(i)        Mradi wa Maji Tabora

141.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu ilitekeleza mradi wa ukarabati wa miundombinu ya maji na maboresho ya kituo cha maji cha Igombe Mjini Tabora kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 4.84. Mradi huo unatekelezwa kwa kushirikiana na Serikali ya Uswisi kupitia Shirika lake la Maendeleo (SECO). Hadi mwezi Machi, 2014, mradi umekamilika kwa asilimia 96 na unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa ifikapo mwezi Juni, 2014. Aidha, ukarabati na upanuzi wa chujio la maji katika kituo cha Igombe Mjini Tabora unaogharamiwa na Mfuko wa Pamoja wa Sekta ya Maji unaendelea kwa kufunga pampu kubwa mpya tatu na kulaza bomba kuu la urefu wa mita 240 kutoka bwawani hadi kwenye chujio. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2015. Kukamilika kwa mradi huo kutawapatia wakazi wa Manispaa ya Tabora Maji ya kutosha hadi mwaka 2032.

(ii)       Mradi wa Maji Mjini Dodoma

142.      Mheshimiwa Spika, katika kuboresha kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Wizara yangu inatekeleza mradi wa ujenzi wa kuongeza majisafi. Mradi huo unahusisha ujenzi wa kituo cha kusukuma majisafi kwenda Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na ujenzi wa matanki matatu (3) ya ujazo wa lita milioni 12. Aidha, mradi wa ujenzi wa mfumo wa uondoaji majitaka unaogharimu shilingi bilioni 27.7 unaendelea. Mradi huo unajumuisha ujenzi wa mtandao wa kukusanya majitaka wenye urefu wa kilomita 32 na ujenzi wa mabwawa ya kutibu majitaka.  Hadi mwezi Machi, 2014 utekelezaji wa kazi za mradi wote umefikia asilimia 54, na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2014. Kukamilika kwa mradi huo kutaondoa kero ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na kufurika kwa majitaka katika maeneo mbalimbali ya chuo.

143.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaendelea na juhudi za kuwapatia wananchi wa Manispaa ya Dodoma majisafi na salama kwa kuendeleza Mradi ulioanza mwezi Desemba 2012, unaotekelezwa kwa kushirikiana na Serikali ya Korea Kusini kwa gharama ya shilingi bilioni 49.62. Hadi mwezi Machi 2014, visima 15 vimekarabatiwa kati ya visima 21 vilivyopangwa na visima vipya viwili (2) vimechimbwa kati ya visima vitatu (3). Kwa ujumla utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 35. Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Januari, 2015 na utaongeza kiwango cha utoaji huduma kutoka asilimia 87 hadi kufikia asilimia 90.

144.      Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na mahitaji makubwa ya maji yanayotokana na ongezeko la watu pamoja na shughuli za kiuchumi na kijamii katika Manispaa ya Dodoma, Serikali imeajiri Mtaalam Mshauri kwa ajili ya kusanifu Bwawa la Farkwa na tayari amewasilisha taarifa ya awali ya usanifu (interim report I) imewasilishwa na anaendelea na usanifu. Pia, bwawa hilo litakuwa chanzo cha maji kwa  Miji ya Kondoa, Chamwino, Chemba na Bahi ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya maji katika miji hiyo. Gharama za usanifu wa bwawa hilo ni shilingi bilioni 1.6. Usanifu huo unaotarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2014 utaonesha gharama halisi za ujenzi wa bwawa hilo pamoja na kiwango cha maji kitakachopatikana.




(iii)     Mradi wa Maji Jijini Arusha

145.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali imeanza kutekeleza mradi wa kuboresha huduma ya majisafi katika Jiji la Arusha. Utekelezaji huo unahusu uchimbaji wa kisima kirefu na ujenzi wa tanki la maji katika maeneo ya kata ya Moshono. Hadi mwezi Machi 2014, uchimbaji wa kisima umefikia asilimia 75 na kinatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2014. Ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita milioni 2.5 umeanza na unatarajiwa kujengwa na kukamilika mwezi Desemba, 2014. Mradi huo utakapokamilika utahudumia wakazi wapatao 28,124 wa Kata za Moshono na Engutoto.

(iv)     Mradi wa Maji Mjini Singida

146.      Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kiarabu (BADEA) pamoja na Mfuko wa Maendeleo wa Nchi zinazozalisha Mafuta (OPEC Fund for International Development-OFID) ilikamilisha ujenzi wa mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya majisafi Mjini Singida. Ujenzi huo ulihusu uchimbaji wa visima virefu 10, kati ya hivyo visima saba (7) vilikamilika na tayari vinatumika katika maeneo ya Mwankoko viwili (2) na Irao vitano (5). Visima vitatu (3) kati ya 10 havikuwa na maji ya kutosha. Aidha, kazi za ujenzi wa matanki mawili (2) katika maeneo ya Airport; kulaza bomba kuu la maji hadi kwenye matanki; na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji katika eneo la Mandewa zilikamilika. Mradi huo uligharimu shilingi bilioni 32.53. Kukamilika kwa mradi huo kumeongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 8 kwa siku kwa sasa hadi kufikia lita milioni 17.76 na utakidhi asilimia 100 ya mahitaji ya wakazi wa Mji wa Singida.


(v)      Mradi wa Maji Morogoro Mjini

147.      Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi wa kupanua na kuboresha upatikanaji wa majisafi katika Manispaa ya Morogoro unaendelea. Hadi mwezi Machi 2014, kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kukarabati matanki matatu (3), ulazaji wa bomba kuu la maji la urefu wa kilomita 1.8, kupanua chujio la maji la Mafiga na kujenga mtambo wa kusafisha maji wa Mambogo. Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 92 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2014. Mradi huo unatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la MCC la Marekani na utagharimu shilingi bilioni 10. Kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 23 kwa siku za sasa hadi lita milioni 33.

(vi)     Mradi wa Maji Songea Mjini

148.      Mheshimiwa Spika, kazi ya ukarabati wa chanzo cha Mto Ruhira, Mjini Songea imeanza mwezi Aprili, 2014. Kazi hiyo ni kujenga banio la maji (weir) ili kukabiliana na upungufu wa maji wakati wa kiangazi. Gharama ya kukamilisha mradi ni Shilingi bilioni 2.6. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea na utekelezaji wa mradi huo ambao utakapokamilika unatarajiwa kuongeza uhifadhi wa maji kutoka lita milioni 3.4 za sasa hadi kufikia lita milioni 6.5 wakati wa kiangazi.

(vii)   Mradi wa Kutoa Maji Mto Ruvuma Kupeleka Mtwara-Mikindani

149.      Mheshimiwa Spika, Kutokana na ongezeko la shughuli za kiuchumi katika Manispaa ya Mtwara, Serikali inaendelea kutafuta vyanzo vingine vitakavyohudumia Manispaa hiyo. Katika mwaka 2013/2014 Serikali illingia mkataba na Mhandisi Mshauri kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi mpya wa kutoa maji mto Ruvuma kwenda Manispaa ya Mtwara na vijiji vitakavyopitiwa na bomba kuu. Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2014 na ujenzi utaanza mwaka wa fedha 2014/2015 ambapo Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huu.

(viii)  Mradi wa Maji katika Miji ya Geita, Sengerema na Nansio

150.      Mheshimiwa Spika, awamu ya pili ya Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Ziwa Victoria (LVWATSAN II) unatekelezwa katika miji 15 iliyoko kwenye nchi tano (5) za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Kwa upande wa nchi yetu mradi unatekelezwa katika Miji ya Geita, Sengerema na Nansio kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 30.4 na unasimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA).

151.      Mheshimiwa Spika, kazi zinazoendelea kutekelezwa ni za vipindi vya muda mfupi na muda mrefu ambazo ni kujenga na kuboresha miundombinu ya majisafi, mifumo ya utoaji wa huduma ya usafi wa mazingira, mitaro ya maji ya mvua na kuzijengea uwezo Mamlaka za maji za Miji ya Geita, Sengerema na Nansio. Mtaalam Mshauri wa kusanifu na kusimamia kazi za ujenzi wa mradi huo amewasilisha taarifa ya usanifu wa mradi.

152.      Mheshimiwa Spika, kazi ambazo tayari zimetekelezwa chini ya mpango wa muda mfupi ni ununuzi wa magari matano (5) na kugawiwa kwa mamlaka za maji za Geita (1), Sengerema (1), Nansio (1) na kwa MWAUWASA (2); ununuzi wa pikipiki nane (8) kwa Geita (3), Sengerema (3) na Nansio (2); ununuzi wa trekta na tela zake tisa (9) kwa Geita (3), Sengerema (3) na Nansio (3); Ununuzi wa magari makubwa ya majitaka matano (5) kwa Geita (2), Sengerema (2) na Nansio (1); na ununuzi wa magari madogo ya majitaka matatu (3) kwa Geita (1), Sengerema (1) na Nansio (1). Aidha, mamlaka hizo zimegawiwa vifaa vya kukusanyia taka ngumu vikiwemo kontena na toroli, Geita (40), Sengerema (37) na Nansio (27). Mkandarasi wa ujenzi wa miundombinu ya maji amepatikana na Mikataba ya ujenzi wa miradi hiyo itasainiwa kabla ya mwezi Agosti, 2014 na ujenzi utakamilika mwezi Desemba, 2015.

(ix)     Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria Unaotekelezwa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) kwa Kushirikiana na Serikali

153.      Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Geita kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (Geita Gold Mining Limited – GGML) wamekamilisha kazi ya ujenzi wa chanzo, chujio la maji, kulaza bomba kuu na tanki moja lenye ujazo wa lita milioni 1.2 kwa gharama za Dola za Marekani milioni 5.4, fedha ambazo zimetolewa na GGML. Katika mwaka 2014/2015, kazi ya ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji itatekelezwa na mradi utagharimu kiasi cha Dola za Marekani milioni 1.4 kati ya hizo mchango wa Serikali ni Dola za Marekani 400,000 na GGML ni Dola za Marekani milioni 1. Maandalizi ya Hati ya Makubaliano (Limited Distribution Network Agreement) kati ya Wizara yangu, GGML, Halmashauri ya Geita na Mamlaka ya Majisafi Geita yapo kwenye hatua za mwisho na inatarajiwa kusainiwa baada ya ridhaa ya Mwanasheria Mkuu. Mradi huo utakapokamilika utazalisha lita milioni 4.8 za maji kwa siku na kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 3.5 hadi asilimia 40. Aidha mwaka wa fedha 2014/2015 Serikali imetenga Shilingi billioni 2.5 kwa ajili ya kupanua mtandao wa usambazaji maji katika mji wa Geita.
154.      Mheshimiwa Spika, mradi wa maji ya mtiririko wa Ihako unaofadhiliwa na UN HABITAT kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliibuliwa kutokana na uhaba wa maji uliokuwepo katika miji ya Muleba na Mutukula. Kwa upande wa Muleba, mradi umelengwa kutekelezwa katika awamu mbili. Awamu ya Kwanza ulihusisha ujenzi wa chanzo cha Ihako chenye uwezo wa kuzalisha maji lita 544,000 kwa siku; tanki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 680,000; ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa kilomita 10.1; na ujenzi wa vituo 19 vya kuchotea maji. Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo umekamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 1.39.

155.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015. Wizara yangu itakamilisha utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huu kwa kulaza mabomba ya usambazaji maji yenye urefu wa kilomita 21.5; uchimbaji wa kisima kirefu na kufunga pampu. Mradi huo ukikamilika utahudumia zaidi ya wakazi 29,000 ambapo kwa sasa mradi unahudumia wakazi wapatao 11,563 na kati ya hao wakazi 10,063 ni wa mji wa Muleba na 1,500 ni wa vijiji vya Bwata, Kamishango, Kabare na Katanga.

156.      Mheshimiwa Spika, katika mji wa Mtukula, kazi zilizokamilika ni ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa kilomita 2.1, kulaza mabomba ya kusambaza maji lenye urefu wa kilomita 5.3, uchimbaji wa visima viwili (2), ujenzi wa vituo 16 vya kuchotea maji na ujenzi wa tanki  la ujazo wa lita 120,000. Gharama za mradi ni shilingi milioni 653.29. Kazi zilizobaki ni kupeleka umeme kwenye visima viwili (2) na ufungaji wa pampu. Mradi huo utakapokamilika utahudumiwa wakazi wapatao 5,000 wa mji wa Mtukula.


(x)      Miradi Mipya katika Eneo la Ziwa Victoria

157.      Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank-EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (French Development Agency-AFD) itatekeleza mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji pamoja na usafi wa mazingira katika Jiji la Mwanza, pamoja na Miji ya Musoma, Bukoba, Magu, Misungwi na Lamadi. Katika utekelezaji wa mradi huo, jumla ya Euro milioni 104.5 zitatumika ambapo Serikali itatoa Euro milioni 14.5, EIB na AFD kwa pamoja watatoa jumla ya Euro milioni 90. Mikataba ya kifedha ilisainiwa tarehe 23/12/2013 na tarehe 5/03/2014 hivyo fedha ziko tayari. Hatua za manunuzi zimeanza na Mtaalam Mshauri anatarajiwa kupatikana mwezi Juni, 2014.

158.      Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa mradi huo kutaongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 35 hadi asilimia 90 kwa Mji wa Magu; asilimia 5 hadi asilimia 90 kwa Mji wa Lamadi; na asilimia 45 hadi asilimia 90 kwa Mji wa Misungwi. Aidha, katika Jiji la Mwanza mradi unategemewa kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi katika maeneo ya miinuko sambamba na kuboresha usafi wa mazingira kwenye maeneo hayo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyoo katika shule za msingi na maeneo ya vituo vya mabasi.

159.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 Wizara yangu iliendelea kutekeleza miradi ya majitaka kwa Miji ya Bukoba na Musoma. Usanifu na uandaaji wa makabrasha vya zabuni kwa mifumo ya majitaka unaendelea na mkataba wa kupata fedha (loan agreement) za kutekeleza miradi hiyo kati ya Serikali na AFD utasainiwa mwezi Mei, 2014. Ujenzi wa miradi utaanza baada ya kukamilika kwa taratibu za zabuni na kumpata Mkandarasi. Miradi ikikamilika itahudumia asilimia 15 ya wakazi wa Bukoba na asilimia 20 ya wakazi Mji wa Musoma.

(xi)     Miradi ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Miji Inayozunguka Ziwa Tanganyika

160.      Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira kwa eneo la Ziwa Tanganyika (LT-WATSAN) unatekelezwa katika nchi za Zambia, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Tanzania, na kusimamiwa na Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT). Kwa upande wa Tanzania, mradi unatekelezwa katika miji ya Kigoma, Kasulu, Mpanda, Namanyere, Uvinza na Kasanga. Mradi huo ulifanyiwa upembuzi yanikifu mwaka 2011, hata hivyo, utekelezaji wake haukuanza kutokana na kutopatikana kwa fedha. Kwa sasa gharama za utekelezaji zimeongezeka ikilinganishwa na makadirio ya awali, hivyo, nchi wanachama walielekezwa wapitie upya gharama za ujenzi ili kupata gharama halisi za sasa. Baada ya mapitio, gharama hizo kwa Tanzania zimekadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 39.18, ambazo zimepangwa kama ifuatavyo:- Mji wa Kigoma ni Dola za Marekani milioni 19.10; Kasulu Dola za Marekani milioni 5.39; Mpanda Dola za Marekani milioni 4.33; Namanyere Dola za Marekani milioni 3.79; Uvinza milioni 3.01 na Kasanga milioni 3.56. Kazi zinazotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na usambazaji wa majisafi na usafi wa mazingira, ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua na uondoaji wa taka ngumu pamoja na kuzijengea uwezo taasisi husika. Wafadhili wa mradi huo wanatarajiwa kupatikana baada ya majadiliano yetu katika Kikao cha Mawaziri wa Maji wa nchi zetu  kilichofanyika Mjini Bujumbura, mwezi Aprili, 2014


3.3.2 Uboreshaji wa Huduma ya Maji katika Miji Mikuu ya Mikoa Mipya


161.      Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha  huduma ya majisafi katika miji mikuu ya mikoa mipya ya Mpanda, Njombe na Bariadi. Miradi inayoendelea kutekelezwa katika miji hiyo ni:-

(i)             Mji wa Mpanda

162.      Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kutumia shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji kwa kujenga miradi mbalimbali katika Mji wa Mpanda. Katika mwaka 2013/2014 Serikali imetuma kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika mji huo. Kazi zinazoendelea kutekelezwa ni pamoja na kulaza bomba kutoka maeneo ya Ikolongo hadi Kazima urefu wa kilomita 13.6; ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita milioni moja; nyumba mbili za watumishi Ikolongo na Kazima na kufungwa solar panel; ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji urefu wa kilomita 48 yenye kipenyo cha milimita 110 maeneo ya Kawajense, Kazima, Nsemulwa, Ilembo na Makanyagio; na ununuzi wa dira za maji 4,000 na viungio vyake.

163.      Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Machi 2014, utekelezaji wa kazi hizo, ni kama ifuatavyo:-

           i.    Mtaro wa urefu wa kilomita 12.4 umechimbwa kati ya kilomita 13.6 na kulaza bomba urefu wa kilomita 1.3. Kazi hizo zinatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2014;

          ii.    Ujenzi wa nyumba mbili na tanki la maji lenye ujazo lita milioni moja umeanza na kazi hii itakamilika mwezi Agosti, 2014; na

        iii.    Ununuzi wa viungio kwa ajili ya ufungaji wa dira za maji umekamilika. Aidha, ununuzi wa vifaa vyote vya mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2014.

Mradi utakapokamilika utaongeza kiasi cha lita milioni tano za maji kwa siku. Vilevile, idadi ya watu wapatao 50,000 watanufaika na huduma hiyo ambapo upatikanaji wa maji utaongezeka kutoka asilimia 38.8 ya sasa hadi kufikia asilimia 72. Katika mwaka 2014/2015, Serikali imetenga shillingi billioni 3 kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa mradi kutoka chanzo cha maji cha mtiririko Ikolongo II awamu ya pili utakaoongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 72 hadi asilimia 82.

(ii)           Mji wa Njombe

164.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 Serikali imetuma kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji katika Mji wa Njombe. Kazi zinazoendelea kufanyika ni ujenzi wa intake ya maji na kulaza bomba kuu la maji kwa gharama ya shilingi bilioni 1.75 na ujenzi wa matanki matatu ya lita 135,000 kila moja kwa gharama ya shilingi milioni 321. Kazi zote zinatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2014. Mradi huo ukikamilika, kiasi cha maji kitaongezeka kutoka lita milioni 3.66 hadi lita milioni 5.77 kwa siku. Wananchi watakaonufaika na mradi wataongezeka kutoka 20,734 hadi 32,734. Na mradi utakidhi mahitaji ya maji toka asilimia 41 za sasa na kufikia asilimia 58.  Katika mwaka 2014/2015 mradi huu utapanuliwa ili ufikie asilimia 79 ya mahitaji ya Mji wa Njombe.  Kiasi cha shilingi bilioni 3.5 kimetengwa kwa kazi hiyo.


(iii)          Mji wa Bariadi

165.      Mheshimiwa Spika, kazi zilizopangwa kutekelezwa katika Mji wa Bariadi ni kuchimba visima sita na kufunga pampu; kujenga tanki la maji lenye ujazo wa lita 45,000; kupanua mtandao wa maji; kukarabati tanki la Somanda; kuunganisha umeme kwa ajili ya visima vya Somanda, Sanungu, Isanzu na Kidinda; na kujenga ofisi ya mamlaka ya maji. Mradi huo utagharimu shilingi bilioni 2. Hadi mwezi Machi 2014, mtaro wenye urefu wa kilomita 6.8 kati ya kilomita 7.6 umechimbwa na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 2.1 umekamilika kati ya kilomita 7.6 zilizopangwa. Nguzo za umeme tayari zimefika katika eneo la ujenzi. Katika mwaka 2013/2014, Wizara imetuma shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hizo. Mradi ukikamilika, kiasi cha maji kitaongezeka kutoka lita 861,000 hadi lita 1,560,000 kwa siku na huduma ya upatikanaji maji itaimarika kutoka asilimia 17 hadi asilimia 30. Katika mwaka 2014/15 Serikali imetenga shilingi bilioni 3.5  ili kuendelea na ujenzi na upanuzi wa mradi wa maji wa Mji wa Bariadi kutoka asilimia 30 kufikia asilimia 75 ya mahitaji ya kila siku.

3.3.3            Usanifu wa Miradi ya Majisafi na Majitaka


166.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea na usanifu wa kina na kuandaa vitabu vya zabuni kwa miradi ya maji katika miji midogo na miji mikuu ya Wilaya za Biharamulo, Muleba, Ngara, Karagwe, Chato na Bunazi (Kagera). Mtaalam Mshauri ameajiriwa tarehe 27/12/2013 na anaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu. Taratibu za kuwapata Wataalam Washauri katika mji wa Kakonko (Kigoma) na Miji ya Namanyere, Chala na Laela (Rukwa) zinaendelea. Kwa upande wa Miji ya Manyoni na Kiomboi (Singida), Mtaalam Mshauri ameanza kazi tarehe 21/08/2013 na anatarajiwa kukamilisha mwezi Juni, 2014. Usanifu unaendelea kwa miradi ya maji ya Miji ya Mombo, Songe, Lushoto, Kasela, Korogwe na Handeni Trunk Main - HTM katika Mkoa wa Tanga; na mradi wa kutoa maji Mto Ugala hadi Miji ya Urambo na Kaliua. Katika Mkoa wa Tabora. Katika mwaka 2014/2015, Serikali itaendelea na utekelezaji wa miradi hiyo.

3.3.4            Miradi ya Maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka katika Miji Mbalimbali


167.      Mheshimiwa Spika, maandalizi ya ujenzi wa miradi ya maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka katika miji mbalimbali yanaendelea. Mradi wa kupeleka maji katika Miji ya Bariadi, Mwanhuzi, Lagangabilili na Maswa utakapokamilika utanufaisha vijiji 40 vilivyo umbali wa kilomita 12 kandokando ya bomba kuu kutoka kwenye Ziwa Victoria. Katika mwaka 2014/2015, kiasi cha shilingi bilioni 3.5 zimepangwa kwa ajili ya mradi huo, na upembuzi yakinifu utaanza mwezi Mei, 2014. Kwa upande wa Miji ya Magu kwenda Kwimba, mradi utakapokamilika utahudumia vijiji na miji ya njiani litakapopita bomba kuu ikiwemo miji midogo ya Sumve na Malya na kiasi cha shilingi bilioni 4 zimepangwa kutumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. Vilevile, Miji ya Kagongwa, Isaka hadi Tinde itapata huduma ya maji kutoka bomba kuu la Kahama-Shinyanga kutoka Ziwa Victoria. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu imepanga kutumia kiasi cha shilingi bilioni 8 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

166.      Mheshimiwa Spika, mradi wa upanuzi wa mtandao wa bomba kuu la maji la Mamlaka ya Maji ya KASHWASA kutoka tanki la maji lililopo katika kijiji cha Mhalo kwenda katika Mji wa Ngudu unatekelezwa na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2014. Mradi huu unasimamiwa na Mamlaka ya KASHWASA.  Kazi zilizokamilika hadi sasa ni uchimbaji wa mtaro na kulaza bomba kutoka kijiji cha Runere hadi Mjini Ngudu umbali wa kilomita 24.6; na ukarabati wa tanki la maji lililopo Ngudu;  na chemba 13 kati ya 75 zimejengwa. Mradi upo katika hatua nzuri ya utekelezaji, ambapo majaribio ya kupeleka maji kutoka Mhalo hadi Runere yamefanyika. Maandalizi ya kazi za majaribio ya kupeleka maji kutoka Runere hadi Ngudu yanaendelea.

3.3.5            Mradi wa Maji wa Chalinze


168.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu iliendelea na utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa maji Chalinze, utakaotoa huduma ya majisafi katika vijiji 47 vya mikoa ya Pwani (42) na Morogoro (5). Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na BADEA, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na Mfuko wa Pamoja wa Sekta ya Maji, utawanufaisha wakazi 197,684 wa Wilaya tatu za Bagamoyo, Kibaha na Morogoro. Wizara yangu inaendelea kutekeleza awamu hiyo ya mradi inayotegemewa kukamilika mwezi Septemba, 2014. Jedwali Na. 11 linaonesha viwango vya utekelezaji wa sehemu mbalimbali za mradi huo.

169.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali iliingia Mkataba na Mtaalam Mshauri ili kufanya mapitio ya usanifu na kusimamia utekelezaji wa mradi wa Chalinze awamu ya tatu utakaogharimu Dola za Marekani milioni 49. Kazi hiyo ilianza mwezi Agosti, 2013 na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2014. Katika mwaka 2014/2015 Serikali itaanza ujenzi wa mradi baada ya kumpata Mkandarasi. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2016. Kazi zitakazotekelezwa ni ukarabati wa chanzo, kujenga matanki ya kuhifadhia maji katika vijiji 20, kupanua mitandao ya bomba kuu na bomba la usambazaji, kujenga tanki kubwa la kuhifadhi maji katika Mlima Mazizi na kujenga vituo vya kuchotea maji katika maeneo ambayo hayakufikiwa na ujenzi wa awamu za I na II.

3.3.6 Miradi katika Jiji la Dar es Salaam


170.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliendelea kutekeleza miradi mbalimbali iliyopangwa ili kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam. Hadi mwezi Machi, 2014 miradi inayoendelea kutekelezwa ni kama ifuatavyo:-

(a)  Ujenzi wa Bwawa la Kidunda

171.      Mheshimiwa Spika, Mtaalam Mshauri aliyepewa kazi ya kutathmini athari za kimazingira na kijamii (ESIA) zitakazotokana na ya ujenzi wa barabara kuelekea eneo la ujenzi wa bwawa la Kidunda amewasilisha rasimu ya mwisho ya kazi hiyo tarehe 24 Februari, 2014. Serikali imekamilisha taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi wa barabara kuelekea kwenye eneo la bwawa na ujenzi unatarajiwa kuanza mara baada ya kukamilika tathmini ya ESIA na ulipaji fidia kwa watakaoathirika na mradi.

172.      Mheshimiwa Spika, upande wa malipo ya fidia, Mthamini wa Serikali amekamilisha mapitio ya uthamini ili kuongeza thamani ya fidia baada ya kuchelewa malipo. Kulingana na Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999, thamani ya fidia imeongezeka kwa asilimia 8. Vitabu vipya vimetayarishwa na rasimu ziliwasilishwa tarehe 28/2/2014. Taratibu za kupata fedha za kulipia fidia hiyo ambayo ni shilingi bilioni 7.9 zinaendelea. Katika mwaka 2014/2015, Serikali imepanga kutumia kiasi cha shilingi bilioni 7.0 kwa ajili ya maandalizi na ulipaji wa fidia.  Aidha, Wizara inaendelea na juhudi za kutafuta fedha za ujenzi wa bwawa na hivi sasa yapo mashauriano kati ya Benki ya Uwekezaji ya Afrika Kusini ikishirikiana na Benki ya Rasilimali ya Tanzania, na Benki ya Dunia kwa ajili ya kupata fedha za ujenzi wa bwawa hilo.

(b)  Visima Virefu vya Kimbiji na Mpera

173.      Mheshimiwa Spika, mradi wa visima virefu vya Kimbiji na Mpera unahusisha uchimbaji wa visima 20 vya uzalishaji na visima vinane (8) vya kubaini mwenendo wa rasilimali za maji chini ya ardhi. Hadi mwezi Machi, 2014 Mtaalam Mshauri wa kusimamia kazi ya uchimbaji wa visima 20 vya Kimbiji na Mpera ametoa maoni yaliyowasilishwa na Mkandarasi kuhusu uagizaji vifaa vya kuchimbia visima pamoja na mabomba (casings and screens) yatakayotumika katika uchimbaji wa visima hivyo. Mkandarasi anaendelea kukamilisha maandalizi ya vitendea kazi na mabomba (equipment mobilization) na anategemewa kuanza kazi mwezi Juni, 2014. Uchimbaji wa visima hivyo unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2014.

174.      Mheshimiwa Spika, mkandarasi wa uchimbaji wa visima virefu vinane (8) vya uchunguzi wa mwenendo wa maji chini ya ardhi amekamilisha uchimbaji wa visima viwili (2) eneo la Mwasonga na Mkuranga. Majaribio ya uwingi (output) wa maji katika visima hivyo na matokeo ya vipimo vya ubora wa maji yameonesha dalili za kuwa na maji mengi yenye ubora unaofaa kwa matumizi ya binadamu. Kwa sasa Mkandarasi anachimba kisima cha tatu eneo la Kibada na amefikia mita 200 kati ya mita 600. Aidha, Mtaalam Mshauri anayetathmini athari za kimazingira na kijamii (ESIA) amewasilisha rasimu ya tatu ya taarifa ya ESIA tarehe 24/3/2014 na kupelekwa Benki ya Dunia tarehe 26/03/2014 kwa ajili ya kuridhiwa.

175.      Mheshimiwa Spika, baada ya ulipaji wa fidia kwenye eneo la mita 60 kuzunguka kila kisima katika maeneo ya Kimbiji na Mpera kukamilika, Serikali ilikamilisha uhakiki wa fidia katika maeneo ya Luzando na Kisarawe II. Ulipaji wa fidia kwa eneo litakapojengwa tanki la Kisarawe II ulianza tarehe 20/8/2013 na kwa eneo la Luzando tarehe 29/10/2013. Vilevile, uthamini katika maeneo ya ujenzi wa njia za mabomba na barabara kuelekea kwenye visima umeanza, na maombi ya kupata Wathamini kutoka Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali yamewasilishwa. Kwa sasa Mtaalam Mshauri anakamilisha usanifu wa kazi hiyo. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kutekeleza mradi wa kuchimba visima katika eneo la Kimbiji na Mpera.

(c)  Upanuzi wa Mtambo wa Ruvu Juu

176.      Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto ya ukuaji wa kasi wa Miji ya Mlandizi, Kibaha na Jiji la Dar es Salaam, Wizara yangu kwa kushirikiana na Serikali ya India inajenga na kupanua mtambo wa kuzalisha maji Ruvu Juu na ulazaji wa bomba kuu kutoka Mlandizi hadi Kimara kuanzia tarehe 15/02/2014. Mradi huo unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 18. Mradi utakapokamilika utagharimu Dola za Marekani milioni 39.7 kwa ajili ya upanuzi wa mtambo na Dola za Marekani milioni 59.3 kwa ulazaji wa bomba kuu. Kukamilika kwa upanuzi wa mradi kutaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 82 hadi lita milioni 196 kwa siku. Aidha, wananchi wanaoishi kwenye maeneo ya Jiji ambayo miundombinu ya usambazaji maji ilikarabatiwa na haikuwa na maji kwa kipindi kirefu watapata huduma hiyo.

(d)  Upanuzi wa Mradi wa Maji wa Ruvu Chini

177.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali kwa kushirikiana na MCC, imekamilisha upanuzi wa mradi wa maji wa Ruvu Chini. Kwa sasa Mkandarasi anafanya majaribio ya mitambo. Hadi mwezi Machi 2014, kazi ya ulazaji wa bomba kuu kutoka mitambo ya Ruvu Chini hadi kwenye matanki ya Chuo Kikuu cha Ardhi lenye urefu wa kilomita 55.93 imekamilika kwa asilimia 62.87 sawa na kilomita 35.16. Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2014. Aidha, kazi ya ujenzi wa kingo za Mto Ruvu katika eneo la Kidogozero ulikamilika mwezi Novemba, 2013 na umekabidhiwa kwa DAWASA, kwa sasa Mkandarasi yuko kwenye kipindi cha uangalizi (defects liability period).

(e)  Ukarabati na Upanuzi wa Mfumo wa Kusambaza Majisafi

178.      Mheshimiwa Spika, Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Mfumo wa Kusambaza Majisafi kati ya Jiji la Dar es Salaam na Mji wa Bagamoyo unahusisha kuunganisha wateja kutoka Tegeta hadi Mpiji na Mpiji hadi Bagamoyo. Mradi huo unajumuisha ulazaji wa mabomba ya urefu wa kilomita 732 ya kusambaza maji yatakayounganisha wateja 24,400 na kujenga magati 30 kati ya Bagamoyo na Tegeta. Mtaalam Mshauri atakayesanifu na kusimamia ujenzi amepatikana. Kwa sasa Mtaalam Mshauri huyo anaandaa nyaraka za zabuni za ujenzi wa mradi (pre-qualification document) na tayari amewasilisha rasimu ya kwanza ya nyaraka za kuwatafuta Wakandarasi watakaoshiriki zabuni. Aidha, kwa mradi wa kuunganisha mabomba ya usambazaji maji ya urefu wa kilomita 300 kwenye eneo la Mbezi hadi Kiluvya uliendelea kutekelezwa. Jumla ya wateja 10,000 wataunganishwa na magati 30 yatajengwa. Kazi hiyo inahusu miradi ya mabomba madogo madogo na kuunganisha wateja kwenye eneo kati ya Mbezi hadi Kiluvya. Mtaalam Mshauri anaandaa nyaraka za zabuni.

179.      Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kuboresha hali ya huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ili iwe endelevu, Wizara yangu imefikia makubaliano ya awali na Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) ili kuwekeza kwenye mradi wa ukarabati na upanuzi wa mfumo wa usambazaji maji katika Jiji la Dar es Salaam. Kwa sasa Mtaalam Mshauri ameanza kazi ya upembuzi yakinifu na kuandaa makadirio ya gharama za mradi ili zitumike kutayarisha Mkataba wa kifedha. Pamoja na majadiliano yanayoendelea na TIB, Kampuni za AVIC International na China Machinery and Engineering Corporation kutoka nchini China zimeonesha nia ya kufadhili baadhi ya miradi ikiwemo upanuzi wa miundombinu ya majitaka. Wizara yangu inaendelea na taratibu za awali za kufikia mikataba ya kifedha.

(f)   Miradi Mingine ya Kuboresha Huduma ya Maji Jijini Dar es Salaam

180.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (BTC) na Umoja wa Nchi za Ulaya imekamilisha miradi tisa (9) kati ya miradi 15 ya kujenga mifumo ya usambazaji maji katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam. Kazi zilizokamilika ni pamoja na kuchimba visima 14; na kujenga vituo 194 vya kuchotea maji na matanki 15 ya kuhifadhia maji. Miradi sita (6) iliyobaki katika maeneo ya Tabata Darajani, Minazi mirefu, Kinyerezi, Mwanamtoti, Yombo Dovya - Msakala na Tandale inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2014 baada ya kuwasha mitambo na kupima msukumo wa maji (pressure test). Vilevile, mradi huo umejenga vyoo bora 21 vya mfano katika maeneo ya jumuiya (shule 6 za msingi, zahanati 4, soko 1 na katika Ofisi za Serikali za Mitaa 10). Vyoo hivyo vimejengwa kwa lengo la watu kujifunza jinsi ya kujenga vyoo bora katika makazi yao. Pamoja na ujenzi wa vyoo hivyo vipya, mradi umekarabati vyoo vya zamani katika shule tisa (9). Vilevile, mradi umetoa elimu ya maji, afya na usafi wa mazingira kwa wananchi na wanafunzi wa shule husika katika eneo la mradi. Jedwali Na. 12 linaonesha utekelezaji wa uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali ya mradi Jijini Dar es Salaam

181.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliendelea kutekeleza miradi ya uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ili kupunguza kero ya maji wakati wa kusubiri utekelezaji wa Mradi Maalum wa Kuboresha Upatikanaji wa Huduma ya Majisafi na Uondoaji Majitaka katika Jiji la Dar es Salaam. Hadi mwezi Machi 2014, DAWASA imechimba visima 44 kati ya visima 46 vilivyopangwa. Kati ya visima hivyo, visima 21 vimekamilika na kuanza kutumika. Visima nane (8) vipo Kimara, katika maeneo ya Mavurunza A, Kilungule A, Kilungule B, King’ongo I, King'ongo II, King'ongo III, Saranga I na Saranga II; Visima vitano (5) vipo Keko/Chang’ombe maeneo ya Keko Magurumbasi, Keko Mwanga A, Chang’ombe A, Unubini na Chang’ombe Toroli; na visima vitatu (3) vipo Sandali katika maeneo ya Sandali, Mpogo na Mwembe Ladu. Vilevile, visima vingine viwili (2) vilivyokamilika vinatumika Mburahati maeneo ya Mburahati National Housing na Shule ya Msingi Muungano; na kisima kimoja kimoja katika maeneo ya Mwaninga-Kigamboni, Kipunguni na FFU yaliyoko Ukonga. Katika mwaka 2014/2015, DAWASA itaendelea na kazi ya ufungaji wa pampu ili kukamilisha visima vilivyobaki.

(g)  Mradi wa Maji ya Bomba kwenda Mloganzila

182.      Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza ujenzi wa Kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Udaktari na Sayansi Shirikishi katika eneo la Mloganzila.  Ili kurahisisha ujenzi, Wizara yangu inajenga mradi wa Bomba la Maji kwenda eneo la upanuzi. Katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu imekamilisha usanifu wa mradi, ununuzi wa mabomba na pampu, ukarabati wa tanki la zamani kwenye kituo cha kusukumia maji na ujenzi wa mnara wa tanki jipya litakalopokea maji kutoka kwenye chanzo cha Ruvu Juu. Kazi zote zilikamilika mwezi Oktoba, 2013. Uchimbaji wa mtaro wenye urefu wa kilomita 1.94 umekamilika ambapo mabomba yenye urefu wa kilomita 1.0 yamelazwa. Kazi ya kulaza mabomba yenye urefu wa kilomita 0.94 zilizobaki inaendelea na mradi utakamilika mwezi Juni, 2014.

3.3.7 Huduma ya Maji katika Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo na Miradi ya Kitaifa


(a)      Miradi ya Maji katika Miji ya Kibiti na Kibaigwa

183.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu ilikamilisha ujenzi wa miradi ya maji katika Miji ya Kibiti na Kibaigwa katika mwaka 2013/2014. Mradi wa Kibiti ambao uligharimu shilingi bilioni 5.3 ulizinduliwa rasmi tarehe 5/10/2013 na Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mradi huo unatoa huduma kwa wakazi wapatao 29,931 wa Kata mbili za Kibiti na Mtawanya. Aidha, mradi wa Kibaigwa uliogharimu shilingi bilioni 2.27 ulizinduliwa na Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Maji tarehe 17/3/2014. Kukamilika kwa mradi huo kumewezesha asilimia 90 ya wananchi wa Kibaigwa kupata maji safi na salama ukilinganisha na asilimia 48 kabla ya mradi.




(b)      Miradi ya Maji katika Miji ya Kisarawe, Ikwiriri, Kilosa, Turiani, Mahenge, Mvomero na Gairo

184.      Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza miradi ya maji katika Mji wa Kisarawe, Wizara imekamilisha uchimbaji wa visima vitano (5) katika maeneo ya Kwala, Mtunani, Chole-Samvula, Yombo-Lukinga I na Yombo-Lukinga II. Aidha, Wizara imeendelea na ujenzi wa miradi ya maji katika miji midogo ya Ikwiriri, Kilosa, Turiani, Mahenge, Mvomero na Gairo. Hadi mwezi Machi 2014, ujenzi wa miradi ya maji katika miji hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kama ifuatavyo:- Ikwiriri asilimia 100, Kilosa asilimia 80, Turiani asilimia 77, Mahenge asilimia 77, Mvomero asilimia 81 na Gairo asilimia 86. Miradi hiyo inatarajiwa kukamilika mwaka 2014/2015.

(c)      Miradi ya Maji Masasi/Nachingwea na Bunda

185.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu imekamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji wa Masasi-Nachingwea. Mradi huo umekamilika mwezi Julai, 2013 na unahudumia Miji ya Masasi na Nachingwea pamoja na vijiji vya Likwachu na Chinongwe vilivyopo Wilaya ya Ruangwa na vijiji vya Chiumbati Shuleni na Chiumbati Miembeni vilivyopo Wilaya ya Nachingwea. Kazi ya kuunganisha wateja na ufungaji wa dira za maji inaendelea. Hadi mwezi Machi, 2014 jumla ya wateja 2,972 wameunganishwa kwenye mtandao wa majisafi. Vilevile, huduma kwa wakazi wasio na maji majumbani inatolewa kwenye magati 68 yaliyojengwa maeneo mbalimbali ya Miji ya Masasi na Nachingwea.

186.      Mheshimiwa Spika, katika Mji wa Bunda, hadi mwezi Machi, 2014 Mkandarasi amekamilisha kazi ya ukarabati wa matanki mawili (2) kati ya matanki matatu (3) yenye ujazo wa lita 225,000  kila moja. Vilevile, ujenzi wa Ofisi ya Mtaalam Mshauri na ununuzi wa magari mawili umekamilika. Kazi ya ulazaji wa bomba inaendelea na imefikia asilimia 40, ambapo kilomita 9.3 kati ya kilomita 25.4 zimekamilika. Katika mwaka 2014/2015 ujenzi huo utaendelea na kutumia shilingi bilioni 3  kukamilisha ulazaji wa bomba na kujenga mfumo wa kusambaza maji katika Mji wa Bunda.

(d)      Mradi wa Maji Orkesumet

187.      Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kiarabu (BADEA) na OFID inatarajia kujenga mradi wa majisafi utakaohudumia Mji wa Orkesumet. Katika utekelezaji wa mradi huo, BADEA watatoa Dola za Marekani milioni 8, OFID Dola za Marekani milioni 8 na Serikali Dola za Marekani milioni 2.4. Mtaalam Mshauri anaendelea na kufanya mapitio (review) ya usanifu uliofanywa hapo awali na kutayarisha vitabu vya zabuni kwa ajili ya kumtafuta Mkandarasi wa ujenzi. Hadi mwezi Machi, 2014 Mtaalam Mshauri ameshawasilisha taarifa ya mapitio ya usanifu wa kina (detail design review), kwa ajili ya kuhakikiwa. Katika mwaka 2014/2015, ujenzi wa mradi huo utaanza baada ya kumpata Mkandarasi.

(e)      Mradi wa Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi Muheza

188.      Mheshimiwa Spika, katika kupunguza kero ya upatikanaji wa majisafi na salama katika Mji wa Muheza, Wizara yangu imetuma shilingi milioni 350 ili kuboresha miundombinu ya maji ya visima virefu vitatu (3) maeneo ya soko la Michungwani, NHC-tank na Kwasemwaiko. Kazi zinazoendelea kutekelezwa ni ununuzi na ufungaji wa pampu na viungio vyake, ujenzi wa chemba mbili (2) na vituo viwili (2) vya kuchotea maji, uchimbaji mtaro, ulazaji wa mabomba na ununuzi wa vifaa vya ujenzi na umeme. Ujenzi huo ukikamilika kwenye kisima cha NHC-tank kitakuwa na uwezo wa kusukuma maji lita 2,000 kwa saa (saa 22 kwa siku), kisima cha Kwasemwaiko kikikamilika kitasukuma maji lita 2,500 kwa saa (saa 22 kwa siku).

(f)        Mradi wa Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi Karatu

189.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Serikali ilitekeleza  mradi wa maji wa dharura katika Mji wa Karatu unaogharimu Shilingi milioni 930. Mradi huo umezinduliwa rasmi tarehe 22/04/2014 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete. Kazi zilizokamilika hadi sasa ni ujenzi wa tanki moja lenye ujazo wa lita 225,000; ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa kilomita 2.9; ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji yenye urefu wa kilomita 4.4; ujenzi wa vituo 12 vya kuchotea maji; ujenzi wa njia kuu ya umeme yenye urefu wa kilomita 1.2; na ufungaji wa transfoma na pampu. Kazi hizo zimegharimu shilingi milioni 609.9 na kuongeza upatikanaji wa maji kwa kiasi cha lita 720,000 kwa siku na hivyo kufikia asilimia 34.5 ya mahitaji ya maji kwa Mji wa Karatu. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu imepanga kutumia shilingi milioni 250 kuendelea kutekeleza kazi zilizobaki ambazo ni pamoja na:- Ujenzi wa tanki moja lenye ujazo wa lita 225,000; ulazaji wa mabomba ya usambazaji wa maji yenye urefu wa kilomita 3.8; na uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba ya kupeleka maji eneo la G-lambo.

(g)      Miradi ya Maji ya Miji Midogo

190.      Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga shilingi bilioni 17.1 kwa ajili ya kukarabati na kupanua miundombinu ya maji katika miji mikuu ya wilaya na miji midogo 46. Fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi inayoendelea na ambayo italeta ahueni kubwa ya maji kwa wakazi wa Miji hiyo.  Miradi hiyo imeorodheshwa kwenye Jedwali Na. 13 linaonesha mchanganuo wa fedha zitakazotumwa kwenye Mamlaka za Miji Mikuu ya Wilaya na Miji Midogo.

(h)      Mradi wa Maji Longido

191.      Mheshimiwa Spika, Mji wa Longido unakadiriwa kuwa na wakazi 21,000 na mifugo ipatayo 13,000. Mahitaji ya maji kwa sasa ni wastani wa lita milioni 1.2 kwa siku wakati uzalishaji wa maji kwa siku ni wastani wa lita 240,000. Utafiti uliofanyika awali umeonesha kuwa maeneo ya karibu na Mji hayana vyanzo vya maji vinavyoweza kutosheleza mahitaji ya maji kwa Mji huo. Kutokana na hali hiyo, Wizara yangu imefanya utafiti wa kina na kubaini kuwa chanzo pekee ambacho kitatosheleza mahitaji ni Mto Meru. Katika mwaka 2014/2015, Wizara imetenga shilingi bilioni 3 kutekeleza mradi wa kutoa maji Mto Meru hadi Mji wa Longido ili kutatua tatizo la maji katika Mji huo.

3.3.8 Miradi ya Maji ya Kitaifa


192.      Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na upungufu wa maji katika Miradi ya Kitaifa na kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma katika maeneo ya miradi hiyo, Wizara yangu ilituma shilingi milioni 870 kwa ajili ya ununuzi wa pampu, mabomba na ukarabati wa miundombinu ya maji. Mgao wa fedha ulikuwa kama ifuatavyo:- Handeni Trunk Main - HTM shilingi milioni 50, Makonde shilingi milioni 60, Maswa shilingi milioni 200, Mugango-Kiabakari shilingi milioni 250, Wanging’ombe shilingi milioni 50, Chalinze shilingi milioni 60, Masasi-Nachingwea shilingi milioni 150, na KASHWASA shilingi milioni 50. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu imepanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 11.6 kukarabati miundombinu ya maji katika miradi hiyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma iliyo bora na endelevu.

193.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaajiri Mtaalam Mshauri wa kufanya mapitio ya usanifu na usimamizi wa mradi wa miundombinu ya maji katika Mradi wa Kitaifa Mugango-Kiabakari na vijiji vilivyopo umbali wa kilomita 12 kando ya bomba kuu. Mradi huo utatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA) na Mfuko wa Maendeleo wa Saudia (Saudi Fund for Development - SFD) kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 30.69. Kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa chanzo, ujenzi wa mtambo wa kusafisha na kusukuma maji, kujenga matanki matatu, kulaza mabomba kutoka Mugango hadi Kiabakari na Butiama urefu wa kilomita 32, kukarabati mitambo ya kusukuma maji ya Kiabakari na kulaza mabomba ya mtandao wa usambazaji maji Butiama hadi Bisalye. Kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha wananchi wapatao 80,000 katika eneo hilo.

3.3.9 Kuzijengea Uwezo Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Mijini


194.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu imeendelea kuzijengea uwezo Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Mijini ili ziongeze ufanisi katika utoaji wa huduma kwenye maeneo yao. Ujenzi wa ofisi za Mamlaka za maji za Miji ya Utete na Mpwapwa umekamilika. Ujenzi wa ofisi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Babati unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2014. Katika Mamlaka ya maji Tunduma, ujenzi wa ofisi utakamilika mwezi Novemba, 2014. Aidha, katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kuziimarisha mamlaka za maji ngazi ya mikoa, wilaya, miji midogo na miradi ya kitaifa kwa kuzijengea mazingira mazuri zaidi ya kazi ili zitoe huduma bora kwa wananchi.

195.      Mheshimiwa Spika, ili kuijengea uwezo miradi ya kitaifa na mamlaka za maji za daraja B na C, Wizara yangu imetoa jumla ya shilingi milioni 435 kwa ajili ya kulipia sehemu ya ankara za umeme wa mitambo ya kuzalisha maji. Katika mwaka 2014/2015 Wizara yangu, itaendelea kuchangia gharama za uendeshaji wa miradi ya kitaifa na Mamlaka za daraja B na C ili hatimaye ziweze kujiendesha zenyewe na hivyo kuipunguzia Serikali mzigo wa kuchangia gharama hizo.

196.      Mheshimiwa Spika, kwa ujumla katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya maji na kuzijengea uwezo Mamlaka za maji za ngazi ya wilaya, miji midogo na miradi ya kitaifa ili kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika maeneo ya mamlaka hizo.




197.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu imeendelea kuisimamia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ili iweze kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa kwenye Kifungu Na. 414 cha Sheria Na.11 ya EWURA ya mwaka 2001. Sheria hiyo inaitaka EWURA kudhibiti utoaji wa huduma kwenye Sekta za umeme, mafuta ya petroli, gesi asilia, majisafi na majitaka nchini. Kwa mujibu wa sheria hiyo, EWURA ina majukumu ya kutoa leseni, kusimamia utekelezaji wa masharti ya leseni, kudhibiti ubora na ufanisi wa utoaji huduma, kutathmini na kupitisha bei za huduma na kutatua migogoro baina ya watoa huduma na wateja wao. Kwa upande wa sekta ya Maji, EWURA imeendelea na udhibiti wa huduma za maji zinazotolewa na Mamlaka za Maji 129 nchini. Kati ya Mamlaka hizo, 23 ni za miji mikuu ya mikoa, 96 za miji mikuu ya wilaya na miji midogo, DAWASA, DAWASCO na miradi ya maji minane (8) ya kitaifa.

198.      Mheshimiwa Spika, EWURA iliendelea kutathmini na kuidhinisha bei za huduma ya maji kwa mamlaka mbalimbali za majisafi na usafi wa mazingira nchini. Katika mwaka 2013/2014, EWURA iliidhinisha bei mpya za huduma za maji kwa mamlaka 23 za maji za Babati, Moshi, Musoma, Kilwa Masoko, Kahama, Arusha, Bariadi, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, KASHWASA, Kigoma, Lindi, Mbeya, Morogoro, Mpanda, Mtwara, Mwanza, Shinyanga, Singida, Songea, Tabora na Tanga. Mabadiliko ya bei hizo yanatokana na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji hususan gharama ya umeme. Aidha, EWURA, ilipokea na kupitia Mipango ya Kibiashara (Business Plans) ya miaka mitatu kutoka mamlaka za maji za Miji ya Kisarawe, Songea na Mtwara. Mamlaka zilizobaki zinaendelea kutekeleza mipango yao ya kibiashara.

199.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, EWURA ilitoa taarifa ya utendaji wa Mamlaka za Maji kwa mwaka 2012/13. Taarifa hiyo inaonesha kuwa mamlaka za maji zimepiga hatua katika ufungaji wa dira za maji, kuongezeka kwa idadi ya wateja wa majisafi na majitaka na ukusanyaji wa maduhuli. Aidha, katika mwaka 2013/2014, jumla ya malalamiko 12 yalipokelewa EWURA. Malalamiko hayo yalihusu ankara za majisafi na majitaka zilizokosewa, ukosefu wa maji, kukatiwa huduma ya maji kimakosa na huduma hafifu kwa wateja (poor customer service). Kati ya malalamiko yaliyowasilishwa, sita (6) yamepatiwa ufumbuzi na sita (6) yaliyobaki yapo katika hatua mbalimbali za utatuzi.

200.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014 EWURA imeendelea kusimamia Sekta Ndogo za Umeme, Petroli na Gesi Asilia, hususan katika masuala ya kusimamia ubora wa huduma ya umeme, kukagua miundombinu ya umeme, gesi asili na mafuta ili kuhakikisha ubora na usalama wa huduma hizo. EWURA imeendelea kuandaa kanuni na taratibu zinazovutia  uwekezaji na kutoa leseni mbili (2) kwa wawekezaji wa miradi midogo midogo isiyozidi Megawati 10 (makampuni ya Mapembasi ya Njombe na Bwelui ya Mbeya). Katika Sekta ndogo ya Petroli jumla ya leseni 15 kwa ajili ya wauzaji wa jumla wa mafuta ya petroli zilitolewa. Vilevile, leseni 19 kwa ajili ya wauzaji wa rejareja wa mafuta hayo zilitolewa. Aidha, EWURA imeendelea kukagua miundombinu ya kuchakata, kusafirisha na kusambaza gesi asilia na kubainika kuwa ni salama kwa matumizi na mazingira.

201.      Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha udhibiti wa huduma ya majisafi na uondoaji wa majitaka inayotolewa na mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira nchini, katika mwaka 2014/2015 vipaumbele vifuatavyo vitazingatiwa:-

(i)             Kuhimiza uwekezaji kwa mamlaka za maji kwa kuandaa miongozo ya jinsi ya kushirikisha sekta binafsi katika utoaji wa huduma za majisafi na majitaka;

(ii)           Kuendelea kufuatilia utendaji wa mamlaka za maji nchini kwa kuchambua na kuhakiki taarifa za utendaji kazi na kukagua miundombinu na utendaji wa mamlaka za maji;

(iii)          Kuandaa miongozo ya viwango vya ubora wa huduma zinazotolewa na mamlaka za maji;

(iv)          Kuendelea kufuatilia utekelezaji wa mipango yao ya kibiashara (Business Plans) kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na EWURA;

(v)           Kuandaa na kutekeleza mipango ya kuhimiza ubora wa huduma wa mamlaka za maji katika miji midogo, miji mikuu ya wilaya na miradi ya kitaifa; na

(vi)          Kuandaa na kutekeleza hatua zitakazosaidia kupunguza gharama za kuunganisha huduma za maji kwa wateja.

202.      Mheshimiwa Spika, EWURA ni mamlaka ya udhibiti wa Sekta kuu mbili za Nishati na Maji. Ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi, nimeiagiza EWURA iendeleze ushirikiano wa karibu na kupokea na kutekeleza miongozo inayotolewa na Wizara zinazosimamia Sekta hizo kulingana na Sheria zilizopo.


203.      Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu la Chuo cha Maendeleo na Usimamizi wa Maji la kujenga uwezo wa kitaalam wa fani za ufundi zinazohitajika kwenye Sekta ya Maji, Chuo kilidahili wanafunzi 412 wa mwaka wa kwanza wa Stashahada (water technicians) na wanafunzi 69 wa Shahada ya Kwanza ya Uhandisi wa Rasilimali za Maji na Umwagiliaji (Bachelor of Engineering in Water Resources and Irrigation). Udahili huo umeongeza idadi ya wanafunzi wote kufikia 1,020 ikilinganishwa na 757 mwaka 2012/2013.

204.      Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Novemba 2013, wanafunzi 144 walihitimu mafunzo katika fani za ufundi sanifu wa mifumo ya usambazaji wa majisafi na usafi wa mazingira (80), utafutaji wa maji chini ya ardhi na uchimbaji wa visima vya maji (Hydrogeology and water well drilling) (22), haidrolojia na hali ya hewa (26) na teknolojia ya maabara ya uchunguzi wa ubora wa maji (Water Quality Laboratory technology) wanafunzi (16). Katika jitihada za kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike kujiunga na fani za ufundi, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ilifadhili wanafunzi 52 wa kike katika kozi za kuwawezesha kujiunga na masomo ya stashahada. Hii imewezesha kuongeza udahili wa wanafunzi wa kike kutoka 67 mwaka 2012/2013 hadi 79 katika mwaka 2013/2014.

205.      Mheshimiwa Spika, vilevile, Chuo kimeendelea kutoa ushauri juu ya ubora wa maji kwa wateja 136 waliowasilisha sampuli za maji na kupima pamoja na kushauri juu ya upatikanaji wa maji ardhini katika maeneo ya  Makambako (Njombe), Ilula (Iringa); Kiwalani, Kibamba na Kigamboni (Dar es Salaam); Gairo (Morogoro);  Sikonge (Tabora), Korogwe (Tanga) na Makongo (Pwani). Aidha, washiriki 135 walipewa mafunzo ya muda mfupi katika fani mbalimbali zinazohusu Sekta ya Maji.

206.      Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mazingira ya utoaji wa mafunzo, Chuo kimesaini mikataba ya ununuzi wa vifaa ikiwa ni pamoja na samani na vitendea kazi vya maabara za hydraulics, ubora wa maji, usambazaji maji, hali ya hewa, na udongo. Katika kukabiliana na upungufu wa watumishi, Chuo kiliajiri watumishi wanane (8) na watumishi 70 walipatiwa mafunzo ya masuala ya ununuzi. Katika mwaka 2014/2015 chuo kitaendelea kutoa mafunzo katika ngazi ya Stashahada (Water Technician) kwa wanafunzi 1,056, sambamba na mafunzo ya ngazi ya Shahada kwa wanafunzi 135. Mafunzo ya muda mfupi kwa washiriki 300 yatatolewa. Vilevile, Chuo kitafanya utafiti na kutoa ushauri katika masuala yanayohusu Sekta ya Maji. Ili kukabiliana na upungufu wa ofisi na madarasa, Chuo kitakarabati majengo yaliyopo na kuanza ujenzi wa jengo la ghorofa sita lenye madarasa, maabara, maktaba na kumbi za mikutano.


207.      Mheshimiwa Spika, Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) uliendelea na uchimbaji wa visima virefu katika maeneo mbalimbali nchini. Hadi mwezi Machi, 2014 visima virefu 100 vilikamilika na ifikapo mwezi Juni, 2014 visima vingine 150 vinatarajiwa kuchimbwa katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, uchunguzi wa maji chini ya ardhi kwa ajili ya uchimbaji visima virefu umekamilika katika maeneo 184 na ifikapo mwezi Juni, 2014 maeneo 244 yatachunguzwa. Jedwali Na. 14 linaloonesha orodha ya visima vilivyochimbwa na DDCA katika mwaka 2013/2014.

208.      Mheshimiwa Spika, Wakala umekamilisha mradi wa ujenzi wa mnara wa kubeba tanki la kuhifadhi maji na ujenzi wa miundombinu ya maji katika ghala la kuhifadhi madawa MSD-Kizota (Dodoma). Vilevile, Wakala unaendelea kutekeleza kazi ya ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji NHC-Kibada (Kigamboni, Dar es Salaam) kazi ambayo imefikia asilima 90. Kazi hiyo itakamilika ifikapo mwezi Juni, 2014. Kazi ya upembuzi yakinifu wa miradi ya mabwawa katika maeneo manne (4) ya bwawa la Aviv Estate Wilayani Songea, bwawa la Saadani National Park Wilayani Pangani, bwawa la Pande Game Reserve Wilayani Bagamoyo na bwawa la Mfilisi (Mbegesela) Wilayani Kilosa nayo imekamilika. Ujenzi wa bwawa la umwagiliaji la Aviv Estate – Lipokera, Songea utakamilika ifikapo mwezi Juni, 2014. Aidha, ukarabati wa mabwawa matatu (3) ya Seke Ididi Wilayani Kishapu, Habiya Wilayani Itilima na Matwiga Wilayani Chunya umeanza. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea na mpango wa kuujengea uwezo Wakala kwa kununua mitambo mbalimbali ya uchimbaji visima na ujenzi wa mabwawa ili kuongeza kasi ya kuchunguza maji chini ya ardhi, uchimbaji wa visima na ujenzi wa mabwawa nchini. Wizara imeiagiza Wakala kuandaa mkakati wa kujitegemea (Exit Strategy), lengo likiwa ni kuwa na Wakala wenye weledi mkubwa na pia inayojitegemea katika kugharamia shughuli zake zote.


209.      Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Bohari Kuu ya Maji inaendelea  kununua, kuhifadhi na kusambaza vifaa na madawa ya kusafisha na kutibu maji  kwenye Halmashauri mbalimbali, Mamlaka za Maji na Miradi ya Kitaifa. Katika mwaka 2013/2014, vifaa mbalimbali vilisambazwa vikiwemo pampu za maji, mabomba na viungio vyake. Aidha, Bohari Kuu ya Maji imekamilisha ujenzi wa uzio na ukarabati wa ghala la kuhifadhi vifaa vya ujenzi. Wizara yangu katika mwaka 2014/2015, itaendelea kuijengea uwezo Bohari Kuu ya Maji ili iweze kununua vifaa  vya ujenzi wa miradi ya maji kwa wingi (Bulk Purchase) na kurahisisha upatikanaji wa vifaa hivyo katika Halmashauri, Mamlaka za Maji na Miradi ya Kitaifa ili kwenda sambamba na Mpango wa “Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa”. Aidha, nimeiagiza Bohari Kuu ya Maji kubuni Miradi ya Ubia (Public Private Partnership-PPP) ili kupunguza utegemezi wake kwa Serikali.


3.5            MASUALA MTAMBUKA


210.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara imeendelea kutoa ushauri wa kisheria na elimu kuhusu utekelezaji wa sheria mbalimbali na hatua za kuchukua dhidi ya ukiukwaji wa sheria hizo. Elimu na ushauri umetolewa katika ngazi ya Wizara, Bodi za Maji za Mabonde, Mamlaka za Maji, Halmashauri, Vyombo vya Watumiaji Maji na Wadau wa Sekta ya Maji kupitia mikutano, kongamano, warsha na mafunzo mbalimbali. Jumla ya nakala 478 za Sheria Na.11 ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji na Sheria Na.12 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira za mwaka 2009 na kanuni zake zimesambazwa. Aidha, mikataba 110 zikiwemo Randama za Makubaliano (MoU) zilipitiwa na kutolewa ushauri wa kisheria.

211.      Mheshimiwa Spika, Wizara ilikamilisha utayarishaji wa kanuni saba (7) za Sheria za Maji ambazo ni:- Usalama wa Mabwawa (The Water Resources Management (Dam Safety) Regulations, 2013), iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 237 la tarehe 02/08/2013; Usambazaji wa Maji (The Water Supply Regulations 2013) na Mfuko wa Taifa wa Uwekezaji wa Maji (The National Water Investment Fund Regulations 2013), Gazeti la Serikali Na. 236 la tarehe 02/08/2013; Usimamizi wa Maji chini ya Ardhi (The Ground Water (Exploration and Drilling) Licensing Regulations, 2013), Gazeti la Serikali Na. 219 la tarehe 02/07/2013; Uunganishaji wa Mamlaka za Maji (Water Supply and Sanitation (Clustering of Water Authorities) Regulations, 2013) Gazeti la Serikali Na 437 la tarehe 06/12/2013; Uteuzi na Sifa za Wajumbe wa Bodi (EWURA (Appointment and Qualifications of Board Members) Regulations 2013), Gazeti la Serikali Na 255 la tarehe 23/8/2013; Uteuzi na Ukomo wa Wajumbe wa Baraza la Ushauri la Watumiaji (EWURA (Appointment and Tenure of Members of the Consumer Consultative Council) Regulations, 2013) Gazeti la Serikali Na 256 la tarehe 23/8/2013; na Baraza la Ushauri kwa Serikali (EWURA (Government Consultative Council) Regulations 2013), Gazeti la Serikali Na. 254 la tarehe 30/08/2013. Nakala 95 za Kanuni hizo zilisambazwa kwa jamii na pia zinapatikana kupitia tovuti ya Wizara ya Maji (www.maji.go.tz).

212.      Mheshimiwa Spika, utayarishaji wa rasimu ya kanuni za Bodi ya Leseni (The Water Supply and Sanitation (Licensing Board) 2014) umekamilika. Rasimu ya tafsiri za Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na.11 ya mwaka 2009 na Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 12 ya mwaka 2009 kwa lugha ya Kiswahili zimekamilika na kuwasilishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali.

213.      Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto za kisheria katika utekelezaji wa Sheria za Maji, Wizara imetayarisha rasimu za marekebisho (amendment) ya Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na.11 ya mwaka 2009, Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 12 ya mwaka 2009 na Sheria ya DAWASA Na. 20 ya mwaka 2001. Maoni ya wadau yanaendelea kukusanywa na kufanyiwa kazi. Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaendelea kutoa ushauri wa kisheria kuhusu utekelezaji wa sheria za maji na kuendelea kutayarisha kanuni sita za sheria za maji.

214.      Mheshimiwa Spika, uanzishwaji wa Mfuko wa Maji (National Water Investment Fund) unalenga kuongeza fedha za uwekezaji katika Sekta ya Maji kwa mujibu wa Sheria Na. 12 ya mwaka 2009 ya Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira. Katika kufanikisha azma hiyo, Wizara yangu imekamilisha Kanuni za uendeshaji wa Mfuko wa Maji (National Water Investment Fund Regulations, 2013) na kuzichapisha kwenye Gazeti la Serikali Na. 236 la tarehe 02/08/2013, na zimeanza kutumika. Maandalizi ya kuuwezesha Mfuko kuanza kazi yamekamilika na kwa mwaka 2013/2014 Serikali ilitenga kiasi cha shilingi milioni 100 kama kianzio (seed money) kwa ajili ya Mfuko. Serikali itaendelea kuutunisha Mfuko huo kwa kubaini vyanzo vingine vya mapato ikiwa ni pamoja na ada na tozo mbalimbali.


215.      Mheshimiwa Spika, elimu na taarifa kuhusu maendeleo ya Sekta ya Maji ni muhimu kwa jamii kama njia mojawapo ya kuelezea masuala ya usimamizi na uendelezaji wa miradi ya maji nchini. Katika mwaka 2013/2014, Wizara iliendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia maonesho, warsha, tovuti na vyombo mbalimbali vya habari. Vilevile, mwezi Agosti 2013, Wizara yangu ilishiriki kikamilifu katika maonesho ya Kilimo ya Nanenane yaliyofanyika Nzuguni Mjini Dodoma ambapo vipeperushi, majarida na machapisho mbalimbali yanayohusu shughuli zinazotekelezwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji vilisambazwa kwa jamii. Pia, elimu ya Sera ya Maji kwa lugha nyepesi ilitolewa kwa wananchi kupitia majarida na santuri za maigizo ili kuifahamu mipango na mikakati ya Wizara. Aidha, katika Maadhimisho ya Wiki ya Maji yaliyofanyika kitaifa Mkoani Dodoma mwezi Machi, 2014, Wizara yangu ilitoa jumla ya machapisho 5,000 na vipindi saba (7) vya redio na luninga.

216.      Mheshimiwa Spika, Wizara ilitoa vipindi maalum kupitia vyombo vya habari kuhusiana na hali ya maji Mkoani Dodoma; mradi wa maji wa kitaifa wa Masasi-Nachingwea; upanuzi wa mradi wa maji wa Ruvu Chini; mradi wa maji wa Kahama-Shinyanga; na kituo cha utafiti cha kuondoa madini ya fluoride kwenye maji kilichopo Ngurdoto, Mkoani Arusha. Vipindi hivyo vililenga katika kufafanua na kuelimisha jamii katika masuala mbalimbali ya Sekta ya Maji. Pia, makala mbalimbali zilitolewa magazetini na kwenye mitandao ya kijamii ya mawasiliano kuelezea kazi mbalimbali zinazotekelezwa na Wizara. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kuelimisha wananchi na kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu Sekta ya Maji; kuandaa na kutangaza vipindi katika luninga na redio; na kuboresha tovuti ya Wizara ili wananchi wengi zaidi waitumie.


217.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu imeendelea kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuboresha utoaji wa huduma na utendaji kazi. Uimarishaji wa matumizi ya TEHAMA ulihusu masuala yafuatayo:-

(i)             Kuboresha mfumo wa kielektroniki wa takwimu na taarifa (Water Sector Management Information system) ili kusaidia masuala ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mipango na miradi kwenye Sekta ya Maji (scaling up/out MIS to cover M&E functions – physical aspects). Vilevile, mafunzo ya mfumo huo yametolewa kwa watumishi 40 kutoka Makao Makuu ya Wizara, 72 kutoka Halmashauri za Wilaya mpya, nane (8) Mikoa mipya, 62 Mamlaka za Majisafi na Majitaka na watumishi 18 wa Bodi za Maji za Mabonde. Matumizi ya mfumo huo yameboresha usimamizi wa fedha za utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji;

(ii)           Matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa takwimu na utambuzi wa vituo vya kuchotea maji vijijini (Water point mapping) kwa kutumia TEHAMA (www.wpm.maji.go.tz). Hadi mwezi Machi 2014, mafunzo ya mfumo huo yametolewa kwa watumishi 50 kutoka Makao Makuu ya Wizara, Wahandisi wa Maji 155 wa Halmashauri, Wahandisi wa maji 26 kwenye Sekretarieti za Mikoa, Wasajili 163 wa Vyombo vya Watumiaji Maji kwenye Halmashauri na Maafisa Maji wa Mabonde watatu (3);

(iii)          Kuendeleza juhudi za Serikali za utekelezaji wa Serikali Mtandao (e-Government) kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (e-Government Agency) katika utayarishaji wa mikakati ya kutekeleza ‘Open Data.’

Mikakati hiyo itahusisha kujenga uwezo wa Wizara na Taasisi katika matumizi ya Serikali Mtandao ili kutoa taarifa mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maji na matumizi ya fedha kwa uwazi zaidi.

218.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ukusanyaji na uchambuzi wa kina wa takwimu pamoja na kutathmini hali halisi ya upatikanaji wa maji vijijini. Tathmini ya hali halisi itafanyika baada ya kukamilisha ukusanyaji wa takwimu na utayarishaji wa ramani za vituo vya kuchotea maji vijijini (Water Point Mapping). Aidha, Wizara itaendeleza juhudi za kujenga uwezo wa Halmashauri za Wilaya na Sektretarieti ya Mikoa katika kutumia mfumo huo.

219.      Mheshimiwa Spika, kazi nyingine zitakazotekelezwa ni pamoja na:- kuimarisha mfumo wa kielektroniki wa takwimu na taarifa ili kusaidia masuala ya ufuatiliaji na tathmini; kutekeleza Mpango wa ‘Open Data’ ili kuwezesha utoaji wa takwimu na taarifa za Sekta ya Maji kwa uwazi. Lengo ni kurahisisha ushiriki wa wananchi na wadau katika kuendeleza Sekta ya Maji nchini kwa kuzingatia maeneo ambayo yataonekana kuwa na mapungufu zaidi ya huduma za maji; kujenga uwezo wa Wizara na Taasisi katika matumizi ya TEHAMA ili kuboresha huduma ndani ya Sekta ya Maji.


220.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kuzingatia umuhimu wa kuwepo kwa  uwiano wa kijinsia baina ya wanawake na wanaume katika ngazi za  uongozi na maamuzi. Katika mwaka 2013/2014, asilimia ya wanawake katika vyombo vya maamuzi kwenye ngazi ya Wizara na Taasisi zake ni zaidi ya asilimia 30 kama ifuatavyo:- Wizara (asilimia 39), Bodi ya Taifa ya Maji (asilimia 33), Bodi za Mabonde ya Maji (asilimia 34), Bodi za Mamlaka za Maji Mijini (asilimia 31), na Bodi za Wakala (asilimia 50). Pia, kwa upande wa vyombo vya watumia maji, suala la ushiriki wa wanawake kwa asilimia 50 linaendelea kuzingatiwa kulingana na mwongozo uliotolewa na Wizara.

221.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu imeshirikiana na wadau wa masuala ya jinsia (Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto; TGNP; na TaGLA) kutoa mafunzo kwa watumishi kwa awamu ili kujenga uwezo wa uongozi katika kusimamia na kutekeleza masuala ya jinsia. Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) inaandaa Mkakati na Mwongozo wa masuala ya jinsia ambao utatumika katika kupanga mipango madhubuti na kubaini changamoto zinazohusu jinsia mahala pa kazi na kuzipatia ufumbuzi.  Katika mwaka 2014/2015, Wizara itaandaa benki ya takwimu ya masuala ya jinsia kwa lengo la kuwa  na takwimu sahihi za ushiriki  unaozingatia jinsia katika mipango, ufuatiliaji na usimamizi wa Programu ya  Maendeleo ya Sekta ya Maji.


222.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu imetoa elimu kuhusu UKIMWI kwa watumishi 580 wa Wizara. Kati ya hao, watumishi 160 walipata ushauri nasaha na kukubali kupima VVU kwa hiari ili kujua afya zao. Aidha, Dawati la UKIMWI la Wizara lilishiriki katika maonesho ya Wiki ya Maji yaliyofanyika kitaifa Mjini Dodoma kuanzia tarehe 16 - 22/3/2014 kwa kutoa elimu, ushauri nasaha pamoja na upimaji wa hiari kwa jamii. Katika mwaka 2014/2015, kwa kuzingatia  maelekezo ya Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) Wizara yangu itaandaa Mpango wa Ukimwi Mahali pa Kazi (HIV Plan at Work Place) kwa kutekeleza yafuatayo:- kutathmini hali ya UKIMWI katika Wizara; kutoa mafunzo elekezi kwa waelimisha rika na watumishi kwa ujumla; kutenga bajeti ya masuala ya ukimwi; kuandaa mpango wa mafunzo utakaoonesha aina ya mafunzo yatakayotolewa; na kuzingatia mahitaji halisi ya watumishi wanaoishi na VVU kama yalivyoainishwa katika sheria ya kazi na mwongozo wa utumishi wa umma. Aidha, Wizara yangu imeendelea kutoa lishe kamili kwa watumishi wake 10 waliojiweka wazi kuwa wanaishi na VVU.


223.      Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Aprili 2014, Wizara imepokea watumishi 22 kutoka Sekretarieti ya Ajira. Kati ya hao, Mhasibu Msaidizi mmoja (1), Wahaidrolojia watatu (3), Wakemia wanne (4), Mhudumu wa Afya mmoja (1), Mafundi Sanifu sita (6) katika fani ya ujenzi, wawili (2) fani ya haidrolojia na watano (5) wa fani ya haidrojiolojia. Katika mwaka 2014/2015, Wizara inatarajia kuwapandisha vyeo watumishi 367 na kuwaajiri watumishi wapya 429 wa kada mbalimbali. Aidha, Wizara inaendelea kufuatilia kibali cha ajira mbadala kwa ajili ya kujaza nafasi 28 zilizo wazi za watumishi wa kada mbalimbali waliostaafu, waliofariki au kuacha kazi.

224.      Mheshimiwa Spika, mwezi Januari, 2014 watumishi 42 walipatiwa mafunzo elekezi kuhusu utumishi wa umma. Vilevile, mwezi Februari na mwezi Aprili 2014, Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) ilitoa mafunzo kwa viongozi 36 wa Wizara pamoja na Maafisa Watendaji Wakuu wa taasisi zilizo chini yake kwa ajili ya kuimarisha uongozi na utendaji kazi. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kutekeleza mpango wa kuwapatia watumishi mafunzo ya muda mrefu na ya muda mfupi ili kukidhi sifa za miundo ya kada zao na kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi. Mafunzo hayo yatatolewa kwa kuzingatia Mpango wa Mafunzo wa Wizara.

(h)      Mapambano Dhidi ya Rushwa

225.      Mheshimiwa Spika, tathmini ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini imeonesha kupungua kwa malalamiko ya kushuka kwa maadili kutokana na vitendo vya rushwa na watumishi wasiokuwa waaminifu kuhujumu miradi na miundombinu ya maji. Mwanzoni mwa mwezi Machi 2014, Wizara yangu kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi ilitoa mafunzo ya maadili kwa viongozi wote wa Wizara na taasisi zake za EWURA, DAWASA, DAWASCO, DDCA, Bohari Kuu ya Maji na Chuo cha Maji. Katika mwaka 2014/2015, mafunzo ya aina hiyo yanatarajiwa kutolewa kwa watumishi wengine wa Wizara ili kujenga uelewa wa pamoja.

(i)        Uratibu wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji

226.      Mheshimiwa Spika, Wizara inatekeleza Sera ya Maji ya Mwaka 2002 ambayo imeweka mfumo madhubuti na endelevu wa kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji nchini. Hii ni pamoja na kuandaa na kutekeleza taratibu za kisheria na kuweka muundo wa kitaasisi wenye uwezo wa kutekeleza Sera. Muundo huo unaohusisha ushirikishwaji wa Wadau wa Sekta ya Maji katika hatua mbalimbali za utekelezaji ikiwa ni pamoja na kubuni, kupanga, kusanifu, kujenga, kusimamia, kuendesha na matengenezo miradi ya maji pamoja na kuchangia gharama za huduma za maji. Sera hiyo inatekelezwa kupitia Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Maji (2006-2015) na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (2006-2025).

227.      Mheshimiwa Spika, Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (Water Sector Development Programme – WSDP) ni ya kipindi cha miaka 18 kuanzia mwaka 2006 hadi 2025. Awamu ya kwanza ya miaka mitano ya utekelezaji wa Programu ilianza mwezi Julai, 2007 na ilipangwa kukamilika mwezi Juni, 2012. Ili kukamilisha miradi iliyopangwa, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo iliamua kuongeza muda wa utekelezaji wa awamu ya kwanza kutoka Juni, 2012 hadi Juni, 2014. Kulingana na Hati ya Makubaliano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo, Wizara yangu imeendelea kuandaa taarifa za utekelezaji wa Programu na kuratibu maandalizi ya mikutano ya majadiliano kati ya Serikali, Washirika wa Maendeleo na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayohusiana na Sekta ya Maji.

228.      Mheshimiwa Spika, lengo la uratibu wa Programu ni kuhakikisha kuwa Programu ya Maji inatekelezwa kulingana na makubaliano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo ikiwemo kuhakikisha kuwa taarifa za utekelezaji na taarifa za matumizi ya fedha zinaandaliwa kwa wakati. Pia, kuhakikisha kuwa ushirikiano wa kiutendaji unakuwepo muda wote wa utekelezaji wa Programu kati ya Wizara ya Maji na OWM-TAMISEMI, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Fedha na Wizara nyingine ambazo ni watumiaji wakubwa wa maji, mfano, Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Kilimo. Aidha, ushirikiano wa kiutendaji kati ya ngazi ya Wizara hizo, Sekretarieti za Mikoa, Halmashauri, Bodi za Maji za Mabonde, Mamlaka za Maji Mijini na Miradi ya Kitaifa unakuwepo muda wote wa utekelezaji ili kuhakikisha kuwa viwango na kasi ya utekelezaji kwa kuzingatia thamani ya fedha inayotumika vinafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kutoa taarifa mbalimbali za utekelezaji wa Programu na kuratibu majadiliano baina ya wadau wa sekta.

(j)        Maandalizi ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Pili

229.      Mheshimiwa Spika, tathmini ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Programu iliyohusisha wadau wa Sekta ya Maji ilifanyika mwezi Februari hadi Mei, 2013. Tathmini hiyo ilipitia maeneo yote yanayohitaji maboresho kwa ajili ya Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (2014/2015 – 2018/2019). Mapendekezo hayo yalihusu kuimarishwa kwa mipango shirikishi ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji; mipango ya ujenzi wa miradi ya maji katika miji mikuu ya wilaya na miji midogo na kuboresha huduma za maji katika miji mikuu ya mikoa; na mipango ya ujenzi wa miradi ya maji vijijini inayohusisha uwekezaji, ukarabati, upanuzi, ujenzi wa miradi mipya na uendeshaji na matengenezo ya miradi katika Halmashauri. Pia, tathmini ilibainisha umuhimu wa kuzijengea uwezo taasisi zinazotekeleza Programu ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira kwa kuhusisha maeneo yote ya vijijini na kwenye taasisi za huduma za jamii zikiwemo shule na vituo vya huduma ya afya kwa kushirikiana na sekta nyingine.

230.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imepokea maoni na ushauri kutoka kwa Wadau kuboresha rasimu ya awamu ya pili ya Programu. Kikosi-kazi kimekamilisha kazi hiyo na kitabu cha awamu ya pili ya Programu kipo tayari kutumika kama mwongozo wa mipango ya utekelezaji na bajeti ya kila mwaka kuanzia 2014/2015 hadi mwaka 2018/2019.



231.      Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika mwaka 2013/2014, Sekta ya Maji imeendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali. Changamoto hizo na hatua zinazochukuliwa ili kukabiliana nazo ni kama ifuatavyo:-

(a)  Kuongezeka kwa Mahitaji ya Maji Yasiyowiana na Uwekezaji kwenye Miradi ya Sekta ya Maji

232.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inakabiliwa na changamoto ya kuongezeka kwa idadi ya watu, hususan mijini. Miji hiyo inakua kwa kasi kubwa sana wakati miundombinu ya kusambaza maji imeendelea kubaki ile ya zamani. Idadi ya watu mijini imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 4.5 ambapo kwa vijijini ni asilimia 2.3 kwa mwaka. Kwa Jiji la Dar es Salaam idadi ya watu inakua kwa wastani wa asilimia 5.6 kwa mwaka. Ongezeko hilo la watu linasababisha mahitaji makubwa ya maji yasiyowiana na uwezo wa Serikali kuwekeza kwenye miundombinu ya maji. Aidha, kwa upande wa vijijini upungufu wa huduma ya maji umesababishwa na uwekezaji mdogo wa miundombinu ya maji katika baadhi ya maeneo nchini. Sababu nyingine ni kuharibika kwa miundombinu ya maji pamoja na vituo vya kuchotea maji vilivyojengwa.

233.      Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo, Wizara yangu imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji kwa kukarabati, kupanua na kujenga miradi mipya mijini na vijijini. Kwa upande wa uboreshaji wa huduma za maji mijini, ujenzi wa miradi ya maji unaendelea katika miji mikuu ya mikoa na wilaya, miji midogo pamoja na miradi ya kitaifa. Katika Jiji la Dar es Salaam upanuzi wa mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu, ujenzi wa bomba kuu kutoka Bagamoyo hadi kwenye matanki ya Chuo Kikuu cha Ardhi, uchimbaji wa visima vya Kimbiji na Mpera na ujenzi wa Bwawa la Kidunda unaendelea. Aidha, kwa upande wa vijijini, Serikali imeendelea kukarabati na kujenga miradi ya kipaumbele ambayo inatoa huduma kwa wananchi wengi zaidi ikiwa ni pamoja na kuendelea kwa ujenzi wa mradi wa maji wa vijiji 10 kila Halmashauri.

234.      Mheshimiwa Spika, uwekezaji kwenye maeneo haya niliyoyaainisha kwa kiasi kikubwa umeathiriwa na uhaba mkubwa wa fedha. Uhaba huu unatokana na kukasimiwa bajeti ndogo ambayo haikidhi mahitaji ya uwekezaji katika miundombinu ya maji. Fedha inayotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji huwa ni kidogo ikilinganishwa na kiasi kinachokasimiwa. Kwa miaka mitatu mfululizo fedha za maendeleo za ndani zilizotolewa kwa Fungu la Wizara ya Maji zilikuwa ni kidogo kulinganisha na fedha zilizokasimiwa.

235.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/2012, fedha zilizokasimiwa zilikuwa ni shilingi 41,565,045,000 na kiasi kilichotolewa ni shilingi 24,746,549,522 ambayo ni pungufu kwa asilimia 40.5. Kwa mwaka 2012/2013 jumla ya shilingi 140,015,967,000 zilikasimiwa ambapo fedha zilizotolewa zilikuwa ni shilingi 104,000,000,000 ambayo ni pungufu kwa asilimia 25.7; na kwa mwaka 2013/2014, kiasi cha shilingi 312,066,164,000 zilikasimiwa na kiasi kilichopatikana hadi mwezi Machi, 2014 ni shilingi bilioni 86sawa na upungufu wa asilimia 72.4. Jedwali Na. 15 linaonesha mwenendo wa upatikanaji wa fedha za ndani za maendeleo tangu kuanza kwa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.

236.      Mheshimiwa Spika, Serikali hujenga miradi ya maji vijijini na baada ya kukamilika huikabidhi kwa wananchi kwa ajili ya kuiendesha. Uendeshaji na usimamizi wa miradi hiyo umekuwa ni changamoto kubwa kwa maeneo mengi vijijini kutokana na kutokuwa na taaluma na uwezo wa kugharamia matengenezo pindi miradi inapoharibika. Kwa hali hiyo, miradi mingi vijijini imeshindwa kutoa huduma kama ilivyokusudiwa na kupunguza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji safi kwa wananchi. Kukabiliana na changamoto hiyo, Halmashauri zimeelekezwa kuunda na kusajili vyombo vya watumiaji maji kwenye miradi ya maji vijijini ili kuwepo na usimamizi wa karibu katika kuendesha miradi hiyo. Aidha, vyombo hivyo vimejengewa uwezo wa mafunzo kuhusu usimamizi na utunzaji wa fedha zinazotokana na mauzo ya maji; na uendeshaji na matengenezo ya miradi ili kuifanya huduma hiyo kuwa endelevu.

237.      Mheshimiwa Spika, ongezeko la mahitaji ya huduma ya maji halilingani na upatikanaji wa vifaa na vitendea kazi vya kutekeleza miradi ya maji na hivyo, kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati. Kutokana na hali hiyo, Wizara inajadiliana na Wadau mbalimbali walioonesha nia ya kuwekeza kwenye miradi ya maji na usafi wa mazingira ili kutekeleza miradi hiyo kupitia ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partinership - PPP). Hadi sasa usanifu unaendelea kwa miradi ya PPP ikiwemo uvunaji wa maji ya bahari (desalination project) kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam na Handeni Trunk Main - HTM. Katika mwaka 2014/2015, Wizara yangu itaendelea kushawishi wawekezaji wengi zaidi ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji na usafi wa mazingira kupitia PPP.

238.      Mheshimiwa Spika, hatua zinazoendelea kuchukuliwa kukabiliana na uhaba wa fedha ni pamoja na Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha kutafuta fedha zaidi kutoka Washirika wa Maendeleo, na kuhakikisha kuwa fedha zinazokasimiwa zinatolewa kama zilivyopangwa na kwa wakati. Hadi mwezi Machi 2014, Washirika wa Maendeleo wameahidi kuongeza jumla ya Dola za Marekani milioni 73 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Sekta ya Maji. Wizara inaendelea kujadiliana na Washirika wa Maendeleo ili watoe fedha walizoahidi kulingana na makubaliano.

(b)  Kupungua kwa rasilimali za maji

239.      Mheshimiwa Spika, upungufu wa rasilimali za maji nchini ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili Sekta ya Maji na kusababisha maeneo mengi kukumbwa na uhaba wa maji. Miongoni mwa sababu za upungufu huo ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, uvamizi katika vyanzo vya maji kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, uchafuzi wa vyanzo vya maji na matumizi holela ya maji.

240.      Mheshimiwa Spika, athari za mabadiliko ya tabianchi katika rasilimali za maji ni pamoja na kutotabirika kwa urahisi majira ya mwaka na mtawanyiko wa mvua. Hali hii husababisha mvua kunyesha kwa uchache au wingi na hivyo kusababisha maeneo kuwa kame na wakati mwingine kukumbwa na mafuriko. Matukio yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi yanaathiri vyanzo vya maji pamoja na miundombinu yake.

241.      Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Wizara yangu imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo kuwekeza katika ujenzi na uendelezaji wa vyanzo vya maji na kuhifadhi maeneo oevu. Hatua hizo zinalenga kuboresha upatikanaji wa maji kwa kipindi chote cha mwaka. Aidha, Wizara yangu imeandaa mipango shirikishi ya uendelezaji na usimamizi wa rasilimali za maji kwa Bodi za Maji za Mabonde kama njia mojawapo ya kukabiliana na athari za mabadaliko ya tabianchi. Utekelezaji wa mipango hiyo, unahusisha sekta na wadau mbalimbali nchini katika kupanga na kutumia rasilimali za maji kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

242.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeandaa mpango mkakati wa kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Mabadiliko ya Tabianchi ili kutekeleza shughuli za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika Sekta ya Maji. Vilevile, kupitia Jukwaa la Majadiliano ya athari za mabadiliko ya tabianchi katika Sekta ya Maji, Wizara yangu imekuwa ikishirikiana na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali pamoja na wadau wa sekta katika utambuzi wa mbinu za kukabiliana na athari hizo kupitia taarifa za shughuli zinazotekelezwa na wadau hao na tafiti mbalimbali zinazofanyika nchini kuhusiana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye Sekta ya Maji. Pia, Serikali inaendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya teknolojia ya uvunaji na uhifadhi wa maji ya mvua katika ngazi ya kaya ili kuongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi.

243.      Mheshimiwa Spika, uvamizi na uchafuzi wa vyanzo vya maji umechangia kwa kiasi kikubwa upungufu katika vyanzo vya maji nchini. Hali hii imechangiwa na ukosefu wa mipango endelevu ya matumizi bora ya ardhi na hivyo maeneo mengi ya vyanzo vya maji kutumika katika shughuli za uzalishaji mali hususan kilimo. Shughuli hizo zisizozingatia matumizi bora ya ardhi zimesababisha vyanzo vingi kuharibiwa na kuchafuliwa hatimaye kupoteza wingi na ubora wa maji. Vilevile, kumekuwa na matumizi yasiyozingatia vibali vya matumizi vinavyotolewa na mamlaka husika na hivyo kusababisha upungufu wa rasilimali hiyo adimu kwa watumiaji wengine na kusababisha migogoro ya mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini.

244.      Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeendelea kuviimarisha vyombo vya kisheria vya usimamizi wa rasilimali za maji ili viweze kusimamia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa. Vyombo hivyo vinaendelea kutekeleza majukumu yao na kuhakikisha rasilimali za maji zilizopo maeneo husika zinagawanywa na kutumiwa kwa mujibu wa sheria. Aidha, maeneo ya vyanzo vya maji yamebainishwa na utaratibu wa kuyawekea mipaka unaendelea ili kulinda maeneo hayo yasiharibiwe na kuchafuliwa na shughuli mbalimbali za binadamu.

(c)  Kiwango Kikubwa cha Upotevu wa Maji

245.      Mheshimiwa Spika, miongoni mwa changamoto ambazo Mamlaka za maji katika miji mikuu ya mikoa, wilaya, miji midogo pamoja na miradi ya Kitaifa inazokabiliana nazo ni kiwango kikubwa cha upotevu wa maji (NRW). Hali hii inasababisha kutofikiwa kwa malengo ya makusanyo ya maduhuli na hivyo kuathiri utekelezaji wa shughuli za uendeshaji kutokana na uhaba wa fedha. Kwa mamlaka za miji mikuu ya mikoa isipokuwa DAWASCO, makadirio ya kiwango cha maji yasiyolipiwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2011/2012 hadi 2013/2014 yanaonesha mamlaka hizo zinapoteza wastani wa zaidi ya shilingi milioni 30 kwa kila mamlaka kwa mwaka, sawa na asilimia 34.2 ya upotevu wa maji. Kwa upande wa DAWASCO, wastani wa upotevu wa maji kwa kipindi hicho ni asilimia 52 ambapo ni sawa na shilingi bilioni 50. Upotevu huo wa maji unatokana na sababu zifuatazo:-

(i)        Uchakavu wa Miundombinu

246.      Mheshimiwa Spika, mamlaka nyingi za maji bado zina miundombinu ambayo ilijengwa miaka mingi iliyopita, hali hiyo imesababisha miundombinu hiyo kuzidiwa uwezo na msukumo mkubwa wa maji yanayotoka kwenye mitambo na kusababisha kuwepo kwa upotevu mkubwa wa maji. Vilevile, uwekezaji wa miundombinu ya maji katika baadhi ya miradi mipya hususan miradi ambayo uwekezaji wake ulilenga bomba kuu pekee na kuacha miundombinu ya usambazaji. Uwekezaji wa aina hiyo umesababisha mabomba ya zamani ya usambazaji kushindwa kuhimili msukumo mkubwa wa maji kutoka mradi mpya na kusababisha kupasuka mara kwa mara kwa mabomba hayo. Upasukaji huo umeongeza upotevu mkubwa wa maji. Mfano wa matokeo hayo ya uwekezaji ni kwenye mradi mpya wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira, Iringa ambayo upotevu wake wa maji ulifikia asilimia 60 baada ya kukamilika kwa mradi.

247.      Mheshimiwa Spika, Serikali inachukua hatua za kukarabati miundombinu ya maji katika mamlaka mbalimbali na kuhakikisha wakati wa kuanzisha miradi ya uzalishaji maji, usanifu unazingatia mfumo wa mabomba ya usambazaji maji. Vilevile, Wizara imeziagiza mamlaka hizo kuviimarisha vitengo vya matengenezo ili viweze kukarabati mitandao ya maji kwa wakati pindi mivujo inapojitokeza.

(ii)       Wizi wa Maji

248.      Mheshimiwa Spika, upotevu wa maji umeendelea kuwa changamoto kubwa kwenye Mamlaka za maji mijini kutokana na baadhi ya wateja wasiokuwa waaminifu kujipatia huduma ya maji kinyume na taratibu (by-pass, and illegal connection). Aidha, udanganyifu wa wateja kuchezea dira za maji ili kubana matumizi ya maji nao umechangia upotevu huo.

249.      Mheshimiwa Spika, Mamlaka za maji kwa kushirikiana na Manispaa za miji husika zimeweka mikakati ya kufuatilia wizi huo wa maji. Vilevile, Wizara kwa kuzingatia matakwa ya Sheria Na. 12 ya mwaka 2009 ya Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira pamoja na Kanuni zake, inazitaka mamlaka hizo kutumia wanasheria wao na vyombo vingine vya usalama kufuatilia wizi wa maji na hujuma kwenye miundombinu ya maji. Kwa sasa Wanasheria wa Wizara, DAWASA na DAWASCO wanaendelea na taratibu za kuziboresha sheria hizo ili kuzipa nguvu katika utekelezaji wake. Aidha, Kikosi Kazi cha kufuatilia na kubaini wezi wa maji katika Jiji la Dar es salaam kimeundwa na kinaendelea na kazi hiyo kwa ufanisi. Hadi mwezi Machi 2014, jumla ya watu 107 walituhumiwa kuwa ni wezi wa maji na wamefikishwa mahakamani na kesi zao ziko kwenye hatua mbalimbali za kisheria.

(iii)     Hujuma kwenye Miundombinu ya Maji

250.      Mheshimiwa Spika, miundombinu ya usambazaji wa maji na uondoaji majitaka imeendela kuhujumiwa kutokana na kushamiri kwa biashara ya chuma chakavu. Biashara hiyo imeleta athari kubwa katika maendeleo ya Sekta ya Maji ambapo wahujumu hao wamefikia hatua ya kuharibu mitandao ya usambazaji majisafi na majitaka kwa kuiba mabomba ya majisafi, mifuniko ya majitaka, pampu, dira na viungio mbalimbali vya mabomba ya maji na hatimaye kuuza vifaa hivyo kama vyuma chakavu. Kutokana na hujuma hizo, kero ya uhaba wa maji kwa wananchi imeongezeka na pia kusababisha uchafuzi na uharibifu wa mazingira.

251.      Mheshimiwa Spika, hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari juu ya utunzaji wa miundombinu ya maji na kusisitiza ulinzi shirikishi wa miundombinu hiyo. Aidha, Mamlaka zinashirikiana na Sekretarieti za Mikoa, Serikali za Mitaa pamoja na Jeshi la Polisi kudhibiti biashara hiyo ya chuma chakavu. Hatua hiyo imesaidia kukamatwa kwa watuhumiwa na kufikishwa katika vyombo vya Sheria katika Mikoa ya Dodoma, Tabora, Mbeya, Moshi na Dar es Salaam na kesi zao ziko katika hatua mbalimbali za kusikilizwa. Kuanzia mwaka 2010 hadi mwezi Machi, 2014 hasara iliyopatikana kwa Mamlaka za majisafi mijini kutokana na kuibiwa kwa mitandao ya usambazaji maji inakadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 1.5 ambapo DAWASA pekee ni shilingi milioni 700.

(d)  Upungufu wa Wataalam katika Sekta ya Maji

252.      Mheshimiwa Spika, Sekta ya Maji inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wataalam 7,211, unaotokana na Serikali kutoajiri kwa muda mrefu, kuongezeka kwa idadi ya Mikoa, Wilaya, Halmashauri pamoja na kustaafu kwa baadhi ya watumishi. Idadi ya wataalam wanaohitajika kwenye Sekta ya Maji katika ngazi ya Wizara, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri ni 8,749. Wataalam waliopo kwenye Sekta ya Maji ni 1,538. Mchanganuo wa mahitaji ya Wataalam wa kada mbalimbali katika Sekta ya Maji umeainishwa katika Jedwali Na. 16.

253.      Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo, Wizara yangu iliomba kibali cha ajira Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma mwezi Desemba, 2013. Napenda kuwajulisha Waheshimiwa Wabunge kwamba mnamo mwezi Machi, 2014 Ofisi hiyo imetoa kibali cha nafasi 475 kwa ajili ya kuajiri Wahandisi wa maji 125 na Mafundi Sanifu 350 ambao watafanya kazi kwenye miradi ya maji iliyopo kwenye Halmashauri. Hatua za kuajiri wataalam hao zinaendelea kufanywa na Wizara yangu kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira.

254.      Mheshimiwa Spika, usimamizi wa mikataba inayosainiwa na Wakandarasi ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maji inajengwa na kukamilika kwa wakati na kwa  kuzingatia viwango vinavyotakiwa. Hata hivyo, kutokana na upungufu wa wataalam katika Sekta ya Maji, usimamizi wa mikataba hiyo umekuwa hafifu na kusababisha miradi mingi kuchelewa na kwa wakati mwingine, kujengwa chini ya viwango na kutumia gharama kubwa. Katika kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maji, Wizara imewasilisha maombi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili kuajiri kwa mkataba Wataalam wa maji wenye uzoefu kwa ajili ya kuwajengea uwezo Wataalam wapya watakaoajiriwa. Vilevile, baadhi ya wahandisi wazoefu kutoka Wizarani wamehamishiwa kwenye Sekretarieti za Mikoa ili kuongeza uwezo wa usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maji kwenye Halmashauri mbalimbali nchini.

(e)  Upatikanaji wa Taarifa Sahihi na kwa Wakati kutoka kwa Watekelezaji

255.      Mheshimiwa Spika, katika kuratibu utekelezaji wa miradi ya maji kumekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa taarifa sahihi kutoka kwa watekelezaji wa miradi hiyo hususan Halmashauri. Aidha, taarifa hizo zimekuwa hazifiki kwa wakati na hivyo kuchelewesha maamuzi na utekelezaji wa miradi inayofuata. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali imeanza kutumia Mfumo wa Taarifa za Mikataba ya Miradi na Fedha (Management Information System - MIS) ambapo mafunzo maalum yametolewa kwa watekelezaji wa miradi ya maji. Serikali pia, inaandaa mfumo wa kompyuta kwa ajili ya kuweka kumbukumbu za hali ya vituo vya kuchotea maji (water point mapping system) utakaounganishwa kwenye Halmashauri zote kwa ajili ya kuweka na kuboresha kumbukumbu.




(f)   Mawasiliano kati ya Wizara na Wadau wa Sekta ya Maji

256.      Mheshimiwa Spika, kumekuwepo mawasiliano hafifu baina ya Wizara na wadau wengine wanaotekeleza miradi ya majisafi na usafi wa mazingira tangu kuanza kwa awamu ya kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Hali hii inasababisha pamoja na mambo mengine, upatikanaji wa taarifa sahihi kuwa mgumu na ucheleweshaji wa utoaji wa maamuzi ya utekelezaji. Mathalan, kwa kipindi kirefu upatikanaji wa taarifa za matumizi ya fedha za utekelezaji wa Programu zimekuwa hazipatikani kwa usahihi na kwa wakati kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu ya uhakika ya mawasiliano katika baadhi ya maeneo nchini.

257.      Mheshimiwa Spika, vilevile, kutokuwepo kwa mawasiliano ya karibu kati ya Sekta ya Maji na Sekta nyingine imesababisha utekelezaji wa miradi ya maji kukwama au kucheleweshwa kwa muda mrefu. Tumeshuhudia utekelezaji wa miradi kama vile ujenzi wa mabomba makuu ya maji kuchelewa kujengwa kutokana na matakwa ya kuomba vibali vya kukatiza katika hifadhi za barabara na zuio za kimahakama. Vilevile, upatikanaji wa vibali au kumalizika kwa kesi za mahakama kunachukua muda mrefu na hivyo kuathiri utekelezaji wa miradi ya maji kukamilika katika muda uliopangwa. Hali hiyo mara nyingi inawavunja moyo wananchi kwa kukosa huduma ya maji pamoja na Washirika wetu wa maendeleo wanaochangia miradi ya maji, hivyo kupunguza michango yao ya uwekezaji katika Sekta ya Maji.

258.      Mheshimiwa Spika, vilevile, kumekuwepo na mawasiliano hafifu na wadau wengine wanaotoa mchango wa kuendeleza utoaji wa huduma ya maji ikiwa ni pamoja na Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Mashirika ya Dini na Watu Binafsi. Upungufu huo umesababisha Wizara kukosa taarifa za miradi ya maji inayotekelezwa na wadau hao ili kujua hali halisi ya huduma ya upatikanaji wa maji kwenye maeneo husika.

259.      Mheshimiwa Spika, hatua zinazochukuliwa katika kukabiliana na changamoto hiyo ni pamoja na kuimarisha mawasiliano na wadau hao kwa kuwashirikisha katika vikao mbalimbali vinavyojadili masuala ya Sekta ya Maji ili kubadilishana uzoefu na kupanga mikakati ya pamoja kukabiliana na changamoto zilizopo. Aidha, Wizara inaendelea kuboresha Mfumo wa Menejimenti ya Taarifa na Takwimu za Sekta ya Maji. Mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati.



260.      Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyofikiwa katika kuendeleza Sekta ya Maji yametokana na michango inayoendelea kutolewa na Wadau mbalimbali, hivyo napenda sasa kutumia fursa hii kuwashukuru wale wote waliochangia na kutuwezesha kufanikisha majukumu ya sekta. Naamini kuwa mafanikio yaliyopatikana katika mwaka 2013/2014 ni kutokana na jitihada za pamoja, ushirikiano na misaada ya kifedha na kitaalam kutoka kwa Washirika wa Maendeleo, ikiwa ni pamoja na nchi wahisani, mashirika ya misaada ya kimataifa, taasisi zisizo za kiserikali, mashirika ya kidini na taasisi za kifedha. Napenda kuzishukuru nchi rafiki zikiwemo Serikali za Ujerumani, Uholanzi, Uingereza, Marekani, Japan, Ufaransa, China, Uswisi, Ubeligiji, Ireland, Korea ya Kusini, Sweden, Denmark, Norway, India na Misri.

261.      Mheshimiwa Spika, napenda pia, kuzishukuru taasisi za fedha za kimataifa na mashirika ya kimaendeleo kwa misaada ya fedha na ushirikiano wa kitaalam katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu na malengo ya Wizara yangu. Taasisi hizo ni pamoja na:- Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), Benki ya Maendeleo ya Ufaransa (AFD), Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya (EIB), Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Afrika (BADEA), Mfuko wa Maendeleo wa Nchi Zinazozalisha Mafuta (OPEC Fund for International Development-OFID), Mfuko wa Maendeleo wa Saudia (SFD), Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC), Shirika la Misaada ya Maendeleo la Norway (NORAD), Taasisi ya Maendeleo ya Uingereza (DFID), Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo (UNDP), Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA), Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Makazi Duniani (UN HABITAT), Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Misaada ya Maendeleo la Sweden (SIDA), Shirika la Misaada ya Maendeleo la Canada (CIDA), Shirika la Misaada ya Maendeleo la Denmark (DANIDA), na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).

262.      Mheshimiwa Spika, aidha, michango ya mashirika ya kidini imeongeza hamasa katika kuyafikia malengo tuliyojiwekea. Hivyo, napenda kuyashukuru mashirika hayo ya kidini ambayo ni:- World Islamic League, Shirika la Ahmadiya Muslim Jamaat Tanzania, Islamic Foundation, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Kanisa la Kilutheri la Ujerumani, Baraza Kuu la Waislam Tanzania, Kanisa Katoliki Tanzania, Kanisa la Kianglikana Tanzania, Catholic Agency for Overseas Aid and Development (CARITAS), Adventist Development Relief Agency (ADRA), Norwegian Church Aid na Livingwater International. Pia, nazishukuru taasisi zisizo za kiserikali za Tanzania Water and Sanitation Network (TAWASANET); Wahamasishaji wa Maji, Maendeleo na Afya (WAMMA); Southern Highlands Participatory Organizasition (SHIPO); WaterAid; World Vision; Plan International; Concern Worldwide; Netherlands Volunteers Services (SNV); Shirika la Kimataifa la Kuhifadhi Uasili na Mali Asili (IUCN); World Wide Fund for Nature (WWF); African Medical Research Foundation (AMREF); Clinton HIV Aids Initiative (CHAI); Bill and Melinda Gates Foundation; na wale wote ambao wameendelea kuisaidia Wizara ya Maji kufanikisha malengo yake.

263.      Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee kabisa naomba nitumie fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati kwa Mhe. Amos Gabriel Makalla (Mb), Naibu Waziri wa Maji; Mhandisi Bashir Juma Mrindoko, Katibu Mkuu; Mhandisi Mbogo Futakamba, Naibu Katibu Mkuu; Wakurugenzi wote na Wakuu wa Vitengo; Maafisa na Watendaji Wakuu wa Mashirika, Wakala na Taasisi zilizo chini ya Wizara yangu; na Wataalam na Watumishi wote kwa ushirikiano wanaonipatia pamoja na kujituma kwao katika kusimamia utekelezaji wa majukumu tuliyopewa.

264.      Mheshimiwa Spika, Napenda nimshukuru sana Mhe. Dr. Mhandisi Bilinith Saatano Mahenge (Mb) na ambaye tulianza kazi hii ya kuwapelekea maji watanzania kwa nguvu mpya.  Leo ninayo furaha kumpongeza Dr. Binilith S. Mahenge (Mb) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira). Napenda pia nimshukuru aliyekuwa Katibu Mkuu, Mhandisi Christopher Nestory Sayi ambaye amestaafu kwa heshima. Ni matumaini yangu kuwa huko waliko kwa sasa wataendelea kuwa mabalozi wazuri wa Sekta ya Maji.



265.      Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 520,906,475,000 kwa ajili ya matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka 2014/2015, ili Wizara iweze kutekeleza majukumu na malengo yaliyoelezwa katika hotuba hii. Kati ya fedha hizo, Matumizi ya Kawaida ni shilingi 30,899,443,000 ambapo shilingi 15,384,999,000 ni Mishahara ya Watumishi (PE), na shilingi 15,514,444,000 ni fedha za Matumizi Mengineyo (OC). Jumla ya Bajeti ya Maendeleo ni shilingi 490,007,032,000 ambapo kati ya fedha hizo shilingi 312,066,164,000 ni fedha za ndani na shilingi 177,940,868,000 ni fedha za nje.

266.      Mheshimiwa Spika, naomba tena nitoe shukurani zangu kwako na kwa Waheshimiwa Wabunge kwa kunisikiliza. Hotuba hii pia inapatikana katika Tovuti ya Wizara kwa anwani: www.maji.go.tz.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

5 comments:

Anonymous said...

What's up to every body, it's my first go to see of this web site; this weblpog
contains remarkable and genuinely fine data
designed for readers.

Anonymous said...

Woah! I'm really enjoying the template/theme of this blog.
It's simple, yet effective. A lot of times it's tough to get that "perfect balance" between superb usability and visual appeal.
I must say that you've done a very good job with this.

In addition, the blog lkads super quick for me on Chrome.
Outstanding Blog!

Anonymous said...

Thanks a bunch for sharing this with all people you really recognise what you're
speaking about! Bookmarked. Kindly also seek adviuce from
my website =). We could have a link trade arranggement among us

Anonymous said...

Heya i'm for the first time here. I found this board and I find It really useful & it helped me out a lot.
I hope to gijve something back and aid others likke
you aided me.

Anonymous said...

whoah this weblog is fantastic i really lik studying your posts.
Keep upp the great work! You realize, a llot off persons are looking around for this info, you could help them greatly.