WAZIRI ASEMA BAJETI NISHATI NA MADINI NI YA UPENDO NA UPOLE


Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini imetajwa kuwa ya upendo na ya masikini, huku ikionesha mafanikio makubwa ikiwamo kuvuka lengo la kuwapatia umeme Watanzania wengi kabla ya muda uliowekwa na kutoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo. 
Aidha, Waziri Profesa Sospeter Muhongo amesema hakuna kushindwa wala kukata tamaa na hawatarudi nyuma katika kutafuta ufumbuzi na changamoto mbalimbali zinazoikabili wizara hiyo. 
Akiwasilisha bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2014/15 juzi usiku bungeni, Profesa Muhongo pia amebainisha kuwa Watanzania wanamiliki asilimia 70 ya leseni za madini wakati wageni wakimiliki asilimia 25. 
Kuhusu umeme, alisema kiwango cha uunganishaji umeme mijini kimeongezeka na kufikia asilimia 24, Machi mwaka huu, baada ya uwezeshwaji wa Mfuko wa Umeme Vijijini (REA). 
Aidha alisema katika mwaka 2013/14, hali ya upatikanaji wa umeme ulikuwa ya kuridhisha ambapo hapakuwa na mgawo wowote kama alivyoahidi mwaka 2012/13. 
“Hadi mwishoni mwa mwezi Aprili 2014, uwezo wa mitambo yote ya kufua umeme (total installed capacity) ulifikia megawati 1,583. 
“Uwezo huu mpya ni sawa na ongezeko la asilimia 78 ikilinganishwa na megawati 891 zilizokuwepo mwaka 2005 wakati Serikali ya Awamu ya Nne inaingia madarakani. Hili ni jambo la kujivunia kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi,” alieleza. 
Alisema mbali ya kutekeleza miradi mikubwa ya kufua umeme, Serikali imeanza kutekeleza miradi mikubwa yenye uwezo wa kusafirisha umeme mwingi kwenye umbali mrefu. 
Aliitaja ni Mradi wa Iringa – Shinyanga (kv 400), Mradi wa Makambako – Songea (kv 220), Mradi wa North East Grid (kv 400), Mradi wa North West Grid (kv 400), Mradi wa Singida – Arusha – Namanga (kv 440). 
Mengine ni Bulyanhulu – Geita (kv 220), Mradi wa Electricity V, Mradi wa Kuboresha upatikanaji wa umeme jijini Dar es Salaam, Mradi wa ufuaji na Usambazaji Umeme – Biharamulo, Mpanda na Ngara. 
Kuhusu miradi ya REA, alisema kwa miradi hiyo awamu ya pili, gharama za kuunganisha umeme ni Sh 27,000 tu, na kwamba kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, gharama ya kuunganisha itaendelea kuwa Sh 99,000 hadi Juni mwakani. 
Akizungumzia miundombinu ya gesi, alisema hadi kufikia Mei mwaka huu, ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Songo Songo kupitia baharini hadi Somanga Fungu lenye urefu wa kilometa 25.6, umekamilika kwa asilimia 100. Kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia na mafuta, alisema Serikali iliidhinisha Sera ya Gesi Asilia, Oktoba mwaka jana na kuwa Muswada wa Sheria ya Gesi Asilia utapelekwa bungeni Novemba mwaka huu. 
“Sera ya Uwezeshaji na Ushirikishaji Wazawa (Local Content Policy) itakamilika ifikapo Desemba 2014. Lengo kuu la sera ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanashiriki ipasavyo katika shughuli zote za rasilimali za gesi asilia na mafuta kwa manufaa ya Watanzania wote bila upendeleo au ubaguzi wa aina yoyote,” alisema waziri huyo. 
Akizungumzia uchimbaji mdogo wa madini, alisema Aprili mwaka huu, Waziri Mkuu alikabidhi hundi zenye thamani ya Sh milioni 88 kwa miradi 11 ya wachimbaji wadogo iliyokidhi vigezo vya kupata ruzuku. 
“Ili kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa mitaji na mikopo, Wizara imetenga shilingi bilioni 2.50 katika mwaka wa 2014/15 kwa ajili ya mikopo yao,” alifafanua. 
Alisema kumejengeka dhana kwamba wawekezaji wageni wanamiliki maeneo mengi na makubwa kuliko Watanzania, na Serikali haijachukua hatua ya kuwawezesha wazawa kushiriki kikamilifu. 
“Ukweli ni kwamba, Watanzania wanamiliki asilimia 70 ya leseni za madini, wageni asilimia 25 na asilimia tano ya leseni hizo zinamilikiwa kwa ubia kati ya Watanzania na wageni,” alibainisha Profesa Muhongo na kuongeza kuwa yeye na “timu yake ya ushindi, hakuna kushindwa, hakuna kukata tamaa.”

No comments: