'MTOTO WA BOKSI' BADO APUMUA KWA MSAADA WA MASHINE MUHIMBILI


Mtoto wa miaka minne aliyekuwa amefichwa kwenye boksi mkoani Morogoro, bado anaendelea kutumia mashine ya kupumua baada ya kushindwa kupumua vizuri. 
Hali hiyo imesababishwa na maradhi ya kichomi yanayomsumbua.
Akizungumza na mwandishi, jana jijini Dar es Salaam, mama mlezi aliyekabidhiwa jukumu hilo Josephina Joel alisema, hali ya mtoto huyo ilibadilika Mei 21 jioni, hali iliyowafanya madaktari waliokuwa zamu kumsaidia kwa kumuwekea mashine ili aweze kupumua.
Alisema hali yake hivi sasa sio mbaya, ingawa anatumia mashine kumsaidia kupumua, lakini pia bado anaendelea na tiba ya awali ya lishe ambayo anaipata katika wodi aliyolazwa ya Makuti B, ya watoto wenye utapiamlo.
“Tulihamishiwa hapa juzi jioni, baada ya baadhi ya majibu ya vipimo vya awali kutoka ambapo yanaonesha mtoto hali yake kilishe ni  duni, hivyo tukaletwa hapa ili apatiwe lishe na wataalamu, na ameshaanza kupewa,” alisema Josephina.
Hivi sasa mtoto huyo ameanzishiwa lishe ya maziwa peke yake ambapo kila baada ya saa mbili hupewa maziwa hayo na kwamba hicho kwa sasa ndicho chakula chake hadi wataalamu hao watakavyoelekeza vingine.

Josephina aliongeza, maziwa hayo kwa mujibu wa wataalamu wa afya na lishe yana virutubisho vyote muhimu vinavyohitajika kutibu tatizo la utapiamlo mkali unaomkabili mtoto huyo.
Akizungumzia hatua walizofanya hadi sasa, daktari bingwa wa magonjwa ya watoto hospitalimi hapo, Dk Mwajuma Ahmada alisema walichofanywa kwanza ni kumhamishia kwenye wodi hiyo ya watoto wenye utapiamlo, ambapo wapo wataalamu wa lishe wanamhudumia.
Kuhusu majibu ya awali ya damu, mama mlezi  wa mtoto huyo alisema majibu ni mazuri na kwamba jana , watamfanyia kipimo cha kumulikwa mwili wote na mashine kwa uchunguzi zaidi.
Mtoto huyo aliibuliwa na majirani waliotoa taarifa katika ofisi ya serikali ya mtaa eneo la Azimio, Morogoro baada ya kuhisi kwamba kuna sauti ya mtoto ndani ambaye hawajawahi kumuona katika familia ya mpangaji  Mariam Saidi na mumewe, Mtonga Ramadhan.
Baada ya mtoto huyo kuibuliwa akiwa katika hali ya uchafu alipelekwa hospitali ya mkoa ya Morogoro kwa ajili ya uchugnuzi wa afya yake, huyo watuhumiwa wa ukatili dhidi ya mtoto huyo, akiwemo baba mzazi Rashidi Mvungi, na  walezi hao, wakishikiliwa na hatimaye kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu mashtaka yanayowakabili ya ukatili.
Imadaiwa mama  mzazi wa mtoto huyo alifariki mtoto akiwa na umri wa miezi tisa na hivyo dada wa marehemu akakubali jukumu la kumlea mtoto huyo.

No comments: