Walimu wanne wa shule ya Sekondari Kindai,
Manispaa ya Singida wametakiwa kuhama mara moja.
Wamepewa agizo hilo baada ya kukiri kuwa
walitoa adhabu ya udhalilishaji kwa wasichana wote wa shule hiyo, kwa madai
kuwa mmoja wao alitupa chooni taulo ya kike
iliyotumika.
Walimu waliohusika na mkasa huo na kukumbwa
na tamko hilo ni Hadija Mussa, Sara Kabogo, Evodia Zablon na Elina Mathias
ambao walikiri kutenda kosa hilo na kuahidi kutorudia tena.
Walimu hao walikiri kutenda makosa hayo mbele
ya mkutano wa dharura wa wazazi, ambao
pia ulihudhuriwa na Ofisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Singida, Omari Kisuda.
Wazazi hao walifikia uamuzi huo, baada ya
walimu hao kukiri kuwa kitendo walichokuwa wamekifanya kwa wasichana wa kidato
cha kwanza hadi cha nne, kilikuwa ni kinyume cha sheria na ilikuwa ni
udhalilishaji wa watoto wa kiwango cha juu.
Kwa mujibu wa walimu hao, walilazimika kutoa
adhabu hiyo baada ya kukuta mmoja wa wanafunzi wa kike wa shule hiyo, akiwa
ametupa taulo hilo ovyo chooni. Tukio
hilo ni la Mei 22, mwaka huu.
Ilidaiwa kwenye kikao hicho kuwa baada ya
kuikuta taulo hiyo ndani ya choo, walimu hao waliamuru wanafunzi wailoweke
kwenye ndoo ya maji ya lita 20 hadi maji yote, yaenee rangi ya damu iliyokuwa
kwenye taulo hilo.
Hapo ndipo, wanafunzi walipopangwa mstari na kuanza kuchapwa viboko
16 kila mmoja kwenye viganja vya mikono yao, kisha kunawishwa kwa nguvu maji
hayo yaliyokuwa na uchafu wa damu ya taulo hiyo iliyotumika, iliyochanganyikana
na uchafu wa chooni.
Inadaiwa kuwa baada ya kitendo hicho
kufanyika, wanafunzi hao waliagizwa kurudi kwao na kwamba wakale chakula bila
kunawa mikono yao.
No comments:
Post a Comment