Wakazi ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa
kushirikiana na manispaa za Dar es Salaam, zitaanza kampeni ya kukagua maeneo
ya makazi ya watu yenye vichaka.
Vichaka hivyo ni vile vinavyofanya mbu wa
kueneza ugonjwa wa homa ya dengue, kuzaliana.
Watu hao watatozwa faini za papo hapo na nyumba zao zitafanyiwa usafi.
Akizungumza na mwandishi jana, Ofisa
Ufuatiliaji wa Magonjwa wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alex Mkamba alisema kampeni
hiyo inatarajia kuanza hivi karibuni.
Alisema watafanya ukaguzi katika makazi ya
watu na shule na lengo ni kukabiliana na homa ya dengue, inayozidi kushika
kasi.
“Tunaanza kampeni ya kukagua maeneo ya watu,
ambayo hayajafanyiwa usafi yanayosababisha mbu kuzaliana na tutashirikiana na
Manispaa zote za jiji,” alisema Mkamba.
Alisema watatoza faini shule ambazo hazijatoa
elimu kwa wanafunzi wao juu ya homa ya
dengue, ambayo imekuwa tishio katika jiji la Dar es Salaam.
Akielezea hali ya ugonjwa huo, alisema jana
wagonjwa wapya 39 walikutwa na ugonjwa huo, ambapo waliolazwa ni 20 na wako
katika Hospitali za Temeke, Amana na Mwananyamala.
“Hivi karibuni hakuna mtu aliyekufa kutokana
na ugonjwa wa dengue na hiyo ni kutokana na kwamba wanafika hospitali mapema
kabla ya kufikia katika hatua ya pili ambayo mgonjwa anakuwa ameshaharibika ini
na figo na hivyo kutokwa damu nyingi, kukojoa na kuharisha damu, tunajitahidi
kutoa elimu,” alisema Mkamba.
Alisema tangu ugonjwa huo ulipuke katika jiji
la Dar es Salaam, watu 2,247 walipimwa ambapo 1,014 walikutwa wamepata homa ya
ugonjwa huo. Wilaya ya Kinondoni inaongoza kwa kuwa na wagonjwa
wengi.
Mpaka sasa ugonjwa huo, hauna tiba maalumu
wala chanjo. Njia pekee ya kukabiliana nao ni kutambua dalili zake kama vile
homa, kupungukiwa maji au damu, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu.
Mgonjwa anaweza kupoteza maisha, endapo
atachelewa kupatiwa matibabu. Wananchi wanatakiwa kuchukua hadhari juu ya
ugonjwa wa dengue, ambao dalili zake ziko sawa na zile za malaria.
No comments:
Post a Comment