Tume ya Uchaguzi nchini Malawi (MEC) imesema Uchaguzi Mkuu wa Rais, ulikuwa
huru na wa haki, ingawa Rais alifuta
uchaguzi huo.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo,
Maxon Mbendera.
“Uchaguzi Mkuu wa Urais nchini Malawi
ulifanyika kwa uhuru, haki na namna ya uaminifu ingawa kulikuwa na makosa,”
alitangaza wakati Wamalawi katika maeneo mbalimbali, wakikesha ili kupokea
matokeo ya uchaguzi huo.
"Kwa raha naweza kusema uchaguzi ulikuwa
wa uhuru na wa haki…pia ulikuwa wazi, kwa tathmini yangu, ulikuwa wa
kuaminika,” alisema Mbendera.
Uchaguzi Mkuu huo ulileta utata na maswali,
baada kugundulika mambo yasiyokuwa ya kawaida katika kwenye vituo vya kupigia
kura 4,000.
Mwenyekiti huyo wa Tume alisema asilimia 99
ya upigaji kura, ulikuwa hauna matatizo na kuwa watu walionesha mapenzi yao.
Matatizo na mivutano hiyo, imesambaa hadi
mahakamani, ambapo mgombea urais wa Chama cha upinzani cha Malawi Congress
Party (MCP), Lazarus Chakwera alitaka kura hizo zirudiwe.
Lakini, Chama cha Democratic Progressive
(DPP) kinachoongozwa na Profesa Peter Mutharika, aliyekuwa akiongoza katika
matokeo ya awali, kiliungana na mawakili wa Tume ya Uchaguzi, kuzuia kuongezwa
siku 30 za kuhesabu kura.
Tume hiyo ilisema inaendelea kujiandaa
kutangaza matokeo ya Urais. Iliahidi kuwa ingetangaza matokeo hayo ya urais
jana na hiyo ni kwa mujibu wa Sheria, labda kama kungetokea zuio la mahakama.
“Chochote kitakachoelekezwa na mahakama,
tutafanya,” alisema Mbendera. Kwa mujibu wa Sheria, tume hiyo inalazimika
kutangaza matokeo katika kipindi cha siku nane za uchaguzi na mwisho wa siku
hizo, ilikuwa ni mchana wa siku ya jana
(Ijumaa).
Juzi Alhamisi, kesi iliyokuwa imefunguliwa
mahakamani, ilikwama baada ya jaji aliyekuwa amechaguliwa kusikiliza, Healy
Potani, alijitoa kwa sababu kaka yake ni
mjumbe wa tume ya uchaguzi. Jaji
mwingine, Kenyatta Nyirenda, alichaguliwa kuchukua nafasi hiyo na alitarajiwa
angetoa uamuzi wake jana.
Mahakama Kuu ilitarajiwa itoe uamuzi Ijumaa,
ambao ungewezesha Tume ya Uchaguzi, kutangaza matokeo uchaguzi huo uliopigwa
Mei 20, mwaka huu au kuna haja ya kurudia kuhesabu kura zote zilizopigwa, hatua
ambayo itachukua miezi miwili.
Kwa upande wake, Rais wa Malawi, Joyce Banda alisema siku ya
Alhamisi, kuwa angekuwa tayari kuondoka madarakani, kama Mahakama Kuu ingetoa uamuzi wake
kumaliza mgogoro huo wa uchaguzi.
Rais Banda alisema bado anaamini kuwa
uchaguzi huo, ulifanyika katika mazingira ya ulaghai. Rais alidai uchaguzi huo,
ulikuwa ‘batili na haukuwa wa uwazi’, kwani ulikuwa umegubikwa na mambo mengi
yaliyokuwa sio ya kawaida. Aliagiza uchaguzi huo urudiwe upya ndani ya siku 90.
Hata hivyo, juzi, Rais Banda alisisitiza
kuwa "Nimeiambia MEC na wadau
husika, kuwa nitakubali maamuzi ya Tume hiyo na uamuzi wa mahakama,”
Matokeo ya awali yalionesha kuwa mpinzani wa
Banda, ambaye ni Profesa Mutharika, alikuwa anaongoza. Rais Joyce Banda alikuwa
anafuatia.
Wapo wagombea wengine katika uchaguzi huo ni
pamoja na Atupele Muluzi, ambaye ni mtoto wa Rais wa zamani, Bakili Muluzi.
No comments:
Post a Comment