Habari zilizopatikana
hivi punde zinasema, wabunge wanaounda kambi ya rasmi ya upinzani Bungeni wamesusia
mjadala unaoendelea jioni hii kwa kile walichodai kuwa mkakati uliopangwa na
wenzao wa CCM kujaribu kufunika madudu yaliyogubika ufujaji wa fedha za IPTL.
Akizungumza muda mfupi
kabla ya kutoka nje ya Bunge, Kiongozi wa kambi hiyo, Freeman Mbowe alisema
kuna kila dalili kwamba wabunge wa CCM walishakaa kikao kabla ya kuanza
kujadili Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwamba wahakikishe
wanasambaratisha kila hoja inayohusiana na suala zima la kampuni ya ufuaji
umeme ya IPTL.
Mbowe alimshutumu Spika
na wabunge wa CCM kujaribu kufifisha hoja za wapinzani waliosisitiza kutaka
suala hilo lijadiliwe kwa kina na bila kutanguliza misimamo ya vyama vyao.
“Mheshimiwa Spika, humu
ndani ni dhahiri kuna wabunge tayari wameingia na misimamo ya vyama vyao bila
kujali suala hili ni zito sana kwa mustakabali wa taifa letu. Najua humu ndani
mpo wengi kuweza kupitisha msimamo wenu kuhusu suala hili, lakini najua
mtahukumiwa huko nje siku moja mbeleni,” alisema Mbowe.
Akahitimisha kwa kusema, “Ili
tuwe na amani, naomba tuwaache muendelee kujadili wenyewe (CCM) suala hili kwa
amani kabisa.”
Kauli hiyo ikazusha
kelele kutoka kwa wabunge wanaomanika kuwa wa chama tawala cha CCM wakirusha
maneno ya kejeli wakati wabunge wa kambi
ya upinzani wakitoka nje ya bunge majira ya Saa 10:30 jioni hii.
Mapema kabla, Waziri
Kivuli wa wizara hiyo, John Mnyika akisoma Bajeti Mbadala ya kambi hiyo
alielekeza shutumu nzito dhidi ya ufisadi uliokithiri kwenye suala zima la
fedha ilizolipwa IPTL, ambapo alimwomba Spika wa Bunge, Anne Makinda kuunda
kamati maalum ya Bunge kuchunguza suala hilo.
Wabunge wa kambi
rasmi ya upinzani wanatoka katika vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi.
No comments:
Post a Comment