SERIKALI YAMTAKA BALOZI WA UINGEREZA AJIPIME MWENYEWE



Serikali imemtaka Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Malrose ajipime kama anafaa kuendelea kuiwakilisha nchi yake, na kuagiza nchi yake kumwondoa mara moja.
Ametakiwa afike mara moja katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kujieleza.
Anatuhumiwa kuihujumu Tanzania kwa kushiriki katika vitendo kinyume cha maadili na Mkataba wa Vienna kuhusu masuala ya kidiplomasia.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele alitangaza hayo jana bungeni wakati alipochangia hoja ya bajeti ya mwaka 2014/15 ya wizara hiyo.
Kwa mujibu wa Masele, Balozi huyo amekuwa akifanya vitendo vya kuongoza vikao vya kuihujumu Tanzania kutokana na suala la IPTL.
“Kuna ushahidi kuwa amekuwa akiendesha vikao mbalimbali Dar es Salaam na Dodoma. Upo ushahidi wa vitendo hivyo vinavyokwenda kinyume cha maadili,” alisema.
Alisema balozi huyo amekuwa akishinikiza nchi wahisani wa maendeleo kukataa kuipa Tanzania fedha za maendeleo kutokana na suala hilo.
Alisema balozi huyo amekuwa wakala wa Benki ya Standard Chartered, kwa kutaka Serikali ya Tanzania ilipe fedha kutokana na mgogoro wa kampuni binafsi.
“Ni aibu kwa Serikali ya Uingereza ya Waziri Mkuu David Cameroon kwa Balozi wake kufanya uwakala wa Benki ya Standard Chartered kuishawishi Serikali ikope fedha ili kulipa madeni ya kampuni binafsi, jambo ambalo Rais amelikataa kwa nguvu zote.
“Tunampongeza Mheshimiwa Rais Kikwete kwa msimamo wa kizalendo na kuipenda nchi yake,” alisema Masele na kuongeza: “Chini ya Mkataba wa Vienna, huu ni uchochezi, kuvuruga amani na kutoheshimu nchi nyingine na kufanya ujasusi,” alisema Masele na kuongeza:
“Serikali inamtaka ajipime kama anafaa kuendelea kuiongoza nchi yake. Uingereza inapaswa kumchukulia hatua. Serikali inamtaka afike katika Wizara ya Mambo ya Nje mara moja.
“Tunaitaka Serikali ya Uingereza ichunguze tuhuma hizi dhidi ya Balozi wake na ichukue hatua mara moja ili kuepuka madhara zaidi ya kidiplomasia yanayoweza kukuzwa zaidi kwa kuwepo kwa Balozi huyo.”
Alisema suala la IPTL ni lazima taratibu zifuatwe na kwamba haiwezekani kulipia kampuni binafsi, na kuwa Tanzania inapaswa kuheshimiwa.
“Tanzania ni nchi huru, lazima iheshimiwe, na hatutasita kuchukua hatua kwa yeyote anayekwenda kinyume na utaratibu na sheria,” aliongeza Masele.
Naibu Waziri amekuwa akiishawishi Marekani kukatiza misaada yake kwa Tanzania, hivyo kutaka kuidhoofisha nchi kiuchumi.
Alisema Marekani ina miradi mingi ya maendeleo nchini, ikiwamo ujenzi wa barabara katika mikoa kadhaa, ikiwamo Tanga, Ruvuma na Zanzibar.
Kauli yake imekuja baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR –Mageuzi), kudai katika mchango wake bungeni asubuhi kuwa Balozi huyo amekuwa mstari wa mbele kutaka ukweli wa IPTL.

No comments: