MBUNGE LUGOLA ATAKA BUNGE LISITUMIWE NA MAFISADI


Wabunge wamemkingia kifua Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na watendaji wake, huku mmoja akilitaka Bunge likatae kutumiwa na wafanyabiashara na mafisadi. 
Katika mjadala wa hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/15 Bunge jana, wabunge wamesifu utendaji wa Muhongo na wasaidizi wake na pia mafanikio katika sekta hizo mbili muhimu. 
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), hakutafuna maneno na kueleza kuwa Bunge linapaswa kuachwa kutumiwa na wafanyabiashara na mafisadi, na kuwaonya wenzake kuacha kuwaghilibu wananchi. 
“Niliwahi kusema kuwa Muhongo ndiyo gate valve (vali ya lango) ya kupambana na mafisadi ndani ya Tanesco. Amewabana mafisadi. Sasa hawa ndio wanaotuletea matatizo ndani ya Bunge. 
“Acheni kuwaghilibu watu, acheni nongwa. Kwa nini Bunge hili kila mara Nishati na Madini, kuna nini Nishati na Madini,” alihoji. 
Lugola na kuongeza: “Wabunge tukatae kutumika, Bunge hili tukatae kutumiwa na wafanyabiashara na mafisadi.” 
Aliwashangaa wabunge ambao wamekuwa wakidai kuwa wao ni wanaCCM halisi, lakini wanayumba na ghafla wamegeuka kuwa wapiga kelele wa ajabu. 
“Wabunge lazima tuheshimu kanuni, hapa kuna Kamati ya Kudumu ya Bunge imeagiza Takukuru na CAG kufanya uchunguzi suala la IPTL, leo tunataka sisi iundwe Kamati Teule, ya nini? Hatuiamini kamati yetu wenyewe ya Bunge tuliyoipa madaraka? 
“Halafu wanakuja watu hapa na makaratasi ya kufungia maandalizi wanadai wana ushahidi. Kama una ushahidi si upeleke Takukuru au kwa CAG? Halafu ninyi mna ujuzi gani wa kutambua hili? Hizo ni photocopy tu. 
“Watu wenyewe ukiwauliza Escrow hawajui ni nini? Zile siyo fedha za umma, zilikuwa fedha za IPTL. Acheni kughilibu watu. Ushahidi gani wa uongo na unafiki,” alisema Lugola na kushangiliwa na wabunge wengi. 
Alimvaa mbunge mwenzake wa CCM, Christopher ole Sendeka (Simanjiro), akimshangaa kupiga kelele za kushabikia suala hilo la IPTL na Escrow. 
Alisema ni vyema suala hilo likachunguzwa na Takukuru na CAG kama ilivyoagiza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na kuahidi ukibainika ufisadi, atashughulika na watendaji wa wizara kuanzia Muhongo na naibu mawaziri wake. 
Katika mchango wake, Sendeka alikataa kuunga mkono hoja hiyo, akisema anataka maelezo ya suala hilo la IPTL na kitalu C katika migodi ya tanzanite. 
Kwa upande wake, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango (CCM), pamoja na kusifu kazi nzuri ya wizara ikiwamo kusambaza umeme,alimtetea Muhongo na suala la kujali wazawa katika masuala ya gesi. 
Alisema Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini ilikutana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TSPF) chini ya Reginald Mengi, na kuzungumza kwa kina kuhusu ushirikishwaji wa wazawa. 
“Wabunge hamjafahamu suala la gesi vizuri. Sisi tulikutana na watu wa sekta binafsi, alikuwapo Mengi na kina Simbeye, na tulizungumza vizuri na kukubaliana kama kuna tatizo warudi kwetu. Lakini hawajarudi. 
  “Msilalamike huko nje. Ugomvi uko wapi? Hamna. Katika gesi sisi hatutaki madalali, mtu anahodhi vitalu halafu anauza,” alisema Kilango.  Kwa upande wake, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), alimkingia kifua Muhongo na wenzake, akisema duniani kote, kufanya kazi ya kupinga ni rahisi sana, lakini ukweli ni kuwa wizara imefanya kazi nzuri. 
Alisema hakuna anayeweza kumng’oa Muhongo, na kusisitiza maeneo ambayo yameachwa nyuma katika huduma muhimu, yapewe kipaumbele. 
Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM), alisema asingependa kuzungumzia suala la IPTL kwa sababu amekuwa wakili wa Serikali kwa miaka 15 na maadili ya kazi yao yanamkataza kufanya hivyo. 
Lakini, aliweka wazi kuwa hana ugomvi na Profesa Muhongo, isipokuwa watu wanatengeneza maneno yao na kushukuru kwa suala la Buhemba kumalizwa. 
Yussuf Salim Hussein wa CUF mbali ya kupongeza kazi nzuri ya Wizara, alisema tatizo kubwa katika suala la IPTL ni makampuni makubwa yanagonganisha na hivyo kuleta mzozo usiokwisha. 
Hoja yake iliungwa mkono na Hamad Rashid Mohammed (Wawi – CUF), aliyependekeza suala hilo limemalizwa sasa kwani la muda mrefu. 
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), aling’ang’ania suala hilo liundiwe Tume ya Bunge na akasema anao ushahidi wa jambo hilo. 
Kafulila pamoja na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), waliagizwa na Spika Anne Makinda, kuwasilisha mezani ushahidi wao katika suala hilo. 
“Leteni ushahidi mezani sio kusema sema tu. Tena muweke signature na tugonge mihuri,” alisema Spika wakati akiahirisha kikao asubuhi. 
Wabunge wengi waliochangia mjadala huo waliisifu wizara na Serikali kwa ujumla kwa kuwapatia wananchi wengi umeme, kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwapa ruzuku, lakini wakisisitiza fedha za Mfuko wa Umeme Vijijini (REA), zitolewe haraka. 
Profesa Muhongo aliwasilisha bajeti yake juzi usiku, na kuliomba Bunge liidhinishe Sh trilioni 1.08. 
Hoja yake ilitarajiwa kupitishwa na Bunge jana jioni na leo itakuwa zamu ya Wizara za Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na ile ya Maji. 
Kwa upande wake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, iliishauri Bunge kusubiri taarifa itakayowasilishwa na Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), baada ya kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na vyombo vingine vilivyopewa jukumu la uchunguzi. 
Akiwasilisha taarifa ya Kamati hiyo, Mwenyekiti wake, Victor Mwambalaswa alisema, “Katika hatua hiyo, Kamati yetu itashirikiana na Bunge kufikia uamuzi wa suala hili.” 
Kwa upande wake, Ndassa alisema wabunge wasipoangalia watajivunjia heshima wenyewe, kwani wanatumika sana, katika suala hilo la IPTL na Escrow. 
Katika michango yao, wabunge wengine wa CCM waliochangia jana jioni, Stephen Ngonyani ‘Maji Marefu’ (Korogwe Vijijini), Abdul Mteketa (Kilombero), Amina Kisangi, Godfrey Mgimwa (Kalenga), Richard Ndassa, waliipongeza Serikali kwa kazi nzuri katika sekta ya nishati na madini. 
Aidha, Mgimwa alitaka kifo cha baba yake, Dk William Mgimwa kutotumiwa katika masuala yao. Mgimwa alisema kuna watu wanapenda kuzungumza kwa matukio.  
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema fedha za REA katika mwaka wa fedha 2013/14 zilizobaki, zote zitapelekwa katika Mfuko huo kabla ya Juni 30, ambayo ni siku ya mwisho ya mwaka wa kifedha wa Serikali. 
Alifafanua kuwa fedha hizo ziliagizwa na Mahakama baada ya mgogoro wa IPTL na kwamba wenyewe wakipatana, wachukue fedha zao, hivyo kuhoji sasa zikirudishwa, zirudishwe kwa nini. 
Alisema kuna tatizo katika suala la gharama kubwa katika suala la umeme na kuhoji ni vipi jambo hilo haliishi na kwamba sasa linafika mwisho, watu wanataka lilirudi tena nyuma.

No comments: