KAMBI YA UPINZANI, SPIKA WAZUNGUMZIA KUSUSIWA BAJETI YA NISHATI NA MADINI



Sababu zilizowafanya Kambi Rasmi ya Upinzani, kutoka nje ya Bunge jana jioni wakiongozwa na Kiongozi wake, Freeman Mbowe, zimewekwa hadharani kuwa ni madai ya wenzao wa CCM walishajipanga kupitisha Bajeti hiyo, huku pia wakilalamikia ratiba ya mkutano huo wa 15 wa Bunge.
Hata hivyo, Spika Makinda alisema ratiba ya mkutano huo ilipangwa na Kamati ya Uongozi ambayo pia inamshirikisha Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, kwa hiyo iliridhiwa na kamati hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, alisema wapinzani hao wametoka nje kwa sababu wamegundua kuwa hawana jipya kutokana na Waziri Profesa Muhongo kujipanga ‘kupangua’ hoja zao.
Ndassa aliwataka wananchi wawahukumu wapinzani, kutokana na mambo wanayofanya, huku akihoji “kuna ubaya gani kwa wabunge wa CCM kukutana. Mbona wao wanakutana na sasa hivi huenda wanakutana huko.”
Akijibu hoja ya IPTL, Waziri Muhongo alisema upo ushahidi kwamba wapinzani wamepewa fedha.
“Picha za CCTV zimeonesha wakisaini huko huko IPTL. Kwa kuwa hawapo, tusubiri tutaona ukweli,” alisema Muhongo jana wakati akijibu hoja za wabunge.
Alisema hakupenda kulizungumzia suala hilo kwa kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda alishasema tusubiri uchunguzi wa Takukuru na CAG.
Alisema suala hilo si jambo jepesi, na kwamba hata yeye anazo hati mbalimbali zinazofikia gari lenye uzito wa tani moja na kushangazwa na wanaotamba kuwa wana hati mbalimbali za mgogoro huo.
“Watu wamekuja hapa wanakurupuka tu, sio watu makini, hivi vitu vya mahakama. Unajidhalilisha, hawa ni mamluki wa kifedha,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema tayari kati ya waliowasilisha hati zao kwa Spika, mojawapo ni feki, na kuonya kuwa Bunge lisitumike kama mahakama.
Alisema ni lazima suala la IPTL lifike mwisho kwa sababu linadhalilisha nchi na linakwamisha uwekezaji.
“Watu msikurupuke na vitu msivyovifahamu, ni aibu sana. Itabidi wakati mwingine watu tuone vyeti vya watu hapa,” alisema.
Aliwataka wote ambao wanapinga uamuzi uliotolewa na Mahakama, kwenda mahakamani kupinga badala ya suala hilo bungeni na kuudanganya umma wakati wanadai kuna kuheshimu mihimili ya Dola.

No comments: