WAGONJWA WA SARATANI ZA TUMBO, INI SASA KUTIBIWA MUHIMBILI



Wagonjwa wa saratani za tumbo na ini wataanza kupatiwa matibabu katika kituo cha magonjwa hayo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo hayo yataanza kutolewa hospitalini hapo baada ya Makamu wa Rais,  Dk Mohamed Gharib Bilal kuzindua kituo cha Tiba, Uchunguzi na Mafunzo ya Magonjwa ya Saratani za Tumbo na Ini.
Kituo hicho ambacho kimetolewa kwa msaada wa Chama cha Magonjwa ya Tumbo cha Munich cha Ujerumani, kupitia taasisi ya Else Kroner-Fresenius Stiftung, kimeelezwa kuwa ni cha kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na cha nne kwa Afrika.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Dk Bilal alisema kinatarajiwa kuwa msaada mkubwa kwa wagonjwa walio wengi na pia kuipunguzia serikali gharama za kwenda kutibiwa nje ya nchi.
"Magonjwa ya mfumo wa chakula na ini ni miongoni mwa matatizo makubwa ya kiafya yanayoikabili dunia nzima kwa sasa. Mtindo wa maisha kama unywaji wa pombe kupindukia na uvutaji wa sigara  ni sababu kubwa," alisema Dk Bilal.
Alisema kuwa ni wajibu wa hospitali hiyo, kuhakikisha inaongeza wataalamu watakaoendesha kitu hicho, pia kuhakikisha huduma hizo zinafikishwa mpaka mikoani na kwenye kanda nyingine ili kuwafikia Watanzania wengi.
"Katika kusaidia kukabiliana na upungufu wa wataalamu waliopo, serikali yangu itasaidia kufanikisha mafunzo kwa wataalamu zaidi ndani na nje ya nchi," alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari wa Matibabu ya mfumo wa Chakula cha Munich, Ujerumani, Profesa Meinhard Classen alisema anaamini kituo hicho kitakuwa msaada mkubwa kwa Watanzania, waliokuwa wakiteseka na magonjwa hayo.
Alisema mbali na kuwasaidia wagonjwa lakini pia itapunguza gharama za kuwapeleka wagonjwa nchi za nje kama vile India kwa ajili ya matibabu ya aina hiyo.
Katika ujenzi wa kituo hicho serikali ilichangia Sh milioni 800 na chama hicho kupitia taasisi ya Stiftung ilichangia zaidi ya Sh bilioni moja kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya matibabu ya kituo hicho.

No comments: