NAIBU WAZIRI AJIUA KWA KUJIPIGA RISASI, AMKABIDHI RAIS FAMILIA



Naibu Waziri anayemaliza muda wake wa Serikali za Mitaa nchini Malawi, Godfrey Kamanya, amejiua kwa kujipiga risasi, baada ya matokeo ya awali ya kura za ubunge, kuonesha ameshindwa kukomboa jimbo alilokuwa akishikilia la Lilongwe, Msozi Kaskazini.
Waziri huyo alijitoa uhai wake, jana saa 9.30 alfajiri akiwa nyumbani kwake Lilongwe.
Katika ujumbe wake aliouacha baada ya kujiua unaoshikiliwa Polisi, Kamanya alisema amechukua uamuzi huo kutokana na mkanganyiko wa kisiasa.
Mbali na sababu za kuchukua uamuzi huo, Kamanya alibainisha namna anavyotaka mali zake alizoacha zigawanywe, ambapo pia alimuomba Rais wa Malawi wa sasa, Joyce Banda asaidie kumsomesha mtoto wake.
Hata hivyo, baadhi ya ripoti zimeonesha kuwa Kamanya alikuwa akiishi kwa hofu, kutokana na vitisho alivyokuwa akipata kutoka kwa watu wasiojulikana. 
Kamanya alikuwa mbunge wa jimbo hilo la Lilongwe, Msozi Kaskazini tangu alipojiunga na chama cha PP.
Katika matokeo yasiyo rasmi yaliyotolewa juzi, yalionesha kuwa Kamanya anashika nafasi ya tano kati ya wagombea saba waliokuwa wakiwania jimbo hilo.
Matokeo hayo yalionesha kuwa Kamanya alipata kura 1,738, wakati mmoja wa wapinzani wake,  kutoka chama cha Malawi Congress, Hilton Jiya, alikuwa amepata kura 4,625. Katika baadhi ya kata na vitongoji,  Waziri huyo alikuwa akiambulia kura zisizozidi 35.
Kwa mujibu wa rafiki yake Kamanya, ambaye pia ni Waziri wa zamani wa Uchukuzi nchini humo, Ulemu Chilapondwa, mke wake alipokea simu kutoka kwa mke wa Kamanya, ikimtaarifu kuwa amesikia mlio wa risasi ukitokea katika chumba ambacho mumewe alikuwa amejifungia.
Alisema alipowasili nyumbani kwa marehemu akisaidiana na watu wengine wawili, walifanikiwa kuvunja mlango wa chumba hicho, na walipoingia ndani walikuta tayari Kamanya ameshakufa kwa kujipiga risasi kifuani.
Hata hivyo, Polisi nchini humo, imesema kuwa inachunguza zaidi tukio hilo.

No comments: