MKUU WA MKOA ATAKA WAKAZI DAR KUWA WASAFI


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik amewataka wakazi wa mkoa wake kuwajibika kusafisha mazingira yanayowazunguka na kuachana na tabia ya kuzilaumu Halmashauri za Manispaa. 
Akizungumza kwenye hafla ya Mradi wa Usafishaji wa Mto Mlalakuwa jijini Dar es Salaam jana, mradi unaofadhiliwa na kampuni zaidi ya nane, Sadik aliwalaumu madiwani na maofisa mazingira kwa kutotekeleza kazi zao  ipasavyo. 
"Unakuta wananchi wanatupa takataka kwenye mto, wanajenga kwenye kingo za mto lakini madiwani na maofisa mazingira hamchukulii hatua zozote," alisema na kuongeza: 
"Sheria ya mazingira na ya manispaa zote zinaeleza mtu haruhusiwi kujenga umbali wa mita 60 kutoka kwenye mto lakini bado wananchi na kampuni wanakwenda kinyume na hilo, watu wa aina hii lazima waripotiwe na kama hatua hazitachukuliwa basi karibuni mamlaka husika zitachukuliwa hatua kwa kukaa kimya". 
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Nabaki Afrika, Tania Hamiliton alisema ni wajibu wa kampuni zilizo karibu na eneo la Mlalakuwa kuhakikisha zinatoa kipaumbele kwenye utunzaji wa mazingira hayo. 
"Sisi Nabaki tumetumia maelfu ya dola za Marekani kusafisha mazingira. Usafi wa leo ni kutimiza miaka miwili ya kampeni yetu ya kusafisha mto huu wa Mlalakuwa na tunaziomba kampuni kama zetu kuwekeza fedha zao kwenye miradi kama hii," alisema Hamiliton. 
Wakazi wa Mlalakuwa eneo la Kawe kwa kushirikiana na kampuni hizo zilizofadhili walifanya usafi huo kwenye mto jana na kumalizia kwa bonanza lililofanyika kwenye ufukwe wa bahari ya Hindi karibu na Klabu ya Azura jijini Dar es Salaam. 
Katika usafi huo kulikuwa na kauli mbiu isemayo, “Mlalakuwa Mto wetu, Afya yetu". Kampeni hiyo imelenga kuonesha matatizo yanayosababishwa na utupaji ovyo wa taka za majumbani na taka za viwandani, hali inayosababisha matatizo ya kiafya kwa wakazi na wafanyabiashara waliopo karibu na mto huo. 
Wanaofadhili mradi huo ni pamoja na Nabaki Afrika, Bodi ya Maji ya Bonde la Mto Wami Ruvu, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Manispaa ya Kinondoni, Coca-Cola Kwanza, Mfuko wa Coca -Cola Africa, Bremen Overseas Research and Development Association (BORDA) na Deutsche Gesellschaft fur InternationaleZusammenarbeit (GIZ.)

No comments: